AN-NUUR 
Na.180 Shaaban 28 - Ramadhan 1419, Desemba 18 - 24, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mashairi
  
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani (jibu la mwokozi Yesu) 
 
Bwana Dettu tafadhali, soma Biblia yakini, 
Niwapi Yesu kakili, kwitwa NENO na Manani, 
Mmemzulia Jalali, Neno kuwa Yesu tubuni, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Tubuni kabla ya Kiama, Yesu mwenyewe kasema, 
Moja tatu Luka soma, katika mbili nne soma, 
Tatu sifuri ukoma, tajua wenye hekima, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Yesu kwanza kazaliwa, Mamaye ni Mariyamu, 
Tamshi lilitolewa, hakuumbwa kama Adamu, 
Umasihi akapewa, alete kwa wanadamu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Kaumba kwanza Adamu, bila baba wala mama, 
Hawa naye binadamu, kaja bila mama soma, 
Yesu mamaye Maryamu, naye kapewa neema, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Mungu anayo hekima, hanaye wa kufanana, 
Yesu dume tumesoma, vipi Mola kulingana, 
Isaya nne sita soma, laini tano taona, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Mungu hana mshirika, Manabii walisema, 
Hata Yesu kasikika, Isaya naye kasema, 
Aya nne tano hakika, tano hadi saba soma, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Yesu alipotundikwa, alomba msalabani, 
Baba yetu mkumbukwa, nondoshee mtihani, 
Usinache nikafikwa, na kifo msalabani, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Yohana moja na moja, hadi sita ulosema, 
Hayo si ya Mola mmoja, bali ya watu nasema, 
Mola hamwambii mja, maneno yasohekima, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Yesu kasema katumwa, wewe wamwita Mungu, 
Moja saba imesema, Yohana tatu kirungu, 
Mungu mmoja imetemwa, Yesu nawe nani Mungu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Yesu hasemi uongo, kuwa na yeye ni Mungu, 
Yohana mbili mzingo, moja saba soma ndugu, 
Kweli tabaini pengo, sote baba yetu Mungu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Memzulia uongo, kuwa mwokozi mkuu, 
Tito mbili yaulongo, moja tatu hadi kuu, 
Yohana moja nne tengo, mbili nane nanukuu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Vitabu vyote vya Mungu, hasa vilivyo sahihi, 
Katika ardhi na mbingu, Muumba Mola walahi, 
Viumbe vya ulimwengu, hakuna wakukebehi, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Dettu kwanza tafakari, kama kweli Yesu Mungu, 
Kwa makini ufikiri, nani alitoa fungu, 
Yesu ndani ya kaburi, siku tatu bila Mungu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Dettu sisi twamini, Mungu wa Yesu na wote, 
Manabii duniani, aliwatuma walete, 
Mungu moja tuamini, hana mshirika kote, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Hajatokea Nabia, tangu Mtume Adamu, 
Tamati wa Arabia, eti mwana wa Maryamu, 
Mkombozi wa dunia, hakika Mungu hakimu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Siku kiama kikija, Mungu kutoa hukumu, 
Utajaona kioja, kumbe Yesu Mwisilamu, 
Kanisa hakulionja, kaketi na Ibrahimu, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Hapa pangu kituoni, kalamu naweka chini, 
Dettu soma Kuruani, ukweli utabaini, 
Uache uhayawani, utakwisha motoni, 
Mwokozi Mwenyezi Mungu, siyo Yesu asilani. 

Juma Hassan, 
P.O. Box 70026, 
Ubungo, Dar es Salaam. 

Mtukufu Ramadhani 
 
Bismilahi Raufu, Mhariri gazetini, 
Mimi sio maarufu, hapo kwenu kilingeni, 
Nataka kuwaarifu, Islamu na Misheni, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Mwezi huu mtukufu, jina lake Ramadhani, 
Utende matakatifu, ninatoa ilani, 
Utapata utukufu, mwisho wake duniani, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Najaribu kuhubiri, bado kupata yakini, 
Imekuwa desturi, ifikapo Ramadhani, 
Kutuuzia futari, bei juu magengeni, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Mwezi huu mashuhuri, asiyejua ni nani? 
Biashara hushamiri, dukani hata sokoni, 
Yafaa ujihadhari, unapo uza sokoni, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Kiumbe fanya nadhari, bei ziwe wastani, 
Usitake utajiri, kudhulumu maskini, 
Watu wote si tajiri, wanunuao sokoni, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Imekuwa staili, ifikapo Ramadhani, 
Bei zenu kubadili, sokoni na madukani, 
Bidhaa kuuza ghali, hata haya hamuoni, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Natoa hii kauli, AN-NUUR gazetini, 
Wasikie Waswahili, walio bara na pwani, 
Lanikera jambo hili, tumugope Manani, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Huo ndio ukafiri, mimi nawaambieni, 
Kudhulumu mafakiri, waliojaa madeni, 
Hii kweli sio siri, mimi sijui kwa nini? 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Mohammadi na kakiri, huko kwao Arabuni, 
Alizifanya safari, akiwa biasharani, 
Aliuza kwa kadiri, hakufanya uhaini, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Katitamati shairi, Mhariri samahani, 
Mungu atakusitiri, uiendeleze fani, 
Na akujaze na heri, upate nishani, 
Mwezi huu Mtukufu, kiumbe wacha dhuluma. 

Ustadh Abdallah Aziz (Darigube) 
Masjid Qiblatain English Medium Primary School, 
DAR ES SALAAM. 
 
Juu 
 
YALIYOMO 
 
Tahariri
Umaskini unachafua mazingira!

Mauaji ya Mwembechai: Spika wa Bunge aombwa atoe gharama za kuunda Tume

UWAWARU yafa Rufiji

UN yaidhinisha udhalimu wa Marekani

Qur’an yachomwa moto Shinyanga

Marekani yadhihirisha Ubeberu wake

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: SEXUAL SADISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Kitengo cha Zaka chazinduliwa Dar

Tume ya Jiji kubomoa Msikiti wa vipofu

Akheri ya zamani
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC. USA

UWAWARU yaleta nusura Ikwiriri

Tamko la Masjid NNUUR juu ya kuanzishwa kwa UWAWARU

Kuanzishwa kwa UWAWARU

Wasomi Waislamu wawajibike
Na Mwandishi Wetu

Albucasis  936 - 1013 (CE)

Ijue Uhuru madrasa - Morogoro

Madrasa Akhlaqil Islamiya yapiga hatua

MADRASATUL Husseiniyi Shadhily
Na Jamillah Nassoro
 
Hatimaye kesi ya kushambulia kituo nayo yafutwa

Changieni vyombo vya mihadhara - Sheikh Said

Misikiti yakosa maji ya kutawadhia

Bakwata Tanga haifuati katiba yake

Sheikh Mbukuzi ataka Waislamu watafute radhi za Allah

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 3
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache - 3
Na Yasin Valerian Massawe

Sheikh Omar Bashir afikishwa mahakamani

Mufti pekee kuidhinisha watu kufunga

Nguruwe wanaofugwa maeneo wanayoishi watu kusababisha magonjwa ya kuambikiza

200 wamesilimu

Sayansi na Teknolojia 
[Kuiweka Modem kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Mlo wa Daku] 
 
Tangazo 
New Book: The untold story of the Muslim struggle against British Colonialism in Tanganyika. 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita