AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!
 

HIVI karibuni viongozi wa kiserikali na taasisi mbalimbali walikutana mjini Dodoma kujadili suala la umasikini na uchafuzi wa mazingira. Jambo lililojitokeza wazi katika mijadala ya wajumbe ni kwamba umasikini huchangia uchafuzi wa mazingira. Mtu mwenye hekalu lake Mbezi Beach au Rasi ya Msasani; huhitaji kumwambia asikate kuni kwani ana umeme na gas. 

Lakushangaza ni kwamba kampeni hizi za kuhifadhi mazingira zinachukua sura ya mashinikizo kama yale yale ya udhibiti wa idadi ya watu, elimu ya familia, haki za wanawake, haki ya mtoto n.k. 

Wimbo huanzia kwingine na sisi kazi yetu kuitikia kibwagizo. Suala la utunzaji wa mazingira ni la azali, lakini leo huletwa kwetu kana kwamba ni jambo jipya na sisi hatujui thamani wala umuhimu wa kutunza mazingira. 

Pengine suala hili limepata umaarufu mkubwa baada ya mkutano wa Rio de Jeneiro. Au pengine ni baada ya kuanzishwa kwa mfuko wa mazingira na kuibuka kwa wimbi la wale wenye tamaa ya kupata nishani ya kimataifa wanaotembea kwenye madampo na wakati mwingine hupanda miti miwili mitatu mbele ya kamera za TV. 

Tunasema kampeni hizi huja kama mashinikizo kwani hazipewi tafsiri sahihi kwa mtizamo wetu wala hazijishughulishi na suala zima la kuondoa umasikini ambao umetajwa kwamba huchangia uharibifu wa mazingira. 

Suala la msingi hapa ni je; kipi kipo kwa ajili ya kingine. Ni watu wapo ili mazingira yarutubike au ni mazingira yapo kwa ajili ya watu. Na je, yote tuyafanyayo ni kwa kuangalia maslahi yetu au ni kufuata maagizo na kuangalia zaidi maslahi ya wengine. 

Juzi hapa wananchi wa Nzasa walichomewa moto nyumba zao na mazao kuharibiwa kwa madai kwamba wamevamia msitu na wanaharibu mazingira. Lakini upo mradi wa kamba Rufiji, wataalamu wote wa mazingira wamesema kwamba utaharibu mazingira na pia kuwafanya wananchi wakose ardhi na wapoteze raslimali zao. Hilo halizungumzwi. Halizungumzwi kwa sababu limetoka kwa wanaotufadhili na kutuletea sera na kampeni za kila aina. 

Zanzibar ina ardhi ndogo sana, lakini fukwe zote zimeuzwa na baadhi ya mashamba ya minazi yamegeuzwa hoteli na bustani za kulewea watalii. Hilo hakuna anayehoji. Wanaonekana tu kina Mtimkavu huko Nzasa. 

Marekani hivi sasa inalipa fedha nyingi sana kuwalipa fidia waathirika wa sigara, lakini ndio kwanza makampuni ya nje yanaongeza matangazo ya sigara zao walizozileta kuzimwaga huku kwetu! 

Vipo viwanda vya madawa ambavyo vilipigiwa kelele sana na wananchi baada ya wataalamu kuthibitisha kwamba vitachafua sana mazingira na kuathiri afya za watu; serikali haikujali. Tunachojiuliza ni je, viongozi wetu wanapokutana na vinara wa sera na kampeni mbalimbali duniani wanazungumza kwa mtizamo wetu au mtizamo wao? 

Lipo tatizo lingine la kulipa suala hili sura ya kitabaka. Mwenye hekalu lake lililozungukwa na bustani ya majani, miti na maua, akipita Manzese, Tandale, Jangwani na kuona vile "vidunda" vilivyojengwa bila ya mpangilio huku maji machafu yakizagaa ovyo, ule ni uchafuzi wa mazingira. 

Wengine katika semina ya Dodoma wakasema kwamba wananchi wahamasishwe wachukie umaskini. Kana kwamba yupo mtu anaupenda umaskini na kwamba utajiri na umaskini ni suala la uchaguzi. Ukisema sitaki umaskini mara unatoweka. 

Huu ni mtizamo wa kitabaka. Suala hapa sio kuwahamasisha wananchi kuchukia umaskini, lakini kuondoa dhulma na misingi yake. 

Leo Jijini Dar es Salaam kiongozi wa chama na serikali ana ekari 5,000 za ardhi, mbali na ardhi alikojenga nyumba yake; wenzake wakajenge wapi. Utawalaumuje waliojenga Jangwani katika hali hii ya wachache kujilimbikizia ardhi na huku mipango miji ikishindwa kugawa viwanja kwa wahitaji. 

Vipi kikao kama hiki kisione suala la wachache kuhodhi ardhi kuwa agenda muhimu ya kuzungumzwa. Mtu mmoja anamiliki maelfu ya ekari wakati wananchi wa Nzasa mpaka leo wanauliza waende wapi, hawapati jibu. Je, wakijenga kwenye maeneo yasiyo na mwenyewe kama Jangwani nani wa kulaumiwa. 

Ni miaka 37 baada ya uhuru ambao ulisemwa utaondoa umaskini, ujinga na maradhi, Leo maradhi bado yapo lakini afadhali zamani dawa zenyewe zilikuwepo. Wananchi wakilipa kodi na matibabu wakapata. Leo kodi wanalipa na matibabu juu yao huku umaskini ukiwa mkubwa zaidi kiasi cha waliojaaliwa unafuu kuwadhania wenzao kwamba wanapenda umaskini. 

Imekuwa bahati kwamba semina hii ya kuzungumzia umaskini imekuja wakati viongozi wa serikali wamelazimika kutangaza mali zao. 

La muhimu hapa sio mali zinazotajwa lakini hizo zilizowatia watu wasiwasi (ambazo hazitajiki) hata ikabidi wajitulize kwa kutaja hizi zinazotajika. 

Na vile vile la muhimu hapa sio kuwahamasisha wananchi wauchukie umaskini, lakini wale ambao leo wanalazimika kujisafisha kwa kutaja mali zao, watueleze wamefanya nini cha kuwapa tamaa wananchi kwamba huenda ile ndoto yao ya kuondokana na umaskini ikaondoka kama si leo kesho. 

La muhimu hapa ni kuondoa dhulma. Isiwe baadhi yanajilimbikizia maelfu ya ekari huku wengine wakikosa japo kiwanja cha meta 18 x 18 kuweka kibanda. 

Tunaposoma kwenye vyombo vya habari kwamba watu sasa wanakusanya mapesa kwa ajili ya uchaguzi 2000 tunabaki kujiuliza je na agenda ya kuboresha hali za wananchi ipo? 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita