|
Na. 082 Jumatano Januari 10 - 16, 2001 |
|
|
|
|
|
Kitendawili cha millenia
Na Maalim Bassaleh WIKI iliyopita Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Wananchi, (CUF),Zanzibar, Ndugu Juma Duni Haji, alikutana na waandishi wa habari, katika ukumbi wa Idara ya habari, MAELEZO, na kuwaeleza kuwa kama serikali za chama tawala zitashindwa kushughulikia kasoro zilizomo katika Muungano, basi chama chake kitalipeleka swali hilo katika Mahakama ya Kimataifa, kudai dola ya Zanzibar iliyomenzwa na serikali ya Muungano! Huku Bara baadhi ya wanasheria, wanasiasa pamoja na vyombo vya habari,vimeibeza na kuiponda kauli hiyo ya chama cha CIUF. Wote,kwa umoja wao, wamedai kuwa CUF inababaisha tu. Wamesema kisheria chama hicho hakiwezi kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa; kwasababu mahakama hiyo ni tofauti na mahakama za kawaida. Mahakama ya kimataifa haipokei mashtaka kutoka kwa watu au vikundi binafsi; bali inapokea kesi kutoka nchi wanachama. Kwaajili hiyo, wanadai, hakuna uwezekano wa CUF kupeleka mashtaka yake, katika mahakama hiyo yakakubaliwa. Kwa vile mimi simweledi wa mambo ya sheria ninashindwa kuelewa ukweli ulipo. Lakini jambo moja ni dhahiri. Wapo viongozi wa nchi waliofunguliwa kesi katika mahakama hiyo bila ya nchi zao kuwafungulia mashtaka. Ni kwa misingi gani Mahakama hiyo husikiliza kesi za watu hao? Hilo ndilo nisilolijua! Lakini hivyo inaingia akilini kuwa chama cha CUF kitakurupuka tu na kudai kuwa kitalipeleka swali hilo katika Mahakama ya kimataifa, kienyeji tu, bila ya kwanza kupata ushauri wakisheria? Hata hivyo kuna mambo mawili yamejitokeza. Kwanza wale wote wanaopinga CUF kwenda katika Mahakama ya Kimatifa wanatokea Bara,hakuna hata mmoja miongoni mwao,aliyetokea Zanzibar! Ni kwanini? Na jambo la pili hakuna hata mmoja kati yao aliyekanusha kwamba hakuna mgogoro ndani ya Muunano. Kwa maana nyingine ni dhahiri kuwa wanakiri kuwapo kwa mgogoro; lakini hawakubaliani na jinsi chama cha CUF kinavyotafuta ufumbuzi wa mgogoro huo. Juu ya hivyo wao wenyewe wameshindwa kutumia ujuzi na utaalamu wa katika kuelekeza namna ya kuutatua mgogoro huo. Chama tawala pamoja na serikali zake, mara kwa mara, zimekuwa zikikataa kuwepo kwa mgogoro ndani ya Muungano. Zinakiri kuwapo kwa kero ndogo ndogo ambazo zinadai zinaweza kutatuliwa na chama hicho pamoja na serikali zake zilizopo madarakani. CUF nayo, kwa upande wake, inaona upo mgogoro, tena mkubwa! Na inaona kuwa sichama tawala wala serikali zake mbili zinazoweza kutatua mgogoro huo. Chama cha CUF kinaamini kuwa mgogoro uliopo unaweza kutatuliwa na serikali ya Zanzibar kwakushirikiana na serikali ya Tanganyika! Lakini katika mfumo wa Muungano, tulionao sasa, wa serikali mbili, serikali ya Zanzibar na serikali ya Muungano, hiyo serikali ya Tanganyika itatokea wapi? Kwa kweli chanzo cha mgogoro wote kinaanzia hapo! CCM inasema Muungano uliokusudiwa ni wa serikali mbili tu kama ulivyo sasa. Mfumo wa serikali tatu utakuwa una gharama kubwa na gharama hizo zitabebeshwa Tanganyika. Ndiyo maana serikali ya Tanganyika ikauliwa ili kupunguza gharama za uendeshaji! CUF inadai kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alifanya ujanja kuiua serikali ya Tanganyika, kwa makusudi, ili apate mwanya wa kuidhoofisha dola yaZanzibar. Akisisitiza hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Ndugu Juwa Duni alisema kitendo cha kuifuta serikali ya Tanganyika hakikuwapo katika makubaliano ya awali ya Muungano. Alidai kuwa hizo zilikuwa ni mbinu za Mwalimu Nyerere katika kutaka kuimeza Zanzibar. Lakini kuna baadhi ya Wana-CCM Bara wanaodhani kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika na kwa hivyo kulikuwa hakuna haja kamwe ya kuwa na serikali ya Zanzibar. Wanaona serikali ingalikuwa ni moja tu! Gazeti moja la Kiwahili, linalotoka kila siku, katika toleo lake la Jumapili, Januari 7, 2001,limeeleza kuwa Mwenyekiti wa CCM, Mikoa wa DaresSalaam, Kapteni Mohamed Ligora amesema eti Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika, hata kabla ya Muungano wa 1964! Gazeti hilo limemkariri kiongozi huyo wa CCM akisema, "Zanzibar ni eneo la Tanganyika, ndiyo maana hata Sultani enzi hizo alitawala visiwa hivyo, mpaka maeneo kadhaa ya mikoa ya Pwani, huku Bara!" Kama kweli Kepteni Ligora ametamka hivyo, basi haoni kuwa maneno yake hayo yanadhihirisha kuwa kumbe Tananyika nisehemu ya Zazibar na siyo Zanzibar eneo la Tanganyika? Pili, Sulani wa Zanzibar hakuwa akitawala mikoa ya Pwani tu ya Tanganyika, bali na mwambao wote wa Kenya ulikuwa chini ya mamlaka yake. Basi kwa hoja hiyo ya Kapteni Ligora Zanzibar itakuwa ni sehemu ya Tanganyika au ni sehemu ya Kenya? Labda jambo la kutafakari hapa ni kuwa jee, CCM-Bara inamwunga mkono Kapteni Ligora kwa hayo aliyoyasema au la? Ingawa CUF inashutumiwa kutaka kuuvunja Muungano kwa kudai serikali tatu; lakini kwa ukweli, hakuna wanaohatarisha kuvunjika kwa Muungano kuliko wale wanaotaka Muungano waSerikali moja au wanaodai kuwa Zanzibar ni eneo la Tanganyika! Ingawa Mahakama Kuu ya Rufaa, Tanzania, imesema kuwa Zanzibar si dola, madamu Wana-CCM Zanzibar, wataona kuwa wanaserikali ya Zanzibar na Rais wa Zanzibar hilo haliwashughulishi. Lakini siku itakaupoamuliwa kuwa kwa vile Zanzibar si dola, basi hakuna haja ya kuwa na serikali wala Rais wa Zanzibar hapo ndipo sokomoko litakapoibuka! Na hapo ndipo itakapoeleweka kama Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika au la. Haidhuru tunaambiwa kuwa Zanzibar si dola, lakini wapi katika ulimwengu huu inapopatikana nchi yenye serikali yake na Rais wake lakini ikawa haina dola? Jee! Hicho sikitendawili? Na kama ni kitendawili basi mwaguzi wake ni nani, kama si Wazanzibari wenyewe? Katika nchi moja yanaweza kuwepo mabunge mawili au hata zaidi. Halikadhalika wanaweza kuwepo Mawaziri Wakuu na Mawaziri viongozi wawili au watatu; lakini hakuna nchi yo yote yenye Marais wawili isipokuwa Tanzania tu! Nikwa nini? Natumai tukiweza kujibu swali hilo ndipo tutakapo pata ufumbuzi wa mfumo gani wa Muungano uliokusudiwa katika Makubaliano ya Muungano baina ya waasisi wa Muungano huo, Hayati Mwalimu Julius Kamabrage Nyerere wa Tanganyika na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume wa Zanzibar. Kama Zazibar haikukusudiwa kuwa ni dola na waasisi hao, mbona walikubaliana kuwa na serikali ya Zanzibar na kwamba kiongozi wa serikali hiyo asiwe ni Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi, bali awe ni Rais na pia awe ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Pili, lazima tujiulize, Mzee Karume aliamini kuwa yeye ni Rais wa Dola ya Zanzibar au ni Rais wa Zanzibar bila ya dola? Tukiuzingatia ushahidi ufuatao wa kimazingira utaweza kutusaidia. Kabla ya Muungano serikali ya Tanganyika ilikuwa na uhusiano wa kibalozi na serilali ya Ujerumani Magharibi (FRG). Baada ya Mapinduzi serikali ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar nayo ikaitambua serikali ya Ujerumani Mashariki(GDR) na kuiruhusu kufungua ubalozi wake Zanzibar. Hicho kilikuwa ni kipindi cha vita baridi. Katika kipindi hicho serikali iliyokuwa na uhusiano na Ujerumani Mashariki haikutakiwa iwe pia na uhusiano na Ujerumani Magharibi ikailalamikiaTanzania kuwa na uhusiano naUjerumani ya Mashariki.Ikaishinikiza serikali ya Muungano waTanzania kama ilitaka kuendelea na uhusiano na Ujerumani Maghribi basi iilazimishe Zanzibar ivunje uhusiano na Ujerumani Mashariki(GDR). MwalimuNyerere akamshauri Mzee Karume afunge ubalozi wa Ujerumani Mashariki na kuvunja uhusiano nao. Mzee Karume alikataa katakata kufuata ushauri wa Mwalimu Nyerere.Jambo hilo lilikaribia kuuvunja muungano; lakini MzeeKarume alisema potelea mbali hata kama muungano utavunjika basi na uvunjike lakini hataufunga ubalozi wa GDR Zanzibar. Tanzania, peke yake, ulimwenguni ikawa ndiyo nchi yenye uhusiano wa kibalozi wa Ujerumani zote mbili. Jambo la kutafakari hapo ni kuwa shughuli za mambo ya nchi za nje zinaangukia katika mambo ya muungano; mbona Mzee Karume alikataa kuvunja uhusiano na GDR? Kwa tukio hilo unadhaniaje Mzee Karume alikuwa akiichukulia Zanzibar kama ni dola au kama nchi isiyokuwa na dola? Tukio jingineni wakati wa kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Azimio hilo lilikataz viongozi wasijilimbikizie mali na majumba ya kupangisha. Mzee Karume aliliponda sana Azimio hilo kutamka hivyo. Nakumbuka aliitisha mkutano wa hadhara, na kusema Azimio gani lisilokuwa na HUSNUL-KHAATIMA? Ni maneno ya Kiarabu yanayotumiwa naWaislamu kumaanisha MWISHO MWEMA. Mzee Karume kwahivyo,alilipinga Azimio la Arusha kwa sababu halikuzingatia maslahi ya viongozi mwisho wao watakapofikia umri wao kustaafu. Kama hawajajiwekea akiba ya vijumba vya kupangisha hawatakuwa na mwisho mwema katika maisha yao. Alisema waziwazi kuwa kama Azimio la Arusha litakuwa hali na HUSNUL-KHAATIMA basi mwisho wake ni kisiwa cha Chumbe! Kama MzeeKarume alikuwa haamini kuwa Zanzibar ni dola angalisema maneno hayo? Rais Mstaafu wa Zanzibar,wa awamu ya tano, Dkt.Salmin Amour aliwahi kusema yeye ni Karume mdogo! Kwanini alisema hivyo? Pia, aliwahi kuwaambia Watanzania Bara waliokuwa wakimpinga wasijaribu kutingisha kiberiti! Maneno hayo yalikuwa yana maana gani? Mwisho, kama alikuwa anajua kuwa Zanzibar si dola na kwahivyo haiwezi kupinduliwa unafikiri angaliwaweka kizuizini wale watuhumiwa 18 wa chama cha CUF na kuwafungulia mashtaka ya uhaini? Aidha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Zanzibar, Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi, ametunga kitabu kueleza kasoro zilizopo katika Muungano na hasa jambo la kudhoofishwa kwa dola ya Zanzibar. Lakini mpaka hii leo ushauri wake haukupatikana sikio wa kuusikiliza! Jee! Huku sikuficha donda? Na ni mgogoro huo huo ndio ulimpelekea ajiuzulu! Kwahivyo, swali hapa siyo kukubaliwa au kukataliwa
CUF kupeleka mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa, jambo la msingi jee
upo mgogoro ndani ya muungano au haupo? Na kama upo vipi utatatuliwa? Wanasheria,
wanasiasa kazi kwenu!
|
YALIYOMO
MAONI
YETU
Wananchi
wamwambia Mkapa:
Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi ‘Hajj Trust’ yaongeza huduma kwa mahujaji MAKALA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Mwenye Macho……
|
|
|
|
|