NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

NA MWINJILISTI KAMARA KUSUPA

UHURU wa kwanza ulikwishapatikana. TANU ikiwa na wazalendo, kuanzia viongozi hadi wanachama iliwaongoza Watanganyika kumng'oa mkoloni na kutawala. TANU kikiwa ndio chama tawala, na chama pekee chenye uhalali wa kuendesha shughuli za kisiasa kulingana na katiba mpya waliojitungia yaani katiba ya kuifanya nchi kuwa ya Chama kimoja cha siasa. Kwa hivi sasa CCM haifanani kabisa na TANU ingawaje inaendelea kujiita chama tawala na papo hapo kuitumia historia ya TANU kujihalalisha.
 
 
 

Katika uhalisi wa mambo, CCM siyo chama cha siasa bali ni chama cha dola, kwani hakina siasa wala sera, badala yake kina nguvu za dola, polisi, mashushushu, na mahakama. Nguvu ya CCM haitegemei utashi wa wananchi bali inategemea utisho wa dola. Hii ina maana kwamba hata baadhi ya watu wanaoishabikia ni kutokana na hofu tu kwamba wakijionesha kwamba wana upinzani dhidi ya CCM huenda watakumbana na nguvu za dola na kwakuwa wengine hawataki misukosuko basi huamua kuimba wimbo ambao watawala wanapenda kuusikia. 

Siasa ya TANU ilikuwa ni kutwaa rasilimali za nchi na kuziweka mikononi mwa wananchi, tofauti na siasa kuu ya CCM chini ya itikadi za kidhalimu kama 'Globalization' na 'Privatisation' ambayo ni kutwaa mali za Taifa na utajiri wote wa nchi na kuuweka katika mikono ya watu wachache ambao wana ujanja na nguvu ya fedha. Hatimaye wananchi watajikuta hawana vyote, hawana uhuru, hawana mali, hawama elimu, wala tumaini la kuishi maisha mazuri ndani ya nchi yao. Mwananchi anapofikia hatua hiyo ya kushuhudia utajiri wa nchi ukitumika kunufaisha wachache huku yeye akiteswa na umaskini na ufukara wa kupindukia, hapo ndipo inapoinuka dhana ya ukombozi wa mwananchi. 

Mwananchi anapofikia hatua ya kushuhudia wageni wakitanua ndani ya nchi yake huku yeye akibaki hohehahe akinyanyasika siku hadi siku, hapo ndipo inapoinuka dhana ya kupigania uhuru kwa mara ya pili. 

Uhuru wa pili, ni uhuru wa kuondokana na utawala usio wanufaisha wananchi, ingawaje utawala huo waweza kuwa wa ndugu zetu wa damu kama vile Wajomba, kaka, binamu, dada, shangazi, bibi, babu au baba na mama zetu. 

Tatizo la awali la nchi hii ni kwamba utawala wake hauko kwa ajili ya wananchi ingawaje wananchi ndio wanaoshirikishwa kuuweka madarakani. 

Utawala wa nchi yetu uko kwa ajili ya wageni kwanza na wenyeji wafuatie baadaye. 

Chukulia mfano mdogo tu wa shughuli ya utalii, hadi sasa Tanzania ndio inayoongoza duniani kwa kutenga asilimia 40% ya ardhi yake kwa ajili ya kuhifadhia wanyama pori. Je, mwananchi ananufaikaje na wanyama wengi walio ndani ya nchi yake? Mwananchi haruhusiwi hata kuishi karibu na hifadhi yoyote ya Taifa, yule aliye karibu, anatakiwa aondoke/ahame. 

Mwananchi haruhusiwi kuwinda wanyama wala akafaidi nyama yao badala yake wanaomudu maeneo ya uwindaji ni wageni tu wanaoweza kutoa kitu kidogo kwa wenye mamlaka. 

Mwananchi haruhusiwi kulima, kuchuma matunda wala kuchimba dawa katika eneo lolote linaloitwa hifadhi ya Taifa, mema yote hayo amehifadhiwa mtalii ili ajapo kutoka Ulaya, alale kwenye hoteli bora (zinazoitwa hoteli za kitalii), aendeshwe na Waafrika kwenye magari ya kifahari yanayoitwa magari ya kitalii kisha awaone hao simba, nyati na twiga ambao kwao Ulaya baba zao waliwaangamiza zamani sana. 

Kitu chema ndani ya nchi kinapogeuzwa eti kiwe kipo kwa ajili ya mgeni kwa kuwa tu mgeni huyo anatoa 'Forex' ambayo Taifa linaihitaji huu ni ukoloni kamili. 

Kwa sababu hadi sasa fedha itokanayo na shughuli za utalii haijamnufaisha chochote mwananchi kinyume chake fedha za kigeni imekuwa ikirudi Ulaya ilikotoka kwa njia nyingi, kwanza, ikiwa ni kwa njia ya wizi wa hao walioko madarakani na utoroshaji wa fedha kupitia akaunti zao walizojiwekea huko Ulaya. 

Pili, fedha ya kigeni imekuwa inarudi Ulaya kwa ajili ya kulipa madeni hewa ambayo mwananchi hakukopa wala hakutumia. Kwa ajili hiyo yeyote mwenye kutazama mambo katika uhalisi wake ataona ya kwamba 'utalii' ni namna mpya ya kuendeleza matabaka, Mzungu kuishi Afrika kama tabaka la kutumikiwa na kufaidi mema ya nchi, na mwananchi kama tabaka la kumtukia mgeni huku akiambulia makombo yadondokayo toka mikononi mwa mgeni. Faida za utalii inapaswa ziangaliwe upya. Je, ni kweli kwamba utalii unamnufaisha mwananchi au unamnufaisha yeye anayetalii? 

Mambo hayaishii kwenye utalii tu, lakini toka CCM ikubali itikadi za kishetani zitolewazo na IMF na Benki ya Dunia sasa hata suala la ajira linaanza kuchukua sura ya ubaguzi na utabaka. Viwanda na Mashirika ya umma vimeuzwa, wanunuzi wakuu ni wageni kwakuwa ndio wenye mitaji mikubwa, matokeo yake hata nafasi za kazi watapeana kwa upendeleo. Itakuwa vigumu sasa kumkuta mwananchi kwenye nafasi za mhasibu au Meneja Mkuu, kwani nafasi hizo watapeana wao kw awoa kwanza ndipo wafuatie baadaye. 

Tutaendelea kuwa na vijana wanaohitimu Chuo Kikuu lakini hawana kazi za kufanya wala hawapewi nafasi ya kutumia elimu yao kwa vitendo. Hali ya ukoloni wa mwisho inakuwa mbaya zaidi ya hali ya ukoloni wa miaka ya hamsini. 

Mambo hayaishii hapo tu kwenye elimu na ajira, bali kuna bomu jingine ambalo linaumbika chini ya utawala potofu wa CCM nalo ni bomu la ardhi ingawaje wakulima bado hawajalistukia. 

Ardhi ya Tanzania kikatiba bado inahesabiwa kama mali ya serikali kuu, na Rais anao uwezo wa kummilikisha mtu (mwombaji) ardhi kwa miaka 33 au 99. 

Tafsiri ya neno hili ni kwamba endapo atajitokeza mgeni aliyeamua kuja kwa jina la mwekezaji kisha akaimwagia serikali kuu fedha za kigeni mithili ya mtu anayetaka kumchinja kuku amwagiavyo mchele, ni wazi kwamba mgeni huyo akiitaka ardhi ya Kazimzumbwi, Rufiji au Kilombero, ama sehemu nyingineyo ambayo ni katiba imemrahisishia kazi ya kumiliki. 

Mwananchi anayo nafasi kubwa ya kupoteza haki yake ya kumiliki ardhi kutokana na ukweli kwamba hata mahakama haina uwezo wa kuingilia maamuzi ya Rais. 

Mwananchi anaishi katika nchi hii kana kwamba amepangishwa tu na siyo ameumbiwa kuishi na kufaidi mema ya nchi yake. Katika hali kama hii ambapo mwananchi hana uhuru, hana ajira, hana huduma muhimu za kijamii, hana ardhi ya kudumu na hata yule aliyefanikiwa kulima na kuvuna bado hana soko la kuuza mazao yake. 

Je, tumaini la maendeleo liko wapi? Li wapi tumaini la kuishi maisha mazuri ndani ya nchi yake! Ni wazi kwamba mapambano ya kuutafuta uhuru wa pili na ukombozi kamili wa mwananchi linageuka kuwa suala la kufa na kupona, maana yule asiyejumuika kwenye harakati za uhuru na ukombozi huu bado dhiki zitamfuata kila siku na kumuua hapo alipo. Mtu asijidanganye kwamba anaweza kuishi katika hali isiyo na matumaini. Ni wajibu wetu sote kuupigania uhuru wa pili kwa nguvu zetu zote na kwa gharama zote hata ikibidi kutoa uhai tuwe tayari, kwa sababu hakuna chema kinachopatikana kirahisi. Mwanaharakati Nelson Mandela aliwahi kusema 'The is no easy way to Freedom', akiwa na maana ya kwamba njia ya kuufikia uhuru ni ngumu. Naam, ni ngumu lakini inawezekana. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita