NASAHA
Na. 082 Jumatano Januari 10 - 16, 2001
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 
 

Uchumi na 'Thiolojia' ..1
Dhana ya kumwabudu Mungu anayeafiki udhalimu lazima tuikatae 





Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

THEOLOGY ni elimu kama ilivyo Biology. Neno "theology" limetokana na maneno mawili ya Kiyunani Theos lenye maana ya Mungu, na ology lenye maana ya hekima ama ufahamu, kwa ajili hiyo thiolojia ni uwelewa wa mtu kuumwelekea Mungu. Hatari ya elimu hii ni kwamba uelewa wa mtu pindi unapochukua mwelekeo hasi kumhusu Mungu, basi na matokeo yote ya uhasi wake, au uovu na udhalimu wote utokanao na mtu huyo kuiacha kweli ya Mungu nao hunasibishwa na Mungu moja kwa moja. Nadhani hapa ndio mwanzo wa chimbuko la dhana ya kumwabudu Mungu ambaye pia anaafikiana ama kuuridhia udhalimu. Hata hivyo napenda ieleweke wazi kuwa Mungu wa kweli, yule aliyeiumba dunia hii na kuifanya iwe hivi ilivyo, Mungu yule aliye asili ya uhai wote ulioko duniani yeye ni Mungu wa haki. Kamwe haridhii udhalimu uwao wote, hata ungefanywa na mtu anayejiita Mtume, Nabii, au Malaika. Mungu yuko kinyume na udhalimu, na udhalimu wote uko kinyume na Mungu. Kwahiyo tusidanyike na hekima iwayo yote.

Kiongozi mmoja wa kidini alitoa kauli yake kwenye gazeti moja la kidini litolewalo kila Jumapili, na alikaririwa akisema umaskini wa Tanzania kama taifa, unatokana na dhambi yake ya kuilaani Israeli. Kulingana na uelewa wa mtu kama huyu, anayeiona Israeli katika mtazamo hasi na ulio tofauti kabisa na uhalisi wa mambo, kama mtu kama huyu angepewa wasaa wa kutuwakilisha Watanzania basi angekuwa ni mtu wa kuridhia mambo yote na kila tendo linalotendwa na Israeli kama dola. Hata haya matendo ya kinyama ya kuuwa Wapalestina yanayolaaniwa na dunia nzima, bila shaka yeye haoni haja ya kulaani kutokana na imani yake hasi kwamba kile mwenye kuibariki atabarikiwa, maana kuna wakati kiongozi huyo alitoa mfano wa utajiri wa Marekani kwamba asili yake umetokana na taifa hilo kuibariki Israeli. Huu ni mfano hai wa uwanja wa mapambano kati ya uchumi na "Theolojia." Uchumi ni elimu ya ina yake wakati theolojia nayo ni elimu ya aina yake wakati theolojia nayo ni elimu ya aina yake lakini elimu zote hizo zinafungwa katika kufungo kimoja tu nacho ni ukweli. Nje ya ukweli elimu yoyote ile itakayokuwa bado haitamfaa binaadamu maana itaishia kumfanya kuwa mtumwa, ndiyo maana Bwana Yesu akasema mkikaa katika neno langu nanyi mtaijua kweli, na hiyo kweli itawaweka huru. Kinachomweka mtu huru siyo ukweli kama ilivyo, bali ni kule kuujua ukweli huo. Kama ukweli utakuwako, lakini mtu asiujua bado ukweli huo kama ulivyo hautamnufaisha kitu mhusika kwani utakuwa nje ya ufahamu wake, na kwa maana halisi utakuwa ni sawa tu na kutokuwako kwani ukweli utakuwa hauko kichwani, na siku zote binaadamu anasema lile analolijua na pia kufanya hilo analollijua. Tuchukue mfano wa umeme, karne nyingi nyuma ukweli kuhusu umeme haukujulikana na kwa maana hiyo umeme ni kama haukuwako, wakati duniani nguvu za umeme zilikuwako isipokuwa kilichokosekana ni ujuzi. Tukitumia lugha ya Yesu, hi kule kutoijua kweli kuhusu umeme ndiko kulikowafanya wakale kuwa watumwa wa giza. Juzi ameibuka Mhubiri mwingine kwa jina Daktari, na Alhaji Omari Juma na kutoa mahubiri yake yenye mweleko hasi kumhusu Mungu. Mahubiri hayo, Dk. Omari aliyatoa wakati wa sherehe za Idd, na alinukuliwa akisema "kama Mungu hataki uwe Rais, hata ukiamua kulipua mabomu na kuua watu wote, au serikali iitishe uchaguzi kila mwezi huwezi kuwa Rais." Kama Dkt. Omari angeyanena hayo katika majukwaa ya siasa, ningemwelewa na wala nisingejisumbua kumjibu lakini hapa alinena, na waumini katika hafla za kidini na kwa jili hiyo anamtaja yule Mungu wa dini na siyoMungu wasiasa. 

Ninaanza kumjibu Alhaji kwa kusema kwanza hakuna Mungu wa namna hiyo. Hakuna Mungu anayeweza kutaka fulani awe Rais, na eti Mungu huyu asitake kabisa fulani awe Rais, badala yake wanaoweza kutaka na kutotaka ni wanadamu. Mungu wa kweli anawatakia wanadamu wote yaliyo mema kwa maana aliwaumba watu ili wafaidi mema, ndiyo maana sehemu fulani Mungu amenena kwa kinywa cha Nabii wake akisema hakika ninayajua mawazo ninayowawasia, kwamba ni mawazo ya amani, nawawazia yaliyo mema, mpate amani. Ingekuwa Urais ni matakwa ya Mungu, basi sisi wananchi tusingekuwa na haja ya kupiga kura wala kufanya kampeni tungelikaa tu na kumwomba Mungu, kisha Mungu kwa kutumia vinywa vya watumishi wake angenena nasi kwamba nataka fulani ndiye awe rais wa nchi fulani. Lakini hapa ambapo mikono yetu imeinuka kutenda, na bongo zetu zimetumika kupanga na kupangua, basi hapo mapenzi, na matakwa ya Mungu yamewekwa kando na badala yake kilichopo ni bidii ya kutekeleza matakwa yetu wenyewe. Katika nukta hii Mungu asitajwe iwe kwa mema au kwa mabaya maana yote yatokanayo na bidii za aina hii ni matokeo ya mapenzi ya wanadamu, ambayo ndani yake mna wingi wa ufisadi. 

Kwa kweli Mungu alitaka viongozi walioko madarakani sasa ndio wawe washindi, kumbe kwanini basi uweko wizi wa kura? Ni kwanini uwepo udanganyifu, na mizengwe mingine? Ni kwanini wahusika hamkusema mapema kwamba wacha mapenzi ya Mungu na yatimizwe, yaani watu wapige kura kwa uhuru, watu wachague hao wanaowaridhia! Ukweli ni kwamba hamkuruhusu uhuru kwa kuhofia kwamba upigaji kura ulio huru na wa haki unaweza kutoa matokeo yaliyo kinyume na matakwa yenu ndiyo maana mkaamua kutumia FFU kutoa mikong'oto, kutumia JWTZ kutisha watu na Ma-RPG, na mwishowe kupora masanduku ya kura. Mapenzi ya Mungu wa kweli hayatekelezwi katika mazingira ya aina hii labda yawe mapenzi ya Mungu wa kuchonga na Mungu wa kutengenezwa na wanadamu wenyewe ili tu ahalalishe tamaa zao chafu. Mheshimiwa Alhaji Omari Juma nachukua fursa hii kukufahamisha kwamba hata wale waliofanya biashara ya utumwa (biashara ya kinyama) bado walitumia maneno ya Mungu ili kuhalalisha udhalimu wao. Walitumia wahubiri wa dini (zote mbili Ukristo na Uislamu) kujenga hoja kwamba ni mpango wa Mungu kwa Waafrika kuendelea kupelekwa ng'ambo wawe watumwa. Huko Marekani kwa mfano, kulikuwako na Wainjilisti waliohubiri Injili kwa watumwa, mara ya kwanza wamiliki wa mashamba, na wenye kuhodhi watumwa walihofia kwamba kwa kuwa Injili inazungumzia masuala ya uhuru isije ikasababisha maasi miongoni mwa watumwa, lakini hatimaye wakaja kugundua kwamba siri iko kwenye msisitizo, endapo Injili itasisitizia watumwa kuwatii mabwana zao, basi Injili hiyo inageuka kuwa silaha nzito kuzidi usimamizi wa kipolisi kwani kila neno mtumwa aliyeiamini Injili atafanya kila neno kama kwamba anamfanyia Mungu. Ni katika kipindi hiki ambapo mafundisho kama ya kudai akupigae kofi shavu moja, mgeuzie na la pili yalipobuniwa na kuingizwa kinyemele kwenye Injili ya YESU wakati Yesu mwenyewe hakuyasema wala hakukusudia neno lake litumike kumpa faida binaadamu mwingine kwa njia ya kumpa hasara mtu mwingine. Hapa pia ndipo lilipo chimbuko la utajiri wa Marekani kama taifa maana kwa muda wa miaka mingi limetumia "cheap Labour" ya utumwa kujiongezea uzalishaji huku familiaza wale wanaotumikiwa zikiwekeza akili zao na muda wao kwenye elimu. 

Kwahiyo mtu kukurupuka na kudai eti Mungu ameibariki Amerika kwa sababu tu ya siasa za Amerika kuelekea Israeli ni sawa tu na kuhubiri ushirikina kwamba hirizi inalinda, hirizi inafanikisha, ama chale za waganga zinafanya kazi. Ni ushirikina huo huo unaopelekea mtu kusema ni Mungu ndiye aliyetaka tuwe marais, wakati kulikuwako na wezi kibao na udanganyifu kem kem. Dhana ya kumhusisha Mungu na udhalimu ni lazima tuikatae...... 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

MAONI YETU
Mapinduzi Zanzibar yameleta kilichokusudiwa?

Wananchi wamwambia Mkapa:
Mbumbumbu wa demokrasia waliomo katika chama tawala ni hatari zaidi

Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi

‘Hajj Trust’ yaongeza huduma kwa mahujaji

DONDOO MUHIMU

MAKALA
Jamii ijihadhari viongozi wasaliti

MAKALA
Msimamo wa Pengo haushangazi

KALAMU YA MWANDISHI
Kitendawili cha millenia: Urais bila dola

MAKALA
Dhana ya kumwabudu Mungu anayeafiki udhalimu lazima tuikatae

MAKALA
Mapinduzi Zanzibar: Dhuluma bado ipo

MAKALA
CCM haiwezi kuondosha umasikini Tanzania

MAKALA
Tirivyogo la sekta ya elimu

Mwenye Macho……
Demokrasia haiwezi kujengwa kwa kuvunja katiba

HABARI ZA KIMATAIFA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Baadaya Mkapa kushindwa kusaidia: Prof. Lipumba aombwa kuiombea Tanzania FIFA
  • Mtwa aanza kulala mapema
  • Salvatory aitwa Mtibwa

  •    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita