NASAHA
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
USHAURI NASAHA

Haya ndiyo mambo ya wanawake - 2 

Na Khadijah M. Idd 

NAKUMBUKA nilipokuwa darasani siku moja, takriban miaka kumi iliyopita, enzi hizo sera za ubaguzi wa rangi zilikuwa zinaendelea katika nchi mbalimbali duniani. Somo la siku hiyo lilikuwa ni mchango wa Malcolm X katika harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi. Mmarekani huyu mweusi alikuwa anapinga ubaguzi wa rangi uliokuwa unafanywa na Wamarekani weupe dhidi yao. Yeye na wanaharakati wenzake wa Nation of Islam walikuwa wanapinga ubaguzi huu na wakati huo huo wakiwachukia na kuwabagua wazungu. 

Baada ya kwenda Hijja, Makka na kujionea usawa na mapenzi yaliyoko baina ya weupe na weusi Malxolm X, aliamua kubadili njia yake ya kupinga ubaguzi. Aliwafundisha wenzake kwamba weusi na weupe ni watu sawa na vile vile aliwahimiza Wamarekani weusi kuwapenda Wazungu ili kupiga vita ubaguzi. Hata hivyo baadhi ya Wazungu na weusi hawakupendezwa na hili.Chama zikapangwa kumuua. 

Nakumbuka pia historia ya harakati za wanawake Ulaya ambapo katika siku zake za mwanzo wanawake waliamua kufanya kazi zile zilizokuwa zinashikiliwa na wanaume. Pamoja na hili wanawake hawa waliamua kuvaa suti kama za wanaume na kuacha magauni marefu yaliyozoeleka. Hata hivyo baadaye waliona kuwa usawa kati ya wanawake na wanaume hauna maana ya kuvaa kama wanaume, suti ya wanawake ikawa na sketi badala ya suruali. 

Wakati nayakumbuka haya yote naziangalia harakati za wanawake hususani katika kuingia katika siasa, nasikiliza yasemwayo kupitia hii Runinga yangu. Nashikwa na butwaa kwa muda, hata hivyo nazinduka na kukumbuka kuwa ni mambo ya wanawake, ofisi zimezidi wingi! 

Kiongozi huyu wa NGO moja anasema kwamba wanawake wawapigie kura wanawake wenzao! Ama! Na kwamba wanawake wanashindwa katika siasa kwasbabu wanawake wenzao wanawapigia kura wanaume! Lengo la wanawake kuingia katika siasa ni kuinua hadhi yao na kuondoa hali iliyopo ya kuona wanawake ni watu duni. Wanawake kama raia wana haki kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. 

Tatizo ninaliona hapa ni hili, je na wanaume wakiamua kusema kwamba wanaume wawapigie kura wanaume wenzao, vijana wawachague vijana wenzao kwa sababu kwa muda mrefu siasa ya nchi hii imekaliwa na wazee! Wasomi wawachague wasomi wenzao kwani wao ndio wanaojua umuhimu wa elimu, n.k!. Itakuwaje?. Hapa nakumbuka harakati za Wamarekani weusi kupinga ubaguzi huku wenyewe wakifanya ubaguzi. Hivi hili jahazi la wanawake litatembea umbali gani kabla yakupinduka. 

Kama hivi ndivyo,je wanawake hawa wana wapiga kura wangapi wanaowategemea. Kwa kuangalia haraka haraka utaona kuwa wanaopiga kura wengi wako mijini, wananchi walioko vijijini mwamko wa siasa ni mdogo, lakini wananchi wengi wako huko. Kwa kifupi, wanawake hawa wana watu wachache tu, yaani wanawake wa mijini, wa kupigia kura. Pamoja na hili wanawake hawa wamegawanyika katika makundi mengine mengi kama vile vyama, kabila, ujirani, undugu n.k. 

Tukizingatia mtazamo wa jamii juu ya wanawake, nafasi na majukumu yao, uwezo wao kifedha, ugeni wao katika siasa ni dhahiri kwamba wanawake hawa hawatashinda iwapo wanategemea kura za wanawake wenzao tu. 

Jambo la pili ni kwamba ikiwa tunaingia katika siasa ili kupinga ubaguzi na uonevu unaofanywa dhidi yetu, inakuwaje basi na sisi tunatangaza sera za ubaguzi? Wanaume nao wakiamua kutopigia kura wanawake, hali itakuwaje. Ikiwa tunatangaza sera za namna hii halafu kwa bahati tunashinda, tunawaambiaje wananchi? Kwamba huduma zetu zitaelekezwa kwa wanawake tu? Baada ya miaka kumi hali ya maisha katika jamii na familia itakuwaje? Kwa hakika wanaume wote watakuwa duni, maskini, wanaonyanyaswa, na kwa ujumla watakuwa na kila udhaifu na umaskini walio nao wanawake sasa hivi. Lakini, hivi hizi ndizo sera zenyewe?! 

Wanawake na viongozi wa vikundi vya wanawake wana kazi kubwa ya kufanya. Tuwaambie wapiga kura wetu kwa nini watupigie kura. Hao wanawake tunaotaka watuchague tu waelimishwe kwanza juu ya sera zetu na sababu za msingi kwa nini sisi tuchaguliwe na si wale wengine. Ninaamini kuwa kwetu wanawake hakutoshi kuthibitisha kwa nini tuchaguliwe. Sababu hizi zitafanya kazi hata pale ambapo kuna wagombea wawili au zaidi wanawake, wanaogombea nafasi moja. Hali ikiwa hivi mpiga kura haangalii mwanamke au mwanamume bali nani ana sera zenye mashiko na hoja zinazothibitika. 

Wanawake kama kundi kubwa na lenye matatizo mengi katika jamii linahitaji mtu anayelielewa, kulionea huruma, na kulijali. Matatizo kama ya shida ya maji, kutokuwa karibu na huduma za afya hususan za mama na mtoto, elimu duni, uhaba wa vitendea kazi n.k. yanahitaji kiongozi mtendaji. Wagombea wanawake waseme watasaidiaje wanawake wenzao katika hili. Na kwa hakika kuwa mwanamke tu hakutoshi, kundi hili linahitaji zaidi ya hapo. 

Wanawake kama raia na binadamu kama walivyo wanaume, hawahitaji upendeleo, kwamba kwa vile ni wanawake na viongozi wanawakeni wachache, basi tuwachague, la hasha! Wanawake wana uwezo wa kutenda na kuathiri sehemu kubwa ya wanajamii kwa muda mfupi. Usemi wa "ukimuelimisha mwanamke mmoja...." Uko wazi na unaeleweka na hao "wana-gender" . Lakini inashangaza wanapowaambia wanawake wawachague wanawake wenzao. Jimbo la uchaguzi halitaendelea kwa vile tu mbunge ni mwanamke, lakini litafanya hivyo kwa kuwa na kiongozi bora. Wanaharakati na wagombea wanawake wawaelimishe wapiga kura ubora na ujuzi walionao na si kuomba kama mtoto aombavyo peremende. Wawaelimishe wapiga kura uwezo waona sera zao na si kuwakumbusha kwamba wao ni wanawake. Hili wanalijua sana. 

Kampeni za siasa zinataka sera zinazomsaidia kila mtu bila kubagua. Kama ambavyo sisi hatupendi kubaguliwa, na sisi tusibague. 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tume, kauli ipi sawa? 

CCM maji shingoni 

Wazanzibar wawaambia Dk. Omar na Karume:
Kura tutawanyima, mtang’oka 

CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea 

Kabobe asisitiza uchaguzi huru 

Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa 

Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa 

Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta 

HABARI ZA KIMATAIFA

USHAURI NASAHA
Haya ndiyo mambo ya wanawake - 2 

MAKALA
Kura ni silaha 

Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo 

MPASHO NASAHA
BEN NA BULLY 

MAKALA
Wimbo wa Umoja na Amani wa CCM  ni ghilba za kisiasa 

KALAMU YA MWANDISHI
Hojini Ubalozi wa Vatican kwanza 

MAKALA
CCM kushinda uchaguzi bila kupigiwa kura? 

MAKALA
Mwenye macho haambiwi tazama - 4 

CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa 

Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa 

Wazee waijibu CCM 

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga watakiona - Kajumulo
  • Simba yajaribu kombe la FAT
  • Tarimba akataa ubabe
  • Jeshi laongeza timu Ligi Kuu

  •  

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita