NASAHA
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
KALAMU YA MWANDISHI

Hojini Ubalozi wa Vatican kwanza 

Na Maalim Bassaleh 

GAZETI moja maarufu humu nchini, katika toleo lake la Jumamosi,Septemba 9,2000, limeeleza kuwa Halmashauri Kuu ya Maaskofu ya Baraza la Kanisa la Pentekoste la Tanzania(PCT), hivi karibuni imetoa kitabu kinachoitaka serikali iitishe kura ya maoni kwanza, kabla ya kuamua kujiunga na Jumuiya ya Mkutano wa Kiislamu, (OIC), ili kupata ridhaa za Watanzania. 

Kitabu hicho, kilichopewa jina la "Amani katika Tanzania italindwa kwa:kutenganisha Dini na Mamlaka ya nchi", kinaeleza kuwa kitendo cha serikali ya Tanzania kutaka kujiunga na OIC si jambo dogo. Nijambo linalowahusu Watanzania wote, Waislamu na wasiokuwa Waislam, na hata wale wasiokuwa na dini yo yote. 

Kwa mujibu wa kitabu hicho inaelezwa jambo hilo, halifai kujadiliwa kijuujuu tu, kwa kupitia katika vyombo vya habari, na wala haifai kuachiliwa Bunge peke yake kuamua juu ya jambo zito kama hilo. 

Halmashauri Kuu ya Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste, kwa kupitia katika kitabu hicho, imesisitiza serikali iitishe kura ya maoni ili ipate kuelewa msimamo wa Watanzania wote, wa dini mbalimbali, juu ya jambo hilo. 

Katika kutaka kufafanua zaidi juu ya jambo hilo, Halmashauri hiyo imesema, "Lakini si kazi ya Bunge kutunga sheria za kidini, kwa kuwa OIC ni taasisi ya kidini, ni muhimu taasisi nyingine za kidini zilizopo hapa nchini nazo zishirikishwe kikamilifu katika uamuzi mzito kama huu." 

Kwa ufupi, Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste, katika kitabu hicho, wametilia mashaka uhusiano huo kama utaanzishwa. Wamedai kuwa lengo la misaada inayotolewa na taasisi hiyo ni kwa ajili ya kutaka kueneza imani ya dini hiyo katika nchi wanachama. Maaskofu hao wamesema kuwa kama Tanzaniaitajiunga na taasisi hiyo basi itakuwa ni sawa na kuwasilimisha Watanzania bila ya nidhaa yao! 

Inaonekana kuwa kitabu hicho kimetolewa na Kanisa la Pentekoste, kama ni onyo kwa serikali isijiunge na OIC, baada ya kumsikia mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya CCM, Mheshimiwa Amani Karume katika madahalo ulioandaliwa na shirika la utangazaji la BBC, akisema kuwa serikali imekwishafanya utafiti na imeona kuwa Tanzania ijiunge na taasisi hiyo, kwa kupitia serikali ya Muungano, na siyo kupitia serikali ya Zanzibar. 

Kwa vyovyote vile, mtazamo huo wa Maaskofu, umekosa uadilifu. Ni mtazamo ulioelekezwa katika kuuangalia upande mmoja tu wa shilingi na kuupuuzia upande wa pili. Ni mtazamo chongo! Ni sawa na mtu mwenye macho mawili lakini akaamua, kwa makusudi, kufumba jicho moja na kuangalia kwa jicho moja. 

Kama serikali ya Tanzania haifai kujiunga na OIC, bila ya kuitisha kura ya maoni, eti kwa sababu OIC ni taasisi ya kidini; basi lazima tukubali kuwa kwa hoja hiyohiyo, serikali hiyo ya Tanzania itakuwa imefanya kosa kuanzisha uhusiano, tena wa kibalozi, na Vatikano, ambayo ni taasisi ya kidini, na siyo nchi yenye raia! 

Uhusisano huo wa serikali ya Tanzania na Vatikano, ingawa ni uhusiano baina ya nchi hii na Kanisa Katoliki duniani, lakini jambo la kustaajabisha hakuna yeyote anayehoji juu ya uhusiano huo, si serikali wala makanisa ya Kikristo! 

Mheshimiwa Aboud Jumbe, ambaye aliwahi kuwa Makamu Rais wa Jamhuri ya Miuungano wa Tanzania, na pia, Makamu Mwenyekiti wa CCM, katika kitabu chake alichokiita, "The Partner-ship" amesema, "Kwa mfano, kuwepo kwa ubalozi wa Vatican nchini Tanzania hakukupata kuhojiwa, pamoja na kuwa serikali hii inadai kuwa si ya kidini. Kanisa, CCM na serikali, vyote vimekaa kimya huku vikijua kutendeka kwa hilo lakini vitazibwa mdomo." (Uk.126). 

Laiti Waislamu wa nchi hii, wangalinikubalia kuwa msemaji wao, basi mimi, kwa niaba yao, ningalikubaliana na matakwa hayo ya Maaskofu, kwamba iitishwe kura ya maoni, isipokuwa kwanza, kwa vile uhusiano wa Tanzania na Vatikano haujawahi kupigiwa kura hiyo ya maoni ili kuwauliza Watanzania kama wanautaka au la, tungelianza kuupigia kura hiyo uhusiano huo, ilitupate kuuhalalisha. 

Aidha mimi naafikiana kabisa na wazo la Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste, kuwa jambo hilo lisijadiliwe katika vyombo vya habari, na pia lisiachiliwe Bunge kuamua peke yake. Nina sababu mbili kuu zilizonipelekea kuunga mkono wazo la maaskofu hao. 

Kwanza, kwa vile vyombo vingi vya habari humu nchini, aidha, vinamilikiwa na kusimamiwa na Wakristo basi kama vyombo hivyo vitalijadili jambo hilo, kuna kila aina ya uwezekano wa kuupendelea Ukristo kuliko Uislamu na kusababisha jambo hilo lionekane halifai. 

Pili, kama jambo hilo litapelekwa Bungeni, basi pia, kwa vile Wabunge wengi wa mabunge yote yaliyopita, katika nchi hii, wamekuwa ni Wakristo, bila ya shaka yo yote, watatumia jazba na ukereketwa wao kukwamisha mswada huo, kama walivyojaribu katika Bunge lililomaliza muda wake hivi karibuni, kupinga suala la wanafunzi wa kike katika mashule kuvaa sare zinazoendana na maadili ya dini zao! 

Na wakati watu wanakatazwa wasichanganye dini na siasa, kuna ushahidi kuthibitisha kuwa, Wakristo, kwa kupitia katika vitengo vyao vya kanisa, wamekuwa wakiandaa mikakati ya makusudi kuhamasishana wagombee nafasi za ubunge. 

Kuthibitisha hayo, Padre wa Kikatoliki, Dkt. John C. Sivalon, katika kitabu chake alichokiita "KANISA KATOLIKI NA SIASA YA TANZANIA BARA -1953 HADI 1985" ameeleza; "Mwishowe, SSY ilitoa msisitizo juu ya jukumu la walei katika jamii. Haya yalitokea wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 1970. 

Dkt. Sivalon akaendelea kusema, "Ingawa hakuna utafiti uliofanywa kuonyesha uhusiano kati ya SSY na wabunge waliochaguliwa, mmoja kati ya watu waliohojiwa alidaikuwa: SSY na Baraza vimeleta msisimko huu ambao umewaamsha Wakatoliki kupigania viti katika uchaguzi wa Wabunge na mimi nikiwa mmoja wao." 

Padre huyo anaendelea kusema, "Baadaye huko Bungeni tulifanya utafiti usio rasmi na kugundua kwamba asilimia 75 ya waliochaguliwa walikuwa Wakristo, na kati ya hao asilimia 70 walikuwa Wakatoliki"(Uk.49). 

Kwa hali hiyo, kama vyombo vya habari vya humu nchini pamoja na Bunge la nchi hii vitaachiwa vijadili juu ya suala hili, kwamba Tanzania ijiunge na OIC au isijiunge, tujue kuwa Wakristo waliomo katika vyombo hivyo, watatumia wingi wao kupinga serikali isiwe na uhusiano na taasisi hiyo! 

Lakini kama suala hilo wataachiwa Watanzania walipigie kura ya maoni, ni wazi kuwa wengi wataliunga mkono kwa sababu katika nchi hii Waislamu ni wengi kuliko Wakristo, ingawa baadhi ya waandishi wa Kikristo wamekuwa wakijaribu sana kuipindua sura hiyo ili kuonesha kuwa Wakristo ndio wengi kuliko Waislamu! 

Ndugu Mohamed Said, mwandishi wa kitabu, "The Life and Times of Abdulwahid Sykes", akieleza juu ya suala hilo amesema, "D.B. Barret anatoa takwimu zinazoonesha Waislamu ni wachache Tanzania. Idadi ya Waislamu imefanywa ionekane kuwa ni asilimia 26, Wakristo asilimia 45, dini za kienyeji asilimi 28. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey, kwa 1973,zimewaweka Waislamu katika Tanzania juu kidogo ya Wakristo, ni asilimia 40,Wakristo asilimia 38.9 na dini za kienyeji asilimia 21.1. Lakini kwa mujibu (wa Kitabu) "Africa South of the Sahara", Waislamu katika Tanzania wanaongoza kwa wingi, ni asilimia 60. Idadi hii imebaki hivyo hivyo katika matoleo yake yote tokea 1982." 

Kwa kuwa haikufanywa sensa ya makusudi ya kutaka kuelewa idadi ya Waislamu na Wakristo katika Tanzania, basi ni vyema tukafuata ushauri na Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste, kuendesha kura ya maoni siyo kwa suala la kujiunga na OIC tu, bali pia na suala la uhusiano na Vatikano, kama hatukuja kushitukia OIC inakubalika na Vatikano inakataliwa, hapo ndipo tutakapoelewa wepi ni wengi Tanzania, ni Waislamu au Wakristo? 

Na kwa nini tufikishane mpaka kwenye kuandaa kura ya maoni? Kwa nini tuvutane? Jambo liko wazi na kigezo tunacho! Ikiwa muasisi wa Taifa hilo, Hayati Mwalimu Nyerere, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuanzisha uhusiano wa kibalozi baina ya serikali yake na taasisi ya kidini ya kanisa Katoliki duniani, Vatikano, vipi sisi, tunaojifanya tunafuata nyayo za kiongozi huyo, na kudai kuwa tunayaenzi mema yake, tupinge serikali kujiunga na taasisi ya kidini ya OIC? Au ni kwa sababu mtazamo chongo umetulevya mpaka tukaona uhusiano na taasisi ya Kikristo ni sawa lakini uhusiano na taasisi ya Kiilslamu ni dhambi? Kwa nini hatufunui macho yote mawili tukaona sawasawa? 

Ama swali la kutaka kuwasilimisha Watanzania bila ya ridhaa yao, hilo halipo, kwa sababu Kur'ani Tukufu inasema, "Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia)katika dini, uongofu umekwisha pambanuka na upotofu" (Al-Baqarah 2:256). Kwa hivyo si sawa kutumia jazba katika kuangalia mambo ya dini. 

Aidha, misaada inayotolewa na OIC si ya kidini na wala haina lengo la kuwaingiza watu katika uislamu. Kama taasisi ya kidini inapotoa misaada huwa lengo lake ni kuwavuta watu waingie katika dini hiyo basi na misaada inayotolewa na Vatikano, kwa kupitia kanisa Katoliki nayo itakuwa inalenga kuwaingiza Watanzania katika Ukristo. Kanisa Katoliki limejenga shule, zahanati na hospitali na zinatumiwa na Watanzania wote bila ya kujali tofauti zao za kidini, jee kanisa hilo nalo nia yake ni kuwabatiza wanaopata huduma hizo? 

OIC inatoa misaada ya kijamii tu. Inajenga mashule, mahospitali, barabara, madaraja na mfano wa hayo, kwa ajili ya faida ya jamii nzima na siyokuwa Waislamu tu. Misaada hiyo haitolewi kwa vikudni binafsi, inatolewa kwa nchi nzima, ndiyo maana taasisi hiyo ikataka nchi inayotaka ifaidike na misaada hiyo ijiunge na taasisi hiyo. 

Uganda na Mozambique si nchi za Kiislamu, na wala hazina Waislamu wengi; lakini serikali za nchi hizo zimejiunga na OIC na zinafaidika na misaada inayotolewa na taasisi hiyo, bila ya kulazimishwa nchi hizo kufuata imani ya Kiislamu. Chuki za kuuchukia Uislamu zisiwe ndiyo sababu ya kutowatendea uadilifu Waislamu. 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tume, kauli ipi sawa? 

CCM maji shingoni 

Wazanzibar wawaambia Dk. Omar na Karume:
Kura tutawanyima, mtang’oka 

CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea 

Kabobe asisitiza uchaguzi huru 

Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa 

Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa 

Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta 

HABARI ZA KIMATAIFA

USHAURI NASAHA
Haya ndiyo mambo ya wanawake - 2 

MAKALA
Kura ni silaha 

Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo 

MPASHO NASAHA
BEN NA BULLY 

MAKALA
Wimbo wa Umoja na Amani wa CCM  ni ghilba za kisiasa 

KALAMU YA MWANDISHI
Hojini Ubalozi wa Vatican kwanza 

MAKALA
CCM kushinda uchaguzi bila kupigiwa kura? 

MAKALA
Mwenye macho haambiwi tazama - 4 

CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa 

Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa 

Wazee waijibu CCM 

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga watakiona - Kajumulo
  • Simba yajaribu kombe la FAT
  • Tarimba akataa ubabe
  • Jeshi laongeza timu Ligi Kuu

  •  

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita