AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri

YAMEKUWEPO majaribio ya nguvu toka kwa viongozi wa Kanisa kuzuia Waislamu wasitumieBiblia katika mahubiri yao. Sababu wanayotoa ni kuwa, Biblia ni Kitabu cha Wakristo, hivyo wasikitumie. Kwa bahati mbaya sana shutuma hizo zinatolewa na Wanatheolojia waliosoma theolojia kwa kiwango cha juu. Hivyo wanajua kabisa wanachokifanya. Wameamua kuiswaga serikali na kuitumia kwa manufaa yao, kwa kuwa wanajua viongozi wa serikali hawana elimu ya dini. Katika makala hii, SHEIKH BERNARD P. NYANGASA anachambua Biblia ni kitu gani, inatumika na dini zipi, na mbinu zipi zilitumiwa na wahubiri maarufu wa

Biblia ni neno la Kigiriki lenye maana ya vitabu. Yaani ni mkusanyiko wa vitabu tofauti. Hii ina maana kuwa , hata ukikusanya vitabu vya Phisics, Chemistry, Biology, Mathematics n.k. ukivikusanya pamoja ni Biblia. Kidini, Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vya Agano la Kale, Injili na nyaraka za Mtume wa Yesu (as). 

Kitheolojia na Kiebrania Agano la Kale tunaliita "Tanaki", yaani `Torati" (Torati - Sheria), "Nebiin" (Manabii) na "Ketubhim" (maandiko). "Tanaki" ni kitabu kinachotumiwa na dini ya Kiyahudi (Judaism). "Tanaki" zipo za aina mbili, ipo ya Kiebrania (Hebrew text) iliyotumiwa na Wayahudi waliokuwepo ndani ya Jerusalem (na Wayahudi wa sasa) na ya tafsiri ya Kigiriki ambayo baadaye iliitwa "Septuaginta", yaani tafsiri ya watu sabini. Imeitwa hivyo kwa kuwa ilitafsiriwa ya watu sabini katika mji wa Alexandria (Misri) katika karne ya tatu kabla ya Kristo. "Septuaginta" ina vitabu vingi zaidi kuliko "Hebrew text".Aidha, baadhi ya vitabu vyake ni virefu na vina maneno yasiyokuwemo katika kitabu cha Kiebrania (angalia vitabu vya Esta na Daniel). Mtume Yesu (as), wafuasi wake na Wayahudi waliokuwa nje ya Jerusalem walitumia "Septuaginta". Hii Biblia tuliyoizoea (Union Vision) imefasiriwa toka "Tanaki" ya Kiebrania ambayo haikutumiwa na Yesu (as), wanafunzi wake wala Wakristo wa mwanzo. Baada ya kuona kwa ufupi maana ya Biblia, sasa tuangalie mbinu zilizotumiwa na wahubiri mashuhuri wa Kikristo.Baada ya viongozi wa Kiyahudi kumkataa Mtume Yesu (as), ilibidi aanzishe `Kanisa' lake (tazama Mathayo 16:18) neno Kanisa kilugha ni mkutano au mkusanyiko (assembly). Kidini lina maanisha jumuiya ya watu wenye itikadi moja (taz. Matendo 7:38). Kwa hiyo, Yesu (as) alimaanisha anaanzisha jumuiya yake (dhehebu) ya waliomwamini dhidi ya jumuiya za Mafarisayo na Masadukayo zilizokuwepo. Hivyo dini yao (wakati huo iliitwa ya Kiyahudi) ikawa na madhehebu matatu. Mafarisayo, Masadukayo (Taz. Matendo 23:6-8) na dhehebu jipya la Yesu (as) lililoitwa Wanazarayo (Taz. Mathayo 2:23, Matendo 24:1-5 na Matendo 28:16-22). 

Jina "Wakristo" mimi naona haya kusema lilikotoka. Nawaachia Wanatheolojia wenzangu waseme lilikotoka. Wanasema "11:26" Wakristo maana yake wafuasi wa Kristo. Hilo ni jina la kupanga walilotumia Wapagani wa Antiokia katika kuwaita wafuasi wa Yesu. Wapagani hao walilifahamu neno "Kristo" kama jina la ukoo (kibongo) tu, si kama jina la cheo kwa asili yake yaani mtiwa mafuta au Masiya" (Taz. Biblia Takatifu Tabora Uk. 1005). 

Wahubiri wa Mtume Yesu (as) walikuwa na kazi kubwa moja ya kuyavunja madhehebu ya Mafarisayo, Masadukayo na dini ya Kipagani. (Taz. Mathayo 28:19-20) na kuwaingiza katika dhehebu lao la Wanazarayo. Mbinu waliyotumia upande wa Wayahudi ni kuwafafanulia kitabu chao kitukufu wanachotumia (Tanaki) badala ya kutumia Injili waliyopewa na Yesu (as). Tuangalie mifarakano ya Apolo na Paulo:"Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso, naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana, na kwakuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu, naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi, hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamwelekeza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokueisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko (Tanaki) ya kuwa Yesu ni Kristo" (Matendo 18:24-28)."Wakisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi. Na Pale Paulo kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao maneno ya maandiko (Tanaki) Sabato tatu (wiki tatu mfululizo), akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu, na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo" (Matendo 17:1-3). "(Paulo) akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile njia mbele ya mkutano, basi akaondoka, akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani" (Matendo 19:8-10).Hapo tumeona kuwa mbinu waliyoitumia akina Paulo ni mahojiano (dialogue) kwa kutumia Tanaki na sio Injili. Na wamefanya hivyo kwa kuwa Wayahudi wanaiamini Tanaki lakini hawaiamini Injili. Hivyo ikawa rahisi kuwavuta baada ya kuwashinda kihoja.Viongozi wa madhehebu ya Mafarisayo na Masadukayo walichukia sana walipoona wananyang'anywa waumini na dhehebu la Yesu (as) (Wanazurayo) (Taz. Matendo 4:1-22). Hivyo wakawatisha, wakawatesa na kuwaua wahubiri wa Yesu (as) (Taz. Matendo 7:54-60).

Walipoona bado wanaendelea kunyang'anywa waumini, waliiomba serikali iwasaidie kuzuia mahubiri na mihadhara wakisingizia kuwa, Wanazirayo wanahatarisha amani na mshikamano. "Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza Liwali habari za Paulo. Naye alipoitwa , Tertulo akaanza kumshitaki akisema, kwa kuwa tunapata amani nyingi chini yako, Feliki Mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya ya taifa hili, basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhila zako. Kwa maana tumemwona huyo mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani (dola ya Rumi), tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo. Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi. Tukamkamata, tunataka kumhukumu kwa sheria yetu (kumuua- Taz. Matendo 21:27-36). Lakini Lisia Jemadari akafika, akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu (Taz. Matendo 23:23-30), akwaamuru wale waliomshitaki waje kwako. Wewe mwenyewe kwa kumuuliza - uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshtaki sisi. Wayahudi nao wakamshitaki wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo" (Matendo 24:1-9). 

Hata hivyo, japo serikali ilikuwa ya Kipagani, ilikataa kutumiwa na kujiingiza katika masuala ya dini. "Mfalme na Liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama, hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, mtu huyu (Paulo) hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa. Agripa akamwambia Festo, mtu huyo angeweza kufunguliwa kama asingalikata rufani kwa Kaisari" (Matendo 26:30-32).Mara nyingi Wayahudi walipopeleka umbea serikalini walifukuzwa. "Hata Galio alipokuwa Liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema, mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, kama lingekuwa jambo la dhulma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi, bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina ya sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu" (Matendo:12-16). 

Pamoja na chuki kubwa waliokuwa nayo viongozi wa Kiyahudi juu ya "Wakristo", viongozi hao hawakuwazuia kutumia Tanaki kitabu chao kitukufu. Hata Wakristo walipoamua kuunganisha Tanaki na Injili kuwa kitabu kimoja (Biblia), hawakulalamikia kitendo hicho wala kusema "hawa wanatumia kitabu chetu, kwanini wasitumie kitabu chao cha Injili? Wanakashifu dini yetu, wana mtukana nabii Musa, wanahatarisha amani, damu itamwagika! Serikali iwashughulikie".Kwa mujibu wa historia hii fupi ya dini katika utawala wa Kipagani wa Kirumi, tumeona kuwa, serikali ilizuia kabisa dini au kikundi kimoja kisinyanyase dini au vikundi vingine. Na pale kikundi kimoja kilipojaribu kutumia nguvu kudhuru kikundi kingine, iliingilia kati na kuokoa kikundi kinachoonewa (Taz. Matendo 21:27-36). 

Hata wahubiri wa Kikristo walipogusa itikadi ya viongozi wa serikali (masanamu), viongozi hao walijikaza sana wasihukumu kwa mapenzi ya itikadi zao. Katika tukio moja, watengeneza masanamu walizua fujo kubwa walipoona Paulo anawahubiria watu waache kuabudu masanamu, hivyo biashara yao ikazorota (Taz. Mdo. 19:23-34), lakini kiongozi wa serikali mwabudu masanamu akaingilia kati. "Na Karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni? Basi, kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, inawapasa kutulia, msifanye neno haraka haraka. Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana Mungu Mke Wetu. Basi ikiwa Demetrio na mafundi (watengeneza sanamu) walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako, na WASHITAKIANE" (Matendo 19:35-38).Inashangaza sana serikali hii ya "Wacha Mungu" na "ma-min kum" wa Mkaalie inamwasi Mwenyezi Mungu kuliko wapagani wa Kirumi.Aidha, tunashangaa sana kuona viongozi wa Kanisa waliokandamizwa na Wayahudi wamekuwa wakandamizaji kuliko Wayahudi "waliomuua" Mtume Yesu (as). Wamefika kukataza watu (Waislamu) wasitumie kitabu ambacho si chao (Tanaki), wakati "wenye" kitabu (Judaism) wamenyamaza. Kukandamiza kutamu, kukandamizwa kuchungu. Nawapongeza kwa kuweza kuiswaga serikali ya Wakristo na Waislamu mpendavyo. Wenzenu (Wayahudi) walishindwa kuiswaga serikali ya Wapagani waabudu masanamu. 

Mwisho naishauri serikali yetu iige mfano wa serikali ya Kipagani na kikafiri ya Kirumi ambayo ilikuwa adilifu sana na haikuthubutu kabisa kuingilia mambo ya dini. Serikali isiwachagulie watu dini au kikundi (dhehebu, jumuiya n.k.) cha kufuata. Wahubiri wa dini zote na vikundi vyote viachwe huru kuhubiri itikadi zao ili wananchi wachague wenyewe kuingia katika dini au kikundi wanachokitaka. Serikali haina haki ya kumzuia mhubiri yeyote hata awe wa shetani. Kwanza ni kitu cha kushangaza wakati serikali inakataa kusajili dini ya shetani, ndiyo hiyo hiyo inayotoa viwanja na leseni kwa Misikiti ya shetani (mabaa, madanguro au makasino, kumbi za dansi, taarabu, disko).

Aidha, viongozi hao hao ndio wanofungua rasmi Misikiti hiyo. Na si ajabu kiongozi akafungua danguro (cassino) akiwa na kibox cha kondom katika mfuko wa koti ili akimaliza kufungua jengo, akafungue pia ibada katika chumba namba moja.Nao viongozi wa Kanisa nawashauri wavumilie tu wakiona wafuasi wao wanawakimbia. Ingawa najua maslahi yao ya kidunia (mishahara, majumba, magari n.k.) yako hataraini, kwani wanaokimbia wanaon doka na pesa (sadaka) na misaada yao wanaipeleka wanakohamia. Hivyo wanapunguza mapato na nguvu ya Kanisa.Cha kufanya sio kuwazuia kwa nguvu watu wasikimbie au kuwazuia wahubiri wa dini zinazohamiwa. Mbinu inayotumiwa na wahubiri wa Kiislamu kutumia vitabu vya nyuma (vya zamani) na mahojiano, ndio hiyo hiyo iliyotumiwa na Wakristo kutoa watu katika dini ya Kiyahudi. Kuwaingiza katika Ukristo. Wakristo walitumia Tanaki kuwavuta Wayahudi kwani Wayahudi wanaimani lakini hawaiamini Injili. Nasi Waislamu tunatumia Biblia ili kuwavuta Wakristo kwa kuwa Wakristo wanaiamini lakini hawaiamini Qur'an. Kama Wakristo wataweza kutumia Qur'an kubatizia Waislamu, wanaruhusiwa kuitumia. Mhubiri wa dini anatakiwa atumie mbinu zote anazoona zinawasaidia kupata waumini kwa wingi, basi mhubiri avitumie, badala ya kutumia ustaarabu unaofukuza waumini. 

 
 

YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita