NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Tahariri 
S.L.P. 72045, Simu: 761753, Dar es Salaam
 
 

Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

WAISLAMU nchini wamethibitisha kulijua wanalolitaka kuhusiana na mauaji ya ndugu zao ya Mwembechai Feburari, 1998:kwamba uchunguzi ufanyike na wote waliohusika wafikishwe katika mkono wa sheria. Waislamu wamedumu katika kulidai hili, mbali na muda mrefu kupita na baada ya kuwa wamezungushwa na kupewa hoja kadhaa za kuwataka waachane nalo.

Kwa vile sasa imethibiti kuwa Waislamu wanalidai jambo lao hilo kwa nguvu za hoja, basi njia pekee ya kuwatuliza ni kuwapa jambo hilo kwa mujibu wa taratibu zilizokubaliwa na jamii nzima wanamoishi.

Februari 13 mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka jana, maelfu ya Waislamu waishio Dar es Salaam na wawakilishi wa Waislamu toka mikoa mbalimbali nchini walikusanyika jijini kusoma khitma kuwakumbuka na kuwaombea dua wenzao waliouawa kwa kupigwa risasi za moto na polisi na wengine kufia mahabusu katika shambulio lililofanywa dhidi ya Waislamu kule msikiti wa Mwembechai jijini Dar es Salaam, Februari 13, 1998.

Aidha huko mikoani, Waislamu walikusanyika msikitini kwa ajili ya shughuli hiyo hiyo.

Waislamu ni sehemu ya raia wa Tanzania ambapo msimamizi wa masuala ya raia wote ni serikali. Hivyo basi ni muhimu sana kwa serikikali kuliona hilo na ikalikiri: kwamba katika mauaji ya Mwembechai, Waislamu kauli yao ni moja bila kujali hawa ni wanaume na wale ni wanawake; ama hawa ni Waislamu wa Dar es Salaam na wale ni wa Mwanza, au hawa ni masheikh na wale ni maofisa-wote ni Waislamu.

Mauaji ya Mwembechai na dhuluma nyingine zilizoambatana nayo zilizotokea Februri 12 na 13 mwaka 1998. Mara baada ya mauaji hayo, Waislamu waliamini kuwa wao ni raia wenye haki sawa na raia wengine wowote katika nchi hii, walitoa msimamamo wao kwamba shambulio lile la polisi wa serikali lililopelekea mauaji ya Waislamu, udhalilishaji wa viongozi wa Waislamu na akina mama wa Kiislamu na pia uharibufu wa mali za Waislamu ilikuwa ni dhuluma kubwa kwa Waislamu. Aidha waliitaka serikali ifanye uchunguzi kwa mujibu wa sheria zinazoitawala nchi hii na wote waliochochea, walioidhinisha na wale waliofanya shambulizi lile lililomwaga damu ya Watanzania wafikishwe mbele ya sheria.

Waislamu hao, kwa mapenzi makubwa ya salama na amani ya nchi hii, hawajathubutu kujichukulia sheria mikononi kuwashughulikia wauaji wa ndugu zao ingawa wanawajua kwa sura, majina, kazi na vyeo vyao katika jamii yetu.

Katika Baraza la Idd Januari 1999, Waislamu waliikumbusha serikali haya ya kufanya uchunguzi wa mauaji ya Mwembe Chai na hatimaye kuwafungulia mashitaka waauaji. Februari 13, mwaka huo huo, Waislamu walikusanyika kuwakumbuka ndugu zao hao ambapo waliendelea kuikumbusha serikali juu ya suala hilo.

Katika Baraza la Idd mwaka huu, Januari 2000, wameikumbusha tena serikali ikiwa ni pamoja na kutaja taratibu za kisheria zenye kuhusiana na masuala kama hayo.

Lakini safari zote hizi serikali imekuwa 'ikilipiga kumbo' dai hilo la Waislamu.

Mwaka huu pia, Februari 13, Waislamu wamekubana tena na dai lao ni lile lile. Uchunguzi ufanywe, wauaji wafikishwe mbele ya sheria.

Tuonavyo sisi, kama tulivyotangulia kusema hapo awali kwamba msimamo wa watu huonekana katika kudumu kwao wakilidai jambo lao tena kwa hoja madhubuti, basi wakati umefika sasa kwa serikali kuwatendea haki raia wake hawa. Uchunguzi ufanywe, na wanaotuhumiwa kuchochea mauaji na wanaotuhumiwa kuua wafikishwe mahakamani. Iwapo mahakama itawaona wanayo hatia basi sheria zilizopo zitumike na ikiwa hawatapatikana na hatia waachiwe huru. Ugomvi utakuwa umekwisha.

Lipo jambo lingine ambalo ni muhimu kwa serikali kulizingatia. Katika mikutano yote hiyo ya Waislamu haijawahi kuripotiwa kuzuka kwa vurugu zozote mbali na kuwa kila Februari 13, huwa ni siku ya machungu kwa Waislamu. Wao hukusanyika kusoma khitma na kutoa salaam zao na kisha hutawanyika bila kuharibu mali, kumdhuru mtu wala kuingilia misafara ya magari barabarani. Ni vema basi serikali ikatambua na kukiri kuwa Waislamu hawa si watu wenye fujo, na juu ya hilo ni kuwa vurugu iliyotokea Mwembechai Februari 12 na 13, 1998 na kupelekea mauaji ilisababishwa na jeshi la polisi.

Waswahili husema penye haki, uongo hujitenga. Mpaka sasa tunaamini kuwa 'ushahidi wa kisayansi' wa kuwa ni nani alikuwa mchokozi umetimia. Sasa serikali ichukue hatua.

Tunataja pia suala la mtoto Chuki Athumani ambaye leo hii kapooza kutokana na shambulizi la risasi za moto za jeshi la Polisi la Tanzania. Mpaka leo hii hakuna yeyote katika jeshi hilo na serikali yote kwa ujumla aliyeweza kutaja na kulithibitisha kosa la mtoto huyo kiasi cha kustahili 'kufumuliwa' risasi za kiuno!

Tunawashukuru Waislamu ambao wamejitokeza kumchangia. Tunasema kuwa kilichopatikana si haba.

Hata hivyo tunawaomba Waislamu wazidi kumkumbuka mdhulumiwa huyu, waangalie uwezekano wa kumtafutia viungo vya bandia (artificial limbs); na lililo kubwa zaidi ni kumpatia mtoto huyo, Chuki Athumani, elimu ya taaluma kuweza kumfaa yeye binafsi na jamii aliyomo.

Mwisho tunapenda kuwakumbusha Waisalmu kuwa mwitiko wa Waislamu katika suala zima la mwembechai ni dalili ya wazi ya mshikamano mkubwa miongoni mwa Waislamu. Hivyo akitokea mtu akadai kuwa Waislamu hawana umoja au mshikamano basi huyo akimbiwe, asipewe fursa ya kusikilizwa. 

Juu
 

YALIYOMO

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita