|
|
| Qur’an
yachomwa moto Shinyanga
WATU wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa dhehebu moja la Kikristo hivi karibuni wamedaiwa kuchoma moto hadharani kitabu kitakatifu cha Waislamu Qur’an. Tukio hilo lilitokea kijijini Malaseko wilayani Maswa mkoani Shinyanga katika mahubiri ya dini yanayosadikiwa kuendeshwa na wafuasi wa dhehebu hilo. Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu, Sheikh wa mkoa wa Shinyanga Sheikh Issa Shaaban alithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo. Hata hivyo, Sheikh huyo hakutaka kuzungumza zaidi kwa maelezo kwamba hakuwa na taarifa za kina na kwamba suala hilo liko katika vyombo vya dola hivi sasa. Imeripotiwa kutoka Maswa kwamba mtu mmoja aliyedaiwa kuugua kwa muda mrefu baada ya kuponywa kwa maombezi katika mahubiri hayo alitakiwa kusalimisha vifaa vya matibabu alivyokuwa akitumia kabla ya kuhudhuria mahubiri hayo. Imedaiwa kuwa mtu huyo aliwasilisha mbele ya muhubiri nakala ya Qur’an kitabu cha Yasin na Maulid Barzanji ambavyo vyote vilipigwa kibiriti na muhubiri huyo. Taarifa za kitendo hicho zilipoenea kijijini hapo, Waislamu wa sehemu hiyo waliwasiliana na wenzao ambao kwa pamoja walichukua uamuzi wa kulifuatilia suala hilo. Wakiongozwa na Sheikh wa Wilaya hiyo Sheikh Nyangenyange, Waislamu hao walipiga ripoti polisi ambayo iliwasaka wahusika na kuwakamata baadhi yao. Imedaiwa kuwa mmoja wa watuhumiwa hao alikamatiwa mkoani Singida. Gazeti hili lilipowasiliana na polisi mkoa wa Shinyanga kuhusiana na tukio hilo, msemaji mmoja alifahamisha kuwa Kamanda wa mkoa alikuwa safarini Zanzibar na kwamba polisi mkoa hadi wakati huo haikuwa na taarifa zozote kutokana na uduni wa mawasiliano kati ya Maswa, Meatu na Shinyanga mjini. KWA mara nyingine Marekani imeonyesha ubabe na uharamia wake kwa kuishambulia Iraq. Shambulio hili limedhihirisha jambo moja muhimu kwamba Marekani ipo tayari kufanya lolote na bila kujali chochote ikiwa ni pamoja na kuua ili muradi tu si Wamarekani, ili kuhamisha matatizo yao au kulinda maslahi yao binafsi. Lakini jambo lingine muhimu ambalo limebebwa na tukio hili ni kwamba mataifa yaliyo mengi hata yale ambayo yalikuwa yenye kuheshimika yamegeuka kuwa vikaragosi yasiyoweza kuhoji mambo kwa kutumia akili zao huru. Kauli zilizotolewa na viongozi wa nchi kama Uingereza juu ya suala hili zimekuwa za fedheha na kuiabisha. Kwamba jambo hata likiwa ovu maadhali limefanywa na Marekani ni lazima liungwe mkono. Zipo nchi ambazo ndio nyingi zimebaki kimya. Hizo hazitarajiwi kuonyesha waziwazi kupinga kwao uharamia huu wa Marekani. Zinachoweza kufanya ni kukaa kimya. Balozi za Marekani ziliposhambuliwa Dar es Salaam na Nairobi kabla hata mhusika hajajulikana nchi hizo hazikukaa kimya. Zilijitokeza kwa jazba kubwa kumlaani mlipuaji wasiye mjua. Leo mtu kautangazia ulimwengu kwamba ni yeye kafanya na ahadi kwamba atalipua zaidi, nchi hizo hizo zinagwaya kauli haitoki ghafla zimegeuka viziwi; vipofu na bubu. Hatujui ni nini kilichofanya nchi hizo ziwe kimya. Je, zinashindwa kuelewa kuwa dhulma ya roho ya binadamu popote itakapofanyika itabaki vile vile kuwa ni dhulma bila ya kujali taifa, kabila, rangi au dini ya mdhulumiiwa? Uvamizi na mauaji yanayofanywa na Marekani huko Iraq yamekuja wakati katika nchi nyingi duniani kuna vitendo vinavyofanana na hali hiyo. Zipo nchi zilizovamia nchi nyingine na kufanya mashambulizi dhidi ya nchi hizo kwa hoja za kulinda mipaka yao. Nyingine zipo katika mapambano ya kuangamiza sehemu ya raia zake kwa visingizio vya kupambana na vurugu za kikabila au kidini. Kwa vyovyote vile, huwezi kuzisikia nchi kama hizo zikilaani vitendo vya Serbia dhidi ya Waislamu huko Kosovo. Huwezi wewe ukawa unaua raia wako bila kujali halafu ukawa na uso tena wa kuwatetea wanaouliwa kwingine. Hata hivyo, zipo nchi nyingine ambazo hazina matatizo yanayoweza kuzifanya zisiwe na uso wa kukemea maovu na dhulma za mauaji kama hzo zinazofanywa na Marekani. Lakini nazo zipo kimya, utadhani hazisikii, hazioni na wala hazisikii vibaya. Tena nchi hizi ni wanachama wa Umoja wa Mataifa. Nchi hizo zipo kimya ili hali zikijua kuwa si Baraza la Usalama wala Umoja wa Mataifa uliotoa amri ya kushambulia Iraq bali ni Marekani! Nchi hizo zinajua kuwa ni Rais Clinton wa Marekani ndiye aliyeamrisha mashambulizi hayo dhidi ya Iraq. Na ni yeye na washirika wake wenye silaha kali ndiyo wanaojigamba kwa kuua wananchi wa Iraq! Nini sababu za kimya cha nchi hizo wanachama wa Umoja wa Mataifa; umasikini, njaa na maradhi ya kutegemea wafadhili wa misaada ya unga wa njano unaosambazwa na taasisi za Umoja wa Mataifa? Hivi nchi hizi hazijui kuwa uhai wao ni mauti wa wenzao? Zipo pia nchi zinazotaka kuamini Marekani ni nchi yenye watu makini na hivyo kila watakalosema au kulifanya basi ni la kweli na lenye maana. Lakini ukitazama historia ya Marekani utagundua kwamba viongozi wake wanamchezo wa kuhamisha mazingatio ya watu wanapofikwa na matatizo ndani ya nchi. Na kwa kufanya hilo wao huwa hawajali roho ngapi zitaangamia. Mfano mwaka 1982 Marekani ilijiingiza kijeshi Lebanon. Wanajeshi wa Marekani wakalipuliwa na kufa kwa mamia. Wamarekani wakaja juu kutaka kujua lipi zaidi kwa watoto wao na ndugu zao kufia Lebanon. Ikawa Reagan yupo kwenye kiti cha moto. Ili kujinusuru akaivamia Grenada. Na huu si mchezo wa Marekani pekee. Lakini ni viongozi wengi wanapokabiliwa na hali ngumu ndani ya nchi hutafuta adui wa nje ili apate kuungwa mkono na wananchi wote. Polisi watavamia raia na kuua, lakini zitasingiziwa Balozi za nje na kutafutwa wanyonge wa kutiwa mahabusu. Huko nyuma Cuba na Iran zilikuwa ndio gunia la mazoezi (punching bag) la Marekani, sasa zimepumzishwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Iraq, Sudan na Afghanistan. Wakati sakata ya Monica inaanza kupamba moto Bw. Clinton aliamuru mashambulizi dhidi ya Sudan akidai kwamba anashambulia kiwanda chenye kutengeneza silaha za sumu. Lakini leo hata Wamarekani wenyewe wanajua kwamba hapakuwa na kiwanda cha silaha za sumu Sudan; bali ulikuwa ni uongo mtupu. Ni jambo la kuhuzunisha kwamba nchi hizo zinazo ienzi Marekani zina hatari ya ubabe utokanao na ghadhabu ya mtu aliyefumaniwa kisha akazomewa. Suala muhimu ambalo ilikuwa kila mwenye akili yake iliyofunga alizingatie katika tukio lile la kuishambulia Sudan ni ule ughafula wa hoja yenyewe na wakati ilipoletwa (timing) wakati sakata ya Monica ikitokota. Kisingizio cha kuishambulia Iraq hivi sasa inadaiwa kwamba imekataa kushirikiana na wakaguzi wa silaha. Inadaiwa kwamba Iraq bado inazo inazificha silaha za maangamizi ikiwa ni pamoja na zile za kemikali. Lakini Marekani na mshirika wake Uingereza hazijasema ni viwanda vipi na vingapi vya silaha za kemikali ambavyo wameishaviangamiza katika mashambulizi yalioanza juzi usiku. Silaha hizo zimekuwa zikisakwa toka majengo ya kijeshi mpaka ofisi za chama na hata vyumba vya kulala Bw. Saddam. Utadhani ni yale ya Mwembechai kusaka mabomu ndani ya tupu za wanawake. Kukariri "kashfa" "kashfa" ili ipatikane sababu. Matatizo yanayomkabili Bw. Clinton hivi leo nchini mwake hayakukusabishwa na Iraq wala wananchi wa Marekani. Yamesababishwa na yeye mwenyewe kushindwa kuidhibiti nafasi yake na matamanio yake. Kuamuru mashambulizi haya katika kilele cha wimbi linaloekea kumtoa madarakani Bw. Clinton ni jambo la kutizamwa kwa makini. Sisi tungependa kuungana na baadhi ya wajumbe wa "Congress" waliojitokeza wazi kusema kwamba hiki si lolote bali kuhamisha fikra na mazingatio ya watu wa Marekani. Moja ya sababu kubwa ya kuletwa mitume ni kuwataka watu watumie akili zao. Sio kufuaata mila, fikra ya mtu mashuhuri, shinikizo la Clinton wala "UN Security Council". Watu watumie akili zao kuitambua haki. Matatizo yanayotukabili hivi leo ni matokeo ya kuongozwa kwa mizani ya masilahi na wala sio mizani ya haki. Pamoja na hali hiyo ya kukithiri kwa kibri ya madhalimu huku baadhi ya watu wenye wajibu wa kutoa japo kauli kukemea kabri hiyo, bado ipo nafasi ya faraja. Tunapata faraja tunapoangalia historia jinsi mijitu kama Firauni walivyoangamizwa baada ya kibri yao kukithiri. Tunafarijika vile vile tunapokumbuka katika historia ya hivi karibuni kwamba "wanyonge" wa Korea ya Kaskazini walipoamua kupambana na uvamizi wa Marekani mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia, jeshi la Marekani lilirudi kwao likiwa na majeneza mengi badala ya mashujaa. Vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa katika uvamizi wao wa Vietnam ya Kaskazini. Tunafarijika zaidi tunapokumbuka jansi jeuri ya askari wa Marekani kwa wananchi wa Somalia ilivyo komeshwa na wananchi wale na kuwafanya wafunge virago pasipo kuaga. Madhali wananchi wa Iraq na wananchi wa nchi nyingi zikiwemo na zile
zenye viongozi wapenzi wa Marekani, wana msimamo wa kulaani ubeberu na
unyama wa madhalimu wasioona haya wala vibaya kuangamiza roho za binadamu
wenzao, Ishallah iko siku madhalimu wataangamia.
|
YALIYOMO
Tahariri Umaskini unachafua mazingira! Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani Qur’an yachomwa moto Shinyanga Marekani yadhihirisha Ubeberu wake MARADHI
YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu Akheri ya
zamani
UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU Wasomi
Waislamu wawajibike
Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua MADRASATUL
Husseiniyi Shadhily
Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said Misikiti yakosa maji ya kutawadhia Bakwata Tanga haifuati katiba yake Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah Je,
hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Njia
ya uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 3
Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|