|
|
Kufutwa kwa kesi hiyo kumezingatia ombi la wakili wa washitakiwa Bw. Twaha Taslima aliloliwasilisha mahakamani hapo hivi karibuni. Wakili Taslima aliiomba mahakama hiyo iwaondolee wateja wake shitaka hilo kwa vile lilikuwa limekwishachukua zaidi ya mwaka mmoja mahakamani hapo bila kusikilizwa. Aidha, kutosikilizwa kwa kesi hiyo kwa muda wote huo kumetokana na mashahidi wa upande wa serikali waliotarajiwa kushindwa kufika mahakamani tangu upelelezi wa kesi hiyo ukamilike hapo Septemba 4, mwaka huu. Hata hivyo, haikuelezwa ni kwa sababu gani walishindwa kufika. Wakili Taslima aliiambia mahakama hiyo kuwa wateja wake wanayo haki ya kufutiwa kesi hiyo kulingana na kifungu cha 225 (5) cha sheria ya kanuni za mwenendo wa jinai ya mwaka 1984 kinachoruhusu washitakiwa kufutiwa kesi husika iwapo itafikisha siku sitini (60) au mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa (RCO) kushindwa kutoa sababu za msingi za kuendelea kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani bila kusikilizwa. Watuhumiwa katika kesi hiyo walikuwa ni pamoja na Uliza Rashid (37), Ally Majapa (42), Ally Athumani (40), Hamisi Swalehe (50), Ramadhani Hamisi (30) na Magezi Shaaban. Awali watuhumiwa hao walidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa serikali Inspekta wa Polisi, Bw. Rashidi Ngonyani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Bw. Ezekieli Ligema, kuwa mnamo Oktoba 1, 1997 majira ya saa 5:30 usiku walivamia kituo kidogo cha polisi cha Msisiri kilichopo Mwananyamala A, wilayani Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na kuharibu mali za kituo hicho ambazo ni milango miwili, meza, mlingoti wa bendera, nyaraka mbalimbali za kituo, madirisha ya kituo na Baiskeli vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 5. Hata hivyo, baadaye shitaka lao hilo lilibadilishwa na kudaiwa katika hati nyingine ya mashitaka (charge sheet) kuwa watuhumiwa watano, ukimtoa Magezi Shaaban kuwa katika muhadhara wao huko Mwananyamala A, Jijini Dar es Slaama waliwafanyia fujo waumini wa dini nyingine na kuwazuia polisi kufanya kazi yao. Ikadaiwa pia katika hati hiyo mpya kuwa baada ya watuhumiwa hao watano kukamatwa na kuwekwa ndani katika kituo hicho cha polisi cha Msisiri, Magezi aliwachochea wafuasi wake kukishambulia kwa mawe kituo hicho na kuharibu mali za kituo hicho. Kufutwa kwa kesi hiyo yenye nambari 1383/97 kumehitimisha jumla ya kesi tano zilizokwishafutwa na mahakama hiyo mnamo miezi kadhaa iliyopita. Kesi hizo zilizofunguliwa na serikali mahakamani hapo zote zilitokana na muhadhara mmoja uliofanyika katika Msikiti wa Koma Koma (Masjid Subra) uliopo Mwananyamala A, Jijini Dar es Salaam. Kesi hizo ni pamoja na kesi nambari 1345/97 ya tuhuma ya kukashifu Ukristo na viongozi wakuu wa jeshi la polisi, kesi Nambari 1380/97 ya tuhuma ya kuwapiga na kuwajeruhi polisi wanne, kesi Nambari 1381/97 ya tuhuma ya kukashifu Ukristo na viongozi wa Kanisa na kesi Nambari 1382/97 ya tuhuma ya kukashifu Ukristo na Wakristo. MASHINE kadhaa za kikundi cha mihadhara cha Kiislamu cha Al-Mallid cha jijini zimechukuliwa na wajanja na kupelekwa polisi na hivyo kukifanya kikundi hicho kishindwe kufanya kazi ya kutoa habari za vitabu vitakatifu na nasaha muhimu kwa waumini wa dini hiyo. Akizungumza kwenye mhadhara wa Kiislamu uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya Temeke Miburani, Jijini Shiekh Said Rwanda alisema kuwa kikundi hicho cha Kiislamu kinashindwa kutangaza neno takatifu kwenye vitabu vya Qur’an na vingine vya kale kwa kwa mashine za kikundi hicho cha Al-Mallid zimechukuliwa na wajanja na kupelekwa polisi. Alisema ili maneno yaweze kuwafikia Waislamu kwa ufasaha zaidi ni lazima kwa Waislamu kutoa michango yao ya hali na mali ili kikundi kiweze kununua vifaa vingine vikiwemo vipaza sauti na mashine ya kuzalishia umeme. "Hivi vipaza sauti tulivyonavyo haviwezi kufika popote na hivyo tunahitaji vipaza sauti zaidi ili ujumbe uwafike wale walio majumbani lakini tunashindwa kufanya hivyo kwa kuwa hatuna fedha", alisema Sheikh Said. Wakati huo huo, Waislamu wametakiwa kufunga Sunnah katika mwezi huu wa Shaaban, mwezi mmoja kabla ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kama alivyokuwa akifunga Mtume Muhammad (s.a.w.) ili kupata fadhila za Mwenyezi Mungu. Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Imamu Jumbe Abdallah wa swala ya Ijumaa iliyofanyika kwenye Msikiti wa Shalsia uliopo Kawe Mzimuni Jijini. Swala hiyo ambayo ilihudhuriwa na waumini wengi alisema Waislamu hawan budi kufunga Sunnah katika mwezi wa Shaaban kwani ni muhimu kama alivyofanya Mtume Muhammad (s.a.w.) ambapo alikuwa anazifunga Sunnah hizo katika siku za Jumatatu na Alhamisi. Aidha katika hotuba yake Imamu Jumbe alisema kuwa Waislamu hawana budi kutubu dhambi zao katika mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani kwani Mwenyezi Mungu hupenda wale Waislamu wenye kutubu dhambi zao na kutakasa nyoyo zao. Alisema Waislamu hawana budi kutubu toba za kweli akifafanua zaidi toba ya kweli ni ile ya mtu kutorudia tena kosa alilolitenda. Alisema, wacha Mungu wameandaliwa makazi mazuri mara baaada ya kufariki
dunia, alisema Mwenyezi Mungu humpenda mtu aliye bora ambaye ni yule aliyeishi
muda mrefu hapa duniani na kufanya mema ikiwa ni pamoja na kumcha Mungu
na mtu mbaya ni yule aliyeishi muda mrefu na kutenda mabaya, alisema ili
kuepukana na moto wa jahanamu lazima Waislamu wabadili mienendo yao.
MISIKITI sita katika kata ya Mbagala, Jijini inakabiliwa na tatizo la maji kwa muda mrefu sasa ambapo baadhi ya waumini wa dini hiyo wameamua kuwatuma wake zao kupeleka maji Misikitini humo. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni umewashuhudia akina mama kadhaa wa Kiislamu wakichota maji kutoka kwenye visima vya Pumpu ama kwenye mabonde na kupelekea Misikitini humo. Baadhi ya Misikiti inayokabiliwa na tatizo hilo ni Masjid Arafa, Aqswaah, Hijra na Faudhia na Misikiti miwili ya Mbagala Kimbangulile na Rangi Tatu. Licha ya kuwepo na mabomba ambayo yamekuwa yakionekana kama mapambo katika Misikiti hiyo, yameonekana kuwa kero kwa waumini wa dini hiyo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni waumini wa dini hiyo walisema kuwa tatizo hilo linaonekana kuwa sugu kwa kuwa viongozi wa serikali katika ngazi za kata na tarafa wamekuwa wakilifumbia macho. Kutokana na hali hiyo, waumini wengi wamekuwa wakifanya usafi toka majumbani kwao, lakini wamekuwa wakipata shida sana mara wanaposhikwa na haja wanapokuwa Msikitini wakati wa swala. Waumini hao waliwaomba viongozi wa serikali katika ngazi hizo kuliangalia kwa mtazamo mkubwa suala la maji katika Misikiti hiyo. Wakati huo huo ukuta wa Madrasat Aqswaah umevunjika kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni na hivyo kuathiri usomeshaji wa watoto katika madrasa hiyo. Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, wanafunzi wa
madrasat hiyo walisema kuwa wanaogopa kwenda chuoni hapo kuhofia sehemu
ya ukuta uliobakia.
IMEFAHAMIKA kuwa shughuli za Bakwata katika mkoa wa Tanga haziendeshwi kwa mujibu wa katiba yake. Hayo yamefahamika kufuatia mazungumzo kati ya Sheikh Wazir Bahorera na mwandishi wa habari hizi kwenye ofisi za AN-NUUR mjini Tanga hivi karibuni. Akiwa ameshikilia katiba na kumbukumbu nyingine Sheikh Bahorera aliutaja mkutano wa wilaya ya Pangani uliofanyika Novemba 26, mwaka huu kuwa ni mfano halisi wa ukiukwaji wa katiba ya Bakwata. Ibara ya 56 ya katiba ya Bakwata imetaja kazi za mkutano kama huo, kinyume chake na maelekezo ni ajenda moja tu ya uchaguzi wa wajumbe ndiyo iliyoshughulikiwa. Hakukuwa na tathmini ya mipango, upangaji wa mipango ijayo wala uthibitishaji maamuzi, mambo ambayo yote yalihitajika. Msimamizi wa uchaguzi wa siku hiyo Bw. Jabir Rashid Kivurande aliondoka kwenye kikao pale alipotakiwa kufuata katiba ili kushughulikia upatikanaji wa Sheikh wa Wilaya badala ya marehemu Said Ali Mahime. Kufuatia kuondoka huko, wajumbe wa mkutano waliendelea na uchaguzi chini ya Bwana Bwanga Iddi ambapo Sheikh Bahorera alichaguliwa kukaimu nafasi hiyo kwa muda mpaka uchaguzi utakapofanyika rasmi. Pamoja na kupokea barua iliyosainiwa na Bwanga bado alimzuia kushiriki kwenye mkutano wa mkoa (Bakwata) uliofanyika Muheza Novemba 28, mwaka huu. Kufuatia ukiukwaji huo wa katiba, Bwana Wazir anakusudia kulitatua jambo hilo katika vyombo vya sheria ambapo atapeleka ushahidi mwingine. Pia Sheikh Bahorera ametuhumu Bakwata Tanga kuendeshwa na watu kwa maslahi
yasiyolingana na madhumuni.
IMAM Masjid Mujahiduun Sheikh Juma Mbukuzi Salim amewataka Waislamu watafute radhi za Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kuuweka mbele Uislamu kuliko kitu chochote katika maisha ya kila siku. Amesema Uislamu ndio imani sahihi mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.) atakaye uchezea Uislamu wake kwa kutafuta radhi za wanaadamu basi kitakachofuatia ni maangimizi mbele ya Allah (s.w.). Sheikh Mbukuzi ameyasema haya alipokuwa akizungumza na waumini hivi karibuni. Katika hotuba hiyo, Sheikh Mbukuzi amesema pindi linapotokea jambo katika jamii ambalo linapingana na Uislamu, ni lazima Waislamu wasimame kuutetea Uislamu dhidi ya jambo hilo kwa kutaraji radhi za Allah (s.w.). Sheikh Mbukuzi alitoa mfano kwa kugusia kuanzishwa kwa umoja wa Wakristo na Waislamu wa Rufiji (UWAWARU) kwa kusema kwamba Waislamu waliokubali kujiingiza katika umoja huo wanahatarisha imani yao kwa sababu pindi umoja huo utakapopanga miradi ya maendeleo ikiwemo ufugaji wa nguruwe, pombe na mengineyo hali itakuwaje? Kwa mnasaba huu, Sheikh Mbukuzi amesema Waislamu hawana budi kuwa macho
na mbinu za namna hii zinazofanywa dhidi ya Uislamu na kwamba Waislamu
ni lazima wazipige vita mbinu hizo kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu
(s.w.) na sio kukubali mambo yanayoonekana wazi kuwa ni dhidi ya Uislamu
kwa kutaka kuwaridihsha wanaadamu.
|
YALIYOMO
Tahariri Umaskini unachafua mazingira! Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani Qur’an yachomwa moto Shinyanga Marekani yadhihirisha Ubeberu wake MARADHI
YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu Akheri ya
zamani
UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU Wasomi
Waislamu wawajibike
Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua MADRASATUL
Husseiniyi Shadhily
Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said Misikiti yakosa maji ya kutawadhia Bakwata Tanga haifuati katiba yake Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah Je,
hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Njia
ya uzimani ni nyembamba, waionao ni wachache - 3
Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza Sayansi
na Teknolojia
Chakula
na lishe
|