AN-NUUR
Na.165 Jamadul Awwal 1419, Septembe 4 - 10, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MASHAIRI
 

Utenzi wa Kongamano la akinamama Tanga 
 

 Hodi hodi Mhariri, Naingia kwa fakhari, 
Niseme yaliyo kheri, Yawafae Islam. 

Salam nakutolea, Ilojaa nyingi dua, 
Na Rehma za Karima, Nazitoa kwa jamia. 

Wageni mlofikishwa, Tanga tumefurahishwa, 
Katu hatutayumbishwa, Msimamo twawapasha. 

Walisema halitawa, Mbona sasa limekuwa, 
Vitisho na nyingi mbawa, Wanawake kufanyiwa. 

Ni askari wa dola, Wasomuogopa Mola, 
Walotanda kila kola, Na maswali kutudanda. 

Kibali kuulizia, Kutafuta kutuzuia, 
Kuivunja yetu nia, Wanawake kukutana. 

Mola wetu kajalia, Kuepusha zao hilo, 
Kongamano limekua, Mawazo tumepeana. 

Tumeonewa vyatosha, Kilobaki twawapasha, 
Katu hatutabakisha, Tutasema vyakutosha. 

Waislamu wanawake, Shime tuunganike, 
Tusije fanya makeke, Adui kutuhadaa. 

Tusijefanya ajizi, Tukawaiga washenzi, 
Tabia na lao vazi, Vitatuangamiza. 

Tuvae nguo stara, Zile zisizo na dhara, 
Ni jadi yetu stara, Kuiga hakutufai. 

Tusimkosoe Manani, Dawa ya ngozi ya nini, 
Mwajichubua kwa  nini, Mola tunamchukiza. 

Tujielimishe kidhati, Madada na wetu binti, 
Tusipoteze bahati, Allah atatuuliza. 

Tusikubali dhuluma, Ikibidi tutasema, 
Sasa basi tunasema, Kuonewa hatutaki. 

Mwembechai ni mfano, Hatulisahau mno, 
Waliokufa mfano, Tuliobaki radhi kufa. 

Kamwe tusiwe wazito, Duniani ni mapito, 
Tusiwe kama watoto, Kongamano twaagiza. 

Wenzenu Tanga twasema, Kosa hatutorudia, 
Elfu mbili kufikia, Kweli tutaionyesha. 
 
 

Haki 

Haki ipo popote wajibu, kwa waja kutimiziwa, 
Vimeandikwa vitabu, ambavyo tumeshushiwa, 
Ameagiza Wahabu, pasiwe kudhulumiwa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Haki neno hili haki, si neno la kuchezewa, 
Husababisha hamaki, wapewa wasipopewa, 
Huzusha kutaharuki, na madhara kuchochewa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Watu hutumia nguvu, haki ikihujumiwa, 
Purukushani – mabavu, huenda yakatumiwa, 
Ukakoma ulegevu, haki yao kupatiwa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Haki mithili ya boya, kwa waliokusudiwa, 
Haiko kama hidaya, ya mtu kuzawadiwa, 
Kuikosesha vibaya, mwisho ni kuadhibiwa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Haki iwe ya ye yote, hakuna kubaguliwa, 
Ni lazima aipate, japo ni kwa kuchelewa, 
‘Dhulumati’ asiote, kwamba atanusurika, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Haki jambo hili zito, yatakiwa kutetewa, 
Ya kauli ama pato, isiwe kubadilika, 
Chumo la dhambi majuto, kwa wale watuhumiwa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu 

Haki ikikosekana, kwa waliodhamiriwa, 
Salama huwa hakuna, ‘woga’ watu huishiwa, 
Huwa radhi kupambana, si kingine kusikiya, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 

Nafanya ufupishaji, shairi latamatiwa, 
Natulia nataraji, ujumbe umesikiwa, 
Ndimi mwana wa Miraji, Kassim mwenye kipawa, 
Haki ikidhulumiwa, huchukuliwa kwa nguvu. 
 

Dk. Kassim M.P. Haumotile, 
S.L.P. 25578, 
Dar es Salaam. 
 
 

Yataka kutafakari 

Lazima kuwa makini, jambo kulifikiria, 
Vizuri uketi chini, uwaze umetulia, 
Utakijua kiini, upate kinofatia, 
Wewe mja kujijua, yataka kutakafari. 

Waweza kuwa huoni, ingawa waangalia, 
Ziko wazi zako mboni, na jicho umekodoa, 
Jiulize nafsini, usende unapamia, 
Njia njema kuijua, yataka kutafakari. 

Tutakuona khaini, kuacha ya sawa njia, 
Yalo mema huyaoni, dalili unafumbia, 
Ukijikuta shimoni, uanze kutulilia, 
Ya kheri ili kujua, yataka kutafakari. 

Kutegemea maoni, na kwako kutamania, 
Uishi huku kidhani, umeiumba dunia, 
Na khatia Insani, hebu kwa Mola rudia, 
Na lengo kuligundua, yataka kutafakari. 

Hata kukaa kitini, wenzio watawalia, 
Huwajali walo chini, walokuweka raia, 
Ni kinyume cha yamini, haufai kubakia, 
Shukurani kuijua, yataka kutafakari. 

Utu unayo thamani, huupati kwa rupia, 
Ni kutenda yenye shani, alofaradhi Jalia, 
Wamepita duniani, haya walokiyajua, 
Matendo kuyatambua, yataka kutafakari. 

Kumjua hayawani, na mtu alotimia, 
Hakuhitaji miwani, bali bongo kutumia, 
Na aya za kitabuni, hili zimetuambia, 
Na ili kuzivumbua, yataka kutakafari. 

Kumkiri Rahmaani, mmiliki wa dunia, 
Mtengeneza kila fani, uluma na hukumia, 
Inahitaji yakini, na nuru kuangazia, 
Njia tutoipotea, yataka kutafakari. 

Kuwajua mumiani, wabakaji wa sheria, 
Waloshika usukani, mbele wakatangulia, 
Kundi moja kuthamini, na jingine kubagua, 
Na dhuluma kuijua, yataka kutafakari. 

Zipo pia za kigeni, siasa tunotumia, 
“Demo” ya Kimarekani, na Ulaya “Shamalia”, 
Ni utumwa uso fani, sisi tumeuridhia, 
Ubayawe kuujua, yataka kutafakari. 

Witiri ninasaini, hapa kituo natia, 
Ni ibada kwenye dini, kutafakari kadhia, 
Ajabu kwa waumini, hili kutozingatia, 
Tafsiri ya “Uwazi”, yataka kutafakari. 

Jihad R. Saballa, 
Box 347, 
Shinyanga. 
 

Mkwezi (swali na. 1) 

Ninawaomba malenga, popote ulimwenguni, 
Mambo yameshanitinga, sijui nifanye nini, 
 Na roho inanitanga, jawabu nipatieni, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Chanzo cha kisa ni kwamba, nilikuhama mjini, 
Nikaenda hamia shamba, huko kwetu minazini, 
Nikalununua shamba, la minazi fahamuni, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Nazi zilipokomaa, nilikuwa furahani, 
Mkwezi nikachukua, hodari kwa hii fani, 
Zana zake akatwaa, akaingia shambani, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Mitiye mirefu sana, inanepa kileleni, 
Mkwezi kavaa zana, akapanda mnazini, 
Yuwaimba akinena, wakati mimi ni chini, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Katikati akakwama, si juu wala si chini, 
Akaanza kulalama, mimi nakufa jamani, 
Ninajiachia jama, nguvu zaenda mwishoni, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Mimi sijui kupanda, huko juu mnazini, 
Kijijini nako kwenda, ni mbali sana jamani, 
Kila ninavyojipinda, la kufanya silioni, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Nabaki najiuliza, huyu ni mkwezi gani, 
Pia na kujisemeza, huu ni mnazi gani, 
Ni jambo la kushangaza, ushauri natamani, 
Mkwezi ameshakwama, walimwengu nifanyeni? 

Nasaha ninazitaka, asianguke mtini, 
Tena hima kwa haraka, asijedondoka chini, 
Mkichelewa hakika, mtaingia lawamani, 
Mkwezi ataanguka, walimwengu tufanyeni? 

Juma M. Bwanakheri, 
S.L.P. 45245, 
Dar es Salaam. 
 
 

Mola muweke peponi (Siraji) 

Bismilahi Muumba, ulioumba ulimwengu, 
Mimi kwako ninaomba, umsamehe mwanangu, 
Machozi yamenikaba, nipo hoi hali yangu, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Juhudi tulionyesha, kikeni na kiumeni, 
Madawa tulimwosha, ya ndani na ya kigeni, 
Na dua hatukuacha, siku zote midomoni, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Siku ya tarehe tatu, Siraji ametutoka, 
Ni siku ya Jumatatu, mwezi wa nane hakika, 
Mola akamtunuku, kamwita akaitika, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Siku ya  tarehe nne, Siraji tukamzika, 
Kwa wake na waume, wote walimiminika, 
Ikafanywa shime shime, mwenzetu kwenda kuwekwa, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Iwapo nilitamka, baya kubwa kwa mwanangu, 
Na Mola ukaandika, nafuta kauli yangu, 
Ila mema nayataka, umjazie mwanangu, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Yarabi takabalia, dua hii kwa mwanangu, 
Pazuri muandalia, muondolee machungu, 
Peponi kwenda tulia, nakuomba Mola wangu, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Beti hizi naishia, mambo yamenizidia, 
Mola ninakuachia, Muweke ulotimia, 
Motoni kutofikia, Siraji wangu nalia, 
Mola muweke peponi, (Siraji) bin Himidi. 

Safina Omar 
C/o Fauziya Jabiry Katundu, 
Magomeni Kondoa St. No. 16 
Dar es Salaam. 
 
 

Ni basi tumeuawa? 
 

Bismillah Rahmani, Mola unoabudiwa, 
Kusudio la imani, Rabi unotegemewa, 
Waweke pema peponi, wenzetu walouawa, 
Mwembechai Magomeni, ni basi tumeuawa? 

Wamekufa watu thani, wenzetu wamelipuliwa, 
Damu ilokuwa chini, kwa mchanga kufukiwa, 
Ni kama vile kunguni, haki yake kuuawa, 
Atatetewa na nani, Ni basi tumeuawa? 

Mauaji ya Jijini, yafaa kushutumiwa, 
Faraka ziwe pembeni, umoja unatakiwa, 
Na tofauti za dini, Kusupa mezitenguwa, 
Wote twapenda amani, ni basi tumeuawa? 

Mbiu yangu Kigamboni, mpaka huko Lujewa, 
Wa Kigoma vijijini, Mbinga, Nzega na Ludwa, 
Mafia, Mlingotini, Ngara, Magu, Kaliuwa, 
Tunachongojea nini, ni basi tumeuawa? 

Rukwa, Mtwara njooni, wenzenu tumeonewa, 
Mwembechai Magomeni, wenzetu wameuawa, 
Sababu khasa ni nini, muuaji hajatowa, 
Tutangoja hadi lini, ni basi tumeuawa? 

Hivi ni amani  gani, ambayo imetishwa? 
Tanga na Ngaramtoni, Morani mnachelewa! 
Serikali ihojini, kwani vipi yalikuwa, 
Mauaji Magomeni, ni basi tumeuawa? 

Iguguno, Turiani, Musoma mnangojewa, 
Kwa pamoja tulaani, kwa huku kuhujumiwa, 
Tuwahi mahakamani, tume tukishaundiwa, 
Tusikae mashakani, ni basi tumeuawa? 

Shinyanga, Hale, Bumbwini, na Kanda yote ya Ziwa, 
Matipwili, Kibaoni, Mwidu kwa Mfuga Njiwa, 
Rombo, Kibororoni, wenzetu wameuawa, 
Mchango wenu ni nini, ni basi tumeuawa? 

Dodoma kule Bungeni, hili lilishangiliwa, 
Kule kusema pigeni, mependa waheshimiwa, 
Wizara Mambo ya Ndani, na Bajeti imepewa, 
Tulichojifunza ni nini, ni basi tumeuawa? 

Kumi ni kaditamani, na ngoja kuitikiwa, 
Wote wapenda amani, kwa hamu mnangojewa, 
Linze, Nitu mlikoni, mlochoka dhulumiwa, 
Serikali ihojini, ni basi tumeuliwa? 

Wabilah Tawfiq 
K.S. Luanda (Nolo) 
Dar es Salaam 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 
 
TAHARIRI 
HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache 

Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa na kesi 
Na Mwandishi Wetu 

Wazazi walia na Mkuu wa shule Mkwawa 
Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Serikali iache kudhulumu  Waislamu - Bakwata  
Na Mwandishi Wetu

KESI YA MIRATHI: Hukumu ya Jaji Agostino yatupwa 
Na Mwandishi Wetu 

Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini 
Na Mwandishi Wetu, Arusha 

Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga, mtihani kwenu – Sheikh Akilimali 
Na Harun Rashid, Sumbawanga 

37 wasilimu  Mwanza 
Na Mwandishi Wetu, Mwanza 

Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! 

MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi 
Na Mwandishi Wetu, Pemba 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 

Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni Marekani? 
Na Maalim Ali Bassaleh 

Profesa amekosea kusema kwamba... 
Na A.M. Hamza 

Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani ni ugaidi 
Na Maalim Ali Bassaleh 

Dhana ya Udugu wa kiislamu 

UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma ya Marekani 
Na HASSAN KIMANGALE 

Jengeni familia bora 
Na Abuu Said, Iringa 

Tuwasaidie Waislamu kielimu na kiuchumi - Bi Zuhura 
Na SAID RAMADHANI KISSIMBA 

Tumieni uhuru wenu vyema 
Na Abuu Zaina, Iringa 

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 4  
Na Muhibu Said 

Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni 
Na Mwandishi Wetu, Handeni 

Ziara ya Kadinali Pengo Moro  
Na Mussa Ally, Morogoro 

Aonyesha ujuzi wa kutengeneza Trekta 
Na Mwandishi Wetu 

Waislamu wasizifanye sharia za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge 
Na Ashraf  Yusuf, Moshi 

Sengerema waomba msaada 
Na Idd Katimba, Mwanza 
 
Mafundisho ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi: 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Matunzo ya mtoto mwenye lishe duni 

Matangazo 
 
 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita