|
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000 |
|
|
|
|
|
CCM kushinda uchaguzi bila kupigiwa kura? Na Francis John Pale palipo na demokrasia ya kweli, unapofika uchaguzi mkuu utakaovishirikisha vyama vingi vya siasa, kila chama katika hivyo hutarajiwa kwamba na kutegemea kupewa kura na wananchi ili kupata ridhaa ya kuwaongoza wananchi hao. Ni muhari chama fulani kitarajie na pengine kijihakikishie kutwaa madaraka pasipo kupigwa kura na wananchi. Ikitokezea chama kimetwaa madaraka ya nchi hali ya kuwa hakikupigiwa kura na wananchi basi lolote katika haya yafuatayo huenda yalitokea. Aidha chama hicho kimepora kura za wananchi kwa kufanya ulaghai katika zoezi la upigaji kura, au chama hicho kimeipindua serikali iliyoundwa na chama kingine kilichoshinda uchaguzi kwa kupewa kura na wananchi. Vyovyote iwavyo, chama kuiongoza nchi bila ridhaa ya wapiga kura ni jambo la hatari sana. Hivi karibuni, kiongozi mmoja wa ngazi za juu serikalini ambaye pia ni mwana-CCM amewaambia wananchi ambao ni wapiga kura kwamba hata wasipopigia kura CCM, bado chama chake kitashinda! Mwana-CCM huyo ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Omar Juma, na mgombea mwenza wa kiti cha Urais wa Jamhuri katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu. Dk. Omari aliripotiwa na vyombo vya habari kutoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi Kisiwani Pemba katika moja ya mikutano ya Kampeni ya chama chake, CCM. Kauli hiyo ya kigogo wa CCM si jambo dogo; siyo kauli ya kupigiwa makofi au hata kukaliwa kimya tu. Kama walivyosema wananchi katika maoni yao, hivi ni kweli CCM imefikia mahali haihitaji ridhaa yetu wananchi kuiongoza nchi hii? CCM inapata wapi jeuri ya kujigamba kwamba sisi wananchi tutake tusitake CCM itashinda uchaguzi? Je CCM inatutaka wananchi tuamini kwamba imejiandaa kuwahujumu wagombea toka kambi ya upinzani au imejiandaa kulihujumu zoezi zima la uchaguzi? Historia inatuonesha wana-CCM wana'utamaduni' wa kuhujumiana wao kwa wao. Zoezi la kura za maoni lililofanyika miezi michache iliyopita kuwapata wagombea wa udiwani na ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu, lilitawaliwa hujuma mbali mbali ikiwemo hongo na vurugu. Hali iliyopelekea kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kutengua matokeo katika baadhi ya majimbo na kuwapiga marufuku baadhi ya wana-CCM kushiriki tena kuomba kugombea nafasi kwa kuhusishwa na hujuma hizo. Lakini utamaduni huu wa Wana-CCM kuhujumiana wao kwa wao umeanza hata kabla ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa nchini 1992. Katika chaguzi kuu zilizowahi kufanyika kabla ya hapo, malalamiko na hatimaye kesi ziliwahi kufunguliwa mahakamani ambapo mwana-CCM mmoja alikuwa akimtuhumu mwana-CCM aliyeshindwa katika uchaguzi husika kuwa "alimchezea rafu'. Sasa basi, ikiwa CCM wanahujumiana wao kwa wao hali ya kuwa katiba yao ni moja, ilani yao ya uchaguzi na moja na sera zao ni hizo hizo, ni vipi watashindwa kuwahujumu wagombea toka kambi ya upinzani na vyama vyao kwa pamoja? Tayari kengele ya tahadhari imekwisha sikika; CCM wamekuwa ni watu wa kuporomosha tuhuma nzito na matusi mazito yakiwemo ya nguoni ambayo, kwa heshima na hadhi ya gazeti hili, NASAHA, hatuthubutu kuyanukuu. Hata hivyo, tunaamini tahadhari mahususi zikichukuliwa, nchi yetu inaweza kunusurika na safari yetu kuelekea uchaguzi mkuu na hali ya baada ya hapo, ikawa ni salama na amani. Tahadhari ya kwanza ni kwa CCM wenyewe. Kwa mwendo huu, wana-CCM imeipeleka nchi pabaya. Inashangaza, kwa sababu ni ninyi CCM hao hao ambao mmekuwa mkipaza sauti kuepuka mambo ambayo yanaweza kutumbukiza nchi yetu katika maafa makubwa kama yale ya Rwanda, Burundi au Somalia, lakini leo CCM ndio ipo mstari wa mbele kutupeleka huko. Jambo linalofaa ni CCM iwaachie Watanzania huru wapiga kura waonavyo wao. Ikiwa wapiga kura wataiambia CCM"sasa BASI"CCM iheshimu na iondoke salama salimini. Au kuna dhambi gani kubwa CCM imewafanyia Watanzania kiasi kwamba inaongopa chama kingine kikitwaa serikali vigogo wa CCM watakuwa matatani? |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wazanzibar
wawaambia Dk. Omar na Karume:
CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea Kabobe asisitiza uchaguzi huru Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta USHAURI NASAHA
MAKALA
Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo MPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MAKALA
CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa |
|
|
|
|