|
AN-NUUR
|
| 'Musiwasingizie
wake zenu maovu'
Na Habiba Swedi, Arusha WANAUME wa Kiislamu wameonywa dhidi ya tabia ya kuwasingizia uovu wake zao, na badala yake wametakiwa kuwaamini, kuwapenda, kuwasaidia na kuwausia kheri ili wote mke na mume wapate radhi ya Mwenyezi Mungu. Onyo hilo limetolewa na Sheikh Swaleh bin Said wakati akitoa hotuba katika Swala ya Ijumaa hivi karibuni kwenye Msikiti wa Zawiyatul Qadiriya, Ngarenaro mjini hapa. Akitoa mifano mbalimbali ya maisha ya kila siku, ambapo mume hutoa idhini kwa mkewe kuhudhuria madrasa, kwenda kazini,harusini, sokoni na kwingineko, lakini alistaajabu kwa kusema kuwa mume humgeuka mkewe pindi anapochelewa kurudi nyumbani na kuanza kumsingizia maovu mkewe huyo. Alizidi kufahamisha kuwa, mume katika maisha ya ndoa ya Kiislamu ni budi awe makini kwa mkewe dhidi ya kila analotamka na kwamba azingatie mipaka ya sheria iliyowekwa na Allah ndani ya Qur'an na mafundisho ya Mtume (saw) ili kuwa na ndoa zenye furaha na amani. Sheikh Swaleh alisisitiza kwamba, mume kumsingizia mkewe uovu, ni kinyume kabisa na mafundisho ya Allah kwani huleta fitna katika ndoa na jamii ya Waislamu kwa ujumla na Mwenyezi Mungu amelikemea vikali ikiwa ni pamoja na kuliwekea adhabu ya kupigwa viboko kwa kila afanyaye hivyo. Akapambanua wazi kuwa, mke anayo sheria inayomlinda dhidi ya kusingiziwa huko endapo atashitaki katika vyombo vya dini. Akinukuu aya katika Qur'an Sheikh Swaleh alisema: "Na wale wanaowasingizia wake zao, na hawana ushahidi ila nafsi zao Mwenyezi Mungu anakunasihini msirudi nyuma kabisa kufanya haya, ikiwa ninyi ni Waislamu wa kweli". Kwa mafundisho ya Mtume, Sheikh Swaleh alitoa hadithi inayokataza Waislamu kushiriki mambo saba yanayoangamiza, mojawapo likiwa hilo la kuwasingizia wake maovu. Aliongeza kuwa mke amepewa heshima kubwa sana katika Uislamu, hivyo anastahili asitiriwe. Pamoja na hilo, Sheikh Swaleh alipinga vikali propaganda za baadhi ya watu kuwa Uislamu unamkandamiza mke na kumpa nguvu mume kumwonea, kumsingizia ama kumtukana namna atakavyo. Waislamu mbalimbali walitoa maoni yao juu ya hotuba hiyo, Bi. Sadia Swaleh wa Mji wa Kati Arusha alionyesha kuvutiwa sana na hotuba kwa kusema kuwa inaigusa jamii ya Kiislamu kwani hayo hutokea kila siku katika maisha ya ndoa kiasi cha kuwa chanzo cha migogoro mingi inayopelekea talaka. Naye Ustaadh Khamswaan wa Yam Investment alisema kuwa, inafurahisha na kutia moyo kuona kuwa viongozi wa dini wanakemea maovu yanayotendeka kila siku katika familia za Kiislamu.
Na Mwandishi Wetu, Songea JUMUIYA ya wanafunzi Waislamu wanaosoma katika sekondari na vyuo mbalimbali mkoani Ruvuma wamefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya watakaondesha shughuli za kidini katika jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka 1998 - 99. Jumuiya hiyo inaundwa na shule tano za sekondari na vyuo viwili katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma. Shule hizo ni Songea Boys na Songea Girls, shule nyingine ni pamoja na sekondari ya kutwa ya Ruvuma, sekondari ya Rukuwiko na sekondari ya Kiislamu ya Msamala. Aidha, jumuiya hiyo inaundwa pia na vyuo vya Ualimu Matogaro TTC na Chuo cha Waganga Wasaidizi wilayani Songea COTC. Uchaguzi huo ulifanyika katika chumba cha mikutano cha TTC siku ya Jumapili Septemba 9, mwaka huu. Waliochaguliwa kutoka Songea Boys ni Hamza Makila kuwa Mwenyekiti, Luhunilo alichaguliwa Makamu mwenyekiti. Kwa upande wa nafasi ya Ukatibu Juma Nchia kijana kutoka Songea Boys alichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji na Hamza Kondo kutoka Luhuniko alichaguliwa Katibu msaidizi. Nafasi ya Mweka hazina alichaguliwa Safia Hassan kutoka Songea Girls na msaidizi wake alichaguliwa Salima Ali kutoka Chuo cha Ualimu Matororo TTC. Wakitoa nasaha zao, viongozi waliokuwa wanastaafu waliwashukuru wanajumuia kwa ushirikiano wao. Wote pia walionyesha masikitiko yao kwa walimu walezi ambao wameitelekeza jumuia na kuwaacha wanafunzi kama watoto yatima. Viongozi hao waliyasema hayo kufuatia kutofika hata mwalimu mmoja katika kikao hicho muhimu. Kwa mujibu wa taarifa za viongozi wa matawi, walisema hawana taarifa zozote kuhusiana na walimu wao kutokufika. "Ni mwalimu mmoja tu mlezi wa Songea Boys ndiye aliyetoa taarifa kwamba ana dharura na hivyo ama atafika basi angechelewa kwa sababu zisizozuilika, hakuweza kufika kabisa", walieleza viongozi hao. Uongozi mpya uliwataka wanajumuia kuacha fikra potofu za kudhani lengo la harakati hizo za wanafunzi ni kupata vyeti na kula pilau pindi watakapohitimu. Waliwataka wanajumuia hao kujua kwamba matatizo ya Waislamu katika nchi hii yataisha tu endapo vijana ambao ndio taifa la leo wataujua vyema Uislamu wao na kuutekeleza ipasavyo. |
YALIYOMO
TAHARIRI Iran ina agenda gani? Mauaji,udhalilishaji Mwembechai: Wanawake
Waislamu waandamana Tabora Na Mwandishi Wetu 'Serikali ieleze hatua iliyochukua
kuhusu mauaji Mwembechai' ‘Musiwasingizie wake zenu maovu’
Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org