NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Makala 

UPINZANI OCTOBA 2000 - 3 

Na J. Hussein 
 

SERA zote za CUF zimeegemezwa katika sera kuu mbili- yaani: HAKI SAWA KWA WOTE NA UTAJIRISHO. Kwa bahati mbaya sana kwa CCM, haya ni maeneo ambayo chama hicho kina rekodi mbaya, mbaya, mbaya. Ni mtu mpumbavu tu anayeweza kusimama hadharani na akatetea kwa dhati kuwa haki za raia wote wa Tanzania zinalindwa kwa kiwango kilekile- yaani bila kujali tabaka lake kiuchumi, imani ya dini yake, au mwelekeo wake kisiasa. Hali kadhalika hakuna mtu ambaye akiwa na akili zake timamu kabisa anaweza kwa dhati yake kukanusha ukweli kwamba watanzania wanaishi katika dimbwi la umasikini na kuwa kwa kiwango kikubwa umasikini huu unafanya kufugwa. 
 

HIVYO basi sera hizi mbili za CUF zina hatari ya kipekee kwa CCM. Mfano halisi wa jinsi CCM inavyotishwa na sera hizi za CUF unajidhihirisha vizuri zaidi katika suala la Uislamu na waislam nchini. Kwa miaka nenda rudi kundi kubwa la wananchi wa Tanzania - waislamu, wamekuwa wakipiga kelele kwamba hawatendewi haki . Serikali ya CCM au imechagua wakati mwingine kukaa kimya na kuwapuuza, au wakati mwingine kutoa majibu ya kejeli, au wakati mwingine inaposhindwa kuvumilia 'kero' hizo za waislam kutumia nguvu za dola. CCM kwa kuona hatari iliyopo ndani ya sera ya CUF ya 'haki sawa kwa wote'kuwa inaweza kuwa ni kivutio kikubwa kwa waislam ambao idadi yao inatosha kabisa kuifanya CUF iipate bara bila msaada wa chama kingine chochote, imeamua kuanzisha vita ya kisaikologia- vita ambayo kutokana na aina ya silaha CCM ilizochagua kutumia, ni chafu na ya hatari kabisa- si kwa chama hicho pinzani tu, bali hata kwa mustakabali wa baadaye wa taifa hili. 

Kwa msaada wa mtandao wa vyombo vya habari unaojumuisha vile vya CCM yenyewe na jumuia zake, vya serikali na vya makampuni binafsi, CCM inatumia nguvu nyingi na gharama kubwa kuuhadaa umma wa Tanzania na ulimwengu kwa ujumla kuwa CUF inatumia misikiti kama majukwaa ya kisiasa. Mbinu hii ina malengo makubwa matatu. Kwanza imelenga katika kuijengea CUF mazingira ya kupoteza muda mwingi kujitetea- na mtu yeyote anayepoteza muda mwingi kila mara kujitetea katika tuhuma fulani ambazo kila mara ni yeye tu zinaelekezwa kwake- kwenye macho ya watu wengi moja kwa moja mtu huyo ni anageuka kuwa mhalifu. Pili, imelenga katika kuwafanya viongozi wa CUF waingie hofu, hivyo wawe wanajiuma uma tu 'haki sawa kwa wote inapoingia kwenye suala la waislam', na hivyo kuwafanya waislam wasiwaamini. Na tatu, imelenga katika kuwatisha wakiristo waone kwamba maisha na maslahi yao yako hatarini sana na tumaini lao pekee ni kutogawa nguvu yao na potelea mbali hata kama CCM wengine hawaipendi, bora waiunge mkono iwe nusu shari kuliko shari kamili. Mbinu hii ya hatari hadi sasa imefanya kazi kwa mafanikio makubwa. Imewafanya wakristo wengi na hata baadhi ya waislam- hasa wale wavivu kufikiri, waiangalie CUF kwa macho ya woga. 

Hata hivyo mbinu hii ina mapungufu makubwa mawili ambayo kama CUF itayaona na iyatumie kikamilifu basi CCM itakuwa imejikaanga kwa mafuta yake yenyewe. Kwanza kabisa viongozi wa CUF wanaweza waamue kuivaa CCM kichwa kichwa na waseme wazi kwamba watakapoingia madarakani miongoni mwa mambo ya kwanza kuyafanya ni 'kuunda tume huru ya kitaalamu' kwa mfano wa ile ya Africa Kusini chini ya askofu Tutu- kuchunguza na kuthibitisha au kukanusha, madai ya waislam, wakiristo, au kundi jingine lolote linalohisi lina madai yake- kama njia pekee ya uhakika ya kuhakikisha kwamba ukweli unajulikana, haki inatendeka na hivyo kuondoa mazingira ya kushawishi kuvunjika kwa amani na kuondoka kwa utulivu. Pili, CCM kabla ya kuanzisha vita hii ilitakiwa isimame kwenye kioo kirefu ijikague kwa makini toka utosini hadi kwenye dole gumba la mguu. Kwa sababu gani? Sababu ni kwamba CCM ndicho chama pekee cha siasa hapa Tanzania ambacho kiko kwenye rekodi zilizofanyiwa utafiti wa kina , kuonyeshwa kuwa kimekuwa kikichanganya siasa na dini kikamilifu kwa nia ya kuendeleza maslahi ya wakiristo na kudidimiza yale ya waislamu katika kipindi chote ambacho imekaa madarakani. Kwa kuwa si kazi kubwa kupata rekodi hizo na kuwa nazo mkononi, CCM inapaswa kujiuliza ni kitu gani itakivuna iwapo watafiti wa CUF watazipata rekodi hizi na viongozi wao wasione kinyaa kuzitumia majukwaani. 

Kwa upande wa sera ya utajirisho, CUF imepata bahati mara mbili- na ambayo ni nuksi mara mbili kwa CCM. Kwanza kabisa hivi sasa watanzania wengi ni maskini mno(CCM haiwezi hata kidogo kukwepa lawama) kiasi ambacho ni wakati mzuri mno wa kuuza sera kama hiyo. Pili, CUF kwa kiasi kikubwa sana inaweza ikaaminika ikitamba na sera kama hiyo kwa sababu wana nyenzo muhimu inayoweza kuibadili sera hiyo kutoka kwenye makaratasi tu kuwa kweli!- Profesa Lipumba. Lipumba si tu kuwa ni Profesa wa uchumi- hawa wako wengi, bali ni mchumi mwenye sifa za kimataifa. Canada, Marekani, Japani, Finland, Uingereza, Brazili, Uganda, Zimbabwe, U.N n.k., ni baadhi tu ya maeneo ambayo Lipumba ameshawahi kutoa ushauri wake katika masuala ya uchumi. Kwa kifupi ni kwamba, kama ni kompyuta ambayo tungeiomba ituchagulie rais kwenye uchaguzi mkuu ujao katika misingi ya yule ambaye ana uwezekano mkubwa wa kututoa katika lindi la umasikini linalotuzunguka hivi sasa- kompyuta haipokei rushwa wala haisikilizi propaganda za kipumbavu- bila kuchelewa ingetutolea jibu kwamba kwa asilimia mia moja rais huyo ni Lipumba! 

Mbali ya yote haya, je Lipumba na CUF wana uwezo wa kutwaa madaraka ya nchi katika uchaguzi mkuu ujao na kuunda serikali? Awali nilisema kuwa siamini kuwa CUF itakaa iujutie uamuzi wake wa kumsimamisha Lipumba katika uchaguzi mkuu uliopita. Sababu yenyewe ni rahisi. Kwanza Lipumba aliingia kwenye uchaguzi ule akiwa hajulikani kabisa kisiasa. Pili, yeye na mwenzake, Juma Duni ndio waliooendesha kampeni kimaskini kuliko wagombea wote ( mapostas ya photocopy nyeusi na nyeupe, magari ya kuazima, uwezo sifuri wa kutoa matangazo, uwezo mdogo mno wa kugharamia mawakala, n.k.) na hata hivyo walifanikiwa- kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi -kupata asilimia sita ya kura na kushika nafasi ya tatu kati ya wagombea wanne! 

Kilichotokea ni kwamba muda mfupi tu baada ya kampeni kuanza ilidhihirika wazi kwa kila mtu kuwa kati ya wagombea wote Lipumba alikuwa bora zaidi.Alikuwa ndiye mgombea pekee aliyeweza kuyaelezea kwa ufasaha matatizo yetu na kuelezea ni kitu gani kinahitajika kifanywe ili kuyatatua. Alikuwa ndiye mgombea pekee aliyeruhusu kuulizwa maswali katika mikutano ya kampeni naye akayajibu kwa uaminifu. Mathalani, katika mkutano uliofanyika katika chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) wanafunzi ambao awali walivaa sura zilizojaa uadui walijikuta wanachangamka ghafla baada ya kukuta maswali yao yote yanapata majibu ya kutosheleza, wakachomoa notibuku zao na kuanza kuchukua notes! Tatizo kwa watu wengi kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe ni kwamba walisita kumpa kura zao eti kwa kuwa walikuwa hawamjui! Sababu hii ukichanganya na maandalizi duni ya CUF kwenye uchaguzi ule vilichanagia sana kumpotezea Lipumba kura nyingi za wazi kabisa. 

Lipumba baada ya uchaguzi mkuu alilazimika kuondoka nchini kwa muda kufuatia chuo kikuu cha Dar es salaam- ambacho ndicho kilichokuwa mwajiri wake, kumwachisha kazi. Ni kiasi gani hali hii ililetwa na shinikizo za kisiasa ni utawala pekee wa chuo hicho unaoweza kutubainishia. Vyovyote iwavyo, Lipumba hakuwa na jinsi. Mbali ya kwamba sasa hakuwa na njia ya uhakika ya kujipatia riziki - naye kutokuwa tayari kusubiri kuvizia vizia ruzuku ya chama- mataifa mengi ya nje yalimbembeleza aende kuyasaidia. Hivyo basi Lipumba kwa kipindi cha karibu miaka mitatu baada ya uchaguzi wa Oktoba 1995, ukiondoa mawasiliano ya karibu yaliyokuwepo kati yake na chama chake, alitoweka katika uwanja wa siasa za Tanzania. 

Mwaka mmoja uliopita Lipumba alirejea nchini na kuanza tena rasmi harakati za kisiasa. Mwaka mmoja ni muda mfupi sana lakini Lipumba amedhihirisha kuwa yeye si mchumi mahiri tu, bali ni mwanasiasa mwenye kipaji cha hali ya juu. Katika kipindi hiki kifupi tu ameweza kuigeuza CUF bara kutoka kuwa chama cha maofisini ( kama vilivyo vyama vingi vingine) na kukikabidhi kwa wananchi tena katika sura ya kitaifa hasa- hatua ambayo ilipelekea wanachama wa chama hicho kumchagua kuwa mwenyekiti wao kwa kauli moja kufuatia aliyekuwa mwenyekiti, mzee Msobi Mageni kuamua kustaafu shughuli za uongozi. Matokeo ya chaguzi ndogo za Ubungo na Temeke na ule wa serikali za mitaa hivi karibuni unatoa ushahidi ni jinsi gani CUF katika kipindi kifupi sana imekuwa ni mali ya wananchi . Ni wazi kabisa kuwa kati ya sasa na Oktoba kabla ya uchaguzi Lipumba ana uwezo kabisa wa kuunganisha sehemu kubwa ya watanzania nyuma yake tayari kwa kuiondoa CCM madarakani. 

Makubaliano ya Cheyo, Makani, na Lipumba ya kuunganisha nguvu zao katika uchaguzi mkuu ujao ni ya kuungwa mkono kwani yatazidi kuibana CCM. Hata hivyo ushauri wangu kwa viongozi hao ni kuwa ni muhimu wananchi tumjue watakayempa nafasi hiyo ya kugombea mapema, na huo uteuzi uzingatie sifa na mahitaji ya taifa hivi sasa na si vinginevyo. Inabidi wawe waangalifu hasa wasije wakaunda umoja ambao utasusiwa na wapiga kura. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita