AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Ijue Uhuru madrasa - Morogoro
 
  • Inatoa wanafunzi wanaokwenda vyuo vikuu vya Kiislamu
Na Rajab Rajab, Morogoro

UNAPOULIZA madrasa kongwe zenye kutoa wanafunzi wanaosoma vizuri Qur’an mjini Morogoro na wanaoingia vyuo vikuu mbalimbali vya Kiislamu kama vile Markazi, Malindi, Tamta na Kenya basi mojawapo ni madrasa ya Uhuru iliyoasisiwa na Sheikh Ramadhani bin Khatibu aliyefariki dunia mwaka 1965 katika hospitali ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam. 

Sheikh Ramadhani bin Khatib alisoma Qur’an kwa Sheikh Maulid bin Diwani aliyefariki dunia mwaka 1938. 

Madrasa ya Uhuru ilianza na wanafunzi sita, ilianzia Mji Mpya nyumbani kwa Sheikh Hassan Maftah ambaye ni marehemu, ilizinduliwa rasmi na Sheikh Ramadhani Haji ambaye naye ni marehemu. 

Miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Ramadhani Khatib ni pamoja na Sheikh Said Musa, Sheikh Shuaibu, Sheikh Ali Diyanga na Sheikh Ahmad Pinto. 

Sheikh Ramadhani bin Khatibu aliiendesha madrasa hiyo na hatimaye akafikwa na maradhi na akafariki dunia huku akiwa ameacha usia kuwa madrasa hiyo ishikwe na mmoja wa wanafunzi wa madrasa hiyo kati ya Sheikh Said Mussa Kariati au Sheikh Shuaibu. 

Tangu kufa kwa muasisi wa madrasa hiyo mwaka 1965, ikashikwa na Sheikh Said Mussa Kariati kwa kushirikiana na wanafunzi wake kina Ustaadh Abdallah Jafary na Ustadh Ramadhani Maftaha. 

Baadaye wakaongezeka vijana wengine kina Ali Kariati (Kidevu), Majuto Halfani, Askaria (ambaye alihamia), Hamis Juma na wengineo. 

Hivi sasa madrasa hiyo inaongozwa na Ustadh Maulid Bago. 

Madrasa ya Uhuru ilihamishwa mwaka 1990 kutoka Mji Mpya na kupelekwa Mwembesongo na hii ilitokana na kuongezeka idadi ya wanafunzi wanaoingia katika madrasa hiyo ambapo hivi sasa ina wanafunzi wasiopungua 160 wasichana kwa wavulana. 

Masomo yanayofundishwa Uhuru madrasa ni tisa ambayo ni Qur’an, Hadith, Fiqh, Sira, Akida (Tawhiid), Tajwidi, Nahau, Swarf pamoja na lugha. Pia madrasa hiyo kwa siku za usoni inategemea kuanzisha Chekechea (Nursery School) ambapo yatakuwa yanafundishwa masomo ya kusoma, kuandika na hesabu. 

Katika madrasa ya Uhuru masomo yanafundishwa katika vitengo tofauti visivyopungua sita ambapo watoto wanaoanza wanakuwa wa darasa la maandalizi ambapo wanasoma somo moja la kusoma na kuandika Qur’an ambapo wanatumia mbao na madaftari. Kitengo kinachofuatia ni darasa la mwanzo la Qur’an, Fiqh ya mwanzo, Akida na Lugha. 

Kitengo kingine kinahusika na masomo ya Fiqh na sira na kufuatiwa na kitengo cha Tajuhidi na Nahau na kuendela na swarf. 

Lengo kuu la madrasa hiyo ni mtoto (mwanafunzi) akae darasani kwa kipindi cha miaka sita mpaka saba. Ada katika madrasa hiyo ni shilingi 1,200 kwa miezi sita, lakini watoto wengi wamekuwa hawakamilishi ada hiyo na kupelekea hata walimu kukosa posho ya kufundishia na kufanya wafanye kazi ya kujitolea. 

Kutokana na ukongwe wa madrasa ya Uhuru imeweza kuwa na matawi yake ambayo ni pamoja na madrasat Najami iliyopo eneo la Msamvu na madrasa Al Jazila iliyopo eneo la Mafisa. 

Pia madrasa hiyo ina ushirikiano wa kimasomo na madrasa Shifahi ya Kihonda - Mbuyuni mjini hapa. 

"Madrasa yetu kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwake imepata mafanikio makubwa sana hasa katika taaluma na hususani kwa msaada mkubwa kutoka kwa Ustadh Al-Hadi Omar wa Dar es Salaam kwa kutusaidia mitaala ya masomo", amesema mmoja wa walimu wa madrasa hiyo Ustadh Maulid Bago. 

Madrasa hiyo kama zilivyo madrasa nyingine nchini inakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kifedha, vifaa vya kufundishia, uhaba wa majengo. Mwalimu anayeshikilia madrasa hiyo kwa sasa Ustadh Maulid Bago amewataka Waislamu kote nchini kusaidia madrasa hiyo watumie akaunti ya Wami - Branch A/C No. 6804900290. 


Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua
 

MIONGONI mwa madrasat maarufu hapa jijini ni madrasat Akhlaqil Islamiya ya Mbagala Rangi Tangu iliyopo karibu na kituo cha Maliasili. 

Madrasat ambayo ilianzishwa mwaka mmoja uliopita imekuwa na maendeleo mazuri ya elimu ya dini ya Kiislamu kutoka kwa mwalimu wake Said Njinga ambaye kwa kushirikiana na wazazi wa wanafunzi wa madrasa yake wameweza kupata mafanikio makubwa ya kitaaluma katika sehemu hiyo ya Mbagala Rangi Tatu. 

Akizungumza mwishoni mwa wiki, Mwalimu Njinga alisema kuwa madrasat yake licha ya kupata mafanikio makubwa kielimu bado inakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa jengo maalum la kufundishia, uchache wa vitabu na shughuli za kifamilia ambazo huwafanya wanafunzi kutohudhuria baadhi ya vipindi. 

Alisema licha ya matatizo hayo, Madrasat yake imeweza kupata wanafunzi 18 katika juzuu ya kwanza, wanafunzi 12 katika juzuu ya pili, wanafunzi watatu katika juzuu ya tatu, katika juzuu ya nne kuna mwanafunzi mmoja. 

Aidha, alisema chuo hicho kina wanafunzi wa awali 13 na hivyo kukifanya kuwa na wanafunzi 47. 

Wanafunzi wapo katika makundi ya umri ya miaka minne hadi sita wanafunzi 10, miaka sita hadi kumi wanafunzi 28 na miaka 10 hadi 12 wanafunzi tisa ambapo wanafunzi wasichana wapo 24 na wavulana 23. 

Madrasa hiyo ilianzishwa mwaka jana ilikuwa na wanafunzi 13 lakini kutokana na mwamko wa wazazi wa eneo hilo chuo kiliweza kukusanya wanafunzi 47 idadi ambayo ipo hivi sasa. 

Akiyataja masomo yanayofundishwa chuoni hapo, mwalimu Njinga alisema kuwa masomo anayofundisha ni pamoja na Qur’an ikiwa ni pamoja na kufanya tafsiri katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza. 

Masomo mengine ni Fiqhi, Sira, Tawheed na lugha ambapo wanafunzi huandikiwa ubaoni na baadaye husimama mmoja mmoja kusoma na kuyaweka kichwani waliyofundishwa. 

Kwa mujibu wa Ustadh Njinga, Madrasat yake inaomba misaada ya hali na mali kwa wafadhili mbalimbali. 

Aliitaja misaada wanayoomba kwa wafadhili ni pamoja na kujengewa jengo la Madrasat yake angalau chumba kimoja 

Alisema yeyote anayetaka kutoa msaada wake awasiliane na Mwalimu Njinga ambaye atakuwepo madrasat hata wakati wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo Madrasat yake itakuwa inatoa mafunzo kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 4.30 kila siku. 


Husseiniyi Shadhily
 

Na Jamillah Nassoro 

MADRASATUL Husainiyyi Khusunul madarisu Shadhilliyya ipo mtaa wa Fundikira Magomeni Makuti wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam. 

Madrasa hii ilianzishwa na Maustadh wawili nao ni Ust. Gharib Bashiri naUst. Ahmad Hassani Bambela. Madrasa hii ilianzishwa mwaka 1972 ikiwa na wanafunzi 30 wasichana kwa wavulana. 

Madrasa hii ni maarufu sana kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na kuwafundisha wanafunzi wa Kiislamu masomo yanayohusiana na dini yao. 

Kipindi hicho chote walikuwa bado hawajaafikiana kumchagua mwalimu mkuu, mpaka ilipofikia mwaka 1993 wakaongezeka walimu wengine wanne nao ni Abdushakur Fadhwila, Ust. Seleman Salum, Ust. Mohammed Idrisa na Ust. Siraju dini Abdallah. 

Hivi sasa madrasa ina walimu wawili nao ni Ust. Gharib Bashiri mwalimu mkuu na Ust. Ahmad Hassan Bambela mwalimu mkuu msaidizi hao ni walimu ambao wameianzisha hiyo madrasa mpaka hivi sasa ina wanafunzi 232 wasichana kwa wavulana. 

Masomo yanayotolewa madrasani hapo ni Qur’an tukufu pamoja na tafsiri yake, Fiqh, Sira, Lugha, Akhlaq (Adabu), Tawheed, Hadith za Mtume Muhammad (s.a.w.) na mengi mengineyo yanayohusiana na dini yenyewe. 

Upo utaratibu ambao umewekwa na walimu kuwa kila mzazi atoe shilingi 300 kila baada ya mwezi mmoja ili kuweza kuwasaidia walimu hao pesa za matumizi yao binafsi. 

Hata hivyo, wazazi hao wamekuwa hawana matatizo yaani sio mpaka wafukuzwe watoto kama madrasa nyingine. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita