AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Tahariri  

Sasa tutafika 

Kumbe Rais anasikia  
 

  • KWA kipindi kirefu umekuwepo mdahalo " wa viziwi" kati ya Waislamu na Serikali. Waislamu wanatoa malalamiko na madai yao kwa serikali kwamba hawatendewi haki, lakini serikali ama inakaa kimya au inaibuka na shutuma dhidi ya Waislamu na kuepuka kabisa kusema lolote juu ya madai yao. Hata pale ambapo serikali imelazimika kutoa ufafanuzi, basi ufafanuzi wenyewe umekuwa ama kuwadhania Waislamu wajinga, wasioelewa kitu au wasioona na kufikiria yanayotokea nchini hapa.Waislamu wameuliwa pale Mwembechai, wengine kujeruhiwa kwa risasi na wanawake kudhalilishwa. Waislamu wadai iundwe Tume huru kuchunguza kadhia hii; Mh. Ali Ameir anasema kwamba, "serikali haifanyi kazi kwa shinikizo".Kumbe shinikizo kwa Waislamu tu? Lile la Paroko je? Lilikuwa agizo!Waislamu wanasema kwa kusema Yesu si Mungu, hawatukani wala hawamkashifu mtu, kwani ndivyo kitabu chao kinavyosema, serikali inasema "mnakashifu". Inawakamata Waislamu, inawaweka ndani na kuwanyima dhamana. Inadai inawanyima dhamana kwa usalama wao. Kwamba wamekashifu sana na watu huko nje wamekasirika, watawadhuru.Lakini wenye dini yao wamejitokeza wamesema waziwazi kwamba Mkristo kusema Yesu ni Mungu si kashfa na Muislamu kusema Yesu si Mungu si kashfa vilevile.Hilo amelitamka mpaka Muadhama Kadinali Pengo. Tafsiri yake wanasema kwamba kama serikali inataka kuwapiga risasi Waislamu, iwapige tu, kama inataka kuwanyima dhamana iwanyime tu na kama inataka kuwanyima matibabu huko jela wafe mmoja mmoja iwanyime tu. Lakini isiwasingizie Wakristo. Wao hawana mashitaka dhidi ya Waislamu.Kasimama Mbunge, tena Mbunge mzito asiyehitaji sifa wala umaarufu. Aliyoyafanya toka kupigania uhuru hadi leo yashatosha kumpa huo umaarufu. Huyo ameishauri na kuitahadharisha serikali yake kwamba kuna dhulma hapa. Watu wanasingiziwa kosa la kashfa, watu wamenyimwa dhamana, watu wananyimwa matibabu, watu wanatishwa kwa sababu ya kusaidia shughuli za taasisi halali.Hoja hazijibiwi. Anasimama Naibu Waziri anazungumza yake. Waziri naye anaibuka na yake. Kana kwamba hawakuzielewa hoja na madai yaliyotolewa.
  • Mpaka leo wananchi hawaelewi kauli na msimamo wa serikali ni upi. Ni ule wa Sigela Nswima, Waziri Ali Ameir au ule wa msemaji mkuu wa Baraza moja mashuhuri nchini!Ndani ya mkanganyiko huo likaja hili la "Parole". Likaundwa na kutangazwa katika sura ambayo inapeleka salamu kwa Waislamu "Mtakoma tunafanya hivi mtafanya nini". Baraza Kuu likahoji, vyombo vingi vya habari vikaona upogo na dosari ile na kuisemea mpaka kwenye tahariri zao. Kwamba jamani hii sasa mmezidi!Mheshimiwa Ali Ameir kaibuka tena kuwajibu (anaowadhania hawaoni wala hawaelewi) Waislamu, kwamba Baraza lile kuwa la Wakristo watupu pamoja na Maakofu wao, sio geni. Wao serikali watu safi, hawaangalii dini! Lakini kwa bahati njema kaja Rais, katuondolewa kukanganyikiwa. Kwanza sasa tumejua msimamo wa serikali utaelezwa na nani. Na zaidi imetuonyesha kwamba kilio cha Waislamu kinasikilizwa.Katika kauli yake Mh. Ameir alisema "sisi " hatuangalii dini "sisi" ile ilimaanisha ama CCM au Serikali. Lakini tunashukuru kwa kauli na hatua alizochukua Rais "sisi" ile sio ya serikali: Labda sasa wakati Waislamu wanampongeza Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa, Bw. Ali Ameir atueleze "sisi" ile yeye na nani?Pamoja na kumpongeza Mh. Rais, tungependa pia kuyataja magazeti ya Rai na Mtanzania ambayo kwa misingi tu ya uzalendo wamesimama na kupinga dhulma ile kwa kuizungumza kwa uzito wake katika tahariri zao.Kwa mwendo huu, tunaamini kwamba tutafika. Kwamba kumbe Rais wa nchi anasikia kilio cha wananchi, na barua anazisoma kama ile ya gazetini. Hii inatupa imani kwamba hata zile za AN-NUUR ujumbe wake unafika kwa Mh. Rais. Lakini Mheshimiwa Rais, Parole haina maana kama tunakuwa na wahalifu na wahalifu wakabaki nje na wasio wahalifu wakabaki ndani. Hawa hawahitaji Parole.
  • Kuna watu wameua pale Mwembechai wapo nje wanakunywa bia zao. Sana sana pengine waweza kutolewa Dar es Salaam wakapelekwa Moshi, Musoma au pengine popote kufichwa. Wapo na wale waliompiga Chuki Athumani risasi na wakamkosesha matibabu stahiki kwa kumfunga pingu. Wapo na wale waliowarusha wanawake kichura wakiwa uchi.Anayehitaji Parole nani. Huyu muuaji au yule aliyekoswakoswa na risasi akawekwa jela! anayehitaji Parole nani, huyu muuaji au Chuki aliyepigwa risasi akipita njia! Anayehitaji Parole nani, huyu muuaji au waliojeruhiwa kwa risasi na marungu na wakanyimwa dhamana na dawa huko Segerea mpaka wengine wakafa! Parole haipo hapa.Nani anayehitaji Parole ,aliyemuweka mtu ndani na kumnyima dawa kwa vile kasaidia taasisi halali iliyosajiliwa na serikali au huyu aliyemfunga mtu bila ya kosa!Anayehitaji Parole nani, huyu aliyewaweka watu ndani akawanyima dhamana na matibabu kwa kusema kwao Yesu si Mungu au huyu anayewekwa ndani kinyume cha Katiba na sheria.Ili Parole ifanye kazi ni lazima kwanza mhalifu awepo. Pili ahukumiwe, afungwe. Na tatu ajirekebishe. Huyu mhalifu anayeua atajirekebishaje wakati hafikishwi mahakamani. Aliyedhulumiwa ajirekebishe awe nani? Ajirekebishe wakati toka mwanzo sio mhalifu! Zaidi atajenga chuki na hasira dhidi ya wale waliomdhulumu.
  • Parole imevunjwa, lakini tuangalie wakati wa kuundwa kwake upya. Kuna watu wa NGOs na Mabaraza ya Kidini hao hawasiti kusimama na kutoa msimamo wa serikali, wakati wao si serikali. Hao hawawezi kuwa na sifa za ujumbe wa Parole. Tunamshukuru Mh. Rais kwa hatua hii, lakini Parole imekuja jana. Yapo yaliyotangulia.

  • Tusingependa tuyarejee malalamiko yote ya Waislamu wa nchi hii. Lakini historia imerikodi kilio chao kupunjwa elimu.Waliopata bahati kusoma kazi hawapati, wanaopata kazi, cheo hapati na anayepata cheo fitna humwandama. Kosa lake aanze kuswali au avae kofia atajizolea kejeli za `siasa kali', Mujahidina', n.k.Lakini yule anayetundika msalaba shingoni, picha au sanamu ya Yesu ofisini na Biblia juu ya meza ya ofisi, huyu husifiwa. Kaokoka, mtu wa Mungu!Haya ya kupakaziana ndiyo yaliyotuletea hili Parole lisilo na mwelekeo. Ndio maana wengi walihoji, vipi Jumanne Mangara asifae? 
     
 
 
YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita