|
|
|
Akheri ya zamani Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA RAIS anapotangazwa hula kiapo cha kuilinda katiba ya nchi. Hapo hapo huchukuwa madaraka ya Ukamanda Mkuu wa Majeshi (ya kivita, usalama, magereza na lile la kujenga taifa). Na katika hali hiyo anakuwa kiongozi wa serikali yetu na pia msemaji wetu mkuu. Hayo yote yanapatikana baada ya kuwa mtu huyo kashinda katika uchaguzi mkuu katika mfumo wetu wa kidemokrasia kwa kupata ridhaa ya wananchi kwa njia ya kura za siri. Mtu akishakubali kuyachukuwa madaraka na majukumu ya Urais, inambidi awe Rais wa watu wote wa nchi hiyo, waliomchagua na pia wale waliomnyima kura zao, wa chama chake na pia wale wa vyama vingine na kadhalika wale wasiokuwa na chama chochote pamoja na wale wote ambao hawakujishughulisha na upigaji kura wenyewe, ili mradi anakuwa Rais wa watu, wananchi na wasiokuwa wananchi lakini wanaishi nchini humo. Hawi Rais wa wafuasi wa dini yake tu. Wala hawi Rais wa hifadhi za misitu, maliasili, milima na mabonde, mbuga za wanyama na mito, hivyo ni mali ya wananchi vinatumika wanavyotaka wananchi kwa manufaa yao, yeye anakuwa kabidhi tu. Kwa hiyo Rais anapokula kiapo cha Urais, alikuwa Anaahidi kulinda sisi watu, kutulindia uhuru wetu pamoja na ule wa kuabudu, kutulindia mali zetu hata kama ni vidungu na kadhalika. Kiongozi ni kiongozi wa watu na mtawala huwa mtawala wa watu, mtu hawi kiongozi au mtawala wa vitu, vitu humilikiwa na watu. Katika hali hii, heshima ya kwanza huenda kwa watu na si kwa vitu. Tangu awamu hii iIngie tumefikwa na masaibu mengi tu. Na kila tunafikiwa na masaibu ya kutusibu, Rais ambaye ndiye msemaji wetu mkuu, huinuka akasema kitu japo kidogo kuhusiana na mkasa huo. Hata mara nyingine na Nyerere naye huinuka na kusaidia kusema kitu, hasa anapolisikia neno "Tanganyika" ambalo hataki litajwe. Mwezi Februari mwaka huu, Tanzania ilifikwa na msiba mkubwa sana. Askari wetu wameua raia wetu. Waislamu wa Tanzania, wakiwa ndani ya Msikiti wao pale Mwembechai, walikuwa wakihadhiri dini yao. Hapakuwepo hata Mkristo mmoja au mtu wa dini nyingine yoyote, aliyeinua mkono wake kutaka kumdhuru Muislamu, wala hapakuwepo Muislamu yeyote yule, aliyeinua mkono wake kutaka kumshambulia Mkristo au muumini wa dini nyingine yoyote. Mhadhara ulikuwa ukiendelea katika hali shwari kabisa wakati huo. Serikali ambayo Rais ndiyo kichwa na jicho, ikaamua kupeleka askari pale ili ipatikane fujo na mapenzi yake yatimizwe. Askari wakaingia mahali petu patakatifu pa kusalia na pa kumwabudu Mwenyezi Mungu wetu na wao (S.W.). Wakapanajisi na viatu vyao (ambavyo Nabii Mussa aliambiwa avivue pale majanini aliposimama kwa kuwa palikuwa patatifu). Wakawapiga watu kwa virungu na kwa risasi, wengine wakajeruhiwa, wengine wakalemazwa na wengine wakauawa. Allahu Akbar! Hayakutosha hayo, wakachukuliwa na wengi wengine wakaswekwa mahabusi, ambako waliteswa na kunyanyaswa (hasa kina mama) kiasi ambacho si vizuri kuyarudia maelezo yake na wala yale yaliyowapata majeruhi kule mahospitalini na hayapendezi kuelezwa na wote tunayajua. Tangu hiyo Februari mpaka hii leo Desemba, hatujamsikia Rais kusema lolote kuhusiana na tukio hili la aibu. Kimyaaa! Wala hatujasikia lolote kutoka kwa Mwalimu Nyerere. Hao ndio wasemaji na watetezi wakuu wa Tanzania na Watanzania. Imekuaje? Je ndugu zangu Waislamu mnaelewa maana ya ukimya huu? Je huku ndio kulindwa na Kamanda Mkuu wa Majeshi? Je, hiki ndio kichwa na jicho la serikali yetu? Tambueni kuwa Rais baada ya tukio hili la aibu, alikaa kimya. Akawaachia kazi ya usemaji Mhe. Yusuf Makamba na Ali Ameir Mohammed, ambao wote ni Waislamu. Naiita hii ni fitna kwa kuwa viongozi hawa wa serikali waliachiwa usemaji wa kikebehi ni viongozi wa Kiislamu. Na nia hapa ni kuwaacha Waislamu wagombane wao kwa wao. Kaanga mbuyu uwaachie wenye meno watafune! Mpo? Kama hatukutanabahi, basi tutaanza kuwachukia, Tusifanye hivyo. Wajibu wetu ni kuwastua na kuwakumbusha warejee kwa Mola wao (S.W.). Fitina nyingine ni ile ya kututaka kutugombanisha na wananchi wenzetu wasiokuwa Waislamu, kwa kupitisha laghai na propaganda kuwa fujo iliyotokea pale Mwembechai ni fujo ya kidini. Na kuwa walioleta fujo ile ni Waislamu na kuwa waliianzisha Msikitini mwao kwa njia ya mihadhara. Lakini ni kama mafuta majini, haufiki, hata ukIyavuruga namna gani maji yakitulia mafuta huja juu tu. Mhadhara uliokuwa ukiendeshwa pale Msikitini Mwembechai, hauKUleta fujo ile iliyotokea. Kama askari wasingepewa amri mbovu, ile fujo iliyotokea pale isingekuwapo. Kama kweli waendesha mhadhara ule walikuwa wamekiuka sheria ya serikali, basi serikali ingeweza kuwatia mbaroni watuhumiwa bila ya kuingiza askari msikitini na kuwabughudhi wale waliokuwa wakiendesha ibada zao. Msikitini kuna kuswali (swala tano za kila siku na zile za sunnah) na pia kuna kuabudu (mfumo mzima wa maisha pamoja na mihadhara) ndani na nje ya Misikiti. Siku zote tunaambiwa serikali ina mkono mrefu. Imekuaje tena serikali ishindwe kuwakAmata wahusika majumbani mwao? Mbona siku zilizopita serikali iliweza kuwakamata wahaini na majasusi majumbani mwao? Je, hao siyo hatari zaidi ya wahadhiri? Ningependa Mhe. Rais akae peke yake atafakari.Kisha ajiingize katika viatu vyetu, ajifikirie yuko Kanisani na waumini wenzake na Muhubiri au Kasisi kasimama madhabahuni, halafu yamtokee yaliyotutokea sisi pale Msikitini Mwembechai, angehisi vipi? Hasa akawa wakati huo kamanda Mkuu wa Majeshi ni Muislamu? Tunayo haki ya kuufikisha ukimya wa Mhe. Rais kwa jinsi tutakavyo, maana katupa nafasi hii yeye mwenyewe. Kunyamaza kimya mtu anapofikwa na mkasa si jambo zuri. Sikumbuki saa, siku, mwezi wala mwaka, wanaokumbuka watanikumbusha, lakini nakumbuka wazi dhahiri kuwa katika miaka kadhaa iliyopita, kipindi cha serikali yetu wenyewe ya awamu ya kwanza, kitendo cha askari kuwaingilia Msikitini na viatu na majibwa kilifanyika huko sehemu za Keko Jijini Dar es Salama. Ema kwa kuogopa kwenda na maji (ndio msemo wa siku hizi) au kwa uzembe wetu wenyewe, Waislamu tulinyamaza tu na wala hatukuchukuwa hatua yoyote ile ya kukomesha kitendo kile. Matokeo yake tunayaona hivi sasa. Imekuwa ndio mtindo siku hizi kupeleka Misikitini kwa visingizio visivyokuwa na uzito wotote. Laiti tungechukuwa hatua kali wakati ule wa mwanzo, mambo haya yasingetokea tena. Lakini tunaambiwa, afadhali kuchelewa kuliko kuacha kabisa. Saa ya kuchukua hatua kali ya kukomesha fitna hizi imefika. Kuna uchaguzi mkuu wa mwaka 2000. Kazi yetu tunaijua, wala tusizungushe zungushe. Tusiwafanyie chuki wale Waislamu wenzetu walioghafilika wala wale wenzetu wasiokuwa Waislamu ambao wanatumiwa tu kama ngazi, ambao hawajui wafanyalo. Unaambiwa ukimuona nyoka, mgonge kichwani na ukiiona serikali haina muafaka au maslahi nawe ivunje vunje madaraka yake kuanzia kichwani. Imefika hadi tunalazimika kumkumbuka mkoloni. Maana wakati ule tulipokuwa utumwani tuliweza kuheshimiwa dini yetu ya Kiislamu. Msikiti ulikuwa "out of bounds" kwa sababu hapo paliheshimiwa kama "sacred place", hivyo tuliweza kufanya swala na ibada zetu bila ya khofu ya kuingiliwa Msikitini wakati wowote, si mchana wala si usiku. Liwali akipewa ndege ya serikali, kwenda juu angani kuangalia mwezi mwandamo kama palikuwa na mawingu siku hiyo. Mwezi mtukufu wa Ramadhan, mikahawa yote na hoteli za chakula zilifungwa mchana kutwa. Ngoma zilikuwa haziruhusiwi kuchezwa mwezi huo. Na Bar zote na vilabu vya ulevi vilifungwa mchana na usiku mwezi mzima. Kule Tanganyika Packers alikuwa hachinjwi ng’ombe ila na Muislamu na Sheikh aliekubalika kushuhudia. Kesi , ndoa na sheria za za Kiislamu ziliendeshwa na Ma-Liwali na Ma-Akida. Uislamu ulikuwa ukiheshimiwa na wakoloni. Lakini leo, katika hali ya kuwa ati tuko huru na tunajitawala wenyewe, imekuwa virungu na risasi mtindo mmoja mpaka Misikitini. Loo, masaibu gani haya yaliyofika? Akheri zamani siku hizi haipatikani! |
YALIYOMO
Tahariri Umaskini unachafua mazingira! Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani Qur’an yachomwa moto Shinyanga Marekani yadhihirisha Ubeberu wake MARADHI
YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu Akheri ya
zamani
UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU Wasomi
Waislamu wawajibike
Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua MADRASATUL
Husseiniyi Shadhily
Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said Misikiti yakosa maji ya kutawadhia Bakwata Tanga haifuati katiba yake Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah Je,
hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Njia
ya uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 3
Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|