|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
|
Umuhimu wa uchumi katika Uislam MWANADAMU ameumbwa na mahitajio mengi ambayo ni budi kuyapata ili
aweze kuishi kwa furaha na amani hapa ulimwenguni. Kwa kuwa binadamu ni
mwili na roho, na pia mahitajio yake yamegawanyika ambapo anayo ya kiroho
na kimwili. Mwandishi RAJAB RAJAB anaelezea zaidi.
MAHITAJIO ya kiroho (spiritual needs) humwezesha mwanadamu kuishi maisha ya utulivu, furaha na amani, na kupatikana kwa utii na unyenyekevu muongozo wa Allah (s.w.). Yapo mahitajio ya kimwili (material needs) kama vile chakula, mavazi pamoja na matibabu hupatikana kwa njia ya uchumi ambapo Allah amejalia mali anayoichuma mwanadamu iwe ndiyo inayofanya maisha yake yafanikiwe. "Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambao Mwenyezi Mungu amezijalia kwa ajili ya maisha yenu.....(4,5). Kuchuma mali siyo jambo la hiari kwa binaadamu na vitu vyote Ulimwenguni vimeumbwa kwa ajili yake i.e yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi (2:29). Lakini vita hivi haviko katika hali ya kutumika na mwanadamu moja kwa moja, bali mwanadamu analazimika kutumia akili, elimu yake, maarifa yake, juhudi zake na vipaji vyake vingine ili ayabadilishe mazingira yake yaweze kumtumikia na kukidhi haja zote. "Na itakapolazimisha swala, tumenyikeni katika ardhi na mtafutie fadhila za Mwenyezi Mungu na mkumbukeni (yeye)Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufuaulu (62:10). Hivyo basi kuchuma ni wajibu unaompasa Mwislamu mara tu baada ya kutekeleza swala ambapo hii inasisitizwa na kubainishwa katika hadithi ifuatayo:- Abdallah bin Mas'ud ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) anasema kutafuta ridhiki ya halali ni faradhi baada ya kutekeleza faradhi nyingine. Pia Mtumbe (s.a.w.) ameeleza wazi ubora wa kujizatiti katika kutafuta chumo halali katika hadhithi ifuatayo: Nigden bin Ma-ad Yalarab ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) amesema hapana mmoja wenu aliyekula chakula kizuri kuliko kile alichokula kutokana na kazi ya mikono yake mwenyewe. Na tunaambiwa kwamba Mtume Daud alikuwa anakula kutokana na kazi ya mikono yake (Bulaheri). Uislam unalaani vikali sana tabia ya uvivu na kutegemea wengine pasipo na sababu au dharura madam kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo: Abdullah bin As-ud ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) amesema kuwa anayeombaomba watu na ilihali ana mahitaji muhimu ya maisha atakuja siku ya kiyama na kuombaomba kwake kama mikwaruzo, vidonda au majeraha usoni kwake. Iliulizwa. Eee Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kiasi gani kinachomtosha mtu? Akijibu Dirham 50 tu thamani yake ya dhahabu (Abu Daud, Jimidh, Nisai, ibn Majah). Hubshibin Junadah ameeleza kuwa Mtume wa Allah(s.a.w.) amesema: kuombaomba si halali kwa mwenye uwezo wala kwa mwenye afya na nguvu za kufanya kazi ila kwa mwenye kupigwa na ukafiri na mwenye deni kubwa asiloweza kulilipa. Na yule anayeomba watu ili ajiongezee mali yake atakuwa na mikwaruzo usoni mwake siku ya kiyana na atayala kwa ulafi mkubwa mawe ya motoni, kwahiyo anayetaka muache aombe kidogo au kingi (Tirmidh). Hivyo uchumi ndiyo msingi wa maisha ya mwanadamu hapa duniani na Uislam unawajibisha kuchuma kwa kila mwenye uwezo. Aidha Uislam una uhuru wake wa kuchuma ambapo ni kosa kubwa kwa serikali kuweka vikwazo vya kuwazuia watu wasitumie vipaji vyao na uwezo wao katika kuchuma kwa njia ya halali. Badala yake Serikali au Dola ya Kiislam inawajibika kuondoa vikwazo vyote vinavyozuia watu kutumia vipaji vyao katika kuchuma na kutoa vishawishi/motisha vya kuvutia au watu waliojiunga katika vikundi wajiingize katika sekta mbali mbali za uchumi kwa juhudi kubwa na kutumia maarifa yao yote waliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Pamoja na uhuru kamili uliotolewa na Uislam vile vile kila mtu ana haki ya kumiliki kile alichokichuma kwa njia ya halali. "Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine." Wanaume wanayo sehemu kamili ya vile walivyochuma na wanawake wanayo sehemu kamili ya vile walivyovichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake hakika ya Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu (4:32). Mbali ya Uislam kuweka wazi kuhusu uhuru wa kuchuma, pia imefafanua na kuwa na miiko ya kuchuma ambapo inajinasabisha na lengo la kuumbwa kwa mwanadamu kuwa ni kumuabudu Allah (s.w.)51:56). Hivyo basi kila kitendo anachokifanya mwanadamu ni Ibada na kutokana na nia anayokuwa nayo wakati wa kuanza na kumzingatia Allah na kuchunga mipaka yake. Endapo wakati wa kuchuma tutazingatia mipaka ya halali, tunaweza kuchunga mipaka ya haramu na halali katika kuchuma kwetu ikiwa tutajenga tabia ya kumkumbuka Allah (s.w.) kila wakati hata tukiwa katikati ya harakati za kuchuma kama tunavyobainishiwa katika Qur-an amri ya kujishughulisha na uchumi imeambatana na kumkumbuka Allah (s.w.) kwa wingi. Mzee Luqman anatupa funzo wakati akimuusia mwanae kwa kusema "Ewe Mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na chembe ya mdudu hardali, likawa ndani ya Jabali au mbinguni au ardhini, Allah atalileta ampe anayestahili, bila shaka Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri (34:16). Sisi kama Waislamu inatupasa kutumia vipato vyetu katika njia anayoridhia Mwenyezi Mungu ama ambazo ameamrisha kama vile kutoa zakat na sadaqa na katika njia yoyote ile ya kuitetea na kuipigania dini yake. Katika Uislam kipato haramu kinaweza kuwa au kupatikana endapo atachuma katika maeneo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake. Mfano kufanya kazi katika Taasisi za riba na kamari viwanda vya bia pamoja na miradi ya nguruwe n.k. Vile vile atachupa mipaka ya Allah(s.w.) japo katika eneo halali mfano kufanya biashara ya udanganyifu kama vile kupunja mizani, kutoa bei ya uwongo na kumuhadaa mnunuzi kwa viapo vya kila aina. Pia kudhulumu haki za wengine kwa kutumia mbinu ambapo Muislam wa kweli anatakiwa ajiepushe na chumo haramu kwani hatanusurika na adhabu ya Allah (s.w.) kama hadithi zifuatazo zinavyoeleza: Hapana nyumba iliyojengewa na vitu haramu itakayostahiki mahali pengine zaidi ya motoni. (Ahmed, Darini, Baihaqi). Abu Bakar naye ameeleza kuwa Mtume (s.a.w.) amesema mwili ulionasuirishwa na vitu harama hautaingia peponi (Baihaqi). Muislam anatakiwa ajitafutie/kuchuma kipato halali ambacho ni kipato kinachotokana na kazi ya halali ambayo ameifanya kwa uadilifu na kuchunga mipaka ya Allah (s.w.). Muislam wa kweli ni budi kufanya juhudi za kujitafutia chumo halali akijua kama hiyo kwake ni Ibada yenye malipo mbele ya Mwenyezi Mungu Subhana Wataala. Uislam pia umebainisha kazi za benki katika uchumi na jamii ambapo mabenki ni muhimu sana kwa kutoa huduma mbali mbali kama vile kuhifadhi akiba za watu na mali zenye thamani kubwa kama dhahabu. Pia benki kukopesha fedha kwa watu wanaozozihitaji ili ziwe mtaji wa kuendeshea biashara, viwanda, kilimo pamoja na sekta mbalimbali ambazo zinatoa huduma kwa jamii. Kazi nyingine ya benki ni kutoa malipo ya mbali popote pale penye matawi yake nchini au Ulimwenguni, huduma hii huwapunguzia watu kusafiri na fedha nyingi mkononi. Vile vile Benki hurahisisha malipo kwa njia ya Hundi (cheque) kuwalipa wafanyakazi kupitia Benki kwenye Akaunti (ACCOUNTS) zao au kwa hundi, huwaepushia walipaji hatari ya kuibiwa na wezi na kuporwa na mjambazi. Uislam kama ulivyo hautarajiwi kupinga au kuharamisha kuwepo kwa mabenki katika jamii, bali Uislam unaramisha mabenki yanayoendeshwa kwa kipato cha riba, kwa kuwa riba imeharamishwa katika Qur-an. "Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini. Na kama hamtafanya hivyo basi fahamuni mtakuwa na vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu basi mtapata rasilimali zenu, msidhulumu wala msidhulumiwe (2:278-79). Enyi mlioamini msile riba na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kutengenekewa. Na ogopeni moto ambao umewekewa wenye kukanusha amri za Mwenyezi Mungu (3:130-131). Pia tunafahamishwa katika hadithi ifuatayo Jabir (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah (s.a.w.) amemlaani mwenye kupokea riba, mwenye kuitoa, mwandishi wake na mashahidi wake. Na alisisitiza kuwa wote ni kitu kimoja (Muslim). Riba ni mali ya ziada anayotakiwa mtu airudishe pamoja na rasilimali au kiasi kile alichokikopa. Riba imeharamishwa kwa sababu ya madhara yake ya kuwadhulumu maskini na wenye kipato cha chini katika jamii na kudidimiza uchumi wake kwa ujumla. Sasa tuangalie tofauti ya riba na faida inayotokana na biashara ambapo kuna baadhi ya watu wanapendelea kukopesha fedha zao kwa riba baada ya kufanyia biashara au sekta nyingine za uchumi. Dhana yao hii Mwenyezi Mungu ameibainisha katika Qur-an. Wale wenye kila riba hawasimami (kuendesha yao) ila kama anavyosimamia yule ambaye shetani kumzuga kwa kumusa. Na haya ni kwa sababu wamesema, "Biashara ni kama riba" hali Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na kuharamisha riba.....(2:275). Pia Allah anasisitiza: "Enyi mlioamini msiliane mali zenu kwa batili. Isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu.....(4:29). Riba nikipato kinachopatikana pasina kutoa jasho lolote au kujiingiza katika harakati za uchumi na mashaka yake. Mtu aliyekopesha kwa riba ana hakika ya kupata riba yake bila ya kujali kuwa huyo aliyekopa amepata faida au hasara katika mradi alioukopea mtaji huo. Mabenki ya Riba (kijahili - yasiyokuwa ya Kiislam) sehemu kubwa ya kipato chake hutokana na riba, ambazo hukopesha watu wenye miradi mbalimbali ya uchumi na kuwatoza riba kubwa katika mfumo wa malimbikizo (compound Interest). Kwa upande wa benki za Kiislamu zenyewe huendeshwa katika msingi wa biashara na sio ule wa riba. Benki za Kiislamu badala ya kukopesha kwa riba hutumia rasilimali yake zenyewe kujiendesha kiuzalishaji kwa kutumia misingi inayokubalika ya Kiislam. Benki za Kiislam zina uzuri wake ambapo huikoa jamii na uchumi wake na madhara yote yanayosababishwa na riba. Vile vile benki za Kiislam huwaingiza katika uchumi hata wale wasio na rasilimali yoyote. Mikopo ya riba ni makafiri tu ndio wanaopata mikopo ya benki za kijahili na masikini wanaochuma patupu. Aidha Benki za Kiislam huinua hali ya uchumi wa jamii, kutokana na umakini na taadhari kubwa zinazochukuliwa katika kuchagua miradi ya uchumi, kwa vile benki zenyewe zinajiingiza katika shughuli za uchumi. Japo benki za Kiislam zimeamrishwa 1975, zimekuwa zikiongezeka haraka na kusambaa kote ulimwenguni. Si wajibu wetu Waislam wa nchi hii kuhakikisha kuwa benki za Kiislam zimeanzishwa ili kujinasua na uchumi wa riba ambao unadidimiza jamii. Kulingana na maelezo hapo juu pato la dola ya Kiislam lazima lipatikane kwa njia za halali. Kilicho haramu kwa mtu binafsi, pia ni haramu kwa Dola. Sehemu kubwa ya pato la dola ya Kiislam hutokana na zakat, Sadaq, ushuru wa bodi. Halikadhalika, Uislam umeweka mgawanyiko maalum wa utajiri katika jamii ambapo kila mwanaume analo jukumu la kuzalisha mali ya kutosha kukidhi mahitaji muhimu ya familia yake na wanaomtegemea. Iwapo hana uwezo wa kukidhi mahitaji yake ya muhimu ya familia yake na wanaomtegemea, anastahiki kupewa fungu la zakat kutoka katika hazina ya Serikali. Iwapo atakuwa na ziada atawaibika kutoa zakat na sadaqa. Fukara, yatima, wenye kushindwa kulipa madeni ya halali, wanahaki ya kupata msaada kutoka kwenye hazina ya serikali. Serikali ya Kiislam pia ina wajibika kutoa huduma zote za kijamii mfano usafiri, elimu, maji mawasiliano, hospitali, umeme na mambo mengineyo. Uislam una mfumo wake wa kiuchumi uliokamilika, ambapo kila Muislam ni budi kuufahamu na anawajibika kuchuma kulingana na mfumo huo na kamwe Uislam na Waislamu hawataweza kusimamisha Uislam katika jamii kama wataendelea na mtindo wa kufuata mfumo wa uchumi wa kijahili. Shime ndugu zangu Waislam tutafakari kwa makini makala hii ambapo ni matumaini yangu kuomba itaweza kutupa mwanga na kuepukana na chumo haramu na kuyaendea machumo ya halal ili kuweza kupata radhi za Allah(s.w.) hapa ulimwenguni na kesho akhera. |
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|