|
AN-NUUR
|
| DARSA/MAKALA
Kikundi cha wanawake wa Kiislamu Bi. Khadija - Dodoma Na Abu Zuberi, Dodoma KIKUNDI cha wanawake wa Kiislamu kijulikanacho kwa jina maarufu Bi. Khadija kilianzishwa Januari 19, 1989 chini ya uongozi wa Mwenyekiti (Amira) Mwanahamisi Abdallah na Katibu wake Mwanaisha Mwinchumu. Kikundi hiki ni maarufu sana kwa harakati zake za kuhuisha Uislamu, kipo barabara ya nane kwa Mwenyekiti au kwa jina lake jingine Mama Haji, ambaye amejitolea nyumba yake kuwa darasa takriban kwa miaka tisa sasa. Pamoja na harakati hizo mwaka 1990 walifungua kituo cha watoto (Nursery School) kikiwa ndani ya uwanja wa saba saba, ambapo walipewa kwa muda katika jengo la Shirika la Reli. Mwaka 1996 jengo hili lilitakiwa na wahusika hivyo ilibidi wahamie Mji Mpya katika Jengo la Madrasati Ramiya, huku wakiwa na wanafunzi 60 wakiongozwa na Ustaadh Khamis Omar, wakisaidiana na Khamis Omar. Jitihada zao ziliendelea hadi mwaka 1992 walipofungua tawi jingine eneo la Hazina - X, wakiwa na wanafunzi 25, kituo ambacho kinaongozwa na Ustaadhat Bi. Zaurat. Masomo kama Qur'an, Fiqh, Siira, Hisabati na Kiingereza hufundishwa katika vyuo vyote viwili. Aidha, Mwenyekiti alitoa malalamiko yake kupitia gazeti hili kwamba pamoja na jitihada zote ambazo zinaonekana kwa waumini wa Kiislamu, na viongozi wote, lakini hawapati ushirikiano na kama upo ni mdogo sana hasa akitoa mfano pale walipohama toka katika uwanja wa saba saba ilibidi watume barua yao ya maombi katika ofisi ya C.B.A, barua iliweza kujibiwa kuwa hakuna Mjini kwa shughuli hizo. Haikushia hapo, walifika walokole na kumuona Afisa Mtendaji wa Kata, naye aliwaeleza kupata uwanja hadi wapitie Bakwata. Hali hii ilizidi kuwatia majonzi kwani hata huko Bakwata hawakupata jibu la kuridhishwa. Mwenyekiti alisema shughuli zao za (Da'awah) zilianza kuandamwa na baadhi ya watu kujawahoji juu ya shughuli na mikusanyiko yao ya kila mara. Alisema hali ilizidi pale tu walipoamua kutoa mchango wa fedha kuwasaidia ndugu zao wa Kiislamu waliopata mateso pale Mwembechai na kusababishwa baadhi ya Waislamu kuwekwa mahabusu na wengine kuuawa kwa kupigwa risasi. Aidha, Mwenyekiti huyo alisema pamoja na matatizo waliyonayo, mafanikio waliyoyapata ni makubwa hasa kuleta ushirikiano na vikundi vingine, kuendesha Da'awah kila mwisho wa wiki kwa kuwaendea Waislamu katika maeneo tofauti ya Mjini Dodoma. Mwenyekiti huyo alijumuisha taarifa yake kwa kusema kuwa hivi sasa wameshafyatua matofali na wataanza kujenga jengo lao.
Na Habiba Swedi, Arusha VIJANA wa Kiislamu watakaomaliza muda wao wa masomo mwishoni mwa mwaka huu katika chuo cha Ufundi Arusha (TCA) wametoa ahadi ya kwenda kufanyakazi kwa jina la Mwenyezi Mungu (sw) Na kwamba watajitahidi kadri wawezavyo kulinda mipaka ya maisha yao kwa mujibu wa maamrisho ya Allah mahali popote watakapokuwa. Ahadi hiyo imetolewa katika risala ya vijana hao wakati wa hafla ya kuagana na kutakiana kheri kwa wahitimu na wanaobaki, hafla hiyo ilifanyika chuoni hapo hivi karibuni na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, watu mashuhuri na wazazi. Walisema kwamba, katika kipindi chote walichokuwepo chuoni hapo, walijitahidi kuhimizana kumcha Mwenyezi Mungu, ambapo walikuwa wakihudhuria darasa za kila wiki ili kukumbushana juu ya maamrisho ya Allah (sw) na Sunna za Mtume (saw). Hata hivyo, walisema matatizo mbalimbali yalijitokeza yanayojumuisha ukosefu wa vitabu vya elimu ya dini, ukosefu wa Sheikh wa kuwafundisha na kutohudhuria swala ya Ijumaa kutokana na muda wa swala hiyo kuingiliana na vipindi vya darasani. Kutokana na matatizo hayo, ambayo vijana hao wameyaita kuwa ni ya muda mrefu, wamewaomba wageni waliohudhuria na Waislamu kwa ujumla kuwasaidia ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Bakwata ili tatizo la kuikosa swala ya Ijumaa litatuliwe kitaifa kwani ni tatizo linalozisibu shule nyingi hapa nchini. Walimalizia risala yao kwa kuwausia vijana wa Kiislamu wanaobakia chuoni hapo kuwa kioo na dira kwa wale ambao hawajapata maadili sahihi ya dini ya Allah (sw). Waliwasisitizia pia wajifunze ama kuuliza kile wasichokijua kwani kwa kufanya hivyo watamwogopa Mwenyezi Mungu na kumcha ipasavyo kama Mwenyezi Mungu alivyosema ndani ya Qur'an kuwa "Sikuumba majini na bindamu ila wapate kuniabudu". Akitoa mada katika hafla hiyo, mgeni rasmi Sheikh Hashim Lema aliielezea nafasi ya vijana katika Uislamu na dhoruba ya mabadiliko ya kiumbile ambapo alisema ni kipindi hatari kinachohitaji tiba kwa vijana ambayo ni kumjua Mwenyezi Mungu (sw) na kwamba vijana wakijitambua kuwa wana wajibu wa kumtafuta Muumba wao, Mwenyezi Mungu huwazidishia imani ya kumwabudu. Naye mtoaji mada mwingine Ustaadh Abu Ayman alizungumzia madhara ya pombe na zinaa kwa vijana wa Kiislamu. Alimnukuu Mtume Muhammad (saw) pale aliposema "Enyi Waislamu jiepusheni na pombe kwani ndio mama (chanzo) wa maasi yote". Alisema mbali na maasi, pombe huathiri pia afya ya mtumiaji. Hivyo aliwaasa kabisa vijana wa Kiislamu kushiriki ulevi kwa namna yoyote ile. Na habiba Swedi, Arusha WANAWAKE wa Kiislamu waishio Tengeni, wilayani Arumeru, wametoa kilio chao kwa Waislamu nchini kuwatembelea mara kwa mara ili kuwafahamisha zaidi juu ya dini ya Mwenyezi Mungu. Kilio hicho kilitolewa na mama Mwafutari Mzee kwa niaba ya wenzake kwenye mkutano na viongozi wa Umoja wa Vikundi vya Wanawake wa Kiislamu Manispaa ya Arusha uliofanyika katika Msikiti Jihad wilayani hapo, mwishoni mwa wiki iliyopita. Awali, mama Mwafutari ambaye ni Mwalimu wa Madrasa ya watoto Moshomo iliyopo mbali kidogo na Masjid Jihad, alifahamisha kuwa Msikiti huo umefunguliwa rasmi katikati ya mwaka jana na kwamba waumini wanawake wako nyuma kidini kutokana na ukosefu wa kuielewa dini na uhamasishwaji. Aidha, alitanabahisha kuwa, Uislamu wilayani hapo umefikishwa na wahamiaji, lakini wenyeji wameupenda na wanawake wengi wameamua kusilimu, jambo ambalo baadhi yao limewafanya watengwe na familia zao na hata hivyo kukosa msaada kutoka kwa Waislamu. Amesema pia vijana wengi waliosilimu na hata watu wazima wengine wanaishi bila ndoa, kutokana na kutokujua waende wapi kufungishwa ndoa. Kwa upande wa matatizo mengine, alielezea kwa kirefu na kwa kutoa mifano mbalimbali kwamba wanawake hawajui mengi yanayowahusu katika maisha yao ya kila siku kwa mujibu wa hali zinazowapata. Mara nyingi amekuwa akilazimika kuwaogesha mara inapotokea mwanamke kuhitimisha siku arobaini za uzazi ambapo hata hivyo yalibainika makosa mengi katika utendaji wa shughuli hiyo. Kutokana na matatizo hayo machache tu aliyoyataja, mama huyo amesema alipatwa na uchungu sana, akawa akihangaika kila siku kufutafuta Waislamu wa kuwapa Da'awa itakayopelekea kuisha kwa matatizo hayo na ndipo alipofanikiwa kuwaita viongozi hao baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa umoja huo mkoani hapa kupitia gazeti hili. Viongozi wa umoja wa vikundi vya wanawake wa Manispaa ya Arusha, walipokea "kilio" hicho kwa masikitiko makubwa na waliwapongeza wanawake hao kwa uamuzi wao wa kuwaita. Alipozungumza nao, Mwenyekiti wa Umoja huo, Ustaadha Maryam Salim Ally, alisisitiza uanzishwaji wa madrasa ya wanawake, lengo kuu likiwa ni kusoma, kuujua Uislamu ili kuwapa radhi za Mwenyezi Mungu na kwamba kila mtu awe na uchungu wa kupata elimu, ndipo wataweza kuyatatua matatizo yao hatua kwa hatua. Amesema, elimu ni sawa na karabai iwakayo katika giza nene, mwangaza wake utakuwa ni faraja kwa waliokuwa gizani. Hivyo, aliwataka kutia nia ya kujitoa katika giza la ujinga ambalo alilifanisha na maradhi mabaya mno yasiyofaa kuwa nayo Muislamu. Aidha, aliwatahadharisha dhidi ya mbinu za Ibilisi na kuwataka wasikate tamaa na wasimame kidete kukakikisha madrasa haivunjiki na pia wawe wasikivu na watiifu kwa mwalimu wao. Naye Katibu wa umoja huo, Ustaadha Sadia alizungumzia kwa kirefu mavazi ya mwanamke wa Kiislamu. Aliwatoa shaka juu ya uvaaji wa baibui refu kuwa eti ndio vazi pekee linalostahili kuvaliwa kwa mujibu wa suala zima la vazi la stara linapohusika. Alisema ikiwa nia ni kujisitiri, hapana budi kufanyike kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah na kwamba kwa kuanzia, khanga na vitenge mavazi ambayo wengi wanayamudu kuyanunua yatumike.
MAPEMA Julai mwaka huu, vikundi vya wanawake wa Kiislamu kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro walikutana Jijini Dar es Salaam kujadili maendeleo yao. WARSHA hiyo juu ya Da'wah na Maendeleo iliandaliwa na kikundi kimoja cha Mtandao wa vikundi vya wanawake wa Kiislamu, Sahiba Sisters kwa madhumuni ya kuyajadili kwa kina masuala muhimu kwa wanawake wa Kiislamu katika karne ya 21 kwa kuzingatia mambo gani yanawarudisha nyuma na ambayo wanahitaji kuyafanyia kazi. Anaeleza Mratibu wa Sahiba Sisters, Bi. Mariam Mtingwa, "Tanzania sasa iko katika kipindi cha mpito. Mabadiliko mengi sana yanatokea ambayo yanawaathiri wananchi moja kwa moja. Mpaka sasa, wanawake wa Kiislamu wamekuwa hawasikiki kuhusiana na mabadiliko haya kama wanawake wengine. Lakini sasa tumeazimia kubadilsha hali hii". Mambo mengi yaliyojitokeza katika warsha hiyo ya siku mbili yakiwemo malezi ya vijana, elimu kwa vijana na hali na haki ya mwanamke nchini na katika jamii ya Kiislamu. Masuala haya yalipangiwa mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu ili kuviwezesha vikundi hivyo kuyadhatiti katika kuleta maendeleo yao. Yanayofuata ni baadhi ya masuali muhimu yaliyoibuliwa na kujadiliwa: Sensa inatuhusu vipi? Mwaka huu ni mwaka wa sensa. Sensa ya kitaifa huendeshwa kila baada ya miaka kumi. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 1988 na baina ya kipindi hicho na sasa kuna mabadiliko mengi yaliyotokea ambayo kwa namna moja au nyingine yanaathiri maendeleo ya kila mtu hususan ya Waislamu lakini ni vikundi vichache vya Kiislamu vilivyojiandaa kuhusiana na suala hilo. Suala kuu lililojadiliwa kuhusu sera ni kuelewa idadi ya Waislamu nchini na hatimaye idadi ya wanawake wa Kiislamu katika kuwezesha maendeleo yao. Kumekuwa na takwimu za kutatanisha kuhusiana na idadi ya Waislamu. Baadhi ya mashirika ya kigeni yanakadiria kuwa Waislamu nchini ni baina ya 23% - 45% wakati katika sensa ya mwisho (1988) walikuwa 33%. Hata hivyo, kabla ya uhuru idadi ya Waislamu nchini ilikadiriwa kuwa zaidi ya 80%. Je, tofauti hizi zinatokana na nini na zina athari gani kwa maendeleo ya wanawake wa Kiislamu hasa ikizingatiwa kuwa idadi ya watu ndicho kigezo kikuu cha kugawa rasilimali zilizopo na kufaidi fursa mbalimbali kama elimu, mikopo na huduma nyinginezo muhimu kwa maendeleo? La kutisha kuliko yote ni kupungua kukubwa kwa idadi ya Waislamu wakiwemo wanawake wa Kiislamu katika kipindi cha miaka 30 Tanzania. Je, zaidi ya 50% ya Waislamu baina ya uhuru na 1988, na 10% baina ya 1988 hadi sasa wamekwenda wapi? Baada ya kuanza kwa sera ya mtoto mmoja huko China kulionekana kwamba idadi ya wanawake imepungua kwa 1%. Mataifa ya Kimagharibi na taasisi za haki za binadamu zikaanza kulipigia kelele suala hilo kwa vile mamilioni ya wanawake walikuwa wamepotea hivi hivi. Je, kati ya Waislamu 60% waliopotea katika takwimu za watu Tanzania wanawake wa Kiislamu wamekwenda wapi? Elimu ndiyo ufunguo wa maisha na katika dini ya Kiislamu, elimu imeshurutishwa kwa kila Muislamu awe mke au mume. Hata hivyo, imebainika kwamba bado kuna wazazi wa Kiislamu ambao hawataki kuwapeleka watoto wao shuleni eti kwa sababu si shule za Kiislamu. Wazazi ambao hupeleka watoto wao mashuleni mara nyingi hulazimika kuwapeleka watoto wao katika shule za kawaida ambapo hukosa mafunzo ya dini yaani madrasa. Kama wasomi ndio tegemeo letu katika kupata viongozi bora na kutuletea maendeleo, kwa hali hii viongozi hao watapatikana wapi? Bi. Latifa Masoud kutoka Kinondoni alipendekeza kuanzishwa kwa shule za Kiislamu ili kuwapatia wanawake fursa za elimu katika misingi inayokubalika katika dini yao kwa mfano katika uvaaji wa vazi la stara. Ingawa shule hizo zipo, je, shule zetu zina uwezo wa kufundisha? Walimu wetu wana uwezo wa kufundisha? Matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka huu ni mfano mzuri. Naye Bi. Ramla kutoka Morogoro alidokeza, "wenyewe Waislamu hatuna imani na shule zetu na huwapeleka watoto huko wakishindwa kuendelea na masomo kwingine tu. Vile vile, walimu tunaowaajili huwa hawana viwango vya kuridhisha vya kufundisha na hili limebainika katika shule zetu za Morogoro". Zaidi ya hapo, mazingira ya shule zetu au sehemu tunapowafundishia watoto hayamvutii mtu au mtoto kuona umuhimu wa elimu. Kwa mfano, madrasa nyingi ni chafu na ndogo kiasi kwamba hewa na mwanga hazipiti vizuri. Nyingi hazina vyoo au vyoo viko taabani na mtoto hulazimika kukimbilia nyumbani kujisaidia! Katika hali kama hii, washiriki walikubali kwamba suala kuu ni kujenga mfumo wa elimu utakaowasaidia wao na watoto wao jidhatiti. Tunakwenda wapi, tuna malengo gani? Dira ya vikundi vilivyowakilisha ndiyo iliyokuwa dhamira kuu ya warsha hiyo. Suala kubwa kwa washiriki wote na mtandao ni kutambua mwelekeo wa pamoja ni upi? Mkufunzi kutoka Sahiba aliwauliza washiriki, "Je, katika vikundi tuna tamaduni ya kupanga mambo yetu au hukurupuka tu tukatenda? Leo likizuka jambo, tunaweza kupata sauti ya pamoja au tutabaki tuna tangatanga na kulalamika tu? Na je, wenzetu watatuunga mkono katika hilo jambo?" Katika kupata ufanisi wa vikundi, dira ilionekana ni nyeti kwani dira nzuri hukiwezesha kikundi kufikia malengo yake. Kwa upande wa mtandao kuwepo kwa msimamo wa pamoja miongoni mwa vikundi huuwezesha mtandao kufanikiwa katika azma yake. Kwanini imani yetu ni dhaifu? Mara kwa mara washiriki walikuwa wakijiuliza nini chanzo cha matatizo yanayowakabili hasa ikizingatiwa kuwa dini ya Kiislamu inarahisisha maisha ya watu na kuwapa uongofu? Baada ya mjadala wa muda, washiriki walikubaliana kwamba chanzo cha matatizo yao ni imani dhaifu. Alisema Bi. Ramla, "Wengi tumekuwa ni Waislamu jina tu. Mafundisho na maagizo ya dini tumeachana nayo. Kwa mfano, wengi hatutaki kujuana na Waislamu wenzetu seuze kusaidiana.Mmoja akipata wadhifa basi anajiona ndio kafika. Hivyo leo katika maofisi au shuleni, Waislamu ni wakuhesabu na katika uchache wao hawana ushirikiano". Wajumbe wengi walimuunga mkono Bi. Ramla. Akichangia Bi. Laula Malekela kutoka Iringa, "Leo hii, ukimuomba Muislamu achangie jambo la kheri la kuwaendeleza wenzake haoni sababu lakini mtu huyo huyo anaweza kutupa pesa zake katika anasa. Mifano tunayo kwani hakuna jamii inayochangia michezo na mashindano ya warembo kama Waislamu". Kweli namna hii tutapata maendeleo? Imekuaje watu waliolelewa katika Uislamu leo wakawa hawana habari nawo? Mazingira yetu yanafaa, yanavutia? Mazingira wanayokalia na kufanyia shughuli nyingi kwa mujibu ya washiriki, hayaridhishi. Misikiti mingi na madrasa havina vyoo vya kuridhisha. Vyoo vingi ni vichafu na huwa makazi ya mbu. Vile vile, majamvi huwa taabani. Ufundishaji na mandhari ya sehemu ambapo Waislamu hukutana hazizingatii mahitaji ya watoto na wanawake. Watoto wengi hutoroka chuo hata kama ni jirani na wanakoishi kwa sababu ya bakora na ufundishaji mbaya. Tatizo ni lipi? Je, wazazi tumejaribu kuwauliza watoto wetu kwa nini wanatoroka chuo au na sisi huwacharaza bakora tu? Tunategemea tutajenga imani za watoto wetu kama hali yenyewe ndio hii? Matendo yetu na kauli zetu havitoi sura ya Uislamu? Washiriki waliamua kuchunguza mienendo yao kwa kutizama matendo na kauli zao kama kweli zinaendana na mafundisho ya Kiislamu. Kwa mfano walijiuliza, "Watoto wetu tunawaitaje? Tunazungumza vipi na wenzetu? Kutokana na migogoro ya hivi karibuni ama baina ya Waislamu na Serikali au Waislamu na taasisi za Kiislamu, Bi. Lateefa alidokeza kwamba, "Madhumuni ya Da'wah ni kupeana ujumbe mwema lakini wengi wetu, kazi yetu ni kuombeana laana tu na si uongofu. Hivyo, badala ya kujenga upendo baina ya Waislamu, huendeleza uhasama. Je, haya yanafanywa kwa manufaa ya nani? Kwanini Waislamu ambao hawako katika mstari hawaendewi kwa busara? Ikishindakana kwanini wasiombewe uongofu? Kweli hivi ndivyo tunavyoagizwa katika Qur'an? Suala la malezi pia lilitiliwa mkazo kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya watoto wa mitaani na mayatima. Je, kweli kesho wanatarajiwa wawe waumini wazuri? Watoto wakiwa taifa la kutegemewa kesho, umma utapata wapi waumini na viongozi wa baadaye? Aliuliza Bi. Laula baada ya kudhihirika kwamba watoto wengi wanalelewa katika misingi isiyokuwa ya Kiislamu. "Jukumu la kuwalea watoto wetu ni la nani?" Wanawarsha waliona kuwa matatizo yanayowakabili ni mengi na vyanzo vyao ni vingi. Muhimu zaidi ni wao wenyewe ndio wahusika wakuu katika kuleta maendeleo yao wenyewe na warsha hiyo imewapa mbinu za kujidhatiti vyema katika kufikia malengo yao na kuleta maendeleo yao. Wanawake hawa waliazimia kukutana tena mwisho wa mwaka kutathmini maendeleo yao.
UKWELI na uwazi ni tamko tunatoa sisi akina mama wa Mkoa wa Iringa, tukiungana na akina mama wenzetu waliopata msukosuko na tabu katika jihadi iliyotokea Mwembechai. Tunasema tabu na adha mlizozipata si yenu pekee, bali ni akina mama wote Waislamu Tanzania nzima, kwa yeyote aliye Muislamu. Tunachosema sisi, enyi wapinzani wa Uislamu, enyi maadui wa Mwenyezi Mungu, kwetu sisi hamna thamani yoyote, hata tuwatukuze na tujidhalilishe! Enyi wapinzani mnadhani kuwa kwa vile mmezitawala kambi zote za ardhi, sisi tumekuwa dhalili? Nanyi mmekuwa wafalme? Mnafikiri kuwa kwa mbinu hizo mmepata nguvu na hivyo mnajitukuza kwazo na kutakabari! Katika tukio la kuuawa mashahidi wa Mwenyezi Mungu na kudhalilishwa wanawake, kuteswa wahadhiri na kuwekwa ndani, ni namna moja kutimiza hija hii kuwa, pale haki inapokanyagwa na kudharauliwa, basi hulazimika kupambana na dhulma na kuwatetea wanyonge. Sisi tumesimama kama ni mashahidi wa Mwenyezi Mungu. Tumesimama kwa sababu mnavunja ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mmeacha mwenendo wa Mtume Muhammad (saw), mmechupa mipaka ya Mwenyezi Mungu? Ambapo Mtume (saw) anasema yeyote atakaye yanyamazia haya bila ya kuyakataza na kuyabadilisha basi makazi yake siku ya kiama yatakuwa motoni pamoja na makafiri wale wanaopinga mipaka ya sheria za Kiislamu na kutupilia mbali Sunna za Mtume (saw). Kwa hivyo watu hao sisi tutapambana nao ikiwa ni kivuli cha kuamrisha mema na kukataza mabaya. Enyi mnaonusuru na kuyapa ushindi mabaya na mkadharau na kuyakanyaga mema, mnawatawala watu pasi na wao kuridhika, na mnaongoza kinyume cha maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuwalazimisha watu wakubali, mbinu na mienendo yenu haina tofauti na ile ya Kisra na Kaisari. Nasi tumekuja ili kuwaamrisha watu mema na kuyakataza mabaya na kuwasomea kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Bwana Mtume Muhammad (saw). Eleweni yakuwa, wale wote waliokufa shahidi, na kuacha maneno yao yenye thamani na mwamko bado yamebakia mithili ya matamshi ya viongozi wetu waliuawa. Yote hayo bado yako yanaelea kwenye nuru ya milele na siku zote tunayakumbuka katika ncha ya maisha, mauti, ushindi na kushindwa. Katika neno shahidi kumeandikwa vipengele vingi vya kimaisha na kiharakati, kimsingi Uislamu unauhesabu ushindi kuwa ni thamani moja kubwa yenye cheo cha juu kabisa. Umuhimu wake hauna budi kuchunguza ndani ya maisha matukufu ya kuikuza na kuitukuza jamii ambayo inaishi katika hamasa ya kujitolea kufa shahidi. Sisi akina mama tunaona kuwa uongozi uliokuwepo unapiga vita misingi ya dini kwa kutumia silaha ya dini kutokana na hasa silaha zote za kijeshi na propaganda yote yamo mikononi mwao, kutokana nahali hii sisi tunachagua kufa shahidi ambako huzaa utambuzi, huleta uhai na harakati na kuipambanua haki dhidi ya batili mbele ya watu waliodanganywa. Tamko letu ni haki ya kujiongoa, kwani hatutaki udhalimu. Harakati zetu ni mapambano dhidi ya dhulma, kufru na batili. Hivyo, kila wakati ambapo shirki, ujinga, udhalimu na kuhusudu haki za watu kutakakokuwepo kwa sura mbalimbali. Sasa kila mtu hana budi kujiangalia yuko upande gani kati ya pande hizi mbili? Je, anajifahamu pamoja na haki? Au anajidhalilisha chini ya batili? Amani ziwe juu yenu kwa roho zote zilizojitoa muhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wa kubakia kwetu hai na kubakia kwa usiku na mchana. |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org