|
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000 |
|
|
|
|
|
WAZO LA MWANDISHI Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu NA Y. KIJUKUU NI JUMATANO nyingine imewadia ndugu wasomaji wapendwa wa safu hii tunapokutana tena kuyajadili yale ambayo ni muhimu kwetu kama jamii.Lakini awali ya yote hatunabudi kumshukuru Muumba wetu aliyatujaalia uhai mpaka hii leo. Katika wazo la wiki hii tunazungumzia umuhimu wa kukiri kosa na kuomba radhi ukiwa kama ndio kipimo cha utu miongoni mwa binadamu. Kuomba radhi ni kitendo ambacho hutokea mara tu mtu au kikundi cha watu fulani kukiri kosa au uovu ambalo mtu au watu hao wamelitenda dhidi ya mtu au watu wengine. Haipingiki na wala haikanushiki kuwa katika jamii hii ya leo ambayo utawala wake kuanzia ngazi ya familia hadi taifa ni ule wa mkubwa kutomthamini mdogo na mwenye nacho kumdharau na kumdhihaki asiye nacho, tendo hili la kuomba radhi halitendwi. Hofu ya kuomba radhi ndiyo inayopelekea watenda maovu mbalimbali kusita au kushindwa kabisa kukiri makosa waliyoyafanya dhidi ya wenzao ingawa hutambua machungu wayapatayo. Ipo bayana kuwa lau kama uovu ungelitendwa dhidi ya waliotenda awali basi kila mtu angekuwa shuhuda dhidi ya malalamiko na ukali wenye wingi wa vitisho kutoka kwa wahusika kwa sababu tu wao ni majabali dhidi ya wenzao. Mifano ipo mingi na ni ya wazi na yenye mashiko ambayo hudhihirisha ukweli wa ninachokisema. Si vema kuificha mifano hii, nianze tu na ile kero kubwa inayowasibu wakazi wa Lindi na Mtwara yaani tatizo sugu la barabara. Mwaka 1995 Watu walisimama kwenye majukwa ya kisiasa wakinadi sera zilizoshindwa kutekelezeka, kwa kuwaeleza wananchi kuwa endapo wangewaweka madarakani basi barabara hiyo ingepitika majira yote. Lakini hadi hii leo ambapo kipindi kingine kimefika cha wahusika kwenda kuomba tena warudishiwe madarakani bado barabara hiyo ni mbovu na ubovu wake hauelezeki. Kimya cha wahusika hao kutokiri kosa la udanganyifu dhidi ya wananchi wa kusini ni kutokana na ukweli kwamba kitendo cha kuomba radhi hakipo katika bongo zao na wanahisi kuwa kufanya hivyo ni utumwa wa hali ya juu. Pamoja na hayo yote, ukweli upo palepale kwamba suala la mtu kumtuma mwingine kumfanyia kazi na hasa kwa manufaa ya wengi hilo ni jambo la busara sana hasa mtumaji akijiona hana nafasi au ujuzi wa kutosha kuhusiana nasuala hilo. Na ni busara pia kwa mtu aliyetumwa aifanye kazi hiyo kwa umakini huku akijua yeye ni tumaini kubwa la waliowengi. Hivyo ni vema akatumia ujuzi alionao na akawa mpole na mwenye hekima katika kuliendea suala hilo. Pindi mtumwaji atakapoifanya kazi hiyo kwa utaalamu wake, hata kama ufanyaji kazi wake haukuendana na matakwa yaaliyemtuma, si vema kwa aliyemtuma kusimama hadharani na kumuumbua mtumwaji kwa kutumia kashfa na dhihaka mbalimbali. Hivyo pindi likitokea hilo ni vizuri mtumaji akarudi tena hadharani baada ya jazba zake kuisha ili akiri kosa la kumdhalilisha aliyemtuma na hatimaye amuombe radhi. Kwa mfano kitendo cha Mheshimia Rais wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania kuiponda iliyokuwa kamati ya Jaji Kisanga ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya 13 yakatiba na kuifedhehesha peupe hilo ni kosa kwa mujibu na makubaliano yao ya awali. Yawezekana Mheshimiwa alighafrika kwa kile alichokitenda lakini sasa ni vema akarudi tena palepale alipomdhalilishia Kisanga ili akiri kosa hilo na amuombe radhimtaalamu huyo. Kwani kile alichomdhalilishia ameshafanikiwa kwa kiwango kile kile alichotaka. Tukiachana na hilo ni vema tukaangalia dhana iliyojengeka kwa Waislamu kuwa Kadinali Pengo ni sehemu ya Ikulu. Dhana hii inatokana na ukweli kwamba mwenendo mzima wa mhashamu Kadinali huyo hauiridhishi jamii hiyo na ni dhahiri unadhiririsha mashiko ya dhana hiyo. Kadinali Pengo akiwa kama kiongozi wa Kikatoliki anatakiwa kushughulika na hisia za watu wa upande wake kiroho. Hakupaswa kuijibia Ikulu katika mambo yanayoihusu Ikulu, bali ana uwezo mkubwa kulijibia kanisa katika mambo yanayohusu kanisa, tena kanisa Katoliki na sio KKKT au Pentekoste. Hivyo kitendo cha kiongozi huyo wa kidini kujibu hoja ya Tanzania kujiunga au kutojiunga na OIC nikosa kubwa kwelikweli ambalo msamaha wake kutoka kwa walioathirika na kauli yake ni kwa yeye mwenyewe kusimama katika kadamnasi kukiri kosa na kuwaomba radhi walioathirika. Kutoomba radhi kwa KadinaliPengo kutaleta hisia kwa walio Waislamu kuwa hulka hii ya kinyama ya kutokiri makosa na kuomana radhi sasa imeingia hata katika nyumba nyingine za ibada. Wakristo ni watu wema kabisa hivyo Pengo asiwatie doa. Kimya cha kiongozi huyo kitasabisha jamii ya Waislmu kutomuelewa nakuendeleza hisia kuwa Mhashamu Kadinali ni sehemu ya Ikulu yaTanzania. Nihitimishe kwa kusema kuwa kuombana radhi hakuashirii kuwa muombaji ni dhalili au kamuogopa aliyemuomba na haimaanishi kuwa muombwaji ni jabali bali tabia hii huongeza mapenzi baina ya wahusika na kwa kweli hiki ni kipimo cha utu. Jamii isijilinganishe na ng'ombe, mbuzi au kondoo walio zizini, ambao hata kama mmojawapo atawakojolea wenzake, aidha iwe kwa kukusudia au kwa bahati mbaya, mnyama huyo hatothubutu kuwaombaradhi wenzake ingawa anatambua kuwa amewakosea. Hiyo ni tabia ya kinyama, nasi sio wanyama na hatutarajii kuwa wanyama kivyovyote vile. |
YALIYOMO
Tahariri:
Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu Ushauri
Nasaha
MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
LISHE
|
|
|
|
|