NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Mashairi


Shime tujiandikisheni 

1. Hodi hodi mhariri, wa NASAHA naingia,
Na hili langu shairi, uchaguzi lahusia,
Ninamuomba Kahari, watu kulizingatia,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

2. Uchaguzi Tanzania yabidi maandalizi,
Hasa kwa sisi raia, tusipige usingizi,
Kwenda jiandikishia, kuchagua viongozi,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

3. Sasa muda umefika, jambo hili kuwa wazi,
Kuingia kwa hakika, kwenye huu uchaguzi,
Kila kitu kukiweka, katika maandalizi,
    Tarehe ikitangazwa nenda kajiandikishe.

4. Itakuwa Oktoba, mwaka elfu mbili,
Lakini pia si haba, tukajinoa kikweli,
Ewe mama pia baba, uchaguzi kuujali,
 Haki yako tekeleza, kwa kwenda jiandikisha.

5. Sio kujishughulisha na kelele mitaani,
Bila kujiandikisha na kuweka maanani,
Mama tutajirudisha na kubaki mkiani,
    Hutaweza piga kura, usipojiandikisha.

6. Hili ni jambo muhimu, nyuma tusijirudishe,
Inabidi kufahamu, msijezuia kasheshe,
Uchaguzi ni lazimu, hima mjiandikishe,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

7. Kuanzia vijijini nanyi pia amkeni,
Na mliopo mijini wote jiandikisheni,
Msikae vijiweni, siasa za mdomoni,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

8. Umoja kama siafu, hima jama tuigeni,
Tusimame safusafu tujitoe unyongeni,
Maneno yameshakifu tuingie matendoni,
    Tarehe ikitangazwa kwa wingi jitokezeni.

9. Kuwapata viongozi, waso na upendeleo,
  Waliowachapa kazi, kwa yetu maendeleo,
Wasio na ubaguzi, na kupendea vyeo
Kura yako ni muhimu, nenda kajiandikishe.

10. Msisahau wabunge mtakaowachagua,
 Nchi yetu waijenge majimboni watokuwa,
  Wawatetee wanyonge, kwa haki kutobagua,
Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

11. Pia nao madiwani tuchague kwa makini,
Sio tu kwa kampeni, wapigazo jukwaani,
Bali tuzingatieni, wafanyayo matendoni,
    Usipojiandikisha hutoweza kuchagua.

12. Raia anachagua rais ampendaye,
Si kwa chama alokua, au uzuri suraye,
Kwa sera zisizobagua, atazingatia yeye,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

13. Vyema kujiandikisha tarehe ikiwadia,
Dodoma hata Arusha ni haki yako raia,
Haki kuikamilisha, ni wajibu zingatia,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

14. Himahima nawaasa, kwa wingi jitokezeni,
Ninawapiga msasa, kuanzia vijijini,
Isijekuwa mkasa, msipo jitokezeni,
    Usipojiandikisha hutoweza piga kura.

15. Kumi nasita tamati kalamu inafifia,
Tuzidishe mikakati, chagueni kutohofia,
Jitokezeni kwa dhati, sio tu kusifia,
Chonde chonde sisahau kwenda kujiandikisha.

Na Baby Fumo, 
Tanga. 


Kobe na kasa - swali (sisitizo) 

1. Hodi tena uwanjani, NASAHANI nimefika,
Nina hamu kijuani, kuing’amua hakika,
Jibu liwe kurasani, nipate kufarijika.
    Kati ya kobe na kasa, nani bora kati yao.

2. Nganenga amebaini, wa ubora hamuoni,
Ingawa atoka pwani, kasa, kobe hatamani,
Magamba yao ngozini, yamchefua “moyoni,
    Kati ya kombe na kasa, ng’amueni alo bora.

3. Alo mzuri ni nani, kati ya kobe na kasa,
Majibu nayatamani, japo nusu ukurasa,
Yanitoe kizimbani, utata nilionasa,
    Baby Fumo nakuuliza, nani bora kati yao?

4. Wote wawili kwa shingo, fupi mabaka ngozini,
Wote wawili kwa mwendo, wapolepole baini,
Wote wawili kwa umbo, magamba tele miwilini,
    Kijukuu nakuuliza, nani bora kati yao?

5. Mwendo wao wa maringo, aibu tele usoni,
Wanafanana viungo, hata macho na ulimi,
Gamba zao kama ungo, mifuniko ya mwilini,
    Rasaki nakuuliza, nani bora kati yao?

6. Kasa ni nambari wani, kwa ugali kwa sambusa,
Hajichimbii mtoni, baharini wamnasa,
Ukipanda mgongoni, kama gari la kisasa,
    Kati ya kobe na kasa, alo mzuri ni nani?

7. Kobe yeye hana shaka, utalii kivutio,
Hataki kuchakarika, mwendo wake si wa mbio,
Kwenye vichaka na nyika, makazi yake tulio,
    Yupi ni nambari wani, kati ya kobe na kasa?

8. Tamati ninaondoka, moyoni ninaumia,
Mwenzenu nahangaika, mwishowe nitajifia,
Jawabu mkinitwika, akili itatulia,
    Kati ya kobe na kasa, alo obora ng’amueni.

Juma Katanga (Jushaka)
"Sugu la Mashairi - Tanzania"
P.O. Box 90329,  DAR ES SALAAM. 



Kobe na kasa - Jibu 

1. Ninakutuma shairi, uandikwe gazetini,
Ukalete umahiri, na ufanisi makini,
Swali lake mshairi, upate kumjibuni,
Kobe na kasa mwenzangu, alomzuri ni kobe.

2. Jibu langu natetea, ili upate ridhika,
Uzuri kajijengea, mwendowe hata viraka,
Kasa vyake nakemea, havipendezi hakika,
Kati ya Kombe na Kasa, kobe ni nambari wani.

3. Sifaze zinavutia, kwetu hata kwa wageni,
Magamba twajipatia, yalo na sifa makini,
Vifaa yatupatia, yeye alotudhamini,
Kati ya KombenaKasa, Kobe ni bora mwenzangu.

4. Japo wanaufanano, kwa baadhi ya matendo,
Lakini Kobe mfano, ulong’ara kwa kishindo,
Japo kuna ufanano, mabaka mwili na mwendo,
    Lakini kobe ni bora, kuliko mwenzie kasa.

5. Wasema kasa ni bora, kwa ugali na sambausa,
Naukubali ubora, ulobaini kwa kasa,
Lakini si kubwa jora, hata uweke msasa,
    Kati y ahawa wawili, kombe bora kati yao.

6. Kobe yeye twafaidi, fedha toka kwa wageni,
Watalii kwa juhudi, kobe wanamtamani,
Fedha mfano wa udi, maendeleo nchini,
    Mwenzangu wajionea, uzuri wa huyu kobe.

7. Uzuri wa huyu Kobe, si wa upande mmoja,
Sura na umbo la Kobe, Havimfanyi mjanja,
Uchumi wa nchi kobe, yaendesha bila hoja,
    Kobe na kasa jamani, kobe ndiye alobora.

8. Tuangalie jamii, kwazo fedha za kigeni,
Mahitaji ya jamii, tunayapata makini,
Uzuriwe msanii, wauona si utani,
   Nang’amua kwa mifano, kobe ni bora zaidi.

9. Mwenzangu nimekujibu, kati ya Kobe na kasa,
Fikiri bila aibu, ni jibu lenye usasa,
Ukiwa nami karibu, hutayaona makosa,
    Hakika kobe zaidi, kwayo niloyabaini.

10. Hapa hapa nakomea, mtuliza washairi,
Jibu nimekuletea, lenye hakina mahiri,
Toka hapa natembea, kungojea yako ari,
Mwenzangu Juma tulia, kobe ni bora zaidi.

Ezekiel Jonathan Lugayana,
Malenga mtumainiwa kishairi,
S.L.P. 666 Vingunguti,
Dar es Salaam. 


Karibuni Form One

1. Karibuni fomu wani, karibuni masomoni,
Igra wote shikeni, asemavyo Rahamani,
Muabuduni mamani, sambamba na masomoni,
    Karibu karibu sana, karibuni fomu wani.

2. Masomo yote someni, namusome kwa makini,
Ya walimu yashikeni, jamani bunge acheni,
Amali njema shikeni, muwapo kwenu nyumbani,
    Karibu karibu sana, karibuni fomu wani.

3. Nidhamu jama jengeni, wenzenu wawaigeni,
Dini yenu tangazeni, niuhuru katibani,
Maswaliwaulizeni, wenyeji wenu shuleni,
    Karibu karibu sana, karibuni fomu wani.

4. Jamanifujo acheni, mtajaaa mkiani,
Bwanatwazitaka wani, ndizo bora divisheni,
Ziromimi sitamani, ni karaha majumbani,
    Karibu karibusana, karibuni fomu wani.

5. NASAHA pia someni, gazeti lenu jamani,
Mutambue kwa makini, ya kweli yaduniani,
Ukweli mtabaini, NASAHA bwana makini,
    Karibu karibu sana, karibuni fomu wani.

6. Hapa nahusiasana, sana nawahusieni,
Qur-anibora sana, kuiwekamatendoni,
KatuhusiaRabana, hiyo na sunnashikeni,
    Karibu karibu sana, karibuni fomu wani.

7. Hapakalamu yagoma, ndipo mwisho karibuni,
Salama Tanga, Kigoma, hadiMorokwa watani,
Na mwishonchi nzima, karibuni fomu wani,
    Karibu  karibu sana, karibuni fomu wani.

8. Nbeti tisa nyingi sana, bai bai fomu wani,
Yangu yashikenisana, kama mwataka kuwini,
Jamani museome sana, wazazi watumaini,
    Karibu karibusana, karibunifomuwani.

Almasi H. Shemdoe, (Mzee wa Hekima),
Dar es Salaam. 


OIC na Vatican

1. Naanza kwa kugusia, OIC na Vatikani,
Napenda kuwausia, nchi ipo lawamani,
Rais umechangia, kutuwekamashakani,
    OIC na Vatikani, Raisi umashakani.

2. OIC ni shirikisho, ni sawa na Vatikani,
Inahusu uamsho, wa kidini duniani,
Msijue ya Kosovo, watu wakawa porini,
    OIC na Vatikani, Rais umashakani.

3. Ubalozi Vatikani, kusudi lake ni dini,
Tofauti siioni, naOIC duniani,
Jambo hili chambueni, akili ziwe makini,
    OIC na Vatikani, Raisi umashakani.

4. Wagalatia husema, OIC hawatamani,
Nchi iwe mwanachama, kitu hicho hukilani,
Wemeandaa lawama, ambazo si za yakini,
    OIC na Vatikani, Raisi umashakani.

5. Kuihami Vatikani, ambayo i lawamani,
CCT wamebaini, OIC kwenda Bungeni,
Hiyo hoja ya kihuni, hawaoni Vatikani?
    OIC na Vatikani, Rais umashakani.

6. Vatikani ya zamani, haikufika Bungeni,
Na sisi tunatamani, OIC nchini,
OIC ina thamani, kama hiyo Vatikani,
    OIC na Vatikani, Raisi umashakani.

7. Mpirira upo Mbale, ya Bongo umebaini,
Haya mambo ni ya kale, ukweli umethamini,
Sasa tunakwenda mbele, wa mbali mpo makini,
    OIC na Vatikani, Rais umashakani.

8. Kuna maoni ya watu, Rais umebaini,
Vatikani ipo kwetu, hahitaji maoni,
Kuihami nchi yetu, shirikisho jiungeni,
    OIC na Vatikani, Rais umashakani,

9. Sasa siku zimefika, ukweli tumebaini,
Akili zimefumbuka, kwa uchambuzi yakini,
Watu mmeshaumbuka, nchi ipo Vatikani,
    OIC  na Vatikani, Rais umashakani.

Mr. Life, 
Box 1466, 
Tanga. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita