NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Riwaya
 
 

Ndoto ya mafanikio

MTUNZI: Abu Firdaus 

NDOTO hii ni ya kweli au si kweli? Sawa na ndoto za mchana yaweza kutokea au ni ndoto za maskini ambaye mara nyingi huota mafanikio au.... Haya ni baadhi ya maswali ambayo Hidaya alikabiliana nayo mara tu aliposhtuka toka alipotokea usingizini. 
 

HIDAYA ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Mzee Yasini Mussa akimfuatia kaka yake Mussa ambaye alipewa jina la babu yake. Hidaya pia ni moja ya watoto waliozaliwa katika familia zenye hali duni ya kimaisha. Familia ambayo haina uhakika hata wa mlo wa kila siku. 

Mzee Yassin ambaye umri wake ulikaribia miaka 50, tayari ngozi yake ilionyesha kuchoka kama mzee wa umri wa miaka tisini. Kazi yake kubwa ilikuwa kuuza maji mitaani kwa kutumia mkokoteni. Mama yake alikuwa muuzaji maarufu wa karanga na ubuyu pale mtaani. Kazi yake hii ilimfanya afahamike kama "Mama Ubuyu" jina ambalo awali halikumpendeza. Lakini baadaye alilizoea na hakujisikia vibaya kuitwa jina hilo. 

Hidaya na Mussa ni miongoni mwa watoto waliolelewa katika nyumba ya Mzee Yassini. Nyumba hiyo haina maji wala umeme. Nyumba ambayo iliendelea kuwepo kwa uwezo wa Mungu kwani wakati wowote ingeweza kuanguka kwa upepo au mvua kubwa ingenyesha. 

Hidaya na Mussa wote walifanikiwa kupata elimu ya msingi japo katika mazingira magumu. Umbali kutoka nyumbani kwao mpaka shuleni ilikuwa takriban kilomita kumi au zaidi. 

Baada ya kupata elimu yao ya msingi, Mussa yeye hakufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari. Hivyo ili kutoa mchango wake katika familia alijikuta akiungana na baba yake katika kazi ya uuzaji wa maji. Hii ilimpa nafuu kidogo baba yake kutokana na umri kuwa mkubwa. Hivyo tayari alianza kupata tabu kupandisha mkokoteni mlimani kutoka bondeni. 

Upande wa pili, Hidaya alichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Jangwani. Alijisikia furaha sana kuona amechaguliwa, lakini swali kubwa ilikuwa ni jinsi gani ataweza kumudu gharama za masomo pale shuleni kuanzia ada, sare na matumizi mengine? Hali ilikuwa ngumu zaidi kimawazo kwa mzee Yassin na mkewe "Mama Mibuyu". Walishindwa kupata usingizi vizuri kwa kutafakari nini la kufanya ili kumsaidia mtoto wao." Tutafanya nini sisi yarabi? Kula kwetu tabu, nyumba inaanguka, hela ya mafuta ya taa tabu, nguo.... Tena maelfu ya Hidaya! Aah!", alimaka Mzee Yassin. Siku zilivyozidi kusogea ndivyo muda wa kuripoti shuleni ulivyokaribia na ndivyo wazee wale walivyozidi kuchanganyikiwa zaidi. 

Jioni moja Mzee Yassin alimwita Mama Mussa na kutoa mawazo yake juu ya kile alichodhani kinaweza kuwasaidia. "Mimi nadhani niende kwa Mzee Faida nimuelezee shida yangu kisha nimuombe atusomeshee mwanetu Hidaya kwa makubaliano kwani nitakuwa namfanyia kazi zake bila kupokea ujira kutoka kwake zaidi ya kumsomesha Hidaya. Kwa kuwa tumeishi naye vizuri nadhani anaweza kutusaidia", alisita kidogo Mzee Yassin na kuendelea, "wewe unaonaje wazo hili", aliuliza "ni wazo zuri, lakini hali ya hapa nyumbani unaifahamu, tutaishi vipi? Alijibu Mama Mussa. Itabidi Mussa afanye kazi yangu ya kuchota maji. Kwa bahati nzuri ameishafahamu wateja karibu wote wa maji. Basi wasiliana naye uone atalipokea vipi wazo hili. 

Mussa! Mussa! Aliita Mzee Yassini. Ilichukua kitambo kabla ya Mussa kutokea. Baada ya muda hivi Mussa alirejea nyumbani na kuambiwa na dada yake kuwa alikuwa anahitajika barazani.Aliondoka kuelekea barazani ambapo aliwakuta wazazi wake.Alikaa chini na kuwasabahi kisha akasema "samahani nilikuwa nimekwenda kwa Mama Karim kuchukua fedha za maji niliyompelekea mchana.Niliporejea nikaambiwa na dada Hidaya kuwa unaniita," alieleza Musa kwa adabu. "Ndiyo mwanangu," alijibu Mzee Yassin. "Mwanangu nimekuita, hali yetu ya hapa nyumbani unaifahamu. Shida tulizonazo unazielewa. Zaidi ya yote shida ya dada yako Hidaya juu ya shule unaielewa vizuri kwa sababu wewe mwenyewe ndio ulituleta barua na kutusomea kutoka huko shuleni kwao Jangawani." Wakati mzee Yasin akiendelea kuzungumza, Mama Mussa alisimama na kuondoka huku akiwaacha wao wawili pale ukumbini. "Tumekaa na mama yako na kukubaliana kuwa mimi nitafute kazi na ujira nitakaopata uwe kwa ajili ya kumsomesha dada yako Hidaya tu, na wewe utatumia mkokoteni wangu kuchota maji. Fedha utakazopata zitatusaidia kwa matumizi hapa nyumbani. Tunadhani hii inaweza kuwa njia pekee ya kumsaidia dada yako Hidaya. Sijui wewe unalionaje wazo letu?",alisema mzee Yasin. "Mimi nafikiri bila shaka, kwa sababu elimu ndio urithi pekee usiofilisika, tushirikiane kwa namna yeyote ile ilimradi dada Hidaya aweze kusoma," alijibu Mussa. Majibu haya yalimpa moyo Mzee Yassini kiasi cha kuona dalili za mafanikio. 

Wakiwa wanamalizia mazungumzo yao mara Hidaya alitokea na kuwakaribisha chakula ambacho alikuwa amewaandalia wakati wakiendelea na mazungumzo. Walinawa na kuanza kula huku wakibadilishana mawazo ambapo Mussa alimhakikishia baba yake juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu kufanikisha yale yanayowakabili. Baada ya kumaliza kula waliagana na kwenda kulala. 

Asubuhi na mapema waliamshana na kufanya ibada ya sala pamoja kama kawaida yao kisha Musa alichukua mkokoteni na vyombo vyake na kuelekea katika kazi yake ya kuchota na kuuza maji. Hidaya alianza shughuli za usafi pale nyumbani na kuwaandaa wadogo zake ili waweze kwenda shule wakiwa wasafi. Mzee Yassini alielekea mtaa wa jirani kutafuta miti miwili mitatu na kamba na kurejea. Alianza kufanya ukarabati katika chumba cha watoto ambacho kilikuwa kimechakaa zaidi huku akisubiria muda wa kwenda kwa Mzee Faida. 

Yapata saa tatu asubuhi Mzee Yassini alielekea kwa Mzee Faida. Ilimchukua dakika kumi kufika nyumbani kwa Mzee Faida." Alhamdulillah", alijisemea Mzee Yassini baada ya kumuona Mzee Faida akizunguuka huku na huko katika banda lake la ng'ombe. Alimsabahi na kisha wakajuliana hali za nyumbani. Baada ya Mzee Faida kumaliza kukagua mifugo yake, walielekea kwenye baraza la nyumba yake. Mazungumzo yaliendelea kitambo, kisha Mzee Yassin alieleza shida yake kuhusu kusaidiwa katika kumsomesha mwanae Hidaya. Mzee Faida alilipokea wazo hilo. Kwa shauku aliyokuwa nayo Mzee Yassin aliuliza kabisa lini na yepi yatakuwa majukumu yake. Mzee Faida aliona ni nafasi ya kumpa majukumu yote mazito kwa sababu Mzee Yassin alikuwa ana shida. "Utakata majani ya ng'ombe wote sita, utasafisha banda lao kila siku, utawapa maji na kujenga banda kila linapoharibika, kwa kifupi utahudumia mifugo yangu yote yaani ng'ombe, mbuzi, kuku na kazi utakazopangiwa hapa nyumbani". Mzee Yassin alikubali yote kwa kujua kuwa shida haijui muda. Alikubali na kurejea nyumbani kwake kunako saa saba mchana . Jioni ile alimwita Mama Mussa na kumueleza "mafanikio" ya safari yake kwa Mzee Faida. Walifurahi kwa kujua kuwa tatizo la jinsi gani watamsomesha mwana wao Hidaya litakuwa limekwisha. 

Siku ya kuanza kazi ilipofika, Mzee Yassini aliamka asubuhi na kuwaamsha familia yake yote. Walifanya ibada yao ya sala kama kawaida. Hivi ndivyo Mzee Yassini, Mama Mussa na familia yao wanavyoianza siku yao yeyote ile. Baada ya hapo kila mmoja alielekea kwenye jukumu lake. Mzee Yassini alifika kwa Mzee Faida asubuhi sana na kuanza kusafisha mabanda yote ya ng'ombe na kuku.Baada ya hapo alielekea bondeni kukata majani ya ng'ombe. Mzee Faida alipoamka yapata saa tatu alikuta Mzee Yassin amemaliza kazi ya usafi na mizigo miwili ya nyasi imeshafika. "Umefika saa ngapi hapa," hili lilikuwa swali alilouliza Mzee Faida baada ya kujuliana hali. "Nilifika asubuhi tu", alijibu Mzee Yassini. Mzee Yassin alifanyishwa kazi nyingi kupita kiasi utadhani Punda lakini yote alivumilia. Kazi ziliendelea vizuri. Kila leo Mzee Faida alizidi kuneemeka kwa kuwa alimpata mfanyakazi mwenye shida na aliyejitoa kwa lolote. 

Tarehe ya Hidaya kuripoti shuleni ilifika na Mzee Faida alimgharimia ada, sare, madaftari na kila chenye kuhitajika. Hidaya alianza shule.Kama ilivyo kwa shule yeyote ile huwakutanisha wanafunzi wenye kutoka katika familia zenye uwezo tofauti. Hidaya alishuhudia wenzake wakiletwa shuleni kwa magari ya kifahari, wakila vyakula na kunywa vinywaji vyenye gharama kubwa kubwa wakati wa mapumziko. Wakati watoto waliotoka katika familia bora wakila chips, mayai, keki n.k. wakinywa soda, maziwa, cone mix n.k. Wenye uwezo wa chini wao walikula vipande vya mihogo iliyokaangwa. Waliotoka katika familia hohe hahe kama Hidaya walibaki kuwaangalia wenzao kwa macho ukiachia siku moja moja ambazo Hidaya hutoka nyumbani na ubuyu aliopewa na Mama yake. 

Vishawishi shuleni vilikuwa ni vingi mno vilivyokuwa vimemzunguka Hidaya. Kuanzia nyumbani, njiani wakati akielekea shuleni na hata shuleni kwenyewe kote ilikuwa hivyo hivyo. Kitu pekee kilichomsaidia Hidaya kupambana na vishawishi ni malezi bora aliyopewa na wazazi wake. Pamoja na kuwa Hidaya alikuwa na umbile na sura nzuri vyenye kuvutia hasa, alijihifadhi vizuri kufuata maadili ya dini yake kitu ambacho kilipelekea vijana wengi ambao huwaharibia mabinti maisha yao kwa tamaa zao, kutothubutu kumsogelea na kumueleza upogo wao. Hivyo Hidaya alibaki na pambano moja kubwa nalo ni kuishinda nafsi yake juu ya yale aliyokuwa akiyashuhudia. Lakini hata hivyo wasichana kama Dama, yule mwigizaji wa Kenya katika mchezo wa Tausi, hawakukosekana. Walijitahidi sana kumfanya Hidaya awe kama Sitti,mwigizaji mwingine wa Kenya mwenye vituko. Ajivue heshima yake na kujiunga katika uchafu na maangamizi mabaya ili tu na yeye eti aweze "kufaidi maisha" kwa kupata fedha za matumizi ya ziada. Halikuwa jambo rahisi kumfanya Hidaya kuwa Sitti. Hidaya alithamini zaidi utu wake, alimuhofu zaidi Mola wake, na aliamini kuwa siku moja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu angeweza kuwa na hali nzuri yeye na familia yake. Lakini pamoja na hilo alikumbuka msemo usemao "mwana wa mbuzi yake kamba". Hivyo pengine alihisi kufaulu kuingia kidato cha kwanza ilikuwa kwa bahati "mbaya". 

Hidaya aliendelea vizuri na masomo yake pale shuleni. Siku moja akitokea shuleni, alikuta mkutano mkubwa wa watu katika viwanja vya Jangwani. Haikuwa kawaida kwa Hidaya kujisogeza na kushiriki mikusanyiko ya watu. Lakini siku hii alihisi hamu ya kujua kulikoni. Aliamua kujisogeza ili asikie na kushuhudia japo kwa muda mfupi kisha arejee nyumbani kumsaidia Mama yake kazi za nyumbani. Alimkuta mama mmoja aliye mahiri sana katika kuzungumza aliyekuwa akiwahutubia watu wengi waliomzunguuka. Alimtambua baadaye Mama huyu kwa jina moja tu la Fatma. Mama huyu alikuwa amevaa stara yake, aliongea kwa kujiamini na kuwa kivutio kwa watu wengi. Hidaya alimsikiliza kwa makini Mama huyu ambaye hotuba yake kwa kiasi kikubwa ilihusu haki za kila mmoja katika jamii. Baada ya mama huyu kumaliza kuongea, alisimama kijana mmoja aliyejitambulisha kama Mohammad Seif. Hidaya hakuendelea kukaa pale, badala yake alielekea nyumbani kwani tayari muda wake wa kawaida wa kurejea nyumbani ulikuwa umepita. 

Akiwa njiani Hidaya alijiuliza maswali kadhaa. Hivi kumbe hata wanawake wapo waliosoma kiasi hiki? Kwanini Mama yangu hakusoma kama mama huyu na badala yake anauza ubuyu? Hivi mama yeye hakupenda kuwa afisa au mkurugenzi? Hivi baba yake hakupenda kuwa mhandisi au meneja? Kwanini basi hawakusoma wakawa katika nafasi na hali bora za kimaisha. Maswali yote haya hayakupata majibu yenye kujitosheleza. Lakini cha msingi kwake ilikua je, na yeye anaweza kusoma na kufikia kiwango cha yule mama aliyemuona jangwani? Ikiwa swala ni kusoma na kufaulu mitihani, hakuona sababu kwanini asifikie huko. 

Hivyo Hidaya aliongeza bidii shuleni. Kitu pekee kilichokuwa kikwazo ni kukosa nafasi na mazingira mazuri ya kusoma awapo nyumbani. Hata hivyo aliutumia vizuri muda wote awapo shuleni na mchana kwa ujumla. Haikumchukua muda mrefu Hidaya kuwa nyota na mwanafunzi wa kutumainiwa darasani. Wanafunzi wengi walimuhitaji awasaidie katika masomo mbalimbali darasani. 

Mwaka wa pili wa Mzee Yassini kufanya kazi kwa Mzee Faida, Mzee Yassini bado alihimili kazi ngumu na nzito ambazo si tu zilimfanya alale hoi bin taabani lakini pia kudhoofisha mwili wake. 

Inaendelea toleo lijalo

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita