NASAHA
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 

Kura ni silaha

Na K.U. Khamis 

ULIMWENGU umeshuhudia ugumu wa kuwabadilisha watawala wa nchi au wa eneo fulani la ardhi. Ugumu huo unaongezeka zaidi pale inapotokea utawala wa kidhalimu ndio unaohusika kuondoshwa au kupunguziwa nguvu zake. 

Tokea enzi za kale binadamu wamekuwa katika mtihani mgumu wa kukabiliana na binadamu wenzao ambao wanashika madaraka ya kutawala watu kimyume na matakwa ya walio wengi. 

Tawala hizi kwa kuelewa upinzani uliopo, huwa na taratibu mbali mbali za kuhakikisha kwamba zinadumu katika madaraka hayo. Njia kubwa inayotumika kuzilinda tawala ni kwa kutumia nguvu za kijeshi za kuwa na wapiganaji wengi na silaha zilizo bora. Mtihani unaowakabili wale wanaotaka mabadiliko ni jinsi ya kukabiliana na nguvu hizo. 

Katika enzi ya kale tawala hasa zile za kidhalimu ziliweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na ugumu wa kuzikabili nguvu za hao. Nyakati hizo njia pekee ya kuwaondoa madhalimu ni kukabiliana kijeshi kwa mapambano. Wakati huo mapamnbano yalikuwa ni ya ana kwa ana. Ilikuwa ni kushika silaha umkabili mwanamume mwenzio nae ni mwenye silaha mkononi. 

Hali ilikuwa ngumu na ya kutisha kweli kweli. Mapambano ya aina hii yalikuwa ni magumu yanayohitaji ushujaa mkubwa na watu wenye afya za hali ya juu. Katika mapambano haya mtu wa mraba mmoja anaweza akakabiliwa na baba la miraba minne na huenda akakatwa vipande vipande kuanzia miguu hadi shingo. Huo ndio ulikuwa ugumu wa kuwang'oa watawala katika zama hizo. Katika wakati huo wanaume wagonjwa, wazee, wanawake na watoto kabisa hawakutarajiwa kuleta mabadiliko katika utawala wa nchi. 

Kwa ugumu huo imetokea falme nyingi za enzi hizo kudumu kwa muda mrefu bila kutarajiwa kwa yeyote kuwaondosha au kuubadilisha mwelekeo wa watawala. Hali hiyo ilisababisha watu kuingia katika utumwa wa muda mrefu pasipo na matarajio ya baadae. 

Katika jamii ambazo tawala zina nguvu kubwa ilikuwa ni vigumu kuweza kuwashawishi watu kujiunga au kutafuta njia ya kuwakabili wale wanaoshika hatamu. Mifano ya hali hiyo tunaiona hata katika vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu. Mfano mzuri ni pale Wana wa Israili walipopewa amri na kiongozi wao Mtume wa Mungu Nabii Mussa A.S. kwamba waingie katika mji mtakatifu na waishi humo. Walijibu. 

"Wakasema ewe Mussa huko kuna watu majabari. Nasi hatutaingia mpaka watoke humo, wakitoka humo hapo tutaingia". (Maida 22) 

Mayahudi hawakuitii amri ya kiongozi wao kutokana na upungufu wao wa imani kwa khofu kubwa ya kuwakabili upanga kwa upanga wanaume wa kifalastina. 

Habari nyengine inayolingana na hiyo ni pale Mayahudi walipochoshwa na dhulma ya mfalme Jaluti na majeshi yake walimwambia Nabii wao: 

"Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu" Yeye (Mtume wao) akasema: "Haielekei ya kuwa hamtapigana ikiwa mtaandikiwa kupigana? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa katika majumba yetu na watoto wetu? Lakini walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua sana madhalimu." (Baqara 246) 

Uamuzi wa kuukabili utawala uso kwa uso, mkono kwa mkono halikuwa ni jambao jepesi. Ugumu wa jambo hilo ulizifanya jamii nyingi kuhiari kubaki na mateso kuliko kufikiria kuleta mabadiliko. 

Hata hivyo kwa taabu kubwa na kwa rehema na ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwasaidia wanaodhulumiwa baada ya miongo kupita jamii ziliweza kuleta mabadiliko baada ya muda mrefu wa udhalilifu. 

Mwenyezi Mungu aliuelewa uzito wa kuzibadili tawala ulivyokuwa kwa njia zilizokuwepo wakati huo za kutumia upanga. Yeye anayewatakia watu unafuu amependa kuuondoa uzito huo kwa kuleta mabadiliko ya jinsi ya kukabiliana na madhalimu duniani. 

Njia mpya ya kuleta mabadiliko 

Mwenyezi Mungu katika kuwapa watu uwepesi wa kuzibadili tawala, amejaalia ulimwenguni badala ya upanga kuwepo matumizi ya silaha za moto. Silaha za kumlenga mtu alie karibu na alie mbali. Kwa kutumia silaha hizo makundi mawaili yaweza kukabiliana bila kugusana wala kukaribiana. Njia hii ni njia ya kutumia bunduki na mizinga na ambayo imetumika kuwang'oa watawala waliokuwa na nguvu kubwa wasiotaka kuelewa haki za binaadamu. Madikteta na madhalimu wengi wameondoshwa kwa njia hii. Baadhi yao ni kama: Dikteta Adolph Hitler wa Ujerumani, Siad Barre wa Somalia, Najibullah wa Afghanistan, Mabutu wa Zaire na wengineo. 

Njia ya kulengana shabaha imekuwa ni nyepesi afadhali kuliko ile ya kale ya kumuingia maungoni adui mwenye nguvu. Wepesi huu wa kuleta mabadiliko umetokana na ahadi aliyoitoa Mwenyezi Mungu katika Qurani pale aliposema. 

"Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yalio mazito.....(185 Baqara) 

Kutokana na uwepesi wa njia hii, makundi mbali mbali katika jamii hata ya vijana na watoto wadogo wameweza kushiriki kuleta mabadiliko ya tawala za nchi. Hayo yameweza kuthibitika hata katika nyakati zetu za karibuni katika nchi za Uganda, R. Congo iliyokuwa Zaire, Liberia n.k. Katika nchi hizo imeonekana jinsi watoto walivyokuwa ni nguvu ya kutegemewa kwa kushika silaha kuwasaidiawazee kuleta mabadiliko. Mabadiliko yaliyotokea kwa njia za kuwang'oa madhalimu kwa njia ya bunduki ilikuwa ni namna ya pili ya kuwakabili madhalimu. 

Mwenyezi Mungu amekuwa bado anaendelea siku hadi siku kuukamilisha ukweli wa tamko lake la kututakia wepesi. Kutokana na Rehema zake Mwenyezi Mungu ameuzidisha wepesi katika kuzibadilisha tawala kwa mtindo ambao hapa tatumika tena upanga wala risasi za moto. Hayo yatawezekana hata kama watawala hao watalindwa na majeshi na silaha nzito. 

Kubadilisha utawala kwa kutumia kura 

Mwenyezi Mungu S.W. ameuzidisha wepesi wa kuwabadili watawala kwa kuleta mfumo mpya ambao badala ya kutumia upanga, na kufyatua risasi za moto, twaweze kubadilisha utawala kwa kutumia kipande cha karatasi. Kikaratasi hicho kinaitwa KURA. 

Kura ni njia mpya aliyoijaalia Mwenyezi Mungu ulimwenguni kwa zama za sasa kubadilishana utawala. Kura ni njia ya ustaarabu sana kulinganisha na njia zilizotumiwa katika nyakati zilizopita. Kupitia utaratibu huu wananchi wanafanya maamuzi ya kuharibu mali. Wananchi wenye sifa ya upigaji kura hujiandikisha kwa ajili ya upigaji kura na hatimaye kupiga kura ya kuwachagua viongozi wanaowataka ili wawaweke madarakani. 

Njia hii ya kuchagua viongozi huitwa uchaguzi. Uchaguzi unapokuwa huru na wa haki wale walioshindwa huyakubali matokeo na kuwaacha washindi washike hatamu za uongozi bila ya mizozo. Upigaji kura, mtu hutumbukiza karatasi ya kura katika sanduku maalum la kura kumchagua yule anayemtaka awe kiongozi. Hatua hii hufanywa kwa siri bila ya kutishwa wala kulazimishana. Kwa hakika ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuueleta utaratibu huu ambao huwapa nafasi hata wazee na wagonjwa kuweza kushiriki katika kubadilisha tawala za nchi. 

Njia ya kura inampa mtu fursa ya kuleta mabadiliko ya utawala bila ya vumbi wala jasho. Njia hii haihitaji ima dume majabari kutunisha misuli wala silaha kali. Ni utaratu unaomwezesha hata mama mja mzito kuleta mageuzi. Kwa hakika huu ni wepesi mkubwa aliotuletea Mwenyezi Mungu. 

Umuhimu wa kura 

Umuhimu wa kura unawafanya viongozi waliomo madarakani kuheshimu kazi na kuwaheshimu raia zao kwani iwapo watawatendea mabaya itapofika siku za kupiga kura bila shaka watawanyima kura hivyo madaraka yatawatoka. Njia ya kura huleta heshima katika nchi baina ya watawala na raia. Na kwa hakika raia huwa ndio wenye mamlaka ya nchi kwa kumpa uongozi yule wamtakae. 

Fursa ya kupiga kura pia huwapa wananchi nafasi ya kupima na kuchagua viongozi ili kuboresha hali zao na ya nchi kwa jumla. 

Kwa maana hiyo viongozi waliochaguliwa hujitahidi kuwa karibu na wananchi kwa kutatua matatizo yanayowakabili ili waweze kudumu madarakani. Katika utaratibu huu haitarajiwi kabisa viongozi walio madhalimu na wajeuri kuwarudia wananchi kuwaomba wawape tena fursa ya kuwaongoza na wananchi nao wakawapa tena fursa hiyo. 

Kura iwapo itatumika vibaya haisaidii kuondoa dhulma katika nchi. Matumizi mabaya ya kura ni pale wananchi wanapodharau umuhimu wa kura na kuwa tayari kumpa kiongozi mbaya kura yake kwa thamani ya mvao wa khanga, kwa pato dogo la fedha au kwa misingi ya ukabila. 

Umuhimu wa kura ni lazimaueleweke bila kudharauliwa. Kura inachukua nafasi ya upanga au mtutu kubadilisha utawala au kuwang'oamadhalimu. Upanga wa kura ni katika rehema za Mwenyezi Mungu za kuwasaidia na kuwapawepesi waja wake kutokanana madhalimu. Kwani upanga huo waweza kushikwa na hata vikongwe nawasiojiweza.Kura isidharauliwe kwani kura moja yaleta mabadiliko. 

Watawala tokea zamani wamekuwa na mmbinu za kutaka kubaki mielele katika madaraka. Hivyo baadhi yawakati hutumia hata faulu katika utaratibuwa kura. Waweza kutumianjia za vitisho na hata kuwanyima wengifursa yakupiga kura. Hata hivyo mbinu zote hizo Mola anazijua na huenda akaleta mfumo mwengine ulio bora zaidi pale atapotaka, kwani yeye ni tajiri wa mambo. Ni jukumu letu na ni ibada kujitahidi kuichunga haki zetu ya kuwabadilisha watawala. Shukrani hizo zisiwe za maneno matupu; bali ni za vitendokwa kuitumia fursa hii muhimu kwa kujiandikisha kwa wingi na hatimaye kupiga kura kuchagua viongozi wazuri. 

Mafunzo ya Mitume yanasema Mwenyezi Mungu anafurahi pale anapompa mja wepesi au fursa na mja akaitumia fursa hiyo. 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tume, kauli ipi sawa? 

CCM maji shingoni 

Wazanzibar wawaambia Dk. Omar na Karume:
Kura tutawanyima, mtang’oka 

CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea 

Kabobe asisitiza uchaguzi huru 

Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa 

Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa 

Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta 

HABARI ZA KIMATAIFA

USHAURI NASAHA
Haya ndiyo mambo ya wanawake - 2 

MAKALA
Kura ni silaha 

Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo 

MPASHO NASAHA
BEN NA BULLY 

MAKALA
Wimbo wa Umoja na Amani wa CCM  ni ghilba za kisiasa 

KALAMU YA MWANDISHI
Hojini Ubalozi wa Vatican kwanza 

MAKALA
CCM kushinda uchaguzi bila kupigiwa kura? 

MAKALA
Mwenye macho haambiwi tazama - 4 

CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa 

Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa 

Wazee waijibu CCM 

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga watakiona - Kajumulo
  • Simba yajaribu kombe la FAT
  • Tarimba akataa ubabe
  • Jeshi laongeza timu Ligi Kuu

  •  

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita