NASAHA
Na. 065 Jumatano Septemba 13 - 19, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
BARUA 

CCM mtashinda vipi? 

Ndugu Mhariri 

KATIKA kipindi hiki cha kampeni vyama mbalimbali vya kisisaa vyenye usajili wa kudumu vinazunguka sehemu mbalimbali nchini kuomba ridhaa ya wananchi ili vichaguliwe kuongoza nchi. 

Hiki ni kipindi cha kuwashawishi wananchi. Ni kipindi cha kuwabembeleza wapiga kura. 

Ninalonishangaza ni kauli ya Makamu wa Rais, Dr. Omar Ally Juma iliyoripotiwa wiki iliyopita. Ilielezwa kuwa Makamu amewaambia wananchi katika mkutano wake wa hadhara kuwa hata wasipoichagua CCM itashinda tu! 

Sasa watashinda vipi bila kura zetu? Jeuri hii ya kuwakejeli wananchi katika kipindi hiki msingi wake nini? Je ni nani anayetaka kushuhudia sera ya jino kwa jini ambayo imeshatangazwa iwapo uchaguzi utavurugwa ikitekelezwa. 

Wananchi tungependa kuona vyombo husika vikikemea kauli hizi zinazoashiria nia ya kuvuruga uchaguzi. 

Joel Fungo,
Dar es Salaam.


Wananchi kataeni kuishi kwa hofu 

Ndugu Mhariri 

NCHI hii inadaiwa kuwa na amani na utulivu ambao wanasiasa wanaapa kuulinda. 

Lipo jambo moja linalonishangaza huku mitaaani. Wananchi wanaishi kwa hofu. Watu wanalazimika kutundika bender na picha za mgombea ambaye hawamtaki ili tu waweze kuendelea kufanya biashara katika eneo fulani. 

Watu wanalazimika kuishi kwa unafiki ili wasibughudhiwe. Wanaotoa bughudha hizi kwa wale wasio na itikadi sawa nao hawaoni aibu kudai hadharani kuwa tuna amani na utulivu. 

Mimi napenda kutoa mwito kwa wananchi kuwa umefika wakati wa kujipatia uhuru. Itumie kura yako kuchagua chama kitakachosimamia haki sawa kwa wote. Kataeni kuishi kwa hofu katika nchi yenu. 

Alfonce Massawe,
Moshi. 


Huu ndiyo mtazamo wa Diria? 

Ndugu Mhariri 

GAZETI moja litolewalo kila siku kwa lugha ya Kiswahili Na. 00093 toleo la Jumanne ya Septemba 12, limemkariri Balozi Diria alidai kuwa CUF haitaki uchaguzi ufanyike Zanzibar. 

Diria ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amedai kuwa CUF imekata tamaa baada ya kutolewa takwimu za waliojiandikisha kupiga kura na Tume ya Uchaguzi Zanzibar. 

Aliendelea kudai kuwa CUF wanaona watashindwa kwa vile Wapemba waliojiandikisha ni 150,000 tu wakati Waunguja ni watu 300,000. 

Mtazamo huu wa Diria ni wa hatari sana hasa kwa wadhifa alio nao katika CCM. 

Kwanza anaonesha kuwa kura zote za Unguja ni za CCM. Hii ni dhana potofu kwani inaligawa Taifa la Zanzibar. 

Ni kipimo gani anachotumia kujua kuwa Waunguja wote ni CCM? Lazima Tume ya Uchaguzi iwakemee watu hawa wanaotoa vigezo vya ushindi ambavyo vinapotosha. 

Ussi Makame,
Magomeni,
Dar es Salaam.


Amani na utulivu mbwa wa nini?

Ndugu Mhariri 

KATIKA ziara yake hapa nchini hivi karibuni Rais Bill Clinton wa Marekani aliisifia Tanzania kuwa ni nchi yenye kuongoza kwa amani na utulivu barani Afrika. 

Nikikubaliana na Rais huyo wa Marekani, napenda kuhoji je vipi aje na mbwa wake na wainuse gari ya Rais wetu Mkapa, kama maneno yake siyo ya kejeli kwa Watanzania. 

Clinton anajua wazi kuwa kwa umaskini unaoikabili nchi hii ni rahisi kwa hata Rais wetu au wapambe wake kama si raia wake kufanya ugaidi ili wapate malipo ya fedha au mengineyo. Kwa ajili hiyo ndiyo maana hakumwamini hata Rais wetu na watu wa usalama wakaamua kuipekua gari ya Rais wetu kwa kuinusisha mbwa. 

Kweli umaskini ni balaa ni hasa inapokuwa umaskini wa kujitakia kama wa nchi hii, na kwamba kwenye umasikini hapana amani isipokuwa uoga tu. 

Peter Maganga,
Temeke,
Dar es Salaam.


Wazanzibari mtaangamiza Taifa lenu 

Ndugu Mhariri 

CHONDE! Chonde! Ndugu zangu Wazanzibari jinsi hali inavyoelekea ipo dalili za kufuta katika uso wa dunia Taifa la kisiwa maarufu duniani cha Zanzibar. 

Inavyoelekea hali hiyo ya kutisha na kuhuzunisha mno! Itatokana na nyinyi wenyewe kwa kuwaendekeza na kuwaunga mkono hawa viongozi wenu wa sasa ambao wanapata maelekezo yao toka Bara. 

Leo tumefikishwa mahali Rais wenu lazima akapatikane toka Dodoma kwa ridhaa ya Watanganyika! Viongozi wenu hao wa CCM wanafumbwa macho eti kwa vile tu maslahi yao yanalindwa. Wako tayari kushuhudia taifa linadhalilishwa na watu wenye mpango wa kufanya Zanzibar mkoa sawa na mikoa mingine ya Tanzania Bara. 

Nawaomba ndugu zangu wa Zanzibar okoeni taifa lenu na mlipe hadhi kamili inayostahili kama taifa ili muweze kunufaika. 

Iwapo mtashindwa kutekeleza wajibu wenu Oktoba 29, muelewe wazi kwamba, taifa la Zanzibar na umaarufu wake wote litaangamia. 

R.A. Lukwele,
S.L.P. 15202,
Dar es Salaam.
 


Kiapo cha kutotoa na kupokea rushwa kimepotea wapi?

Ndugu Mhariri 

TUMESIKIA au hata kuona toka Madiwani wa CCM mpaka wabunge wao rushwa ikitolewa na kupokelewa. Je, kiapo chao CCM kimekwenda wapi? Au kile kiapo kilikuwa enzi za TANU tu? 

Wakati wa pilika pilika za udiwani, mkubwa mmoja wa CCM katika kujiosha aliwahi kusema kwamba vurugu za rushwa ilisababishwa na Chama cha upinzani na alikitaja ni CUF. 

Sasa namuuliza Mheshimiwa, je, na hizo vurugu za wabunge Tanzania nzima mchawi nani? Udiwani ulidai CUF wametowa milioni nani (8), Mheshimiwa, je, na ubunge milioni ngapi za CUF iligawa kwa waheshimiwa hao Tanzania nzima? Uongo una mwisho. 

Mwaka 2000 ni ukombozi tu. 

Mohamed Mlawa,
Dar es Salaam. 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Tume, kauli ipi sawa? 

CCM maji shingoni 

Wazanzibar wawaambia Dk. Omar na Karume:
Kura tutawanyima, mtang’oka 

CCM ni nguruwe aliyenona - Mtopea 

Kabobe asisitiza uchaguzi huru 

Mkapa aomba kura kwa hoja ya uzawa 

Vifaa vya uchaguzi vimeanza kusambazwa 

Mizengwe yatupwa,wagombea upinzani wapeta 

HABARI ZA KIMATAIFA

USHAURI NASAHA
Haya ndiyo mambo ya wanawake - 2 

MAKALA
Kura ni silaha 

Kampeni za uchaguzi Zanzibar zimetosha kumvua chui ngozi ya mwana kondoo 

MPASHO NASAHA
BEN NA BULLY 

MAKALA
Wimbo wa Umoja na Amani wa CCM  ni ghilba za kisiasa 

KALAMU YA MWANDISHI
Hojini Ubalozi wa Vatican kwanza 

MAKALA
CCM kushinda uchaguzi bila kupigiwa kura? 

MAKALA
Mwenye macho haambiwi tazama - 4 

CUF Tanga wamsihi Mufti wa BAKWATA aachane na siasa 

Kodi ya Maendeleo haitaondolewa -Mkapa 

Wazee waijibu CCM 

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga watakiona - Kajumulo
  • Simba yajaribu kombe la FAT
  • Tarimba akataa ubabe
  • Jeshi laongeza timu Ligi Kuu

  •  

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita