|
AN-NUUR
|
| 'Serikali
ieleze hatua iliyochukua kuhusu mauaji Mwembechai'
Na Kassim Juma BARAZA Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini limeitaka serikali iwafahamishe Waislamu na wananchi kwa ujumla hatua iliyokwishafikia hadi sasa kuhusiana na mauaji yaliyofanywa na polisi katika Msikiti wa Mwembechai. Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano wiki hii, Katibu Mkuu wa Baraza hilo Sheikh Abasi Kilima alisema kuwa Baraza limekuwa likipokea barua kutoka kwa Waislamu na wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini zinazolitaka kuhoji msimamo wa serikali juu ya mauaji ya Mwembechai. Sheikh Abasi Kilima alisema Baraza kwa niaba ya Waislamu linaitaka serikali ieleze msimamo . wake ili iondoe dhana na utata uliowakumba Watanzania hivi sasa. "Tunaitaka serikali itupatie jibu hili ili tuwaelimishe Waislamu na wananchi wanaoitakia mema nchi hii", alisema Sheikh Abasi. Aidha, akiongelea kuhusu kuundwa kwa Tume huru, Katibu huyo alionyesha mshangao kwa kuhoji ni kwa vipi serikali imeshindwa kuchukua hatua hiyo yapata miezi saba sasa, wakati yapo masuala mengine yanayofanana na hili ambayo yaliundiwa tume haraka. "Au kwa sababu waliouawa ni Waislamu, ili kuondoa dhana hii tunaiomba serikali ikamilishe hatua za 'Inquest' na pia ihakikishe inaunda tume hiyo", alisema Sheikh Abasi. Kutokuundwa kwa Tume hiyo, Baraza Kuu limedai kuwa kunaweza kujenga dhana na hisia mbaya dhidi ya serikali miongoni mwa wananchi haswa Waislamu kwamba huenda hawatendewi haki nchini mwao. "Waislamu na wananchi wengine wanaoitakia mema nchi hii ambao wameshiriki katika kuiweka madarakani serikali hii watajua hawatendewi haki", alisema Katibu huyo wa Baraza Kuu. Akijibu maswali ya waandishi waliotaka kujua ni muda gani ambao Baraza lake limeipa serikali kutekeleza hatua hiyo, Sheikh Abasi alisema kwa kuwa serikali inatambua, kuheshimu na kuendeleza misingi ya haki za binadamu angetarajia kutekelezwa haraka kwa hatua hiyo. Mwezi Februari mwaka huu, Jeshi la Polisi lilivamia Msikiti wa Mwembechai kuwasaka waliodaiwa kuendesha mihadhara ya kashfa. Katika uvamizi huo, polisi waliwapiga na kuwadhalilisha Waislamu ndani
ya Msikiti huo kitendo ambacho kilisababisha kuzuka kwa vurugu siku iliyofuata
ambayo ilipelekea watu kadhaa kuuliwa na wengine kujeruhiwa. Na Nooh Mustafa, Bukoba JUMUIYA ya vijana wa Kiislamu Bukoba imefungua matawi kadhaa mkoani humo na kuahidi kujenga shule na zahanati siku za usoni. Maeneo ambayo jumuiya hiyo imefungua matawi yake ni pamoja na Ruhoko, Nyakibimbiri, Kyange, Muleba na Kemondo. Pia jumuiya hiyo imeazimia kujenga zahanati katika kila kituo ili kuondolea wananchi wa maeneo hayo adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali. Mwandishi wa habari hizi alipotembelea maeneo ya vijijini na kuhojiana na wananchi wa sehemu hizo, baadhi yao walisema, wao wako tayari kutoa viwanja vyao kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Ibada (Misikiti), shule na zahanati. Hata hivyo, walisisitiza kuwa vituo hivyo vya maendeleo ya Waislamu visiwe chini ya viongozi ambao hawataki maendeleo ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla. Sambamba na hilo, uongozi wa vijana umewaomba Waislamu kote nchini kufika mkoani humo (Kagera) ili kushuhudia wenyewe juhudi zao pia kutoa mchango wao wa mawazo na kielimu. |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org