AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Bakwata ithamini juhudi za wengine

HIVI karibuni kumetokea tukio la kujiamini sana kwa BAKWATA. Inaelekea kwa kuwa BAKWATA ilianzishwa hapa Iringa mwaka 1968 yaani miaka thelathini (30) iliyopita, basi bila shaka viongozi wa BAKWATA mkoani wanafahamu vizuri zaidi sio tu sababu na madhumuni ya kuundwa kwa BAKWATA bali pia kazi muhimu za Baraza hili.

Mara kadhaa na kwa miaka kadhaa tangu kuanzishwa kwa BAKWATA Waislamu wenye kuelewa mambo na wenye nia ya kuona maendeleo ya dini yao walilikataa Baraza hili kwa kufahamu kuwa kuundwa kwa BAKWATA lengo lake ni kudumaza maendeleo ya Uislamu na Waislamu nchini.Kila aliyejaribu kuingia BAKWATA kwa lengo la kutaka kurekebisha mambo na kufanya yale yanayotakiwa na Uislamu aliondolewa. 

Kwa miaka yote 30 mpaka leo BAKWATA haijafanya lolote la maslahi kwa Waislamu. Hata hivyo hija wanayoisimamia ufanisi wake umekuwa duni kiasi kwamba waumini wengi sasa wanakwenda Hija kwa kupitia Kamati ya Hija iliyo nje ya BAKWATA na ufanisi wake ni wa hali ya juu.Kwa kuelewa malengo na shabaha za BAKWATA viongozi wa ngazi zote mkoa na wilaya hapa Iringa walimwita kwenye kikao Sheikh mmoja (jina tunalihifadhi) kwa ajili ya kumhoji juu ya juhudi nyingi anazozifanya za kuendesha na kusimamia mambo ya Kiislamu. Sheikh huyo ni mtendaji wa taasisi moja halali kwa maana ya kupata usajili wa Serikali. Taasisi ina katiba yake na ndani ya katiba hiyo yako malengo ya kuundwa kwa taasisi hiyo. Mambo yote yanayofanywa na taasisi hii ni kwa mujibu wa katiba yake. Yaani haijafanya lolote kinyume cha katiba.

Kwa namna ya utendaji mzuri wa taasisi katika mambo ya ujenzi na kusimamia misikiti, uendeshaji wa taaluma mjini na vijijini, misaada ya futari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na mengine mengi, Waislamu wa mkoa huu wamevutiwa na uadilifu huu kiasi cha kwa hiari yao, kujiombea wawe chini ya uongozi wa taasisi hii. Kwa maana hii kumejitokeza bahati ya taasisi kujipanua kinyume cha matumaini yake.

Tulidhani hii ingekuwa ni faraja kwa BAKWATA mkoani kwamba kazi iliyodhaminiwa na Waislamu kuwa ingefanywa na BAKWATA sasa kumepatikana chombo kingine cha kuisaidia BAKWATA. Tungetaraji viongozi wa BAKWATA mkoani na wilayani wangeshirikiana vyema na taasisi hii. Lakini wamediriki kumwita Sheikh na kumuuliza maswali ya jeuri kama baadhi ya maswali hayo yanavyoonyesha. Maswali yenyewe yalikuwa hivi:
 

  • Taasisi hii mipaka yake ni ipi?
  • Tumeona baadhi ya taasisi na misikiti inajinasibisha na taasisi hii, ruhusa hiyo imetoka wapi?
  • Tunaona unajenga chuo ruhusa ametoa kwa nani?- Taasisi inachukua vijana vijijini na kuwaweka chuoni kupata mafunzo ya dini idhini ya kufanya hivyo imetoka wapi mbona BAKWATA mkoani haijui?
  • Umefanyika uchaguzi wa maimamu katika misikiti yenu bila BAKWATA kuambiwa kwa nini?

Haya ni machache kati ya maswali mengi aliyoulizwa Sheikh huyo. Hatukusudii kutoa majibu yaliyotolewa na Sheikh huyo itoshe tu kusema kwamba, kwa ufupi Sheikh alisema yeye si mwenye taasisi hiyo kwa hiyo maswali yao au wayatume kwa maandishi kwa wahusika Wadhamini).

BAKWATA inajisahau kuwa wao wamesajiliwa na Serikali hii hii ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia vyombo vyake halali vilivyopewa jukumu la kusajili taasisi kama hizi. BAKWATA kama Ansar Sunnah, Markaz Tabligh, Shadhily Baraza Kuu n.k. ni chombo chenye hadhi sawa na vyote hivyo. 

Tunachokusudia kusema hapa ni kwamba si viongozi wa BAKWATA wilayani au mkoani Iringa, wala si viongozi wa BAKWATA kwenyengazi ya taifa wenye haki ya kuiuliza taasisi yoyote iliyosajiliwa kihalali na mamlaka za nchi juu ya utendaji wake au kutotenda kabisa. Hiyo ni haki ya hizo mamlaka. Kama BAKWATA ina taasisi zake zilizo chini yake kama vile shule ya Kinondoni waziulize hizo. 

Tunawaomba viongozi wa BAKWATA, KAMA WAO WAMESHINDWA KUWAFANYIA MAZURI Waislamu angalau wawapongeze hao wanaofanya hayo mazuri. Ingekuwa busara zaidi kama wangeshirikiana nao. Hii ni nasaha japo BAKWATA haipendi nasaha. Sisi tunatekeleza dhimma zetu kwa Mwenyezi Mungu. 

 
 

YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita