|
AN-NUUR
|
| S.L.P. 55105,
SIMU 181365, DSM
TAHARIRI Iran ina agenda gani? UPO usemi wa watoto wa "kijiweni" usemao kwamba kama ni kushangaa kashangae 'Feri', meli kuelea shilingi kuzama. Afghanistan ilikuwa ikipendwa na kupewa msaada na Marekani ikiwa ni pamoja na silaha kuisaidia kupambana na Urusi. Zama hizo suala la dhana ya Waafghan kuwa 'Mujahidina' haikuwa tatizo kwa Wamarekani. Leo Afghanistan ile ile haipendezi tena inashutumiwa eti kuwagandamiza wanawake kwa kuwalazimisha kuvaa Hijab utadhani wanawake wa Afghanistan wameanza kuvaa hijaab leo. Afghanistan si mwanachama wa Umoja wa Mataifa na kwa propaganda za Marekani na washirika wake mashirika yote yaliyokuwa yanatoa misaada kwa wenye matatizo ya chakula, ukosefu wa dawa na huduma nyingine za kijamii yamesitisha huduma zake. Lakushangaza nchi za Kiislamu nazo zimeisusa Afghanistan. Watu wengi wana njaa, watoto wana utapiamlo na madawa hakuna. Wanaoteseka ni ndugu zetu Waislamu na lau nchi za Waislamu zingetekeleza wajibu wao asingetokea yeyote kufa njaa au kukosa dawa Afghanistan. Lakini, lakushangaza zaidi ni kuona serikali inayojiita ya Kiislamu kuvizia kisingizio ikusanye jeshi mpakani huku ikifanya mazoezi na kusubiri kisingizio kingine iingize jeshi Afghanistan. Ni jambo lisiloingia akilini serikali inayojiita ya Kiislamu kujenga hoja kutaka Umoja wa Mataifa iichukulie hatua Afghanistan. Umoja wa Mataifa ambao uliiachia Marekani iisagesage Iraq. Umoja wa Mataifa ambao uliwaacha Waislamu wachinjwe huko Bosnia na leo hauchukui hatua yoyote madhubuti kuwahami Waislamu wanaouliwa na kuchomewa nyumba zao huko Kosovo. Umoja wa Mataifa ambao umeiachia Marekani ikaipiga Sudan na Afghanistan na ikashindwa japo kutoa kauli. Nani asiyejua kwamba Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama ni chombo ambacho Marekani hukitumia ipendavyo. Amerika imekipiga makombora kiwanda cha madawa cha nchi masikini kama Sudan bila hata idhini ya Baraza la Usalama. Na ni jambo lililo wazi kwamba Baraza la Usalama haliwezi kuingilia mgogoro kama ule wa Ireland. Lakini ikipatikana fursa au kisingizio chochote Marekani haitasita kuipiga Afghanistan kama ilivyofanya juzi tu. Nchi ya Kiislamu haiwezi kusimama leo 1998 katika Baraza la Umoja wa Mataifa kuzungumzia unaodaiwa ugaidi wa Afghanistan na kusahau kwamba leo ni miaka hamsini Wapalestina hawajala, kunywa wala kulala kwa amani kutokana na ugaidi wa Israeli. Nini Baraza hilo limefanya dhidi ya Israeli? Tunadhani kama ipo nchi ya Kiislamu yenye nguvu za kijeshi, uwezo wa kifedha n.k. ikawasaidie Waislamu wa Kosovo; Kashmir, Wapalestina, Burma na Chechnya kupambana na madhalimu. Iran sasa hivi ni Mwenyekiti wa nchi za Kiislamu (OIC) vipi ikatafute suluhisho la mgogoro wake na nchi nyingine ya Kiislamu kwa Marekani! Kwanini isiitishe kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa OIC! Au inataka Marekani iwapige Twalaban ili nayo iingie? Lakini kwa maslahi ya nani? Aibu tupu! Leo tunaambiwa Iran haina haja tena kutekeleza hukumu yake dhidi ya Sulman Rushdie. Wengi watashangaa kwa vile walidhani kwamba hukumu ile ilikuwa kwa ajili ya Uislamu na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Lakini kadri mambo yanavyozidi kujitokeza huenda Waislamu wasishangae tena. Lamuhimu tu ni kwamba kauli hizi haziwawakilishi Waislamu. Hata hivyo ni muhimu Waislamu ulimwenguni kote kuyasoma mabadiliko haya yanayotokea kwa kasi ya kutisha, kuyapa tafsiri sahihi, na kuchukua msimamo na hatua stahiki. |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org