AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu

  • Wanaume Waislamu wasibweteke
  • Nchi kuwa huru imekuwa balaa kwao
Na Mwandishi Wetu 

Wanawake Waislamu waliokutana jijini Dar es Salaam hivi karibuni wamemuomba Mh. Rais Benjamin William Mkapa awawajibishe wale wote waliowaua au kuhusika na mauaji ya Waislamu na kuwadhalilisha wanawake Waislamu. 

Wakizungumza kwa uchungu katika mkutano wao, wanawake hao walihoji inakuwaje Waislamu wauliwe bila Serikali kujali? 

Aidha wanawake hao ambao walikutana katika Msikiti wa Sinza walielezea kwa uchungu na masikitiko makubwa jinsi ambavyo wenzao waliokamatwa katika msikiti wa Mwembechai walivyodhalilishwa wakiwa rumande.

Ilielezwa kwamba wanawake hao walikuwa wakivuliwa nguo na askari wanaume wakidai kuwa wanawapekua wasije wakawa wameficha mabomu katika tupu zao.Akizungumzia udhalilishwaji huo Katibu wa mkutano huo Bi Fatma Juma alihoji ni "bomu gani linaingia katika utupu wa mwanamke"? Akawataka akina mama wote nchini kila mmoja wao ajifikirie kama ni yeye angelazwa chali uchi kukaguliwa utupu wake angejihisi vipi! 

Bibi mwingine toka Kisarawe akizungumza kwa uchungu alieza jinsi wazee na akina mama wa mkoa wa Pwani na Waislamu wote kwa ujumla walivyopata taabu katika kuleta Uhuru. 

"Yaani sisi tumeomba Uhuru wa kuja kuteseka! Babu zetu walipata taabu sana kuomba Uhuru huu wengine walisoma Misahafu (Dua, Qur-an) kwa ajili ya Uhuru huu. Leo Uhuru umekuwa balaa kwetu.... tunavuliwa nguo hadharani. Serikali gani ya kuwavua nguo wanawake wa Kiislamu ..... Jamani Yaa Rabbil Alamina". Alilalama mama ........... huku akitoa machozi.

Ni kutokana na manyanyaso na udhalilishwaji huo wanawake wasiopungua elfu moja wakiwepo wawakilishi kutoka takribani mikoa yote, walimwomba Mh. Rais awawajibishe wote wale ambao wamehusika na "kashfa" hii kwa njia moja au nyingine, wamewataja watu hao kwamba ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Ali Ameir; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Yusuf Makamba, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Alfred Gewe na Kamishna wa Magereza.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya akina mama; Mama Fatma Lazaro alieleza kwamba sababu iliyochochea Mayahudi wa Banu Qainuka, kuzingirwa na kisha kufukuzwa Madina wakati wa Mtume (s.a.w); ni kudhalilishwa kwa mwanamke wa Kiislamu.

Mwanamke huyo alivuliwa hijab yake na Myahudi tena si kwa kumuacha uchi. Muislamu aliyekuwa karibu hakuvumilia unyanyasaji ule. Akamuua yule Myahudi. Mayahudi nao wakamuua yule Muislamu. Badala ya Mayahudi kukiri kosa lao, wakatakabari Waislamu wakajiandaa kwa vita wakawazingira; Banu Qainuka wakakimbia.

Bi Fatma anasema tukio hilo limerudiwa kwa wanawake wa Tanzania tena si kwa kiwango cha kuvuliwa gauni la juu bali kuachwa uchi kabisa.La kusikitisha anasema Bi Fatma, wanaume Waislamu hawaonyeshi kuguswa na suala hili.

"Tunawauliza wanaume ni vipi wanabweteka wanatembea barabarani wanavaa kanzu nzuri za darzi na kujitia manukato mazuri kwenda msikitini wakati wanawake wa Kiislamu wanadhalilishwa namna hii!" Alihoji Mama Fatma na kuongeza kwamba wanaume wana maswali ya kujibu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mjumbe kutoka Ruvuma baada ya kutoa salamu kwa uchungu aliokuwa nao aliishia kulia akaomba dua na kukaa.Mjumbe kutoka Mzenga Bi Kidawa Mwinyimvua asiyepungua umri wa miaka 70 alizungumza kwa masikitiko huku akitetemeka kwa uchungu na akawambia Waislamu kuomba dua na kuzidisha umoja na mshikamano.

Katika jumla ya nasaha zilizotolewa ni za mama mmoja ambaye alitoa wito kwa wanawake wote wajitoe muhanga kama alivyojitoa Bi Sumaiya, Zainab Ghazal na wengineo. Mama huyo ambaye mwandishi wa habari hizi hakubahatika kulipata jina lake aliwaambia akina mama kwamba kama wakiogopa kufa kwa ajili ya Uislamu wajeue waweza kuzolewa na gharika kama zile za Mererani,  Air Msae, No Challenge, Mafuriko n.k. Gharika hizo amesema hazichagui huyu ni wa Mwembechai au wapi.

Aidha alisisitiza kwamba yaliyowapata Waislamu wa Mwembechai ni ya Waislamu wote kwani Uislamu hauna mipaka ya kijiografia na kwamba Waislamu wote ni ndugu.Mikoa iliyowakilishwa katika mkutano huo ni Kigoma, Kagera, Ruvuma, Iringa, na Mbeya. Mingine ni Mtwara, Pwani, Arusha, Singida, Morogoro na Kilimanjaro. 
 

 
 

YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita