|
Na. 082 Jumatano Januari 10 - 16, 2001 |
|
|
|
|
|
Tirivyogo la sekta ya elimu
KUMEKUWEPO na madai ya serikali ya kuboresha sekta ya elimu hapa nchini. Pia kumekuwepo na malalamiko kwamba sekta ya elimu kama zilivyo sekta zile muhimu kama sekta ya afya zimepuuzwa na serikali. Pamoja na madai ya serikali yetu hayo ya kuboresha sekta ya elimu tumekuwa tukishuhudia kudorora kwa sekta ya Elimu. Ripoti za tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanataaluma zipo zinazozungumzia kushuka kwa kiwango cha elimu itolewayo hapa nchini. Hata hivyo bado taarifa zinazotolewa na maafisa elimu wakati wa kutangaza matokeo ya darasa la saba wamekuwa wanasema kwamba wanafunzi wanapata alama ndogo mno. Sidhani kama kuna Mtanzania yeyote ambaye hajui hali halisi ya shule zetu kuanzia shule za msingi na sekondari. Shule zilizo nyingi hazina walimu wa kutosha hasa zile za vijijini; hazina vitabu hata vile vya kiada achilia mbali vile vya ziada (Rejea). Shule nyingi za sekondari hazina maktaba. Hata maktaba zile za mikoa hazina vile vitabu vya kumsaidia mwanafunzi wa sekondari Kwani maktaba hizo zimejaa vitabu vya zamani wakati wa mkoloni na vile vilivyopitwa na wakati huko Marekani na kuvitoa msaada kwetu. Walimu hao wachache walioko mashuleni, kwanza malipo yao yaani mishahara yao ni midogo mno. Mishahara hiyo haiwezi kumfanya ayamudu maisha yake yeye peke yake, sembuse akiwa na familia. Pamoja na vimishahara uchwara wanayotakiwa kulipwa hawalipwi kwa wakati! Matokeo yake walimu wanakuwa na mazingira magumu sana kimaisha na hivyo kutokufundisha jinsi inavyotakiwa. Wengi wao wamekuwa wanakiuka maadili ya kazi zao kwa sababu ya mkanganyo wa maisha unaowakabili. Mazingira ya shule zetu ndio kabisa hayasemeki. Kwani madawati hayapo na pale yalipo hayaotoshi. Vyumba vya kutosha kufundishia havipo. Hata hivi vilivyopo bado ni vichakavu, vinavuja. Hakika havifai kwa mtu kukaa ndani kwa jinsi vinavyotisha. Zana za kufundishia hazipo. Hii yote inapelekea matokeo mabaya ya wanafunzi katika mitihani yao. Shule nyingi za sekondari hazina maabara kwa ajili ya "practicals" za masomo ya Biolojia, Kemia na Fizikia. Hivyo wale wanachaguliwa kusoma masomo hayo ya sayansi katika kidato cha Tano na Sita wanashindwa kusoma kama inavyotakikana. Matokeo yake ni kushindwa katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita. Kama hali ndio hii kwanini kiwango cha elimu kisishuke? Kwani hali hii haijulikani mpaka tupate wataalamu kutoka nje kuja kutuambia hili? Serikali kwanini haifanyii kazi ripoti za tafiti zilizofanywa. Wazazi wengi wamekuwa wakishindwa kuwaandikisha watoto wao kwa ajili ya kujiunga na darasa la kwanza. Sababu ya kushindwa kufanya hivyo ni kutokuwa na uwezo wa kulipia ada na michango mbalimbali inayotakiwa shuleni. Michango hiyo ambayo haizidi shilingi hamsini elfu, pamoja na kumnunulia mtoto sare ya shule! Hili liko wazi kwa serikali kwani kila mara hasa mwaka huu watoto wameambiwa waandikishwe. Hapa mkoa wa Dar es Salaam wameambiwa walimu wakuu wasitoze gharama zozote mbali na ada. Walimu wameambiwa waandikisha watoto wengi. Wengi wamewaandikisha na kuahidi kuwapeleka kwa afisa elimu aliyewataka waandike ili awapatie sehemu za kusomea! Hebu angalia mvutano huu, jamani! Kuna watoto wengi ambao wanachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za serikali, lakini wameshindwa kufanya hivyo. Sababu kubwa ni kushindwa kupata gharama za kulipia. Wengine wengi wamekuwa wanashindwa kuendelea na masomo yao kwa sababu hiyo hiyo ya umaskini. Misingi hii ndio hali halisi ya wananchi wa Tanzania, kwamba ni maskini mno. Hakuna juhudi zozote ambazo zinafanywa na serikali yetu kuweza kurekebisha hali hii; mbali na kuwadanganya wananchi kuwa hakuna mtoto atakayefukuzwa kwa kukosa ada au kulipia gharama za masomo. Wanafunzi wamekuwa wanafukuzwa mashuleni kwa kukosa kulipia gharama za masomo yao hasa ada. Wengine wengi wanashindwa hata kufanya mitihani yao ya mwisho kwa kukosa ama kulipa ada ya mtihani ambayo ni kati ya shilingi 15,000/- hadi 20,000/-! Wengine vyeti vyao vinashikiliwa na utawala wa shule husika kwa kudaiwa ada n.k. Hivi sasa Baraza la mitihani limeanzisha utaratibu wa kutoa "result slip". Katika ofisi zake; ambako kila mwanafunzi anatakiwa atoe sh.2,000/-. Hivi hawa walioko huko Kigoma, Mtwara, Karagwe na kwingineko watafikaje hapa Dar kuchukua hizo "result slip" zao? Na kwanini waje hapa Dar es Salaam na wasitumiwe huko mashuleni kama ilivyokuwa zamani? Sasa yule ambaye hana hizo pesa ndio kabisa cheti chake hapati. Hivi ni kweli kwamba wananchi ambaye hana pesa ya kugharimia matibabu wanapata huduma bure katika zahanati na hospitali za Serikali? Lakini si serikali ilishasema kwamba atakayeshindwa kuchangia gharama atatibiwa bure! Pamoja na hayo hospitali zilizo nyingi hazina madawa. Mara nyingi tunaandikiwa kwenda kununua dawa hizo. Huyu ambaye ameshindwa kulipa sh. 500/- atapata wapi dawa? Hivi ni nani hasa anayetakiwa kuihoji serikali inayowadanganya wananchi juu ya haya? Kwanini, wananchi tunashindwa kuwahoji viongozi wetu? Wasomi wa vyuo vikuu walipokuwa wanataka kusitishwa kwa awamu ya tatu ya uchangiaji gharama za masomo ambayo inategemewa kuanza mwaka ujao wa fedha na masomo 2001/2002; tumeona yaliyowapata. Walisimamishwa masomo kwa kipindi cha miezi mwili na zaidi. Hata wengine kuambiwa wasiguse ardhi ya vyuo husika yaani wametolewa kafara! Wanafunzi hao walikuwa na madai mbalimbali ambayo ni pamoja na kuongezewa mkopo wanaopata kwa siku, mazingira mabaya ya kusomea na kuishi na ukosefu wa mafunzo kwa vitendo. Maskini, hawa wanafunzi wameonekana ni vijana wabaya, wasiojua hali ya serikali yao, wasio na fadhila kwa serikali yao, wasiojali watu wengine! Haya madai yao yanayojulikana kwa mtu yeyote Mtanzania, kwanini wanawatesa vijana hawa na hata kuwatishia amani. Pindi waendeleapo kudai haki zao? Makala mbalimbali zimeandikwa kuelezea madai ya wanafunzi hawa. Vipindi vya Luninga vimerushwa hewani kuonyesha mazingira na kuzungumzia madai ya vijana hao dhidi ya serikali. Pamoja na yote hayo vijana hawa wamebezwa sana na serikali yao ya Tanzania na kutishiwa kuwafukuza chuo. Nadhani, serikali bado hawataki wananchi wajikomboe kwa kupata elimu. Wanafunzi walipewa masharti mbalimbali lakini moja limenishangaza sana. Kuambiwa eti suala la mkopo ni la mwanafunzi binafsi na serikali. Hivi serikali kama ilijua hili tangu hapo nyuma kwanini ilikuwa inajadili masuala ya wanafunzi na serikali za wanachuo? Kwanini kila mwanafunzi hakuitwa pekee pekee? Hapa ni kuwatia hofu wasomi bila shaka. Hata hivyo bado kuna hata watu wengine ambao wanajua hali halisi ya uzito wa madai ya wanafunzi hao, lakini bado nao wanawabeza! Wanawajengea hofu! Hivi kama mzazi anashindwa kumpeleka mtoto wake shule ya msingi, anashindwa kumlipia ada shule ya sekondari, mzazi huyu ataweza kuchangia gharama za kumsomesha mtoto chuo kikuu? Mimi binafsi bado naamini kwamba wanafunzi wa Taasisi za elimu ya juu hawatokata tamaa kuendelea kudai madai yao. Ni lazima wapate elimu iliyo bora. Ni lazima kila raia awe na haki ya kusoma kwa kadri yao uwezo wao. Sidhani kama watabweteka eti kwa sababu wametishiwa kufukuzwa. Hili lazima wasomi walijue fika kwamba, mara nyingi serikali inatumia mbinu hizi kuwanyima watu haki zao.Mifano iko mingi sina haja ya kuibainisha hapa. Cha msingi ni kuwa na msimamo wa pamoja. Kuna Mhariri wa gazeti moja la kila siku ambaye amewaasa wanafunzi wa vyuo vikuu kwamba wasichezee nafasi zao. Mhariri huyo aliamua kuchukua nafasi ya serikali ya kuwaasa vijana na kuonyesha kwamba serikali haina uwezo wa kuyatekeleza matakwa ya wanafunzi hao. Mhariri huyo alisema, "Pesa wanayodai haiwezi kuwaondoa kwenye umaskini wowote. La msingi ni kufikiria nini kitafuata baada ya kumaliza masomo. Huko vijijini na mitaani ndiko kuliko maisha ya kweli, siyo chuoni ambao wanapewa fedha bila kujua zinapatikana wapi na Watanzania wengi wanaishije." Ameendelea kusema Mhariri huyo, "Fedha wanazolipwa wasomi wetu hawa ni nyingi zaidi ya wanazolipwa watumishi wengi wa Taifa hili kama vile walimu, polisi, makarani, wauguzi na wengine katika idara na taasisi mbalimbali." Mhariri huyu, mimi binafsi nampongeza kwamba anajua vyema hali ya Watanzania. Lakini ninapata walakini naye, kwani hashauri njia muafaka ya jinsi watu wanavyoweza kutatua matatizo yao. Sidhani kama kumlaumu mtu aliyekosea na kumjengea mazingira ya woga unakuwa unamsaidia. Huku ni kupindisha madai yake kwa makusudi kabisa. Mhariri huyo anegonekana kwetu kuwa mtu wa busara zaidi kuwajenga moyo vijana wetu. Hivi huyu ni nani atakayetetea haki zako kama wewe unayedhulumiwa huonyeshi kusikitishwa na kumlaani huyo anayekudhulumu? Si sahihi kwa wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu kutetea maslahi ya walimu, polisi, makarani, wauguzi na wengine katika idara na taasisi mbalimbali. Bali hawa watumishi wenyewe ndio wanaotakiwa kupigania maslahi yao. Hata hivyo si sahihi kulinganisha kipato cha mtu mmoja na mwingine bila kujali mazingira, kazi na majukumu mbalimbali anayoyatekeleza mlipwaji. Mbona huyu Mhariri hajawahi kukemea au kulaani hao viongozi wanaojipangia mishahara minono minono. Mbona hao wanaoshikilia madaraka wanajipangia masurufu makubwa kama vile kiinua mgongo cha mamilioni ya fedha, magari ya kifahari n.k. hawajaambiwa na kulaaniwa kwa kuendelea kujineemesha na kuishi maisha ya anasa bila kujali watumishi aliowataja Mhariri? Hii inanionesha kwamba Mhariri huyo ama ana nidhamu ya woga au anatumiwa. Ni matarajio ya wananchi kuwa vyombo vya habari vitawasaidia katika kuonyesha kero zao na madai yao kwa viongozi wanaojifanya vipofu na walimwengu wanaopenda haki. Mchango wa vyombo vingi vya habari umekuwa mara nyingi ni wa upande mmoja. Yaani vinaonekana kuegemea kwa watawala wafisadi, wanaotenda dhuluma na wasiojali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Na pia vyombo hivi kama alivyofanya Mhariri huyo anayeandikia gazeti ambalo linadhaniwa kuwa huru, kuwalaani na kutaka hatua kali zichuukuliwe kwa wale ambao wanaotaka mazingira, mishahara na maslahi yao viboreshwe. Mhariri huyo alionyesha kwamba wasomi hao wanapenda maisha ya anasa wawapo vyuoni. Nadhani huyu Mhariri ana upeo mdogo wa kuchambua mambo. Maisha gani ya anasa? Namshauri Mhariri huyu awe anafanya uchunguzi ama utafiti wa mambo kabla ya kuzungumzia suala lenyewe. Sina haja ya kuonesha mchanganuo wa madai ya wasomi kwani makala mbalimbali za watu mbalimbali zilishafanya hivyo. Hivi sasa ni wakati ambao haki inapaswa kutendeka. Ni wakati ambapo vyombo vya habari vinapaswa vizungumzie hali halisi ya wananchi. Tunapaswa kuainisha kwa upeo yale yote yanayowakabili wananchi na yale wanayofanyiwa na serikali. Kusema kweli nasikitika kwamba vyombo vingi vya habari ambavyo vinaegemea upande mmoja wa serikali havikuwa tayari kuelezea vilivyo yale yaliyokuwa yanazungumzwa na wasomi. Sio kweli kwamba wasomi walitaka tu kuongezewa maslahi (mkopo) bali hata suala la mazingira ya kusomea na kuishi, mafunzo kwa vitendo, awamu ya tatu ya uchangiaji wa gharama katika taasisi za elimu ya juu n.k. Mhariri ameeleza katika tahariri yake kwamba Taifa hili linahitaji wataalamu watakaoweza kuliendeleza. Asante. Sasa hawa wataalam watapatikana vipi bila ya kuwa na mazingira mazuri ya kusoma na kuishi? Wataalam gani ambao hawajifunzi kwa vitendo? Tunahitaji kubadili mawazo yetu na muelekeo wetu, kama kweli tunataka maendeleo ya kweli. Suala la "Elimu" si suala la mchezo. Ni budi kwetu sisi tuonyeshe jinsi viongozi wetu wanavyowadanganya wananchi katika sekta hii muhimu. Na pia inabidi tuwasaidie wale wanaodhulumiwa ama wanaodai haki zaokwa kuonesha ukweli wa madai yao. Tusiwakatishe tamaa. Tusiwe wasaliti wa wananchi wetu kwa kuficha ukweli wa mambo. Mara zote yule anayedhulumiwa huonekana ni muovu, asiye na fadhila, mtovu wa nidhamu, mbabaishaji na kadhalika mbele ya yule anayemdhulumu. Huyu anayefanya dhuluma mara zote hutumia hila na kila aina ya ujanja na ikiwezekana pesa kuonesha kwamba yeye ni mtu safi. Atatumia kila aina ya nguvu aliyonayo kumjengea hofu na nidhamu ya woga mdhulumiwa. Huku ni kujenga volcano ambayo siku moja itajalipuka. Mwisho wa hayo yote upo. Ipo siku ambapo watu watachoka kudhulumiwa, kuonewa ama kuibiwa na kudanganywa. Hapa ndipo volcano iliyokuwa inajengwa itakapolipuka. Nawaasa wasomi kwamba wasikate tamaa kwani mara
zote kupigania haki si suala la mchezo wala lele mama. Kuna kuuawa. Hivyo
ni suala la kuangalia kwa busara na kuwa makini. Mimi nawatakia kila la
heri katika mapambano yao.
|
YALIYOMO
MAONI
YETU
Wananchi
wamwambia Mkapa:
Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi ‘Hajj Trust’ yaongeza huduma kwa mahujaji MAKALA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Mwenye Macho……
|
|
|
|
|