|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
|
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa
WAZAZI wa wanafunzi wa Kiislamu katika baadhi ya shule za sekondari za serikali jijini Dar es Saaam wameilalamikia hatua ya shule hizo kuwazuia wanafunzi wa Kiislamu kushiriki hafla za kidini na kutoa vitisho ambavyo vitawafanya wawe wakisoma kwa hofu hali ambayo wamesema itaathiri matokeo yao kitaaluma. Imeelezwa kuwa katika shule ya sekondari ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, wanafunzi kadhaa wa Kiislamu waliitwa na uongozi wa shule na kisha kuhojiwa siku za Ijumaa na Jumatatu kufuatia kuonekana tangazo lilobandikwa shuleni hapo kuwaalika Waislamu kuhudhuria khitma ya kuwaombea dua Waislamu waliouawa Mwembechai. Wazazi wa wanafunzi wa Kiislamu waliohojiwa na timu ya waalimu wameliambia gazeti hili kwamba watoto wao walihojiwa maswali ambayo wao wanaamini hayakuwa na sababu yoyote kitaaluma na wala kiutawala. Bw. Masoud, mmoja wa wazazi hao amesema miongoni mwa maswali waliyoulizwa ni nani kati ya Sheikh Ponda na Sheikh Mbukuzi angehutubia. Kwa mujibu wa mzazi huyo baada ya kuhojiwa siku ya Ijumaa, Februari 11, wanafunzi hao waliitwa tena kuhojiwa siku ya Jumatatu Februari 14, siku moja baada ya kufanyika kwa khitma hiyo ambapo waislamu wote walikuwa wamealikwa. "Walimu hawa hawakuchoka hata kidogo. Mahojiano ya Ijumaa hayakuwatosha, wakawasalisha (wakawahoji) tena jana Jumatatu. "Eti wamewauliza, 'wangapi mlihudhuria khitma'; tajeni wanasheria waliozungumza; 'Ponda alisema nini; (Ponda) alipoingia mlishangilia kwanini?" alisema mzazi huyo. Mzazi mwingine alisema ameshangazwa na hatua hiyo ya shule ya Kisutu kuwazuia wanafunzi wa Kiislamu kuhudhuria khitma hiyo iliyoandaliwa na Halmashauri Kuu ya Waislamu ambayo inatambuliwa na Rais na imekuwa ikifanya mazungumzo na Rais Mkapa juu ya dhuluma wanazofanyiwa Waislamu na serikali. Mzazi huyo ambaye hakupenda kutajwa gazetini alisema, "kuwatisha wanafunzi wasihudhurie khitma ni kuwazuia wasifanye mambo ya ibada zao. Isitoshe khitma yenyewe ilikuwa Jumapili, (siku hiyo) hakuna kazi wala shule sasa kikwazo ilikuwa nini kama sio uonevu?" Aidha sekondari ya Kisutu ni shule ya kutwa ambapo wanafunzi hawalali shuleni. NASAHA ilipotaka kujua vitisho walivyopewa wanafunzi hao, mzazi huyo ambaye alijitaja kuwa ni afisa mstaafu serikalini alisema kwamba wanafunzi hao waliambiwa kuwa maelezo yao waliyoyatoa kwa walimu hao, majina yao na mahali wanapoishi vitapelekwa katika vyombo vya dola. Aidha wazazi hao wamesema wanakusudia kuwaona viongozi wa HALASHAURI Kuu ya waislamu ili suala hili walipeleke kwa Mh. Rais kama ushahidi wa unyanyasaji dhidi ya Waislamu. NASAHA ilibahatika kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wa Kiislamu wa shule hiyo ambao waliieleza kwamba wamekuwa wakitakiwa wasijihusishe na jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu katika shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam DAMUSSA. "...wanatuambia (kuwa) DAMUSSA siyo nzuri kwetu na wakati mwingine viongozi wake (DAMUSSA) huwa wanazuiliwa wasiingie shuleni hapa", alisema mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu. Mwanafunzi mwingine wa Kiislamu alimuunga mkono mwenzie na kuongeza kuwa kizuizi hicho hawakioni kwa jumuiya za wanafunzi wa Kikristo kama vile UKWATA na TYCS. "Viongozi wa UKWATA na TYCS wanakuja hapa kila mara kuzungumza na (wanafunzi) Wakiristo, lakini sio DAMUSSA", alisema mwanafunzi huyo. Juhudi za gazeti hili kuzungumza na uongozi wa shule hiyo hazikuzaa matunda kwa maelezo kuwa wasemaji wa suala hilo hawakuwepo. Mwalimu mmoja ambaye hakukubali kutajwa gazetini aliwataja walimu wenzake ambao wanaweza kuzungumzia suala hilo kuwa ni Mkuu wa shule Msaidizi, Mama Shaba, Mwalimu wa Taaluma, Mama Kilama, Mwalimu Mlezi wa wanafunzi Waislamu, Mama Issa na Mama Nzingo kwa vile wao ndio walihusika kuwahoji wanafunzi hao. |
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|