AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais

KATIKA kupaza kilio cha Waislamu juu ya dhulma inayoendeshwa nchini hapa, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu lilimuandikia Mh. Rais kumfahamisha rasmi juu ya malalamiko hayo ya Waislamu. Ifuatayo ni sehemu ya Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais. 

Azma ya kuzuia mihadhara ya Waislamu na vifo vya Waislamu katika Msikiti wa Mwembechai 

IBARA ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko wazi juu ya uhuru wa kuabudu na kueneza dini.Wakristo wanaijua vizuri Ibara hii, ndio maana licha ya kuhubiri neno la Bwana mpaka ndani ya nyumba zetu, wameandika vitabu 16 vya uzani wa kitabu "Wana wa Ibrahimu" kushadidia imani yao.Tunachoomba katika kadhia ya mihadhara ni: 

Maana sahihi ya neno "kashfa" ipatikane katika mintarafu ya dini.Wanaokashifiwa wajitokeze na kuonyesha wazi kauli zilizowakashifu na waliokashifiwa. 

Kuwa na utaratibu wa kisheria na wa uwazi kuwafikisha mahakamani wale wanaokashifu dini za wenzao.

Kauli za viongozi wa serikali zizingatie Katiba ya nchi na utawala wa sheria badala ya kauli za ubabe wa Dola.

Kamata kamata ya wahadhiri wa Kiislamu iliyopangwa kwenye vikao maalum bila ya makosa halisi iachwe haraka iwezekanavyo.

Katika msiba wa vifo vya Waislamu wa Mwembechai, kuna orodha ndefu ya makosa ya kukiukwa kwa Katiba na sheria za nchi. Kwa mizani hiyo Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania linakuomba kuitisha Tume ya Uchunguzi kuhusiana na vifo hivyo na chanzo cha fujo kilichosababisha vifo kutokea. Tume hiyo iwe na uzito inaostahiki kwa kuwakilishwa kikalimifu na wajumbe kutoka Baraza Kuu chombo kinachoomba Tume hiyo iundwe.

Kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi na kutekeleza kazi yake ipasavyo, ndiyo njia pekee ya kisheria na ya kistaarabu ya kurudisha mshikamano wa kidugu wa Watanzania na kuondoa imani inayojengeka kwa haraka sana kuwa Waislamu ni raia wa daraja la pili katika nchi hii.

Kuna umuhimu katika risala hii kutaja kwa uwazi madhila mengine ya Waislamu. Tunafahamu kuwa kulikuwepo uwiano mbaya wa nafasi za madaraka serikalini mara baada ya uhuru dhidi ya Waislamu. Sababu zake zinaelezeka. Lakini nafasi hizo za madaraka zimetumiwa vibaya katika kuendeleza na kusimamia maslahi ya dini na watu maalum na kuwabana Waislamu na Uislamu katika nyanja za elimu na ajira. 

Fursa ya kujiendeleza kielimu 

Katiba inatoa nafasi sawa kwa wote raia wa nchi hii kujiendeleza kielimu. Ibara ya 11 ya Katiba inahusika. Lakini kuna vikwazo vya elimu ambavyo Waislamu tunakuomba wewe binafsi kuchukua azma ya kuvirekebisha Mheshimiwa Rais, umekuwamo katika serikali za awamu zote tatu kama Waziri. Sasa wewe ni Rais wa nchi hii, na ni rahisi kwako kurekebisha mfumo wa kuendesha elimu kwa manufaa ya Taifa kwa kipimo cha uzoefu ulioukusanya.

Baraza la Mitihani lina uwiano mbaya wa uwakilishi dhidi ya Waislamu. Taratibu za kuendesha mitihani, kusahihisha na kutoa majibu zifanywe kwa wazi na ziondoshe upendeleo kufuatana na majina ya watahiniwa.

Idara ya Elimu ya Juu na Mabaraza ya uteuzi wa wanafunzi wapya wa vyuo vya elimu ya juu nchini yote yana wawakilishi wachache Waislamu. Hizi ni sehemu muhimu ambazo Waislamu wanaweza kubaguliwa kinyume cha Katiba inavyoelekeza. Uwazi wa kuendesha Wizara ya Elimu ya Juu na uteuzi wa wanafunzi huenda ukapunguza ubaguzi.

Elimu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi, hatutakwenda mbele kama taifa ikiwa sehemu kubwa ya wananchi wataachwa bila elimu. 

Uwiano mbaya katika vyombo vya utoaji maamuzi ya kitaifa 

Tunajua umuhimu wa vyombo tulivyoachwa nje na athari zake kwetu. Risala hii itapoteza mizani iliyokusudiwa tukiainisha hasara zote tunazozipata kwa kufanywa duni au hatupo. Kwa sasa tutaorodhesha tu Tume tuliyoachwa nje na kukuachia wewe utafakari hali hii ya kibaguzi.
Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma
Tume ya Uchaguzi
Tume ya Kurekebisha Sheria
Tume ya Kurekebisha Katiba (Nyalali)
Tume ya Jiji - Dar es Salaam
Tume ya Serikali za Mitaa
Wizara, Idara, Mikoa, Wilaya na Mashirika ya Umma vina uwiano mbaya sana dhidi ya Waislamu. Kama vile haitoshi, hivi karibuni katika awamu ya tatu, uteuzi wa "Regional Administrative Secretaries" umefuata mtindo ule ule wa kibaguzi. 

Hali hii ya uwiano mbaya inasababisha upendeleo maalum kwa Wakristo na ukandamizaji kwa Waislamu. Tunayo haki kama raia wa nchi hii kukuomba uizuie hali hii kuendelea. 

Sheria za Kiislamu za Mirathi 

Serikali iko makini kufuta, kubadilisha au kurekebisha sheria ya Mirathi ya Waislamu. Juhudi zilianza kuonekana wazi mwaka 1963 katika mkutano wa Luther House. Juhudi hizo zinaendelea hadi sasa katika mbinu mbalimbali siri na dhahiri. 

Kwa Waislamu, Sheria Mama inayotawala maisha yao ni Qur'an. Wasia wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu kuhusu mirathi umo ndani ya Suratul-Nisaa. Vipi kuwa na uhuru wa kuabudu katika Katiba na wakati huo huo misingi muhimu ya ibada ifutwe kinyemela? Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu Tanzania linatoa kauli ya Waislamu kwako kuwa: 

Waislamu hawataki Sheria zao zichafuliwe wala kuchezewa.Kama kutunga sheria mpya basi zitungwe kwa watu wa dini nyingine wasiokuwa na Sheria ya Mirathi.Waislamu watapinga kwa nguvu zao zote jaribio lolote la Bunge la kupitisha muswada wa kubadilisha Sheria ya Mirathi ya Kiislamu. 

Tunamaliza kwa kutoa tahadhari kwa Bakwata isilazimishwe kwa Waislamu kwa mabavu ya Dola. Waislamu wanafahamu jinsi Bakwata ilivyoundwa. Katiba iko wazi juu ya hiari na uhuru wa kujiunga na kundi, shirika au vyama vya kidini. Iko wazi juu ya shughuli za kuendesha dini kwa kuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi. Serikali kujiingiza katika kuendesha Bakwata kutasababisha vikundi vya kidini kutafuta ufumbuzi wa kisiasa wa kuondoa dosari hiyo ya Kikatiba. 

 
 

YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita