NASAHA
Na. 082 Jumatano Januari 10 - 16, 2001
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Mwenye Macho...

Demokrasia haiwezi kujengwa kwa kuvunja katiba 

Na Torika Kanyika

MOJA ya sifa za nchi inayodai kuongozwa kidemokrasia ni kuwa na viongozi wanaoijali, kuihifadhi na kuilinda katiba. Sifa hii ya uongozi wa nchi ndiyo inayoipa haki serikali kudai kuwa nchi yake inaongozwa kwa misingi ya sheria.

Suala la kuijali katiba katika nchi yetu ni la msingi sana kwa sababu viongozi wetu huapa mbele ya Jaji Mkuu au Rais wa Jamhuri kuwa wataitetea, kuilinda na kuihifadhi katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Ni dhahiri kuwa kiongozi yeyote anayeamua kutenda au kuamua jambo linaloashiria kuipuuza katiba ya nchi basi anaipunguzia serikali yake sifa ya kuwa ni yenye kuongozwa kwa misingi ya sheria na pili anavunja na kwenda kinyume na kiapochake. 

Iwe itakavyokuwa, kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia itampasa aiheshimu katiba ya nchi. Endapo ataona kufungu chenye utata katika katiba hiyo aliyoapa kuilinda bado itampasa kuilinda hadi taratibu za marekebisho ya katiba zitakapofuatwa na kifungu hicho kubadilishwa. 

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Nenjamini William Mkapa katika hotuba yake ya mwaka mpya alikaririwa akisema kuwa anaunga mkono hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Wakati Polisi wakitoa sababu ya kuvunjika kwa amani endapo mikutano hiyo itafanywa, Mheshimiwa Rais alitoa sababu ya kupata muda wa kulijenga taifa. Ilielezwa kuwa rais anaona kuwa bora wananchi watumie muda wao kufanya kazi za uzalishaji kuliko kuhudhuria mikutano ya hadhara. 

Hakuna taaifa kuwa ipo sehemu yoyote nchini ambapo Chama chaMapinduzi (CCM) kimetoa taarifa kufanya mkutano wa kuwashuru wapiga kura halafu polisi wakazuia mkutano. Bali zipo habari za uhakika kuwa vyama vya upinzani hususan chama cha Wananchi (CUF), CHADEMA na TLP vimetoa taarifa ya kufanya mikutano na kuzuiliwa na polisi. 

Dhana iliyojengeka miongoni mwa watu ni kuwa polisi ilikuwa inazuia mikutano ya vyama vya upinzani kwa maelekezo ya Ikulu. 

Juma lililopita Maspika wa Jumuiya ya Madola waliitembelea Tanzania. Bwana Maura Mwingira ambayeni mwandishi wa habari msaidizi wa Rais aliongea na Maspika hao kwa niaba ya Rais. Katika mazungumzo hayo Rais alionekana kusikitishwa na mwamko mdogo walionao wananchi wa Tanzania juu ya demokrasia ya vyama vingi. Kisha akaongeza kuwa bado kuna tatizo katika utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi. 

Rais alinukuliwa kusema maneno yafuatayao:- "Moja ya jukumu tulilonalo ni namna tunavyoweza kumudu kipindi hiki cha mpito kwa sababu ufahamu wa watu wetu kuhusu mfumo wa vyama vyingi bado ni mdogo na itachukua muda mrefu....". Rais akaongeza kusema, "Tunajaribu kutoa elimu ya uraia kupitia mikutano ya hadhara lakini athari yake bado ni ndogo." 

Kwa sura ya nje inajengeka hisia ya serikali kuwa na shauku kubwa ya kuwaona watu wake wanakuwa na mwamko wa demokrasia ya vyama vingi. Pia inaonekana kuwa serikali inasikitishwa na ugumu wa kufikiwa lengo hili unaotokana na udhaifu wa mbinu zinazotumika sasa na athari (side effect) ya mfumo wa chama kimoja uliodumu kwa miaka mingi hapa nchini. 

Kwa sisi ambao Tanzania ni nyumbani kwetu halihii inatia mashaka. Mimi siamini kwamba eti rais ana kosa usingizi kwa vile mfumo wa vyama vingi haujaeleweka kwa kwa watu wake. Wala siamini kuwa mfumo huo haujaeleweka kwa kiasi ambacho serikali ingependa ionekane. Na sidhani kwamba Maspika hao wanayodawa ya tatizo hili kama lipo, bila kujali kuwa lipo kwa kiasi gani. 

Moja ya sababu za kunifanya kuwa na mashaka na kauli hiyo ya serikali kuhusu mwamko wa wananchi juu ya mfumo wa vyama vingi ni kauli ya rais katika salamu zake za mwaka mpya kama nilivyodokeza awali. Kauli hiyo ya kuunga mkono kuzuiwa mikutano ya hadhara ni kinyume na katiba yetu Ibara (20) kifungucha (I), kwamba "Kila mtu anastahili kuwa huru....kukutana na watu wengine kwa hiari yake..., kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hata zaidi. Kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo. 

Sababu ya pili ni kuwa serikali tuliyonayo inaonekana zaidi kuvutiwa na kuwepo kwa mwamko mdogo wa wananchi juu ya mfumo wa vyama vingi kuliko vile inavyokerwa na mfumo huo. 

Ukosefu wa mwamko unadaiwa kuwepo zaidi vijijini kuliko mijini. Awali iliwahi kuripotiwa katika vyombo vya habari na mikutano ya hadhara vya vyama vya upinzani kuwa wananchi wa vijijini wanatishwa kuwa kukubali chama cha upinzani ni kukaribisha vita. Hata gazeti la Chama cha Mapinduzi (MZALENDO) liliwahi kuandika habari ya upotashaji kuhusu vigezo vilivyotumika kumpata Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba kwa kudai kuwa ni msomi wa dini ya Kiislamu aliyebobea ambaye ataweza kutimiza agenda ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Kiislam. Imewahi kuelezwa pia kuwa video za vita vya Rwanda zilioneshwa sehemu mbali mbali nchini kwa lengo la kuwatisha wananchi wasivipigie kura vyama vya upinzani eti kwa kisingizio kuwa vitaleta vita. 

Haya yalifanyika 1995,na kituo kimoja cha Television jijini kilishutumiwa mwaka jana kwa kuonesha picha zilizokusudiwa kuwatisha wananchi kipindi cha karibu na uchaguzi. 

Sababu nyingine inayonifanya niamini kuwa serikali inapendezewa na kuwepo mwamko mdogo ni jinsi inavyoitumia redio yaTaifa (RTD) na televisioni yaTaifa (TVT). 

Muda mwingi zaidi umetumika kuvibomoa vyama vya upinzani kwenye RTD na TVT na wakati huo huo kuijenga CCM. Sikumbuki kumwona na kumsikia kiongozi wa chama cha upinzani akipewa nafasi alieleze taifa ni kwanini anapingana na CCM na anazo sera gani mbadala. Ila wengi tumesikia vipindi kama Zama za Uwazi na Ukweli (TVT) na meneno hayo (RTD). 

Kila mwenye kupima anaweza akajua ni kwa kiasi gani vipindi hivyo vinasadia harakati za kujenga au kubomoa mwamko wa siasa za ushindani. 

Kama kwamba hayo hayatoshi Bunge likapitisha sheria yakuondoa ruzuku ya uchaguzi kwa vyama, sheria ya kukata rufaa kwa Tshs.500,000 (diwani) na Tshs. 5,000,000 (mbunge) na pia kuzia mamlaka yoyote kuihoji tume ilipomtangaza rais. Yote haya kwangu mimi ni maamuzi yanayofanywa na chama tawala yenge lengo la kuusimika mfumo wa chama kimoja ndani ya vyama vingi. 

Wakati mwingine mwamko wa wananchi uwe ni juu ya kupenda nchi yao au mfumo fulani unaweza kupimwa kwa kuangalia kiwango cha ugoigoi wao. 

Kama sheria zinazoelekea kuwakandamiza au kuwabagua zitapitishwa nao wasionekane kuhoji, basi hicho chaweza kuwa ni kigezo cha mwamko duni. Kama kiongozi au mamlaka fulani itaamuwa jambo ambalo ni kinyume na katiba licha ya kula kiapo cha kuilinda katiba na wananchi wasitie neno lolote,. Hali hiyo pia itachukuliwa kuwa ni mwamko mdogo. 

Mimi naamini kuwa kesho itakuwa tofauti na leo. Naamini pia kuwa wananchi ndiyo mamlaka iliyo juu ya mamlaka zote, ndiyo maana tunasikia dhana ya ridhaa yawananchi. 

Historia imeonesha kuwa wananchi wanapojaribu kutekeleza wajibu kama raia na kukutana na vigingi mwishowe huchoka. Hapo tena kujiamulia kufanya mambo yao kama wananchi. Na wakati huo hawatahijaji kibali cha mamlaka yoyote. 

Itakuwa tu wananchi ndiyo wenye nchi yao na ndiyo wenye maamuzi ya mwisho. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 
 

MAONI YETU
Mapinduzi Zanzibar yameleta kilichokusudiwa?

Wananchi wamwambia Mkapa:
Mbumbumbu wa demokrasia waliomo katika chama tawala ni hatari zaidi

Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi

‘Hajj Trust’ yaongeza huduma kwa mahujaji

DONDOO MUHIMU

MAKALA
Jamii ijihadhari viongozi wasaliti

MAKALA
Msimamo wa Pengo haushangazi

KALAMU YA MWANDISHI
Kitendawili cha millenia: Urais bila dola

MAKALA
Dhana ya kumwabudu Mungu anayeafiki udhalimu lazima tuikatae

MAKALA
Mapinduzi Zanzibar: Dhuluma bado ipo

MAKALA
CCM haiwezi kuondosha umasikini Tanzania

MAKALA
Tirivyogo la sekta ya elimu

Mwenye Macho……
Demokrasia haiwezi kujengwa kwa kuvunja katiba

HABARI ZA KIMATAIFA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Baadaya Mkapa kushindwa kusaidia: Prof. Lipumba aombwa kuiombea Tanzania FIFA
  • Mtwa aanza kulala mapema
  • Salvatory aitwa Mtibwa

  •    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita