AN-NUUR
Na.168 Jamadul Akhir 1419, Septembe 24 - Oktoba 1, 1998

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita

 

Wanawake Singida walaani mauaji Mwembechai
  • Wasema Waislamu hawatarudi nyuma
  • Wamchangia Mama Chuki 17,000/-

Na Mwandishi Wetu

WANAWAKE wa Kiislamu mkoani Singida wamelaani udhalilishaji wanawake na mauaji yaliyofanywa na polisi mwezi Februari mwaka huu katika Msikiti wa Mwembechai Jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ilitolewa kufuatia mada iliyohusu kadhia ya Mwembechai ambayo iliwasilishwa na mmoja wa wahadhiri wa kongamano lililofanyika mwanzoni mwa wiki hii mjini humo.

Mhadhiri huyo kutoka Dar es Salaam alieleza kwa kina yaliyowasibu Waislamu na jinsi propaganda za kuficha ukweli zilivyokuwa zikiendeshwa na viongozi kupitia vyombo vya habari.

Wakitoa mawazo yao kufuatia mada hiyo, baadhi ya kinamama waliwataka Waislamu kutorudi nyuma baada ya mkasa wa Mwembechai bali "wanoe" imani zao ili wawe tayari kufa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Kongamano hilo lililofanyika katika viwanja vya Islamic Centre lilihudhuriwa na wanawake wanaokisiwa kufikia 2000 wa Singida mjini na vijijini.

Mwishoni mwa kongamano hilo, wanawake hao walichanga kiasi cha shilingi 17,000 kwa ajili ya pole kwa Mama Chuki ambaye walielezwa bado anauguza mwanawe (Chuki) aliyepigwa risasi katika kadhia hiyo.

Kina mama wa kijiji cha Sepeku waliahidi mchango zaidi kwa mama Chuki siku chache zijazo.



Sekondari ya Kiislamu kujengwa Maere Tanga

Na Abu Abdullah, Tanga

WAZAWA na wakazi wa Mtang'ata mkoani hapa wamesema watasimama kidete kujenga shule ya sekondari kwa ajili ya watoto wao.

Azimio hilo lilitolewa katika mkutano wa pamoja uliofanyika Septemba 13, mwaka huu kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Jumuiya.

Baada ya kuelezwa hatua zilizokwishachukuliwa na Kaimu Mwenyekiti Sheikh Hussein Abdallah kwa niaba ya Mwenyekiti Sheikh Jumbe Hamza waliohudhuria walipewa nafasi ya kutoa mawazo yao juu ya ufanikishaji shauri hilo.

Wengi waliopata nafasi kuchangia walisema kuwa wanamtang'ata wenyewe wanajitayarisha kwa nguvu kazi ya vijana wao, na suala la fedha taslimu za kugharimia, wameuacha mlango wazi kwa Waislamu wenzao kutoa sehemu yoyote kuwasaidia na wenyewe pia wameahidi kutoa chochote kwa kila itakavyowezekana.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria ni Mzee Abasi Dama wa serikali ya Kijiji cha Maere ambako liliko eneo hilo.

Mzee Dama alishukuriwa na wajumbe wa kamati ya ujenzi kwa ujasiri wake kusimamia upatikanaji wa eneo hilo ngazi ya kijiji.

Katika nasaha za ufungaji mkutano, Sheikh Hussein alikumbusha kwamba kheri nyingi za duniani na akhera zimeambatana na utoaji mali, hivyo Waislamu wasiwe wazito kwa hilo iwapo kweli wanataka mafanikio.

Alisema elimu tu ndio ufunguo kweli wa maendeleo, kwani hata mali unaweza kushindwa kujua pa kuitumia bila elimu.

Vijiji vilivyowakilishwa kwenye mkutano huo ni Kivindani, Kiwavu, Darugube na Maere.

Vingine ni Wanga, Sitakishari, Sadani, Tongoni, Tambarani na Mworongo.

Hata hivyo kwa vile eneo la Mtang'ata ni kubwa zaidi ya vijiji hivyo, na shule itawafaa Waislamu wa maeneo yote hayo, Wanamtang'ata ambao hawakuhudhuria siku hiyo, wamesikika wakisema wanajitayarisha kwa mkutano mwingine ujao, tayari tayari na sadaka zao.

Mkutano huo pia ulipata wawakilishi kutoka Pemba na Lushoto ambao walitoa salamu zao na kuzidi kuwatia moyo wenzao wa Mtang'ata.



Sheikh ahimiza Waislamu Lindi wafuate mafunzo ya Uislamu

Na Mohamed Mussa, Lindi

WAISLAMU wa mjini Lindi wametakiwa kufuata barabara mafunzo ya Uislamu ambayo msingi wake ni Qur'an na Hadithi za Mtume (saw) katika kuendesha maisha yao ya ndoa.

Hayo yalizungumzwa na Sheikh Jamaldin Salim, Imam na Mhadhiri wa Msikiti wa Chikongola mjini Mtwara katika sherehe ya ndoa iliyofanyika hapa hivi karibuni.

Sheikh Jamaldin alifafanua kuwa pale Mwenyezi Mungu aliposema: "Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu" anakusudia pendo linalofuata mafunzo ya Mtume (saw).

"Mtu asije akadhani kuwa kumuachia mkewe afanye mambo ambayo ni kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kama vile kuacha kusali, kutembea uchi, kwenda katika sherehe ambazo hazichungi mipaka ya Uislamu, zenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume na nyimbo za matusi kuwa ni kumpenda mkewe", alionya Sheikh Jamaldin.

Sheikh Jamaldin alielezea kuwa ndoa ni mkataba unaofungwa baina ya mume na mke chini ya usimamizi wa wazazi kwa kufuata misingi iliyowekwa na Allah (sw) mwenyewe na kama itabidi ivunjike basi ni kwa kufuata misingi hiyo hiyo.

Katika nasaha zake hizo ambazo zilikuwa na mvuto wa aina yake kwa kila aliyehudhuria katika sherehe hiyo, Sheikh Jamaldin alionyesha masikitiko yake kutokana na hali ya Waislamu kuacha mwongozo wao yaani Qur'an na Sunnah na kuhiari kukuhukumiwa kwa sheria za Kitwaghuti, "mwanaume na mwanamke wa Kiislamu kudaiana takala kwenye mahakama za Kitwaghuti ni makosa makubwa sana kwani mahakama hizo hazihukumu kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah na Allah" katika kusisitiza hilo Sheikh alinukuu aya isemayo: " Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri". (5:44)

Sheikh Jamaldin alisema: "Kama sheria ingelifuatwa katika taratibu za kutoa talaka, basi talaka za ovyo ovyo zingelipungua kwa Waislamu", akitoa ufafanuzi alisema talaka ina wakati maalum wa kutoa kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'an Suratul-Talaq.

"..Mtakapotoa talaka kwa wanawake toeni talaka wakati wa tahara zao ambazo hamkuwahi kuwaingilia " (65:1)



Sheikh Zuberi awataka Waislamu Dodoma kuimarisha Misikiti

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

IMAM wa Masjid Nunge Sheikh Zuberi amewataka Waislamu kuimarisha michango kwa ujenzi wa Msikiti.

Aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya michango ya fedha inayofanyika kila siku ya Ijumaa katika Msikiti wa Nunge.

Katika taarifa yake, Sheikh Zuberi alisema katika Ijumaa ya Septemba 11, mwaka huu jumla ya shilingi 71,600 zilikusanywa toka kwa waumini waliokusanyika kwa sala ya Ijumaa.

Msikiti wa Nunge ni miongoni mwa Misikiti mikongwe mkoani Dodoma, lakini uwezo wake ni mdogo sana katika kukusanya watu wengi katika sala ya Ijumaa au katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani na sala zingine zenye mikusanyiko mikubwa ya waumini kutokana na udogo wake.

Ni hali ya kawaida wakati wa sala hizo kufunga barabara zote nne zinazokutana hapo Msikitini na hadi upenuni mwa jengo moja la serikali barabara ya Mtendeni.

Hivi sasa Msikiti huo upo katika mpango wa kupanuliwa kwa kuunganishwa na kiwanja kilichokuwa kikikaliwa na Sheikh Kiza.

Wakati huo huo, Sheikh Abdul Azizi na Imam wa Masjid Bilal, amewausia Waislamu juu ya kuitukuza siku ya Ijumaa kwa kuoga mapema, kusoma Qur'an na kuleta nyiradi, pia kuomba sana maghfira kwa Allah (sw).

Nasaha hizo zimo katika khotuba ya Ijumaa aliyoitoa Msikitini kwake Septemba 18, mwaka huu.

Aidha, aliwaeleza Waislamu kuwahi sana kuingia Msikitini ili waweze kupata thawabu nyingi sana zinazothaminishwa na mtu kujikurubisha kwa Allah (sw).

 

Juu 
 

YALIYOMO  
 
TAHARIRI 
Iran ina agenda gani?

Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu

BUCHA YA NYAMA YA NGURUWE KATIKATI YA WAISLAMU
Na Mwandishi Wetu

'Serikali ieleze hatua iliyochukua kuhusu mauaji Mwembechai'
Na Kassim Juma

Vijana wa Kiislamu wajiimarisha Bukoba
Na Nooh Mustafa, Bukoba

Sheikh Mzonge awataka Waislamu Moshi wasimamishe swala
Na Ashraf Yussuf, Moshi

TAMKO LA PAMOJA LA MISIKITI SABA YA MWANZA-KUPINGA OMBI LA BAKWATA KWA SERIKALI LA KUIFUTIA USAJILI WAKE

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 7

MAKALA: Baadhi ya Watanzania wangali wanaishi ‘Tanganyika’
Na Mwandishi Wetu

HOJA BINAFSI: Maendeleo ya Tanzania ni ndoto
Na Fatma Mussa

‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Na Habiba Swedi, Arusha

Wanafunzi Waislamu Songea wapata viongozi
Na Mwandishi Wetu, Songea

Kikundi cha wanawake wa Kiislamu Bi. Khadija – Dodoma
Na Abu Zuberi, Dodoma

Waahidi kutekeleza majukumu kwa jina la Allah
Na Habiba Swedi, Arusha

Arumeru wahitaji Da’awa
Na habiba Swedi, Arusha

Wanawake wa Kiislamu wazungumzia maendeleo yao

Kauli ya wanawake wa Kiislamu Iringa kuhusu kadhia ya Mwembechai

Uislamu ulivyoingia Zanzibar

Wanawake Singida walaani mauaji Mwembechai Wamchangia Mama Chuki 17,000/-
Na Mwandishi Wetu

Sekondari ya Kiislamu kujengwa Maere Tanga
Na Abu Abdullah, Tanga

Sheikh ahimiza Waislamu Lindi wafuate mafunzo ya Uislamu
Na Mohamed Mussa, Lindi

Sheikh Zuberi awataka Waislamu Dodoma kuimarisha Misikiti
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mafundisho ya Quran 
Dhikiri maana yake nini? - 2

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Matatizo ya tumbo yanayosababishwa na utumiaji wa maziwa

Matangazo 
 

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org  

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita