|
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000 |
|
|
|
|
|
Wimbo wa Umoja na Amani wa CCM ni ghilba za kisiasa Na Rajab Kanyama UMOJA, amani na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanganyika ulikuwepo kabla, na hata wakati nchi ilipokuwa chini ya uangalizi wa Serikali ya Uingereza. Umoja uliokuwepo, ulikuwa na shabaha maalum zilizohusiana na haja iliyokuwepo wakati ule, ambayo ilikuwa ni nia ya kujikomboa kutoka katika 'kongwa' za kutawaliwa. Kuwepo kwa haja hiyo, ndiko kuliko zaa chama cha TANU, kwa lengo la kuikomboa nchi. Wakati huo, hapakuwepo na ubaguzi wa kidini, wala wa kikabila, japokuwa kulikuwepo na kundi kubwa la baadhi ya wananchi ambao kwa sababu ya kutaka kulinda maslahi yao binafsi, hasa ajira katika serikali ya mkoloni, hawakushiriki kikamilifu katika harakati za kuleta uhuru. Hawa hawakutengwa, lakini walisamehewa kwa vile ilifahamika wazi kwamba, hata wao pia walipenda nchi ijikomboe kutoka katika makucha ya madhalimu. Kwa kuundwa chama cha TANU, malengo ya muda mrefu na dhana ya umoja iliainishwa upya na kuwa na maana pana zaidi, ambapo nia ya kutaka kujikomboa kisiasa ikaheshimiwa kuliko tofauti na hitilafu zilizokuwepo katika jamii. Hitilafu katika mtazamo, hapa ni dini na kabila za wananchi, na kwa kuthibitisha hilo, uongozi wa juu wa chama cha kudai uhuru akapewa Mkristo, Hayati J.K. Nyerere. Tungependa jambo hili lieleweke vizuri, maana mara baada ya uhuru kupatikana, kukazushwa fikra mpya, tena potofu ya kutaka kutenganisha nguvu iliyoleta uhuru ya waumini wa dini ya Kiislam na shughuli za kisiasa za undeshaji wa nchi. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, jambo hilo ndio ilikuwa mwanzo wa njama dhidi ya kundi fulani la wananchi. Waasisi wa fikra hiyo wakatangaza kwamba, dini na siasa visichanganywe kwa madai kuwa eti, kwa kufanya hivyo, umoja, amani na utulivu vitatoweka. Ukweli ni kwamba uhuru ulidaiwa kwa nguvu zote ili kuondoa tabaka lililokuwa linajengwa na wakoloni, kwa misingi ya kidini, ukatupwa kapuni. Mfumo wa siasa, wakati huo siasa ya ujamaa na kujitegemea ukatangazwa kuwa ni imani yenye uwezo wa kipekee wa kuweza kutupatia ufumbuzi wa matatizo ya kijamii yaliyokuwa yanatukabili nchini wakati huo, yaani ujinga, umaskini na maradhi. Kwa vile hapakuwepo na dhamira ya kweli ya kuondoa matatizo hayo, ujamaa na kujitegemea umekufa, bila ya kuleta mabadiliko yoyote. Hali ya kuendelea kukua kwa tabaka la waliopata elimu katika shule za misheni, na wale ambao hawakuipata elimu hiyo kwa kuogopa kubatizwa, iliyosababishwa na utawala wa Kikoloni, ikaachwa iendelee. Jambo hilo likakuza ile dhana ya kuwepo kwa wananchi watawala na wananchi wengine wakabaki kuwa ni wa kutawaliwa. Wimbo wa amani na utulivu ndani ya nchi imegeuka na kuwa hila na ghilba ya kuficha ukweli wa kuwepo 'mataifa mawili', ndani ya nchi moja. 'Taifa la wananchi bora' wenye haki ya kutawala, na wengine kusema na kutoa matamko wayatakayo dhidi ya serikali, bila ya hofu yoyote. Hawa wana uwezo wa kutoa maelekezo, na serikali ikalazimika kuyafanyia kazi. Taifa jingine ni la wananchi wanyonge, ambao mpaka leo hii bado wanaendelea kunyimwa nafasi za uongozi ndani ya nchi, kwa visingizio vya kutokuwa na elimu ya kutosha. Hawa hawaruhusiwi kuongoza au hata kujiunga na vyama vya siasa, maana wasije wakapata nafasi ya kuongoza nchi, jambo ambalo halitakiwi. Wakijiunga na chama cha siasa, chama hicho kitatupiwa kila aina ya lawama kwa lengo la kukipaka matope ili kisikubalike na waumini wa dini nyingine. Kimsingi, lengo kuu ni lile lile, la kutaka kuwazuia wasishike hatamu ya kuongoza nchi, japokuwa ushahidi unaonyesha kwamba, hawa wasiotakiwa kuongoza ndio hasa wenye uwezo wa kuleta ustawi ndani ya nchi pindi wanapokuwa madarakani. Kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Awamu ya Pili, ni ushahidi tuliokusudia katika nukta iliyotangulia. Wananchi katika tabaka hili ndio hasa wanaohitaji mabadiliko ya uongozi wa kisiasa nchini, kwa lengo la kuondoa kasoro hii kubwa ambayo ni 'Bomu' linaloweza kulipuka wakati wowote na kuisambaratisha nchi. Kupuuza ukweli huu, ni kufilisika kifikra, na kuukataa ukweli wa Kihistoria katika nyendo za mabadiliko ya kijamii. Ni jambo lililowazi kwamba, dhana ya umoja, amani na utulivu na hata demokrasia yenyewe, ni vitu vinavyoweza kuainishwa, au kupindwa na tabaka tawala, pamoja na wafuasi wengine ambao ni watetezi wa mfumo fulani wa utawala ambao kwa kawaida huwa si rasmi, ili muradi tu waendelee kuhalalisha matendo na misimamo ambayo kwa hakika hunufaisha wachache, badala ya taifa. Matatizo huanza kujitokeza pale taifa teule linapotaka kuendelea kujizatiti katika kuhodhi madaraka ya kuendesha nchi. Kimantiki, ainisho la kuwepo kwa amani na utulivu, ni ile hali ya kutokuwepo kwa vita kati ya nchi na nchi, au vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi. Lakini amani, utulivu na umoja wa kitaifa utadumu kwa muda gani, wakati wananchi wanakufa kwa njaa sehemu moja ya nchi, na sehemu nyingine ya nchi vyakula vinaoza kwa kukosa soko? Amani, utulivu na umoja wa kitaifa utadumu kwa muda gani, wakati ufa kati ya walionacho na wasio nacho unazidi kuongezeka? Wananchi, ni jukumu letu sasa kupigia kura sera na mipango ya kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, zinazopendekezwa na vyama vya siasa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba 2000, ili tuachane na kundi la wahafidhina waliokaa madarakani miaka nenda miaka rudi, kwa ghilba na hila mbali mbali, kwa lengo la kulinda maslahi ya kundi la wateule, ambao wamejenga dhana kuwa ni waotundio wanaopasa kutawala nchi hii. Wananchi, safari hii tuchague chama ambacho kina viongozi wanaoweza kutuondolea matatizo ya kiuchmi yanayoikabili nchi yetu badala ya hawa wapiga porojo kwenye majukwaa ya kisiasa wakisaidiwa na akina Mtopea. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wazanzibar
wawaambia Dk. Omar na Karume:
CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea Kabobe asisitiza uchaguzi huru Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta USHAURI NASAHA
MAKALA
Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo MPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MAKALA
CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa |
|
|
|
|