|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
|
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO Wananchi Tanzania amkeni
Bunge, Serikali na Mahakama ndio vyombo vya Dola na vyote hivyo huundwa na katiba ya nchi ambayo kimsingi ni mali ya wananchi ambao pekee ndio wenye mamlaka ya kuongeza au kupunguza chochote kutoka ndani ya Katiba hiyo. Mwandishi RAJAB KANYAMA anaelezea zaidi. WAKATI wowote utakapoona serikali, moja ya vyombo vya dola tulivyotaja "imechemka" na kuanza kutoa maoni na mapendekezo yake kwa wananchi ili wachangie kwa lengo la kufanyia mabadiliko katiba ya nchi, fahamu mambo mawili muhimu. Mosi, ni kwamba katiba hiyo ni ya kurithi kutoka kwa Wakoloni na kwa maana hiyo si ya wananchi na pili fahamu kwamba wananchi ndani ya nchi hiyo bado wako katika usingizi mkali na kasumba iliyowageuza watumwa kwa kutokufahamu namna ya jinsi serikali inavyopaswa kuendesha mambo yake au kwa sababu ya kutokujiamini kwamba wanaweza wakaleta mabadiliko wanayoyataka kwa kutumia wingi wao. Ni vema wananchi wakafahamu sasa kwamba katiba ya nchi inapaswa kuwa ni mali yao na tena inayo mahusiano ya moja kwa moja na maisha yao ya kila siku na kwa mantiki hiyo ni lazima pia mabadiliko yoyote yaanze kutoka kwao. Ni vema pia wananchi wakafahamu kuwa Bunge, kama lilivyo halina mamlaka ya kuifanyia katiba ya nchi mabadiliko. Yenye uzito unaofanana na haya mabadiliko ya kumi na tatu yaliyofanywa kwa sababu ya kukosekana kwa uwiano wa Wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani. Tangu mwanzo, mtindo uliotumiwa na serikali wa kukusanya maoni ya wananchi kupitia waraka namba moja (White Paper) ulipigiwa kelele na wananchi wengi wenye upeo wa kufahamu mambo, vyama vya siasa vya upinzani, pamoja na wasomi kadhaa walioendesha midahalo na makongamano wakipinga utaratibu huo, moja ya sababu ikiwa ni ufujaji wa fedha za wananchi bure. Kwa kiwango fulani wananchi walielimika na ndio maana wengi walisusa na wala hawakuchangia maoni kama walivyotakiwa wakati Kamati iliyokuwa ukiongozwa na Mheshimiwa Jaji Kisanga ilipozunguuka nchi nzima kwa lengo hilo. Mapokezi ya taarifa ya Jaji Kisanga sote tunayajua, Rais alionekana kukasirishwa sana na taarifa hiyo kwa sababu ilidhihirisha kwamba Kamati haiafikiani na matakwa ya Serikali. Tunaelezwa kwamba ni wananchi laki sita tu ndio waliochangia maoni na katika hao wapo pia waliopinga moja kwa moja maoni ya serikali, na kubakisha idadi ndogo tu ya wananchi wasiozidi laki nne waliokubaliana na maoni ya Serikali. Hawa ni wananchi wachache sana ukilinganisha na idadi ya wananchi wa Tanzania wanaokisiwa kuwa ni karibu milioni thelathini ya tatu hivi. Kudai kwamba muswada huo unawakilisha maoni na matakwa ya wananchi wengi ni ulaghai wa hali ya juu kabisa. Hata hivyo bado muswada huo ulikuwa na kasoro nyingi za msingi, moja ya kasoro hizo ni kutokutolewa kwa taarifa ya Kamati ya Jaji Kisanga kwa wananchi au kwa Wabunge ili na wao waisome na kutoa maoni kabla ya muswada huo kutayarishwa na kupelekwa Bungeni, tutajuaje kama kweli muswada ulizingatia maoni ya wananchi? Kasoro ya pili kubwa ni ile ya muswada kutaja tarehe 1.07.2000 kuwa ndio tarehe ambayo marekebisho hayo yataanza kuwa na nguvu za kisheria, kabla ya muswada wenyewe kupitishwa na Bunge jambo linaloashiria dharau ya hali ya juu kabisa ya serikali dhidi ya Bunge. Pamoja na mambo mengine, marekebisho yaliyofanywa ni kinyume na mwenendo wa kidemokrasia, katika nchi ambayo wananchi wake wako huru. Kifungu cha kumi cha muswada huo, kinachorekebisha Ibara ya 66 ya Ibara ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais amepewa uwezo wa kuteua si zaidi ya watu kumi na kuwafanya kuwa ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muswada haukutaja kama kabla ya uteuzi huo Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar ili kuwapata watu hao kumi, na wala haieleweki kama uwezo huo anaopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano una uhusiano au la na mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964? Kuhusu mfano wa nilichokusudia katika nukta iliyotangulia, nitamnukuu mwandishi moja kutoka katika gazeti la Alasiri la tarehe 10, Februari 2000 alipoeleza "Wakati fulani, Mbunge mmoja mmoja kutoka Zanzibar alisimama kupinga mapendekezo yaliyokuwa na mguso kwao kama Wazanzibari, lakini fimbo ya wingi wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi ndani ya Bunge iliwakaba koo na kuwanyamazisha". Hivi ndivyo nchi inavyoendeshwa kwa kukabana makoo, haki na demokrasia ni maneno tu yanayotumiwa ili kuwalaza usingizi wananchi wengi mambo kishabiki bila ya kutafakari kwa kina kama inavyostahili. Wananchi , ni muhimu, sasa wakaachana na ushabiki wa kisiasa na kuanza kufikiria kuhusu mustakbali na hatima ya nchi yao, wasipoamka haraka, Chama Cha Mapinduzi kitatufikisha pabaya. Hali ya kisiasa na kiuchumi tuliyonayo ndani ya nchi yetu sasa ni matokeo ya sera mbaya za chama tawala ambazo zimepelekea wananchi wengi kuwa masikini katika ardhi yao iliyojaa kila aina ya rasilimali na ardhi yenye rutuba. Kama unalo wazo ambalo unadhani linaweza likaleta manufaa usikae kimya shiriki kwa namna moja au nyingine ili upate au ipatikana fursa ya kuweza kulitumia wazo lako katika utekelezaji wa jambo lenye manufaa na njia rahisi ni kujiandikisha na kupiga kura. Katika muswada wa Serikali Ibara ya 41(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayomtaka mshindi wa kiti cha Urais awe amepata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa, imerekebishwa ili kumuwezesha mgombea wa kiti hicho sasa kutangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura nyingi tu zaidi ya wagombea wengine. Hili ni jambo la hatari kubwa lakini kwa sababu viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wanaamini kuwa usingizi waliolala wananchi wa Tanzania ni mzito kiasi cha kuweza kuwafananisha na maiti, wao wanapongezana na kusifiana nyuma ya migongo yetu kwamba wamefanya kazi nzuri ya kujihakikishia ulaji unaendelea, maana wao wanafahamu kwamba maslahi yao ya kiuchumi yatakuwa hatarini kama demokrasia ya kweli itaota mizizi nchini. Unapowasikia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, wakisema tumefanya hivi au vile kwa sababu ndivyo wananchi wanavyotaka, fahamu kwamba wananchi wanaokusudiwa hapo ni Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa serikali, wewe mlalahoi mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi huna chako, wewe utapewa wali na pilau, kanga na kikoi na kisha utupwe kwenye mavumbi mpaka baada ya miaka mitano tena ndio ukumbukwe kuja kupewa tena wali, pilau, kanga na kikoi. Kwa sababu hiyo, katika kampeni za uchaguzi mwaka huu pilau sasa imehalalishwa rasmi kwamba ni ruksa. Haya ni mambo ya dharau iliyovuka mipaka kwa wananchi. Wananchi amkeni sasa na kuhakikisha kwamba hakuna hata Mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi anapata kura za kumrudisha Bungeni maana kama ni mitaji wamekwisha pata, mapesa watakayolipwa baada ya Bunge kuvunjwa yanawatosha kama hawakutujali wakati wakiwa maskini, watatujali leo wana mapesa? Katika uchaguzi ujao kura zetu tuwape wapinzani, tena wale walioungana na sio wale mamluki wa Chama Cha Mapinduzi ambao hawataki umoja. Wananchi amkeni na muwaepuke watu wanaowafanya kuwa ni majuha kwa kutumia umaarufu wao uliojengwa na vyombo vya habari ili kuwapotezea mwelekeo mkatupe kura zenu kwa kuwapa watu wasiofaa. Mamluki wamepewa kazi ya kuhakikisha kwamba mwajiri wao ambaye ni Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake wanaendelea kubakia madarakani ili na wao waendelee kuwakokota watu kama ng'ombe, akienda Manzse mashabiki wanafuata akienda Ilala mashabiki wanafuata, ukiwaulizia ajenda mnaijua? Hawana la kujibu. Wananchi amkeni na mfahamu kwamba lengo kuu la marekebisho haya ya Katiba yanayofanywa kidogo kidogo badala ya kuandikwa kwa katiba mpya nchini ni kuhakikisha kwamba Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kutawala. Ili deomokrasia ya kweli ipatikane hapa nchini ni lazima vyombo vya dola vipatiwe majukumu mapya yanayoianisha mipaka ya kila kimoja badala ya mfumo uliopo sasa ambao unamfanya Rais kuwa juu ya vyombo vyote vingine pamoja na wananchi waliompa kura kwa ridhaa zao. Sambamba na mkakati wa kutokuwapa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi kura,
tuendelee kudai kuandikwa kwa Katiba mpya ya nchi yetu.
|
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|