|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
|
CCM kugawanyika? Na Mwandishi Wetu UAMUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu azma ya Wazanzibar kuifanyia marekebisho Katiba ya nchi yao ili kuondoa kipengele kinachoweka ukomo kwa mtu kushika wadhifa wa urais wa visiwa hivyo kuwa vipindi viwili bado haujafahamika kama ilivyotarajiwa jana jioni. Hali hiyo imetokana na kuongezwa muda wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM maalum (NEC) Zanzibar. Awali kikao hicho kilipangwa kumalizika jana Jumanne na kwamba taarifa za kikao hicho zingetangazwa jioni ya siku hiyo. Taarifa kutoka Zanzibar zimeeleza kuwa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na kwamba kikao kitakapomalizika taarifa zitatolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Mussa Hassan Takrima. Mwishoni mwa wiki iliyopita palikuwepo na mfululizo wa mikutano ya wazee wa CCM kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar ambao waliahidi kuunga mkono adhma ya serikali ya Mapinduzi kubadilisha katiba ya Zanzibar kuondoa ukomo wa Rais wa nchi hiyo kuiongoza kwa vipindi viwili tu. Katika siku za karibuni watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, wabunge, na wanasheria wote kutoka Tanzania bara walitoa misimamo yao kupinga mapendekezo yakubadilisha katiba ya Zanzibar "kumwezesha Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, kuongoza tena Zanzibar kwa kipindi cha tatu." Wazee hao wa CCM Zanzibar walisema wamekutana kutoa msimamo wao kwamba Tanzania Bara hawawezi kuwachagulia Zanzibar viongozi wake. "Tumekutana kutoa msimamo wetu kama wazee kwamba, CCM ya Tanzania Bara hawawezi kutuchagulia kiongozi (wa Zanzibar)..... kwa sababu (Bara) hawajui kinachoendelea hapa Zanzibar", walisema wazee hao. Wakizidi kufafanua walisema, "Suala hili sio la (Dk.) Salmin, ( bali ) ni suala la Urais wa Zanzibar...kwa nini (Tanzania ) Bara watuingilie ? Katika kile kilichoonekana kuwa ni kufafanua msimamo wao wa kutaka Tanzania Bara isijiingize katika masuala ya Zanzibar wazee hao walisema historia za Zanzibar na Tanzania Bara ( wakati huo ikiitwa Tanganyika) ni tofauti. Walisema Zanzibar ilipigana na kufanya mapinduzi ambapo damu ilimwagika ili kujikomboa lakini Tanzania Bara iliupata uhuru wake "mezani" Kuhusu habari kuwa wana-CCM Zanzibar wanamtaka Dk. Salmin agombee tena urais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu wazee hao walisema Dk Salmin ndiye chaguo lao na kwamba hawatateua mtu mwingine yeyote kuiwania nafasi hiyo. "... chaguo letu ni Salmini ...hatutamteua ) mtu mwingine yeyote kugombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM ", alisema mmoja wa wazee hao. Kulingana na msimamo huo wa wazee wa CCM wa Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi kitakuwa na wakati mgumu sana mwaka huu. Baadaye mwezi huu Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) inatarajiwa kukutana mjini Dodoma kupokea na kujadili matokeo ya kikao maalumu cha Kamati ya CCM -Zanzibar. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya CCM, NEC, ndiyo yenye kauli ya mwisho juu ya Mwana-CCM atayesimama kugombea Urais wa Visiwa hivyo. Taarifa zilizolifikia NASAHA zinasema kuwa kiongozi mmoja mwandamizi wa SMZ aliwahi kutamba kwamba iwapo kikao cha NEC Dodoma hakitampitisha Dk. Salmin, basi wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar watarudi Visiwani humo wakiwa sio CCM tena bali ni Afro-Shiraz. Chama cha Afro Shiraz (ASP) ndicho kilichoongoza mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 chini ya kiongozi wake Marehemu Abeid Amani Karume. Baadaye mwaka 1977, ASP na Chama kilichokuwa kikitawala Tanzania Bara, Tanganyika African National Union(TANU) viliungana katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliopatikana Aprili 1964. |
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|