|
MASHAIRI
Ngangari inameremeta
Hodi hodi uwanjani, Sabaya nipe kalamu,
Nataka kuwapasheni, hakika muifahamu,
Baby Fumo pita ndani, mkombozi Mariamu,
Inameremeta sana, Lipumba nuruye sana.
Nuru haitoki mbali, Tabora si Ukaguru,
Imechomoza miali, si kwengine Lolanguru,
Msitafute muhali, si Mtwara si Luguru,
Inameremeta sana, Lipumba nuruye sana.
Nuru uchumi “ngangari”, kichwani umetulia,
Nuru siasa “ngangari”, mahiri kupindukia,
Nuru haitakabari, Ikulu ikiingia,
Inameremeta sana Lipumba, nuruye sana.
Nuru yatikisa miti, miamba na majabali,
Nuru imejizatiti, vikongwe wako chakali,
Nuru sio afriti, “Bwana Madeni” muhali,
Inameremeta sana, Lipumba nuruye sana.
Nuru sasa inavuma, Kikongwe anachachawa,
Nuru imeteka umma, namba wani kapagawa,
Nuru hairudi nyuma, yenda mbele maridhawa,
Inameremeta sana, Lipumba nuruye sana.
Shime ndugu zangu shime, nuru yetu tuienzi,
Namba wani tuinyime, ikose kiti cha enzi,
Hata roho ziwaume, nuru ndo yetu kipenzi,
Inameremeta sana, Lipumba nuruye sana.
Kaditama namaliza, ngangari wote vipenzi,
Mwiko nuru kufifiza, Oktoba tuienzi,
Nambawani kunagiza, watatukwea makonzi,
Anameremeta sana, Lipumba huyo ngangari.
Na Juma S. Katanga (JUSHAKA)
S.L.P. 872
Mapumzikoni
(Mwishowanchi) - Kigoma
Sera za kweli
Bismillahi Rahimu, kwa jina lake Manani,
Salamu Alaykumu, mhariri nasahani,
Nina khabari muhimu, naomba unisaini,
Wana-CUF ni ngangari, kwa sera zao za kweli.
Khutuba zake Lipumba, zinaingia kichwani,
Akinena mwana Yomba, husherehesha makini,
CUF dume watalamba, Oktoba karibuni,
Wana-CUF ni ngangari, kwa sera zao za kweli.
CCM yanyanyasa, na waumini nchini,
Wanaua kama kasa, damu yamwagika chini
Na mpige yule khasa, yule kamuweke ndani,
Wana-CUF ni ngangari, kwa sera zao za kweli.
Wakati wakaribia, kuingia chaguzini,
Tusije tukarudia, makosa yetu mwanzoni,
Tukusudie kwania, kuiaga namba wani,
CCM baibai, twakuaga buriani.
Lipumba Sefu Sharifu, nawaomba tulieni,
Pasiwe wasi na khofu, sera zenu enezeni,
Kiongozi wetu CUF, elufu mbili mwishoni,
CCM kwa herini, hatukutakeni tena.
Beti sita nimefika, kalamu naweka chini,
Kitini ninainuka, nakwenda zangu shambani,
Huenda nikafarajika, na maisha haya duni,
CCM mmeoza, dawa ni kukuzikeni.
Ustadhi Seifu Omari,
S.L.P. 100054,
Dar es Salaam.
Maisha
Amina lete kalamu, na karatasi mezani,
Na tena fanya muhimu, nataka kwenda shambani,
Sada Vumi na Mshamu, Nyambi njooni uani
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Tamaa si kitu chema, wanangu nawambieni,
Yangu muyashike vema, msije fanya utani,
Ya sasa sio ya zama, Dunia yenda mwishoni,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Tamaa huleta kilio, mijini na vijijini,
Fungueni masikio, yangu muweke kichwani,
Sio tu ndio ndio, mkaniona punguani,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Wapo walio wengi, sasa wameshapotea,
Kisa ni kuvuta bangi, na mapombe kujinywea,
Wengine ni mashangingi, ukimwi wanaugua,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Nisemayo si upuuzi, huu ni wangu wasia,
Mkija kufanya wizi, moto mtajaungua,
Na kama ni ujambazi, risasi zitawaka,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Kuna mengi ya hatari, msifanye masihara,
Mkijakuwa taperi, mtaja ozea jera,
Zitulizeni akiri, acheni zenu papara,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Nasema someni wana, elimu kupigania,
Msijefanya hiyana, maisha mtajutia,
Msiendekeze ujana, ujana wapita njia,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Kaditamati watama, hapa ninaishilia,
Nakimbilia kulima, mvua inakaribia,
Na nyinyi fanyeni hima, kengere imeshalia,
Maisha kushinda moyo, tamaa si kitu chema.
Mnyonge wa haki, Kasimu J. Ndava,
S.L.P. 100054,
Mbagala.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Tume, kauli ipi sawa?
CCM maji
shingoni
Wazanzibar
wawaambia Dk. Omar na Karume:
Kura
tutawanyima, mtang’oka
CCM
ni nguruwe aliyenona - Mtopea
Kabobe
asisitiza uchaguzi huru
Mkapa
aomba kura kwa hoja ya uzawa
Vifaa
vya uchaguzi vimeanza kusambazwa
Mizengwe
yatupwa,wagombea upinzani wapeta
HABARI
ZA KIMATAIFA
USHAURI NASAHA
Haya ndiyo
mambo ya wanawake - 2
MAKALA
Kura ni
silaha
Kampeni
za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo
MPASHO NASAHA
BEN NA
BULLY
MAKALA
Wimbo wa
Umoja na Amani wa CCM ni ghilba za kisiasa
KALAMU YA MWANDISHI
Hojini
Ubalozi wa Vatican kwanza
MAKALA
CCM kushinda
uchaguzi bila kupigiwa kura?
MAKALA
Mwenye
macho haambiwi tazama - 4
CUF
Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa
Kodi
ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa
Wazee
waijibu CCM
BARUA
MASHAIRI
MICHEZO
Yanga watakiona - Kajumulo
Simba yajaribu kombe la FAT
Tarimba akataa ubabe
Jeshi laongeza timu Ligi Kuu
|