AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani
 
  • Kesi nyingine za Waislamu zaahirishwa

WAKATI kesi ya tuhuma ya "uchochezi" inayomkabili aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwembechai, Sheikh Omar Bashir ikitajwa mahakama ya Kisutu Jijini, kesi nyingine mbili za tuhuma ya "kufanya ghasia" maeneo ya Mwembechai zinazowakabili Waislamu 23 zimeahirishwa na mahakama hyo hadi Januari, mwakani.

Kesi hizo ni pamoja na kesi namba 192/98 inayowakabili watu kumi na mbili, wakiwemo Waislamu tisa na Wakristo watatu na kesi Nambari 184/98 inayowakabili Waislamu kumi.

Kesi hizo zilifunguliwa na serikali mahakamani hapo mapema mwezi Machi, mwaka huu.

Kesi Nambari 192/98 imeahirishwa na mahakama hiyo hadi Januari 26, mwakani ambapo inatarajiwa tena kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo. Kesi hiyo imekwishasikilizwa mara moja hapo Novemba, mwaka huu.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mwalimu Ramadhani, Hamadi Salum, Yusufu Salum, Hassan Mtyani, Gaudence Gervas na Omari Hassani.

Wengine ni Kassim Ally, Abdallah Sufiani, Richard Kobelo, Said Rashid, Bernard Augustine na Haji.

Aidha kesi namba 184/98 imeahirishwa hadi Januari 25, mwakani. Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Hatamu Saidi, Hamidu Mohamed, Hussein Mohamed, Ally Kassim, Kivuele Mawazo Abdallah na Abdallah Juma Bakari.

Wengine ni Rashid Mohamed, Kombo Hassani, Hemed Ramadhani, Hamza Amani Ally na Abdulrahmani Juma.

Sababu ya kuahirishwa kwa kesi hizo hadi tarehe hizo, imetokana na mashahidi wa upande wa serikali kushindwa kufika mahakamni ambapo walitarajiwa kutoa ushahidi wao hapo Desemba 14 na 15, mwaka huu.

Nayo kesi namba 621/98 inayomkabili Sheikh Omar Bashir imeahirishwa na mahakama hiyo hadi Desemba 30, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni Sheikh Bashir alikuwa bado anaendeleo kusota rumande kwa kukosa dhamana.

Sheikh Bashir bado anaendelea kutibiwa mguu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili chini ya ulinzi wa polisi, ambapo kwa kushindwa kufika kesi yake ilitajwa mahakamani mwenyewe akiwepo hospitali.

Kukosekana kwa dhamana kwa Sheikh Bashir kumetokana na kesi yake kutajwa asubuhi mapema mahakamani hapo, jambo ambalo lilimfanya Wakili anayemtetea Bw. Twaha Taslima kutokuwahi kesi hyo kwa kuwepo mahakama kuu kikazi.


Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga
 

BARAZA Kuu la Kiislamu nchini Tanzania (BAKWATA) limesema kuwa mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhani utatangazwa na baraza hilo kupitia kwa Mufti Sheikh mkuu Hemed bin Juma bin Hemed.

Akizungumza mara baada ya swala ya Ijumaa iliyofanyika kwenye Msikiti wa Ijumaa uliopo Kinondoni, Jijini, wiki iliyopita Sheikh Gorogosi alisema kuwa Waislamu Watanzania watafunga Ramadhani baada ya Muft Sheikh Mkuu kutangaza kuonekana mwezi huu huo.

Alisema bazara la Kiislamu halitakubali taarifa za kuonekana kwa mwezi kutoka sehemu yoyote iliyo nje ya ukanda wa Afrika Mashariki.

"Hatutafuata mwezi utakaoandama Saudia wala London bali nchini na sehemu nyingine za Afrika Mashariki", alisema Sheikh Gorogosi.

Sheikh Gorogosi alisema kuwa mwezi huo unatarajiwa kuonekana mwishoni mwa wiki na yeyote atakayeuona atoe taarifa kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Kinondoni na kwa walio mikoani wapige simu nambari 668893.

Awali, akitoa hotuba kwenye swala hiyo Sheikh Ali Mbarak aliwataka Waislamu kumaliza tofauti zao kabla ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan ili Waislamu hao wawe na mshikamano, upendo na amani wakati wa funga ya mwezi mtukufu.

Sheikh Ali alisema kuwa Waislamu hawana budi kumaliza uhasama wao na kusameheana yale waliyokoseana.

"Mume aliyemwacha mke wake kwa matatizo madogo madogo anapaswa kumrejesha mke huyo, wazazi waliowakosea radhi watoto wao nao wawasamehe watoto hao na Waislamu kwa Waislamu walihitilafiana wamalize tofauti zao kabla ya mfungo huu", alisema Sheikh Ali.

Sheikh alisema Waislamu wanapaswa kufuata ibada zilizotolewa kwa wakati tofauti wakati wa mwezi mtukufu waitumie swala ya Taraweh ambayo inapatikana katika mwezi unaokuja tu wa mfungo wa Ramadhan.


Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza
 

WATU wanaoishi maeneo yanayofugwa nguruwe wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na magonjwa ya kuambukiza iwapo hatua za haraka za kuzuia ufugaji na uuzaji wa nguruwe katika maeneo hayo hazitochukuliwa.

Tahadhari hiyo imetolewa hivi karibuni na ofisi ya Mwenyekiti wa serikali za mitaa Yombo Kisiwani, Jijini katika uamuzi wake juu ya mgogoro baina ya mfugaji wa nguruwe Bw. Shayo na waumini wa Masjid Tahiyyatu wa Yombo Kisiwani Jijini Dar es Salaam.

Ili kuepusha athari hiyo, ofisi hiyo imempa Bw. Shayo miezi mitatu kuanzia Desemba 12, mwaka huu hadi Machi 20, mwakani awe amekwishawaondoa nguruwe wake katika maeneo hayo.

Mapema akisoma hukumu hiyo katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu katika ofisi hiyo iliyopo mtaa wa Mamboleo B, Kata ya 14- Temeke, eneo la Yombo Kisiwani, Jijini, Katibu wa ofisi hiyo alisema ofisi yake imefikia uamuzi huo baada ya kamati yake kupokea malalamiko kutoka kwa watu kadhaa wanaoathiriwa na wanyama hao.

Katibu huyo aliongeza kuwa baada ya kamati yake kupokea malalamiko hayo, ilifanya uchunguzi wa kina kwa kukagua eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa kuhifadhiwa nguruwe hao na kugundua kwamba harufu pekee ya wanyama hao inaweza kuhatarisha afya za watoto na vikongwe kama si watu wote.

Awali, waumini wa Masjid Tahiyyatu waliilalamikia ofisi hiyo kuwa tangu Bw. Shayo awalete nguruwe wake eneo hilo wamekuwa wakikerwa na harufu mbaya ya wanyama hao.

Pamoja na harufu hiyo, waumini hao ambao waliongozwa na Imamu wa Msikiti huo, Mzee Abdu Jabiri Shangama Ngasi pia walilalamikia kuwa Bw. Shayo amekuwa akiwaachia kuzagaa ovyo kinyesi cha wanyama hao, hatua ambayo imekuwa ikiwaathiri wakazi wa eneo hilo.

Mbali na kero hizo waumini hao pia walidai kuwa wamekuwa wakipata taabu wakati wa kuswali kuathiriwa na harufu mbaya ya nguruwe hao hasa kwa zizi kujengwa karibu na Msikiti wao.

Aidha, kutokana na kuzagaa ovyo kwa kinyesi cha wanyama hao, maji ya kisima kilichopo katika bonde lililopo eneo hilo ambayo pia hutumika kwa kutawadhia Msikitini hapo yanahofiwa kuingiwa na najisi ya nguruwe hao.


200 Wasilimu
 

WATU wapatao 200 wamesilimu kufuatia mahubiri ya Kiislamu yanayoendelea kutolewa mjini hapa na mtoto Said John anayedhaniwa kuwa na kipaji maalum (Gifted).

Katika mahubiri yake mtoto huyo amekuwa akichambua maandiko ya dini za Kiislamu na Kikristo na kuonyesha kuwa Uislamu ndiyo dini anayostahiki kufuata mwanaadamu.

Kabla ya kufika Mtwara, mtoto huyo ambaye anaongozana na wahubiri wengine maarufu kutoka Dar es Salaam ameshapita sehemu kadhaa za kanda ya kusini ikiwa ni pamoja na Rufiji (Pwani), Kilwa Masoko (Lindi), Nachingwe, Liwale, Luangwa, Lindi Mjini na tarafa zake.

Kikundi hicho kitaelekea nchi jirani ya Msumbiji mara baada ya zaira ya Mtwara na vitongoji vyake. 

 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita