AN-NUUR
Na.153 Safar 1419, Juni 12-18, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu:

Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja

Na Maalim Mwalim
INAELEKEA kuna baadhi ya wasomaji wa AN-NUUR ambao wamekusudia kuitumia vibaya fursa iliyotolewa na Mhariri wa gazeti hili ya kujadiliana kwa nguvu ya hoja. Hali hii ikiachiwa kuendelea italigeuza gazeti hili kuwa ni la porojo kinyume na sifa ambayo tayari limejijengea ya kuandika habari zilizofanyiwa utafiti wa kina. 

Makala ya Bwana John Mtaki AN-NUUR Na. 150 yenye kichwa cha habari "Mohamed Saidi usiwapotoshe wenzako" ni mfano wa dalili za matumizi mabaya ya fursa na kujadiliana iliyotolewa katika AN-NUUR. 

Bwana Mtaki hakuridhika na makala ya Mohamed Saidi AN-NUUR Na. 148 iliyomhusu Tewa Saidi Tewa. Hata hivyo badala ya Bwana John kuleta hoja za kutokubaliana na Mohammed Saidi, yeye akachagua kutoa kejeli.Naamini kuwa makala ya Mohammed Saidi imetokana na utafiti ambao ulifanyika kwa makini sana. Uzuri, makala yake imejitetea yenyewe. Mategemeo yangu nikuwa mtu anaetaka kutofautiana na kazi iliyofanywa kiutafiti lazima pia afanye utafiti. Hili Bwana John hakulifanya. Hapa nitarejea baadhi ya maneno katika makala yake ili kuthibitisha kuwa hakufanya utatifi wowote.

Katika para ya kwanza ya makala yake John anasema, "Nimesikitishwa sana na propaganda iliyoenezwa na ndugu Mohammed Saidi ...". Akiendelea anasema, "kwa propaganda hii Bwana Mohammed Saidi anajaribu kutushawishi wasomaji kuwa Waislamu wa Tanzania wako nyuma kimaendeleo kwa sababu Mwalimu Nyerere alipanga njama ya makusudi kabisa kufanya hivyo. Nasema huu ni uzushi na uongo mtupu".

Kutumia maneno ya mwisho kama propaganda, uzushi na uongo katika aya ya mwanzo tu za makala yake kutupilia mbali aliyoandika Mohammed Saidi bila kutoa maelezo ya kina, Bwana Mtaki anaonyesha kukata tamaa, chuki na kutopea katika maadili mazima ya kutumia hoja kuvunja hoja.Ningependa kutumia fursa hii kumtaka Bwana Mtaki anapoamua kuzijibu hoja zilizoandikwa kitaalamu akubali kupoteza muda wake ndani ya maktaba badala ya kukaa kwenye kiti na kutumia maneno matatu yasiyo na msingi kukanusha hoja zilizojaa kwenye kurasa mbili za gazeti.Utaratibu huu utamfanya aache kufoka na badala yake atoe hoja. Ukifuata utaratibu huu wa kujibu utafiti kwa utafiti basi hakuna atakayekulazimisha ukubaliane na Waislamu juu ya madai yao. Wasomi wana tabia ya kukubali kutokubaliana. Kwa makala yako sidhani kuwa itakuwa ni uadilifu kukuita msomi hata kama una vyeti kwa sababu maadili ya usomi hayakubaliani na watu wanaojibu hoja kwa utabiri hali wao siyo Manabii wala Mitume.

Pamoja na udhaifu ulio katika makala ya Mtaki inashangaza kuona msomaji mwingine Bwana Elia Batendi akimuunga mkono. Kinachoshangaza hapa siyo kitendo cha kuunga mkono bali ukweli kuwa kama alivyoandika Bwana John, Bwana Elia naye anatoa hoja za nguvu kuonyesha sababu zake za kuunga mkono makala ya John Mtaki.Turejee kwenye makala ya Ndugu Elia iliyochapishwa katika 

AN-NUUR Na. 152 yenye kichwa cha habari `Kasema kweli Mtaki, acheni hisia za kuonewa'. Kinachogomba hapa siyo msimamo wa ndugu Elia bali ni mtindo wa uandishi wake wa kuhitimisha makala kabla ya kuiandika. Tungetegemea Bwana Elia athibitishe kuwa dhana kuwa Waislamu wanaonewa hapa nchini ni hisia tu jambo ambalo hakulifanya.Jambo angeweza kulifanya endapo angeamua kutumia baadhi ya muda wake kufanya utafiti 

(research) ili ugunduzi wa utafiti huo autumie kukanusha madai ya Waislamu, kinyume na hivyo Bwana Elia unachemsha! 

Turejee nukuu ya Bwana Elia inayothibitisha ukosefu wa uadilifu wa ndugu huyu pamoja na uongo aliotumia katika makala yake. Anasema: "miaka ya nyuma Waislamu walijishughulisha sana na elimu -akhera kiasi cha kusoma madrasa tu... hawakujikujishughulisha na kujenga...". Sasa huu ni uongo kwa sababu tunao ushahidi kuwa Waislamu walikuwa mstari wa mbele kusoma na pia Waislamu walijenga shule ambazo kihistoria zinalingana na wakati na mahali husika. Ndugu Elia atakapohitaji ushahidi huu mimi niko tayari kumpatia. Kwa sasa ninaona tu bora zaidi kumpa fursa ya kuthibitisha madai yake ambayo mimi nimeamua kuyaita uongo kwa sasa kutokana na ushahidi nilionao. 

Ndugu Elia anaendelea kujenga uongo wake kwa kusema "ukweli huu Waziri Kapuya ameubainisha, lakini wale waliojengea Waislamu hisia za kuonewa na kudhulumiwa walianza kupinga (Angalia AN-NUUR la tarehe 1-7, Mei, 1998 na Maalim Mwalim) na kutolewa sababu za hovyo hovyo kuwa Waislamu shule zao hazifanyi vizuri kwa sababu zimejengwa mijini kwenye kelele za madisko".Linganisha maneno hayo na haya hapo chini yaliyo katika makala yangu, 

AN-NUUR Na. 147 Uk. 10, "Tofauti nyingine kubwa ni kuwa wanafunzi wote wa Seminari za Kikristo hulala shuleni wala hawana habari za usumbufu wa madaladala au nyumba zilizojirani na mabaa yanayoporomoshwa muziki usiku kucha..."Itaonekana wazi kwamba mimi sikusema kuwa shule zetu zimejengwa mijini kwenye kelele za madisko. Kwa maelezo zaidi soma makala hiyo yenye kichwa cha habari "kulinganisha seminari za Kiislamu na Kikristo ni propaganda zisizo na msingi". 

Badala ya ndugu Elia kukimbilia kwenye hitimisho na kudai kuwa hoja nilizotoa kwenye makala yangu ni za hovyo hovyo ilikupasa kwanza ujenge hoja zitakazozivunja hoja zangu, ambazo wewe umeamua kuziita za hovyo hovyo, kauli kama hizi wenzetu huziita "sweeping statements" na kwa kawaida hazitolewi na wasomi au wataalamu waadilifu. Kwa faida ya wasomaji ambao hawakuisoma makala yangu hiyo, hoja zangu za kupinga ulinganishi huo ni kuwa shule za Kikristo: 

. Zimejengwa zamani sana kuliko zile za Kiislamu. 

. Shule hizi zinasomesha wanaume watupu hasa zile za Kanisa Katoliki. 

. Wanafunzi wao wote wanaishi shuleni ndani ya mabweni. 

. Haziendeshwi kwa ada za wanafunzi na pia wanafunzi hulipa ada ndogo kuliko ile ya serikali.Kwasababu hiyo, shule hizi zinauwezo wa ku chukua wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule za serikali kwani huko Seminari watasoma bure au kwa ada kidogo.Mishahara na huduma nyingine katika shule hizi haitegemei ada za wanafunzi.Serikali ya awamu ya kwanza ilikataza Waislamu kuanzisha Seminari zao.Kwa hiyo, kama Bwana Elia angependa kuonyesha ustaarabu wake, basi ilimpasa kujibu hoja hizi ili awe na haki ya kuzibainisha kama ni za ovyo ovyo! 

Napenda kuachana na hawa mabwana kwa kusema kuwa maneno kama propaganda, uzushi, uongo na hisia kama walivyotumia hayatabadilisha hata nukta moja ya ukweli kuwa Waislamu wa Tanzania wamekandamizwa, wameonewa na kubaguliwa na serikali yao wenyewe.

Uzuri ni kuwa hata majina ya watu au vikundi vilivyohusika na ubaguzi huu ni mambo ambayo Waislamu wameyaweka bayana. Kama kina Mtaki mnaoubavu basi muulize Mwalimu kwanini miaka zaidi inapita na hataki kujibu hoja za Waislamu dhidi yake.

Kama Uislamu unazuia watu kusoma ni kwanini Waislamu wa Malaisya wamesoma na kufikia maendeleo makubwa ya kisayansi kiasi cha kuwa wawekezaji hapa kwetu?Kwanini Waislamu wa Libya, Misri, Iraq, Iran wamesoma na kufikia daraja ya kujitosholeza kwa wataalamu na kusafirisha wengine nje?

Sisi tunasema hali ya Waislamu hapa nchini si bure bali kuna mkono wa mtu.Kwa kuhitimisha makala hii, ningependa kutoa ushahidi zaidi juu ya ukweli kuwa Waislamu wameonewa na kubaguliwa kielimu. Nachukua eneo hili kwa vile ninalimudu zaidi.Wamishenari walishirikiana na wakoloni kuwabagua Waislamu. Tazama rejea zifuatazo kwa ushihidi:Camerron and Dodd (1970), Society, School and Progress.George Malekela (1983), Access to Secondary Education in Sub Sahara Africa. Unpublished PhD Thesis.Ishumi, Abel (1980) Inequalities in the Distribution of Education Opportunities. Origins and Trends in Tanzania Education and Social change. 

Roland (1970), The Missionery Factor in East Africa.Shule za Wakristo zilijengwa na kuendeshwa kwa kodi za Watanganyika. Angalia kitabu cha akina Dodd ukurasa wa 76. Pia rejea ukurasa wa 114 ambapo wanasema, "... there can be no denying that, educational system, even under government had a great Christian bias...". Tafsiri. "Hakuna upinzani kuwa mfumo wa elimu hata pale serikali iliposimamia ulikuwa unawapendelea Wakristo....". Pia ukurasa wa 25 wanasema: "The British government having taken all the burden both recurrent and capital for the mission schools ...". Tafsiri. "Baada ya serikali kikoloni ya Uingereza kuchukua mzigo wote wa kugharimia shule za Kikristo katika matumizi ya kawaida na ya maendeleo...". Katika ukurasa wa 76 Bwana Dodd anasema. "In 1957, Muslim Association Agencies received only Pound 6,848, out of total government expenditure in education in grant - in - aid of pound 1,338,925 ...Christian missions ... greately expanded their education services by the means of grant-in-aid received from the government". Tafsiri. "Katika mwaka 1957 mawakala wa Jumuia za Kiislamu walipokea paundi 6,848 kati ya paundi 1,338,925 zilizotolewa na serikali kusaidia shule za mashirika ya dini ... hivyo Wakristo walitumia fedha hizo kupanua huduma zao za elimu.

Ifahamike kuwa hizi ni kodi za Watanganyika, Waislamu wanapata paundi 6,848, Wakristo wanapata paundi 1,332,077. Tukisema mnadai ni hisia. Ukristo na ukoloni wote waliuona Uislamu kama adui mkubwa. Tazama kitabu cha Roland ukurasa wa 205, utaona maneno yafuatayo: "In British territories, strongly it was the governments rather than the missions which saw the dangers of the Islamic expansion and which took whatever steps they could to forestall it". Tafsiri; "Katika makoloni ya Waingereza ndio walioona hatari ya kupanuka Uislamu (kuliko wamisheni) na walichukua kila hatua waliyoweza kuzuia hali hiyo". Kuhusu chuki dhidi ya Waislamu rejea barua ya kichungaji ya Askofu Pengo (1993) na kitabu cha Sivalon (1992). Pia ifahamike kuwa Watanganyika wa kwanza kupata ajira maofisini wakati wa utawala wa Mjerumani walikuwa Waislamu kwa vile ndio waliokuwa wamesoma. Rejea kitabu cha akina Dodd ukurasa wa 25 na ukurasa 50-51 pia kitabu cha Roland ukurasa wa 203.

Nataka nimalizie kwa kusema kuwa kwa wale ambao Ibilis amewaingia sana hata wajapokupewa ishara bado itakuwa ni vigumu kwao kuamini rejea maneno ya Bwana Yesu yaliyo katika Luka 11:29.

Ifahamike wazi kuwa Waislamu hawakutarajia wamishenari ambao uhusiano wao na wakoloni ni kama ule wa Yohana Mbatizaji na Yesu wawapendelee heri yoyote. Gharama ya huduma ya wamishenari ilikuwa ni kubatizwa. Kwa Waislamu wengi hili halikuwezekana kwa sababu heri upoteze mwili lakini uponye roho. Hoja kuhusu elimu kwa ubatizo zimo kwenye maandishi ya akina Ishumi, Malecela, Dodd, Roland n.k. Sitegemei tena mtu asema hii ni hisia.Kwa kujua ukweli huu wamishenari na wakoloni, Waislamu walipigana kupinga kutawaliwa wakati Wakristo wazawa waliwakumbatia wakoloni (rejea kitabu cha Bergen 1981: Development and Religion in Tanzania).Mashujaa waliopigana ni akina Mkwawa, Abdallah, Chaburuma, Mirambo, Abushiri n.k.Ulipofika wakati wa kuanzisha vyama, Waislamu walianzisha TAA na hatimaye TANU.

Kwa hiyo basi hatutegemei kuwa akina Elia mtaibuka na hoja kuwa tunataka upendeleo. Tumepigania uhuru ili tupate haki zetu. Miaka 37 baada ya uhuru bado serikali inadai hakuna hata Muislamu mwenye sifa ya uingia kwenye mabodi ya Parole . Hapa ndipo tunapoihoji serikali, kulikoni?

 
 

YALIYOMO

TAHARIRI  

Uvamizi wa Polisi Mwembe Chai:  Mwanafunzi aliyepigwa risasi apooza Muhimbili   

Maoni yetu: Vipi watu wafurahie mateso ya wengine?  

Wanawake wakutana na kudai:  Gewe, Makamba wajiuzulu    
  
Maelezo ya Mjumbe wa Kisarawe katika mkutano wa kina mama   

Waraka wa Baraza Kuu kwa Mh. Rais   

BARUA ZA WASOMAJI  

Mmiliki wa Biblia na mbinu za kuhubiri   

MAONI YA WASHAIRI  

MAKALA:   
KAMATI YA KINA MAMA WA KIISLAMU - TAARIFA YA MATUKIO JUU YA UNYANYASAJI WA POLISI DHIDI YA WANAWAME WA KIISLAMU   

MAKALA MAALUM   
Waziri Dossa Azizi: Shujaa aliyesahaulika - Na. Mohammed Said  

Mdahalo juu ya kudhulumiwa Waislamu: Tuache hisia na kejeli, tutoe hoja  

TAMKO LA WANAWAKE WA KIISLAMU DHIDI YA MAUAJI YA WAISLAMU MWEMBECHAI NA KUDHALILISHWA WANAWAKE WAISLAMU MAHABUSU   

Hali ilivyokuwa kwenye shule za Misheni   

Makala: Baada ya miaka 34 Zanzibar yakosa Majaji - na S. Mzee   

Bakwata ithamini juhudi za wengine  

Masheih Arusha wamuunga mkono K.K.   
Na Mwandishi Wetu Arusha  

Makamba aliongezea  AN-NUUR 'Mashitaka'  

MSAUD wafikisha suala la Chuki AMNESTY  
  
Wazee Handeni wakwamisha mhadhara 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita