|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
IMEELEZWA kuwa chimbuko la kadhia ya Mwembechai halikutokana na kashfa za kidini kama ilivyotakiwa iaminike kwa wananchi, bali limetokana na shinikizo la baadhi ya viongozi wa kanisa kuitaka serikali iwadhibiti wahadhiri wa Kiislamu ambao wanadaiwa kuukashfu Ukristu. Aidha imeelezwa kuwa Waislamu wote ni kama mwili mmoja, hivyo msiba unapomfika mmoja wao basi huwa umeufika umma wote wa Waislamu na hivyo suala la mauaji ya Mbwembechai ni la Waislamu wote na si la Waislamu wachache kama ambavyo imekuwa ikidaiwa. Waislamu wameeleza pia kuwa hawatakuwa kimya mpaka serikali imefanya uchunguzi wa kisheria na kuwafikisha katika "mikono ya sheria" wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya ndugu zao. Hayo yameelezwa katika risala iliyosomwa katika khitma iliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa ajili ya kuwaombea dua Waislamu wenzao waliouawa katika mauaji ya Mwembechai ya Februari 13, 1998. "Leo tumekusanyika hapa kwa ajili ya kuwaombea dua ndugu zetu waliopoteza roho zao katika kadhia ya Mwembechai, pamoja na Masheikh zetu, waliokwisha tutangulia mbele ya haki ambao walikuwa mstari wa mbele katika kuupigania Uislamu na haki za Waislamu katika nchi hii", imesema risala hiyo. Risala hiyo iliyosomwa na Mwenyekitiwa kamati ya maandalizi Sheikh Ali Bassaleh imesema kwamba jazba za vyombo vya dola katika kutekeleza amri ya viongozi wa kanisa iliyotaka mihadhara ya Kiislamu idhibitiwe ndiyo iliyosababisha maafa yaliyotokea Mwembechai. Risala hiyo iliyosomwa mbele ya maelfu ya Waislamu waliokusanyika katika kituo cha Waislamu, Magomeni, imeeleza kuwa Waislamu hawaamini kuwepo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni "kashfa ya kidini." "....hatuamini kuwapo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni 'kashfa za kidini'' kwani shutuma za kashfa za kidini zinazotolewa dhidi ya wahadhiri wa Kiislamu zinadai kuwa wahadhiri hao badala yakutumia Kur-ani ambacho ndicho kitabu chao wao wanatumia Biblia ambacho ni Kitabu cha Wakristo", imesema risala hiyo. Waislamu wamesema katika risala hiyo kwamba ikiwa wafuasi wa dini moja kutumia kitabu cha dini nyingine ndiyo kashfa basi Wakristo ndio walioanzisha mtindo huo. Wamesema: "Huku kwetu Afrika Mashariki tafsiri ya kwanza ya Kur-ani Tukufu kwa lugha za Kiswahili iliandikwa na Padre Geofrey Dale wa Shirika la UMCA, Zanzibar. Na katika tafsiri yake hiyo ameukosoa Uislamu. Mbona hatukusikia kuwa Padre Dale akiambiwa kuwa ameukashifa Uislamu kwa kutumia kitabu cha dini nyingine. Akizungumza katika khitma hiyo, Amiri wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mukuzi aliwatanabaisha Waislamu, kama raia wa nchi hii,kutumia vema haki yao ya kidemokrasia katika uchaguzi mkuu ujao wa Wabunge na Rais utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. "....Waislamu hatupendezi mbele ya macho ya watawala.... Malalamiko yetu hayasikilizwi, lakini hivi karibuni watakuja kutuomba kura, (sasa) mwenye macho haambiwi tazama, mtu unamkopesha anakudhulumu halafu akija tena unamkopesha, (basi) akili ni nywele", alisema Sheikh Mbukuzi. Naye katibu wa kamati ya kutetea haki za Waislamu Sheikh Ponda Issa Ponda, akizungumza katika kumbukumbu hiyo ya mauaji ya Mwembechai, alisema yeye hakujificha kama ambavyo imekuwa ikitangazwa na serikali ili kuwaficha wauaji. "Kuanzia Machi 29 mwaka juzi (1998) niliamua kukaa kimya, (kwa vile) nilitaka kuiondolea serikali mazingira ya kuficha mauaji ya Mwembechai", alisema Sheikh Ponda na kuongeza kuwa anawashukuru Waislamu kwa vile waliendeleza juhudi za kuwakumbusha wananchi juu ya unyama wa mauaji yale. Khitma hiyo ambao awali ilikuwa imepangwa kufanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, ilihamishwa katika kituo cha Kiislamu Magomeni baada Waislamu kuambiwa kuwa "hakuna nafasi" japo walikuwa wamekubaliwa kuutumia ukumbi huo. |
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|