AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua
Hongera, shukrani Mohammed Said

Ndugu Mhariri 

NAANZA kwa kutoa pongezi na shukrani nyingi na za dhati kabisa kwa ndugu yetu mpendwa Mohammed Said kwa kazi kubwa, ngumu na ya kizalendo ya kuiandika upya historia ya harakati za ukombozi wa Tanganyika kutoka mikononi mwa wakoloni. 

Kutokana na utafiti wa kina, unyeti na usahihi wa data pamoja na ushahidi wa kinywa wa baadhi ya wahusika wa harakati hizo ambao mwandishi amezungumza nao, Mohammed ameiweka sawa historia ya nchi yetu ambayo kwa miaka yote tokea tupate uhuru, ilikuwa imedhoofika kwa maradhi ya chuki, udini na ubinafsi. 

Kwa mantiki hiyo, Bw. Mohammed Said anastahili kupata heshima kubwa katika duru za kisomi. Msomi huyu mzalendo, mwenye moyo wa kujituma, upendo na nchi yake na huruma na wananchi wenziwe, anastahiki hadhi hiyo ya juu kutokana na ukweli kwamba yeye amewapiku waandishi wa historia waliotangulia ambao walikabiliwa na uhaba na upotofu wa habari muhimu kuhusu harakati na wanaharakati walioikomboa Tanganyika. 

Kwa maana hiyo, kitabu cha Mohammed Said ndicho hasa kinachostahiki kutumika kama rejea katika ufundishaji wa somo la historia ya nchi yetu kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu. Kwa kweli hii ni bahati kubwa sana iliyowaangukia wasomi wa leo. 

Kwa ujumla maudhui ya kitabu cha Bw. Mohammed Said yanalenga kumkomboa Mtanzania kifikra na kisiasa. Kwa watu waliozaliwa miaka mingi baada ya uhuru wataondokana na ile fikra potofu kuwa uhuru wa nchi hii uliletwa na Julius Nyerere peke yake kama walivyofundishwa kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba na kuendelea, sambamba na propaganda za vyombo vya habari. 

Kwa hali hiyo, kitabu hicho kitafutilia mbali ile dhana kuwa nchi hii ni ya "baba wa taifa" na kwamba hakuna anayeruhusiwa kwenda Ikulu bila ya ridhaa yake. 

Kwa pande wa raia waliodhulumiwa na kukandamizwa muda mrefu kwa sababu ya dini yao, kitabu cha Bwana Mohammed Said kinawapa yote mawili; hamasa na majonzi. Hamasa yapatikana kwa ule ujasiri na moyo wa kujitoa muhanga waliokuwa nao wazee wetu licha ya vitisho vya serikali ya kikoloni. Ili kuweza kujikomboa wazee wetu walijitolea kwa hali na mali tena kwa kuzingatia utamaduni wa Kiislamu. 

Na majonzi yanampata raia wa dini ya Kiislamu pale anaposoma kuwa, wazee wetu hawakupata elimu ya taaluma sio kwamba walikataa elimu hiyo, bali walikataa ubatizo. Babu na baba zetu walikubali kukosa elimu pale walipotakiwa kuchagua "moja" ama "wawe Wakristo wasome" au wabaki "Waislamu wajinga". 

Kwa kweli tukikifanyia tathmini kitendo cha wazee wetu kukataa elimu kwa sababu ya sharti la kubatizwa, ni wazi tutaona kimekuwa na manufaa makubwa kwetu hasa tukiona jinsi wale waliobatizwa walivyoathirika wao na vizazi vyao. Kama wazee wetu wangetetereka basi leo tungekuwa "washirikina wasomi" au "wasomi murtadi". 

Simanzi pia inatupata pale tunaposoma jinsi Nyerere alivyokuja kuwageuka wazee wa Kiislamu baada ya wao kumkaribisha, kumkirimu, kumjenga na kumfanyia kampeni kwa wapigania uhuru ambao takriban wote walikuwa Waislamu. 

Sio tu Nyerere aliwatupa wazee hao magerezani bali pia alihujumu mipango na mikakati ya wazee wetu ambayo ingekuwa na manufaa makubwa kwetu, mathalani ujenzi wa shule za msingi, sekondari na Chuo Kuu kwa udhamini wa serikali ya Misri. 

Uchungu unatupata zaidi tuonapo wenzetu ambao wazee wao walijitenga kabisa na harakati za kutafuta uhuru, wakifaidi tena kwa jeuri, jasho la kina Abdulwahid Sykes ambaye kama si moyo wa uzalendo wa Waislamu asingemuachia Nyerere apite katika uchaguzi wa TAA mwaka 1953 ambao ndio unaotugharimu hadi leo. Kwa kuzingatia mazingira ya harakati na tabaka la wanaharakati ni wazi kama kungekuwa na hisia kali za udini, Nyerere asingekuwa na sababu ya kubwaga chaki Pugu. 

Kuna matukio ndani ya kitabu cha ndugu yetu Muhammad Said ambayo humfanya msomaji muathirika afikirie kuendesha harakati za ukombozi kwa mara nyingine. Kwa kweli tusifanye masihara na kura zetu wakati wa uchaguzi. 

Cha kuhuzunisha zaidi ni kusahaulika kabisa kwa mchango mkubwa wa Waislamu katika mapambano dhidi ya wakoloni. Hapa sina budi kuwalaani wale wote waliokula njama ya kuihujumu historia ya nchi yetu. 

Nahitimisha kwa kuwahimiza Watanzania wenzangu tukisome kitabu hiki. 

Saleh Hussein Saleh, 
Moshi - Kilimanjaro 


Kutolewa kibali cha silaha, Waislamu Tanzania tumekwisha

Ndugu Mhariri 

TANZANIA kama inavyofahamika kwa viongozi wake ni nchi ya amani. Pamoja na hivyo nimesikitishwa sana tena sana niliposoma gazeti la AN-NUUR toleo Na. 172 la Oktoba 23-29 barua ya ndugu yetu katika Uislamu Abdul Omar wa Kijitonyama Dar es Salaam ambayo kichwa cha habari kilikuwa "Kutolewa kwa kibali cha kuuza silaha, Waislamu lazima tuelewe uzito wake". 

Ndugu yetu huyu ametuzindua kwa kweli kama sisi ni wenye kutafakari. Na pia kama tunashikamana na Qur’an na Sunnah za Bwana Mtume (s.a.w.) kwani nikitu ambacho hakiwezekani, nchi yetu ni kisiwa cha amani, halafu ikae kutoa vibali vya kuuza silaha. 

Kwa kweli kiakili aingii. Je, hii amani ilitoweka lini? Mpaka vibali vya uuzaji silaha vyatolewa. Kwa hiyo ndugu zangu Waislamu kama kweli tunatafakari basi tutaona kuwa ipo agenda ya siri hapa. 

Tangu gazeti hili kuiuliza serikali kuhusu tume ya majeshi ya vita ya Kikristo mpaka sasa kimya tena hatutegemei kujibiwa. 

Kwa hiyo huoni kuna kitu kinapangwa juu ya Waislamu wa nchi hii. Kwa hiyo ndugu Waislamu tupatapo habari muhimu katika gazeti la ANNUUR tuzifanyie kazi, kwani bila ya hivyo tusijeshangaa kisiwa cha amani kuwa Bosnia Nambari 2. 

Omar H. Omari, 
Gare - Umoja, 
Box 178, 
Lushoto - Tanga. 



Madai ya mashujaa wa vita vya Kagera 

Ndugu Mhariri 

NIMEGUSWA na mahojiano ya "wiki hii" yaliyochapishwa katika toleo Na. 1757 la Jumapili Oktoba 25, 1998 kati ya MT 3835 Sajini Joseph Kweka - Shujaa wa Vita vya Kagera na Bw. Martin Malera - Mwandishi wa "Maisha Wikiendi" wa gazeti la Majira. 

Amani na utulivu vinavyoimbwa na viongozi na wanasiasa wa chama tawala CCM, ukipenda; kwenye majukwaa ya kampeni za uchaguzi na kwenye hotuba za kujiimarisha kutawala, vimepatikana kutokana na askari vita kujitolea muhanga kwenye mstari wa mbele wa vita iwe ni ya Bosnia - Hezegovina, Angola, Kashmir, Algeria, iwe ni vya Ireland na kwingineko pamoja na vya Kagera. Aidha jeuri au kibri ya Serikali iwayo ile ni "nguvu za jeshi - vita". 

Nimetaja jeshi - vita kutokana na tafsiri pana tuliyonayo ya "jeshi" kwa sasa tuna: Jeshi la Polisi badala ya Polisi Tanzania (Tanzania Police); jeshi la Magereza badala ya Magereza Tanzania (Tanzania Prisons) tuna jeshi la Kujenga Taifa badala ya vijana wa huduma za taifa (National Youths Service) n.k. 

Sasa tuwarudie mashujaa wa vita vya Kagera (askari vita). Kama Sajini (Sergeant) shujaa wa vita vya Kagera alipata (alilipwa) shilingi 10,600 sijui Praveti (private) alilipwa shilingi ngapi? Katika hali yoyote ile shilingi 10,600 alizolipwa Sajini Joseph Kweka na mashujaa wenzake haziwiani na uhai wao achia mbali na kujitolea kwao muhanga; wakati familia zao zilikosa wa kutegemewa (Breade armer) kwa muda wote wa vita. 

Labda ni kweli kipindi hicho (baada ya vita) serikali haikuwa na fedha za kutosha kuwaenzi vilivyo mshujaa hao; lakini Watanzania walishuhudia sherehe kubwa kubwa na dhifa nzito zilizofanyika nchini katika ngazi zote za serikali. Viongozi wengi walitajirika na kuwaacha hohe hahe akina Sajini Joseph Kweka na mashujaa wenzake. 

Si kweli kwamba serikali ya sasa haina fedha za kutosha. Tazama magari ya kifahari yaliyomo nchini, smiling face, grass hoppans eyes n.k., yanayotumiwa na viongozi wa chama tawala na ya serikali mbali ya yale yanayotumiwa na maafisa wake waandamizi na ya waheshimiwa Wabunge, kutaja wachache tu. Kwa askari - vita akina Kweka na wastaafu katika awamu ya pili; walie tu! Kulikoni vijana na wananchi wa kawaida wengi wasio na ajira. Kuthibitisha kwamba serikali ina fedha nyingi za kutosha kuwaenzi mashujaa wake vilivyo, fuatilia miswada inayojadiliwa bungeni: Mishahara na marupurupu ya wabunge juu, wabunge wadai ruzuku ya mafuta iongezwe. 

Hivyo ndiyo sawa; lakini kina Sajini Kweka na wastaafu askari - vita wanapodai haki zao; hao ni omba omba! Angalau waheshimiwa wabunge kutoka visiwani Zanzibar na Pemba wamekuwa wakitoa hoja nzito nzito kuitaka serikali iwape askari vita wastaafu hadi awamu ya pili nyumba bora (makazi bora) na mikopo laini kutokana na viwango vya chini mno vya kiinua mgongo walivyolipwa na vya pensheni wanayolipwa. 

Majibu ya serikali kwa hoja hizo huwa: Namwomba Mhe. Mbunge aje ofisini (kwangu) tujadiliane ..." Matokeo yake siyajui. Labda wenzetu wa Pemba na Unguja. 

Mchango wangu kwa madai mbalimbali ya Wahanga wenzangu hautokamilika bila kukariri sehemu ya hotuba ya Mhe. Rais iliyotangazwa na RTD kipindi cha Majira ya Jumatano Novemba 4, 1998 saa tatu usiku. 

Sehemu ya hotuba hiyo niliyoisikia siku na saa hiyo dhidi ya rushwa ilinisisimua sana. Haina budi iende sambamba na vitendo vya vita dhidi ya watendaji wakubwa kwa wadogo serikalini wanaopuuza madai ya wastaafu na wale wanaochelewesha malipo kwa madai hayo. Vitendo hivyo sio tu vinapunguza thamani (halisi) ya madai bali pia vinaashiria rushwa. 

Naungana na MT 3835 Sgt. Kweka Joseph katika maombi yake ambayo ni maombi ya mashujaa wa vita vya Kagera wote; aidha naungana pia na wastaafu askari - vita wa awamu ya pili katika madai ya haki zao zinazoendelea kucheleweshwa na kwamba: 

Serikali iwaenzi mashujaa wa vita vya Kagera wapate nyumba bora za kuishi, wapate shamba la kutosha ukubwa wa familia kisheria na wapatiwe mkopo laini kama ni mtaji wa kuendesha shughuli za kujikimu. 

Wastaafu askari -vita katika awamu ya pili ya serikali walipwe madai yao mapema zaidi kwa viwango vitakavyokuwepo wakati wa kulipa madai yao. Wao pia wapewe mkopo laini kama hapo juu na viwango vya pensheni wanvyolipwa sasa viongezwe waweze kumudu gharama za lazima: Afya, elimu n.k. Shilingi 2,000 hadi shilingi 8,000 kwa mwezi ni nini mbele ya kodi na michango mbalimbli ya lazima. 

Nina imani kwamba serikali yetu ina uwezo kabisa wa kufanya hayo. 

V. M. Kapaya, 
Mej (RTD). 



Napinga muungano wa Waislamu na Wakristo Rufiji 

Ndugu Mhariri 

NAANZA kwa kutoa shukrani kwa Allah aliyeniwezesha kushika kalamu na karatasi na kuamuwa kutoa maoni yangu kuhusu Uislamu katika wilaya ya Rufiji nasema Alhamdulillah. Lengo langu la kuandika barua hii ni kupinga umoja wa Waislamu na Wakristo wa Rufiji. 

Kwanza nawapongeza Waislamu wa Kibiti kwa kuonyesha kusita kuunga mkono muungano huo baada ya kupata maelezo ya ujumbe kutoka kwa Waislamu wa Ikwiriri. 

Mimi baada ya kusoma taarifa hiyo katika gazeti la ANNUUR la tarehe 20-26/1998 Shaaban 1419 umoja huo umenitia wasiwasi kwani sijawahi kusikia hata siku moja hivyo napinga kwa sababu kuu mbili, kwanza Sheikh wa Bakwata anataka kupandikiza Ukristo Rufiji kwa tamaa ya misaada. 

Pili, katika wilaya ya Rufiji hakuna Mkristo hata mmoja wa kurithi kwa hiyo sasa Kanisa linafanya kila njia kwa hiyo ninatoa tamko kwa Waislamu wa Rufiji wote kupinga muungano huo pia naomba wazazi wenye watoto katika Kanisa hilo kuwatoa watoto hao kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuwabatiza. 

Wameshaanza kuwalazimisha kuomba Kikristo kabla ya kuanza kula chakula. 

Aly A. Swafi, 
Mwananyamala, 
Dar es Salaam. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita