AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Maoni yetu

Vipi watu wafurahie mateso ya wengine? 

Awali ya yote tungependa kuuliza ni kitu gani hasa Serikali inanufaika iwe ni kisiasa au usalama wa nchi kwa Chuki Athumani kuteseka hospitalini akiwa kapooza miguu huku akiwa bado kafungwa pingu.

Manufaa gani hasa serikali inapata kwa Chuki kuota vidonda kwa vile kafungwa pingu na hana mtu wa kumsaidia kumgeuza na kumbadili nguo mara kwa mara kama hali yake inavyohitaji!

  • Manufaa gani hasa Serikali inapata kwa Chuki kuendelea kukosa matibabu stahiki, zaidi ya kujenga hisia kwamba kuna watu wanafurahi Mwislamu akiteseka.

  • Usalama gani wa nchi hii mtoto huyu wa umri wa miaka 17, anahatarisha hata afungwe pingu pamoja na kupooza kwake kutokana na risasi alizopigwa na polisi wa Serikali!

  •  
  • Usalama gani wa Serikali hii anauhatarisha! Kwamba mtoto huyo wa miaka 17 kaoneka hatari sana anatengeneza pengine mabomu ya kuua au kupindua serikali! 

  • Hata kama ni jambazi lililoua, si anatibiwa kwanza akipona ndio umshitaki! Hata kama mwisho wake itakuwa kuhukumiwa kunyongwa! Huu ndio utaratibu duniani kote.

  • Tunaamini uhai na umauti upo katika milki ya Mwenyezi Mungu. Kila mtu ana siku yake ya kuzaliwa na siku ya kufa. Lakini mwanadamu hubeba lawama anapokiuka hulka na busara katika maamuzi na matendo yake.

  • Huyu mtoto kwanza kapigwa risasi ya kifuani (kwa kosa lipi?). Pili anakosa matibabu yanayostahiki na kafungwa pingu. Tatu anakosa huduma na uangalizi wa karibu katika hali yake hii ya kupooza mpaka anaota vidonda. Inachokikusudia hasa Serikali kwa mtoto huyu nini? Mwenyezi Mungu akichukua roho yake, kwanini Waislamu wasidhanie kwamba hilo ndilo mlilokuwa mkitaka litokee!

  • Katika suala la "Parole" Mheshimiwa Rais ametufariji kwamba yupo pale kwa maslahi ya nchi hii. Na kwamba uadilifu na haki itazingatiwa bila kujali dini ya mtu.Kwa moyo huo haya yanayomkuta mtoto Chuki hatudhani ni agizo la Mhe. Rais Benjamin William Mkapa au hata kama anajua.Kama Mhe. Rais Mkapa ameliona hili la "Parole" likamgusa hatuoni ni vipi, aagize askari wamtie pingu mtoto aliyepooza akose kutibiwa; akose; huduma na kuota madonda kwa kulalia mikojo na hata kupewa chakula iwe taabu!Yawezekana wapo watu ndani ya Serikali ambao pengine kwa chuki zao wanayafurahia haya. Lakini tunaamini pia kwamba wapo watu wanaiona hatari iliyopo mbele yetu! Mwenyezi Mungu atunusuru. Na kwa kuhofia hilo na jukumu letu la kuinusuru nchi yetu inabidi tuyaseme haya. Watu wasiangalie "furaha" ya nafsi zao kuona wenzao wakiteseka wakatuangamiza sote.Yapo mambo mengi yanayoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi, lakini hili linaloleta picha kwamba wapo watu wanafurahi kuona Muislamu akiteseka ni la hatari zaidi.

  • Pingu hufungwa mtu na nguvu zake na anayeweza akaleta vurugu akatoroka. Huyu mtoto mgonjwa, kapooza mwenyewe hajiwezi maskini kiasi anatoka vidonda kwa kushindwa kujigeuza, kama si chuki na ukatili tu wa baadhi ya viongozi, pingu anafungwa za nini! Na je inadhaniwa hili ndugu zake Waislamu hawalioni! Na je inadhaniwa watalikubali tu na kutokujiuliza kwanini?!

  • Wakristo na Waislamu wanaishi kwa pamoja mitaani kwa udugu wakisaidiana kwa furaha na shida. Wanasaidiana na kushirikiana kufukuza wezi na vibaka ambao wamekuwa kero mitaani. Hawa tupo nao bega kwa bega tunakula nao magengeni na kwa Mama Ntilie. Nao wanateswa na hali hii. Wana wasiwasi kesho hali itakuwaje. Ndio maana tunashindwa kuelewa hao wanaohisi kunufaika kwa namna yoyote na kuteswa kwa Chuki Abdallah wana agenda gani! Wapi wamekusudia kuizamisha nchi hii.

  • Chuki Athumani (17) anateseka; yupo mikononi mwa Serikali toka Februari 13, 1998. Ndugu zake Waislamu na Watanzania wenzake wenye upendo, huruma na uungwana ambao wangeweza kumsaidia kwa gharama yoyote na mahali popote ndani na nje ya nchi wamezuiwa japo kumjulia hali.

  •  
 
YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita