AN-NUUR
Na.168 Jamadul Akhir 1419, Septembe 24 - Oktoba 1, 1998

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita

 

BARUA

Akina dada mashuleni hijab ni haki yetu

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipe nafasi ili nami nitoe machache kuhusu suala la hijabu mashuleni.

Kwa sababu ya kulinda usafi, tabia na heshima, Allah (sw) ameweka sheria ya kuvaa vazi la stara kwa akina dada (wanawake).

Ametuwekea ili kujenga jamii bora ya watu wenye maadili mema. Kutopinga amri hii ni kutekeleza aya ifuatayo Allah (sw) anasema:

"Haiwi kwa mwanamme aliyeamini, wala kwa muumini mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri wawe na khiari katika shauri lao".

Allah (sw) ameshatuwekea sheria ya kuvaa mavazi ya stara na si kwa kumfurahisha yeye tu, bali ni kwa faida yetu. Hivyo basi hatuna haja ya kuhoji juu ya hili. Allah (sw) anasema:

"Na waambieni Waislamu wanawake wainamishe macho yao, wazilinde tupu zao wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vile vinavyodhirihika (vitanga vya mikono na uso) Na wajishushie shungi zao mpaka vifuani mwao "

Mtume (saw) pia anasisitiza kauli ya Allah (sw):

"Mwanamke atakapobalekhe hairuhusiwi sehemu yake yeyote ya mwili kuonekana isipokuwa uso na vitanga vya mikono".

Kwa kulifahamu suala la hijabu na umuhimu wake, Baraza la Waislamu kupitia sherehe za Maulidi zilizofanyika mwaka 1995 mjini Dar es Salaam liliomba ruhusa kwa serikali kutekeleza amri hii ya Allah (sw).

Nayo Serikali kwa kujua kuwa hii ni amri ya Allah (sw) na ni sehemu ya ibada ya Muislamu ambayo utekelezaji wake wala haukuhitaji ruhusa ya serikali, serikali ikauruhusu kupitia kwa Rais.

Cha kushangaza ni pale Mkuu wa Shule anapojitokeza kwa moyo mgumu usiotaka kutii sheria za Allah (sw) kuwakataza dada zetu wa Kiislamu kuvaa vazi hili la heshima, kwa visingizio vya umoja utavunjika au utofauti!

Kama ni utofauti upo siku nyingi kati ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Tunatofautina kwa majina na hata tabia. Wapo wanaofanya ibada Jumapili na wapo wa Jumamosi na sisi Waislamu kila siku japo hawataki kulitambua hili. Na hatuoni mambo yoyote ya kuvunja umoja katika haya.

Lakini jambo la kujiuliza labda ni hili, wapi anapata jeuri huyu Mkuu wa Shule? Licha ya kikao cha Bodi kupitisha hili, hijabu katika shule inakuwa bado ni kitendawili.

Kuna umuhimu wajitokeze akina Musa kuwasaidia akina dada hawa wanaotaka kutekeleza amri ya Allah (sw).

Musa alipowakuta akina dada wale wawili wa Madyani aliwauliza mbona hamnyweshi mifugo yenu? Na alipogundua kuwa kuna watu licha ya kuwa na nguvu hawakuwajali aliamua kutoa msaada yeye mwenyewe.

Hali ya Waislamu inatisha sana jamani. Watu wananyimwa matibabu, wanapotezewa muda wao wa masomo kwa vikao, wanabezwa na walimu na wafanyakazi, wanatukanwa na manyanyaso ya kila aina, fanyeni uchunguzi msingoje mwandikiwe kwa maandishi, Uislamu hauendelezwi kisekula.

S.S. Kilakala,
Iringa.


Uadilifu katika ndoa

Ndugu Mhariri

NAPENDA kumuunga mkono Ndugu Abdallah A. Abdallah katika barua yake ya Jamadul - Awwal 1419 H, Septemba 18 -24, 1998.

Barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari "Uadilifu baina ya mke na mume wanapokhitilafiana".

Ama kwa hakika barua hiyo ni "darsa" ya kutosha kwa kila aliyeingia katika maisha ya ndoa.

Hakika Uislamu ni dini ya uadilifu kweli, ulimwengu wa leo watu wengi dunia wameiweka mbele zaidi kuliko Akhera.

Kila mtu laiti angaliisoma Qur'an vilivyo na Sunnah sahihi za Mtume wetu Muhammad (saw) lazima ukweli ungelionekana.

Ni tofauti kabisa na asilimia kubwa ya ulimwengu wa kileo baada ya watu kupatwa na matatizo ndio wanarejea kwenye Qur'an na Sunnah na kuuona ukweli.

Ndoa nyingi huvunjika baada ya kutokezea kutokuelewana baina ya mke na mume kwa kukosekana uadilifu kati ya wazee wa mtoto mwanamke au mwanamme.

Ilivyo hasa ni kupatanisha lakini ulimwengu wa leo jinsi ujinga ulivyokithiri inapojitokeza hitilafu na mmoja wao kupeleka mashitaka kwa wazee, badala ya kufuata kama sheria ilivyo, wao huona "damu nzito kuliko maji" humpa kichwa zaidi mwanawao na kumwambia "hapa umefika mwanangu".

Mara nyingi ndoa ikiingiliwa haidumu, vile vile jamaa wa karibu wa mtoto mwanamke au wanaume ambao hawana amri mbele za wake zao hawa ndio wanaoharibu ndoa.

Hamna ndoa hata moja yenye maelewano ya kila siku, lazima hitilafu zitajitokeza si watu wa kawaida wala Masheikh, wafalme hata Marais.

Asilimia kubwa ya ndoa huvunjika kwa sababu ya kukosa busara, hekima, uadilifu na hasira.

Mwisho napendekeza ndugu Mhariri kiundwe kitengo maalum au taasisi maalum inayohusiana na mambo ya ndoa katika jamii, watu waelimishwe, wafuate sheria, haki, uadilifu n.k.

Said Saleh Omar,
P.O. Box 5252.



Msikiti una nafasi pana katika Uislamu

Ndugu Mhariri

KATIKA gazeti la AN-NUUR Na. 163 la Agosti 21-27, 1998 sawa na Rabiul-than 1519, ilichapishwa barua yenye kichwa cha maneno "Maulidi na kujenga Misikiti hatufiki mbali" ya Bw. Haddi.

Naamini kuwa ndugu Haddi alikuwa na lengo zuri tu la kuwazindua Waislamu kujenga mahospitali na shule nyingi zao binafsi ili kuendeleza Uislamu wetu katika upeo mpana na tuepukane na usumbufu wa kunyanyaswa kwa njia moja au nyingine kama hali ilivyo hivi sasa.

Lakini Bwana Haddi kama uhimizaji wake ameingiza mambo mengine kwa kuyaona kuwa sio muhimu sana katika kipindi hiki tulichonacho. Lakini ameshindwa kujua nafasi ya vitu hivyo alivyovielezea navyo ni sherehe za Maulidi na ujenzi wa Misikiti kwa wingi.

Inshaallah kupitia barua hii ataweza kuelewa vema vitu viwili hivi kwa maana yake, kazi zake na umuhimu wake katika kipindi hiki kigumu cha kuuhami Uislamu wetu.

Nikianza na Misikiti ikiwa ndio jambo lililochomoza zaidi, namnukuu pale aliposema kuwa "Misikiti haiwezi kujenga hospitali na shule bali bali hospitali na shule zinaweza kujenga Misikiti".

Hapa niligundua mapema kuwa ndugu yetu ameshindwa kuelewa nini maana ya Msikiti na unamaendeleo yapi au nafasi gani katika Uislamu.

Hivyo akadhani Msikiti ni mahala pa kuswalia tu, ndio maana akadiriki kuhoji mwishoni mwa barua yake kuwa, 'Je, ni Muislamu gani katika nchi hii amekosa nafasi ya kuswalia eti Misikiti ni michache?".

Hivyo kwa muhtasari huu napenda Bwana Haddi afahamu kuwa kazi ya Msikiti si pahala la kusalia tu, ingawa sala ni sehemu ndogo katika kazi za Msikiti.

Kwa kifupi, vema afahamu kukazia Msikiti ni nyingi mno, lakini kwa kusema kuwa Misikiti ni kwa ajili ya Ibada, ambayo ndio lengo pekee la kuumbwa na kuwepo kwake mwanadamu katika dunia.

Hivyo utakuta kuwa kila kipengele anachokipitia mwanadamu (Muislamu) katika kuyaendea maisha yake ya kila siku katika siku za maisha yake ni Ibada, hii inakusanya pamoja na matibabu (hospitali) kusoma (shule) biashara (masoko) malezi bora ya watoto (familia), ukulima (mashamba), n.k. Hivi vyote ni Ibada lakini vikifanyika katika misingi aliyotuelekeza Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wetu (saw).

Bwana Haddi ni lazima akumbuke kuwa mara baada ya Mtume (saw) kuhamia Maddina, jambo la mwanzo kuamrishwa na Allah (sw) ni kujenga Msikiti, hivyo katika kipindi chote cha maisha yake Mtume (saw) akawa shughuli zote za kimaisha kama afya, elimu n.k. vilifanyikia Misikitini na ndio zikawa na ufanisi mzuri hata leo mimi na Hadi tumebahatika kuona Uislamu.

Ni dhahiri kutatoka hoja kuwa huenda wakati wa Mtume (saw) walifanya hivyo kwa kukosa mahala muafaka kufanyia shughuli za kiafya, kielimu n.k. Jibu lake ni hapana, bali Mtume (saw) alifanya hivyo kwa hekima kubwa, kwani ilikusudiwa kuwa ni kigezo kwa sisi tufuatao nyuma kwamba tujengapo Misikiti lazima tufuate ramani ya maandishi aliyotuachia Mtume (saw) ramani ya kugawa maeneo ya Msikiti kutokana na mgawanyiko wa utekelezaji wa ibada mbalimbali kama zilivyogawiwa.

Hivyo, utagundua kuwa katika eneo la Msikiti lazima pawepo ndani yake shule, hospitali, mahakama, kumbi za mikutano na ofisi mbalimbali za kiutendaji kimaisha na hata viwanja vya michezo mbalimbali vinapasa viwepo ndani ya ramani ya Msikiti.

Hii ndio ramani ya Msikiti ambayo ametuachia Mtume (saw). Lakini kutokana na ufinyu wa kihali na maeneo yenyewe katika upatikanaji wake, sio lazima kila Msikiti ukusanye hayo yote niliyoyataja, lakini ni budi kwa Waislamu tujenge misikiti yenye sura hii karubu katika kila wilaya za nchi yetu bila kusahau kujenga Misikiti midogo migogo katika mitaa tunayoishi na kujenga sekta zingine za ibada kama shule za watoto, hospitali n.k. katika maeneo mengine, kwani na zenyewe ni Misikiti.

Bwana Haddi lazima pia ufahamu kuwa ili kujenga hospitali na shule za Kiislamu, ni budi Waislamu wapate mahala pasipoingiliwa kirahisi na maadui wa Uislamu, ndio waweza kufanya mipango ya utekelezaji humo, hivyo utakuta hakuna sehemu ambayo Waislamu wanayoweza kukutana na kupashana habari kirahisi zaidi ya Msikitini.

Hivyo, wingi wa Misikiti ni hatua nzuri ya kuwafanya Waislamu wawe na nafasi nzuri na salama katika kujadili na kupanga mambo yao kirahisi ndani ya Misikiti iliyopo katika kila kitongoji au mtaa na hii italeta wepesi wa kuwasiliana baina ya Waislamu walioko tofauti kimakazi.

Wabilah A'alam

Said A. Mbegani,
S.L.P. 163, Mikumi,
Morogoro.



Waislamu shule ya Usagara hijabu ziko wapi?

Ndugu Mhariri

NAOMBA kutoa mawazo na malalamiko yangu kupitia gazeti lako hili tukufu ili kuwza kuwahamasisha ndugu zetu Waislamu kuhusu sheria hizi za kujistiri kufuata taratibu alizoziweka Allah (sw) na sheria zake katika vazi la hijaab hasa kwa wanawake wa Kiislamu.

Jambo hili lilikuwa likinikera tangu siku za nyuma. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya Usagara Sekondary Tanga ambapo sisi wanafunzi wa Kiislamu tumekubaliwa kuvaa Hijaab lakini sisi wenyewe hatulitilii mkazo ndio maana tunalizembea.

Ambapo mtu akivuliwa hijaab na mwalimu msimamizi wa wasichana (matron) hulalamika, lakini utamkuta huyo huyo akija jioni katika michezo utamwona amevaa nguo za ajabu ajabu na ukiwaambia wanakutolea maneno ya kashfa.

Sasa je tusipoangalia hili sisi wanafunzi wa Usagara tutakuja kusema nini mbele ya Mola Karima. Au kama hamtaki kuvaa hijab basi vaeni sketi na blauzi wanazovaa Wakristo ili musituaibishe sisi wanafunzi wenzenu tunaopenda Uislamu.

Sio asubuhi unavaa hijab, jioni unaonekana umevaa nguo za ajabu, msituharibie Uislamu wetu bado tunautamani.

Wabilah Taufiq

Mwanafunzi,
S.L.P. 330,
Usagara,
Tanga 

Juu 
 

YALIYOMO  
 
TAHARIRI 
Iran ina agenda gani?

Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu

BUCHA YA NYAMA YA NGURUWE KATIKATI YA WAISLAMU
Na Mwandishi Wetu

'Serikali ieleze hatua iliyochukua kuhusu mauaji Mwembechai'
Na Kassim Juma

Vijana wa Kiislamu wajiimarisha Bukoba
Na Nooh Mustafa, Bukoba

Sheikh Mzonge awataka Waislamu Moshi wasimamishe swala
Na Ashraf Yussuf, Moshi

TAMKO LA PAMOJA LA MISIKITI SABA YA MWANZA-KUPINGA OMBI LA BAKWATA KWA SERIKALI LA KUIFUTIA USAJILI WAKE

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 7

MAKALA: Baadhi ya Watanzania wangali wanaishi ‘Tanganyika’
Na Mwandishi Wetu

HOJA BINAFSI: Maendeleo ya Tanzania ni ndoto
Na Fatma Mussa

‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Na Habiba Swedi, Arusha

Wanafunzi Waislamu Songea wapata viongozi
Na Mwandishi Wetu, Songea

Kikundi cha wanawake wa Kiislamu Bi. Khadija – Dodoma
Na Abu Zuberi, Dodoma

Waahidi kutekeleza majukumu kwa jina la Allah
Na Habiba Swedi, Arusha

Arumeru wahitaji Da’awa
Na habiba Swedi, Arusha

Wanawake wa Kiislamu wazungumzia maendeleo yao

Kauli ya wanawake wa Kiislamu Iringa kuhusu kadhia ya Mwembechai

Uislamu ulivyoingia Zanzibar

Wanawake Singida walaani mauaji Mwembechai Wamchangia Mama Chuki 17,000/-
Na Mwandishi Wetu

Sekondari ya Kiislamu kujengwa Maere Tanga
Na Abu Abdullah, Tanga

Sheikh ahimiza Waislamu Lindi wafuate mafunzo ya Uislamu
Na Mohamed Mussa, Lindi

Sheikh Zuberi awataka Waislamu Dodoma kuimarisha Misikiti
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mafundisho ya Quran 
Dhikiri maana yake nini? - 2

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Matatizo ya tumbo yanayosababishwa na utumiaji wa maziwa

Matangazo 
 

 

 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org  

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita