AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kuiweka Modem kwenye Kompyuta
 
Na Hassan Omar
 
 

Modem (MODulator-DEModulator) kimekuwa ni kifaa muhimu sana katika zama hizi tulizonazo za maendeleo makubwa sana katika nyanja mbali mbali za mawasiliano. Kuibuka kwa utando wa Intaneti (Internet) kumeongeza sana haja ya mtu kuwa na modem kuweza kuunganisha kompyuta yake na utando huo maarufu wa mawasiliano ya kompyuta. Hapa chini tutajifunza namna ya kuiweka modem kwenye kompyuta yako inayotumia Windows 95 ( au Windows 98). 

 

Kuiweka Modem ya Nje 

Kama modem yako ni modem ya nje (external modem) utahitaji kuwa na waya wa modem (modem cable), wa kuunganishia modem hiyo na kompyuta. Waya huo pia unajuilikana kama RS-232 serial cable. Ukitaka kujua waya utakao kufaa, kwanza angalia nyuma ya kompyuta yako. 

Kikawaida, kuna soketi mbili ambazo zina visumari ama tisa (9) au ishirini na tano (25). Soketi yenye visumari tisa, mara nyingi huwa ni serial port inayojuilikana kama communications port 1 (COM1). Serial port hii hutumiwa kuchomekewa na mouse. Soketi ya visumari ishirini na tano, mara nyingi huwa ni serial port inayojuilikana kama communications port 2 (COM2) na hiyo ndiyo utakayochomeka ncha moja ya waya wa modem. Lakini mara nyengine COM1 na COM2 zote soketi zake huwa na visumari tisa, kwa hivyo utahitaji waya wa modem ambao ncha yake moja ina plagi yenye tundu tisa badala ya tundu ishirini na tano. 

Waya wa modem una plagi mbili. Plagi moja ina ama tundu tisa, kama ni ya aina ya DB-9, au tundu ishirini na tano, kama ni ya aina ya DB-25. Plagi hii ni ya kuchomekwa kwenye serial port ya kompyuta. Plagi yenye tundu husemekana kama ni ya kike (Female) na plagi yenye visumari husemwa kuwa ni ya kiume (Male). Plagi iliyo kwenye ncha ya pili ya waya wa modem mara nyingi (kama sio zote), huwa ni ya kiume (Male), na huwa ama na visumari tisa, kama ni ya aina ya DB-9, au visumari ishirini na tano, kama ni ya aina ya DB-25. 

Kwa hivyo unaponunua waya kwa madhumuni ya kuutumia pamoja na modem yako, kwanza angalia soketi iliyo kwenye serial port ya kompyuta yako unapokusudia kuichomeka modem, na pia soketi iliyo kwenye modem yako. Kama soketi ya serial port ina visumari ishirini na tano, na soketi ya modem ina tundu ishirini na tano, basi utahitaji waya wa modem wa aina ya DB-25 Female/DB-25 Male kama unavyoonekana kwenye Picha 1. Kama soketi ya serial port ina visumari tisa, na soketi ya modem ina tundu ishirini na tano, basi utahitaji waya wa modem wa aina ya DB-9 Female/DB-25 Male kama unavyoonekana kwenye Picha 2. 
 
Picha 1: Waya wa DB-25 Female/DB-25 Male 

Picha 2: Waya wa DB-9 Female/DB-25 Male 

Tumia mfano huo hapo juu kuchagua waya wa modem unaofaa kwa soketi za aina nyengine. Ukishaupata waya unaofaa, utahitaji kuuchomeka kwenye modem na kwenye serial port ya kompyuta yako. 

Kila modem ya nje pia huja pamoja na "power adapter" ya kuipatia umeme modem hiyo. Hatua inayofuatia ni kuichomeka power adapter hiyo kwenye soketi ya umeme na kwenye sehemu ya kuchomeka waya wa umeme iliyo kwenye modem. Iwashe modem yako kwa kutumia swichi yake. 

Ukinunua modem pia unapatiwa waya wa simu (telephone cord). Chomeka ncha moja ya waya huo wa simu kwenye soketi iliyoandikwa TELCO au LINE iliyo nyuma ya modem, na ncha nyengine ichomeke kwenye soketi ya simu iliyo ukutani ili kuiunganisha na line ya simu yako. Unaweza kuichomeka simu yako kwenye sehemu iliyoandikwa PHONE iliyo nyuma ya modem yako. Ukifanya hivyo utaweza kuitumia line ya simu yako kwa modem na pia kwa simu ya kawaida. Ikiwa huitumii modem, mtu akikupigia simu itapokelewa na simu yako ya kawaida, lakini wakati ukiitumia modem kuunganisha kompyuta yako na kompyuta nyengine, mtu akikupigia simu atapata BUSY signal, yaani ataona kuwa simu yako inazungumza. Wakati kompyuta umeiwasha tu na kuitumia kwa kazi zako zisizohitaji modem (kwa mfano kutumia MS Word), simu yako ya kawaida itaweza kupokea simu zinazopigwa bila ya matatizo yoyote. 

  

Kuunganisha Modem ya Ndani 

Kama modem yako ni modem ya ndani (yaani inayohitaji kuchomekwa ndani ya kompyuta), utakuwa na mambo mengi zaidi ya kuyafanya. Lakini utakuwa na bahati kama modem yako ina sifa ya kuwa "Plug and Play" ambayo pia huandikwa "Plug-n-Play" au "PnP" kwa ufupi. Modem nyingi za siku hizi ni za PnP. Kifaa ambacho ni Plug and Play kinatambuliwa kirahisi na kompyuta na wewe hutahitajika kufanya chochote cha ziada. Lakini mara nyengine Plug and Play haisaidii sana na ndio maana watu wanaifanyia utani kwa kuiita "Plug and PRAY" – yaani kichomeke kifaa chako na uombe Mungu kifanye kazi vizuri! Kuendeleza utani, PnP unaweza kuiita, "Pwagu na Pwaguzi"! 

Kama modem yako ni ya PnP, hakikisha kuwa "jumpers" zote (kama zipo) zilizo kwenye modem hiyo, za kuchagua communications (COM) port na interrupt request (IRQ), zote zimechomolewa. Hatua hii inahitajika kwa modem nyingi za namna hiyo lakini kwa maelezo zaidi soma manual ya modem yako. 

Kama modem yako si ya PnP, kabla hujaanza hatua za kuiweka modem yako ndani ya kompyuta, kwenye Windows 95, bonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Modems -> Diagnostics, na uangalie COM ports zote ambazo tayari zinatumika. Mara nyingi utakuta COM1 tayari inatumiwa na mouse. COM1 na COM3 zote zinatumia interrupt moja ambayo ni IRQ4. Kama COM1 tayari inatumiwa na mouse, huwezi kuiweka modem kwenye COM3 kwa vile kutakuwa na mgongano wa IRQ kati ya modem na mouse. Kwa mfano huo unaweza kuiweka modem kwenye COM2 au COM4 ambazo zote zinatumia IRQ3. Ukiamua kutumia COM2, utahitaji kuchomeka jumpers kwa mujibu wa maelezo yaliyo kwenye manual ya modem hiyo ili kuchagua COM2 na IRQ3. 

Ukishachomeka jumpers kuchagua COM port na IRQ, hatua inayofuatia ni kuhakikisha kuwa kompyuta yako imezimwa, kisha chomoa vifaa vyote vilivyoungwa kwenye kompyuta hiyo isipokuwa mouse na keyboard. Hii ni kuepusha uharibifu ambao unaweza kutokezea kama utafanya makosa yoyote. 

Ifungue kompyuta yako na uichomeke modem yako kwenye upenyo (slot) wa motherboard ulio mtupu, kama inavyoonekana kwenye Picha 3. Ifunge msumari wake vizuri na kisha ifunike kompyuta kama ilivyokuwa. 

 Picha 3: Kuchomeka modem ndani ya kompyuta. 

 

  

Chomeka ncha moja ya waya wa simu (telephone cord) kwenye soketi iliyoandikwa TELCO au LINE iliyo nyuma ya modem. Ncha nyengine ya waya huo ichomeke kwenye soketi ya simu iliyo ukutani. 

Iwashe kompyuta yako kama kawaida. Kama kompyuta yako ina PnP BIOS, yaani uwezo wa kutambua vifaa vya PnP, ikiwashwa tu itaelewa kuwa imechomekewa modem mpya ya PnP na itaichagulia COM port na IRQ zilizokuwa hazitumiwi na kifaa chochote. Lakini kama BIOS sio ya PnP au/na modem sio ya PnP, itabidi uiambie kompyuta kutenga, kwa mfano COM2 na IRQ3, kwa ajili ya matumizi ya modem. 

Hatua ya kwanza ya kufanya hivyo tumeshaizungumza hapo juu tulipoelezea jinsi ya kuzichomeka jumpers za modem kuchagua COM port na IRQ. Katika hatua ya pili, kwa kompyuta za zamani kidogo zinazotumia kadi za I/O (Input/Output cards au pia inaitwa Input/Output controller), utapaswa kuilemaza (disable) COM port uliyoitenga kwa ajili ya modem, kwa kutumia jumpers zilizo kwenye kwenye kadi hiyo ya I/O. 

Kikawaida kuna jumpers mbili zinazohusika: moja ya kulemaza COM1/COM3, na nyengine ya kulemaza COM2/COM4. Kama modem imeamuliwa kuwekwa kwenye COM2 au kwenye COM4, basi utahitaji kulemaza COM2/COM4, na kama modem imeamuliwa kuwekwa kwenye COM1 au COM3, utalemaza COM1/COM3. 

Kwenye kompyuta za miaka ya karibuni I/O controller imejengewa kwenye motherboard (yaani Onboard I/O) na hazina kadi maalum za I/O. Kwenye kompyuta hizo unaweza kuilemaza COM port inayotumiwa na modem kwa kurekebisha kumbukumbu za CMOS yaani "CMOS setup". Unapoiwasha kompyuta ukibonyeza kifungo cha Delete au F1 utaweza kuingia kwenye CMOS setup. Ukishaingia kwenye CMOS setup, chagua sehemu ya kurekebisha Onboard I/O – kwenye Award BIOS sehemu hiyo imeandikwa INTEGRATED PERIPHERALS. Ukiingia kwenye sehemu hiyo, kwa mfano kama unataka kuilemaza COM2, kwenye Onboard Serial Port 1 chagua COM1 na kwenye Onboard Serial Port 2 chagua Disabled. Baada ya hapo chagua Save and Exit ili uweze kuhifadhi marekebisho uliyoyafanya. 

Ukifuata utaratibu ulioelezwa hapo juu modem yako ya nje au ya ndani itaweza kutambuliwa na kompyuta yako bila ya matatizo yoyote na mara tu Windows 95 itakapoanza itakupeleka kwenye hatua nyengine ya kuingiza drivers za modem hiyo. Hakikisha kuwa unapoiwasha kompyuta yako, na modem ya nje nayo pia imewashwa. 

  

Kuingiza Driver ya Modem 

 
Mara tu Windows 95 itakapoanza itatoa kidirisha cha New Hardware Found. Sasa utahitaji kuingiza kwenye kompyuta driver ya modem yako. Driver ya modem ni programu ya kuiwezesha kompyuta yako kuitumia modem hiyo. Fuata utaratibu ufuatao kukamilisha kazi ya kuingiza driver ya modem yako. 

  1. Kwenye kidirisha cha New Hardware Found chagua Select from a list of alternate drivers, kisha bonyeza OK.
  2. Kwenye kidirisha cha Select Hardware Type, bonyeza Modem, kisha bonyeza OK.
  3. Kwenye kidirisha cha Install New Modem, chagua jina la kampuni iliyotengeneza modem yako, (kwa mfano U.S. Robotics), kwenye sehemu ya Manufacturers.
  4. Kwenye sehemu ya Models chagua jina la modeli ya modem yako, (kwa mfano Sportster 28800 bps), kisha bonyeza OK. Kama hukuona jina la modeli ya modem yako unaweza kuchagua modeli ya mtengenezaji huyo huyo iliyo karibu na modeli yako, au unaweza kuchagua Standard Modem yenye kasi sawa na modem yako.
Kama Windows 95 haikuiona modem yako, itabidi uitambulishe kwa mitulinga (manually). Bonyeza Start -> Settings -> Control Panel -> Modems, na ubonyeze Add, na kisha bonyeza Next. Baada ya hapo fuata hatua nambari 3 na 4 zilizotajwa hapo juu. 

Baada ya kukamilisha taratibu zote hizo, utakuwa tayari umefanikiwa kuiweka modem yako kwenye kompyuta yako. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita