|
|
| Kwa
nini walengwa wa mabomu wawe ni Marekani?
KAULI ya Mhariri wa gazeti la Msemakweli toleo Namba 024, ina ajenda ya siri dhidi ya Waislamu. Imelenga katika kujenga chuki baina ya Waislamu na wale wasio Waislamu. Imekusudia kuleta hisia kuwa Waislamu ni watu makatili walio tayari kutoa roho za binadamu wenzao, bure, kwa sababu tu siyo Waislamu. Fuatana na Mwandishi Maalim Ali Bassaleh katika makala hii. Nikiinukuu sehemu ya kauli hiyo, katika jitihada za kuelezea wale wanaohusika na milipuko ya mabomu, hapa jijini Dar es Slaam na kule Nairobi, Kenya. Gazeti hilo limeandika "…pia wahusika hao, wanahisiwa kuwa ni makomandoo wa mujahidina ambao kwa mujibu wa imani yao kumwua ‘kafiri’ tayari wamekata tiketi ya kuingia peponi". Ni dhahiri kuwa maneno hayo yamekusudiwa kuipa nguvu ile dhana yakuwa waliolipua mabomu hayo lazima wawe ni Mujahidina wa Kiislamu, kwa vile kama anavyodai Mhariri huyo ni imani yao wakiua makafiri, yaani wasio Waislamu, wataingia peponi. Kwanza kumtuhumu mtu kuwa ametenda kosa fulani haitoshi kuwa ndiyo sababu ya kumtia hatiani mtuhumiwa huyo. Lilipolipuliwa jengo la kibiashara, kule Oklahoma, Marekani, watu wa mwanzo kushukiwa kufanya ugaidi huo walikuwa ni Mujahidina. Lakini baada ya kufanywa uchunguzi wa kina, imekuja kubainika kuwa waliohusika ni Wamarekani wenyewe na siyo Mujahidina kama ilivyokuwa ikihisiwa. Haitashangaza hili likiwa hivyo. Katika tukio hili pacha, lililotokea sambamba kati ya Dar es Salaam na Nairobi, tayari vyombo vya habari vingi vimekwisha wajengea watu hisia kuwa waliofanya uharibifu huo ni Mujahidina. Kwa kweli ni mapema mno kujua, kwa hakika ni akina nani waliofanya hujuma hizo na kwa lengo gani. Wachunguzi wa nchi zetu mbili, Tanzania na Kenya wakishirikiana na FBI, wanaendelea na uchunguzi wao kujua nani waliohusika, kwanini basi sisi tuwe wepesi kuwatia hatiani watuhumiwa, Mujahidina, hata kabla ya uchunguzi kukamilika? Ninavyoona walipuaji wa mabomu hawana dini maalumu. Wanaweza kuwa ni wafuasi wa dini yoyote ile, au pegine wasiwe na dini kamwe. Je! Lile bomu lililolipuka juzi kule Omargh, Ireland, likaua watu 28 na kujeruhi zaidi ya watu 200, nalo limelipuliwa na Mujahidina? Siyo Wakristo, wenyewe kwa wenyewe, ndio waliofanyiana unyama huo? Wanaogombana huko Ireland ni Wakatoliki na Waprotestanti. Tuseme nao hao wanaamini kwamba yule atakayemua mwenzie ataingia peponi? Bomu lililolipuliwa Dar es Salaam limeua watu kumi. Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na vyombo vya habari majina ya maiti tisa miongoni mwa hao waliouawa yanaonyesha ni ya Waislamu. Kama hao waliofanya hivyo walikuwa wakitekeleza imani ya dini yao, mbona basi wamewaua Waislamu wenzao? Au wana imani, pia hata wakiua Waislamu wenzao wataingia peponi? Uislamu ni dini ya amani. Inajali sana uhai wa binadamu na hata wa viumbe vingine. Muislamu wa kweli hawezi kuwatendea wanadamu wenziwe vitendo vya kikatili kwa jina la jihadi. Kuua makafiri bure bure bila ya makafiri hao kuufanyia uadui wa dhahiri Uislamu siyo jihadi wala si Uislamu. Jihadi ni kupambana na yule anayetaka kuudhuru Uislamu au Waislamu. Uislamu unaheshimu nafsi ya kila kiumbe. Wachilia mbali kuua mtu mwingine, Uislamu unamkataza Muislamu asijiue mwenyewe, amesema: "Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuhurumieni". (An Nisaa 4:29). Pia Uislamu umekataza kuua wengine. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza (kuiua) isipokuwa kwa haki. Na haki ya kumuua mtu mwingine ni kuwa mtu huyo awe yeye ametangulia kuwaua binadamu mwenzie. Hapo tena mtu kama huyo atakamatwa na kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria vinavyokubalika na kuhukumiwa. Ukipatikana ushahidi wa kuaminika kumtia hatiani ndipo atakapouawa. Hata huku kuwachoma moto vibaka au kuwapiga matofali na kuwaua ni kinyume na mafundisho ya Uislamu. Au unaweza kuua kwa kutaka kujihami na adui anayekusudia kukudhuru. Na neno NAFSI lina maana pana zaidi. Siyo wanadamu tu, bali linatumika hata kwa roho za wanyama. Hata wanyama huna haki ya kumwua isipokuwa kwa ajili ya chakula. Mtume (saw) amekataza kumfunga mnyama kwa ajili ya kulenga shabaha. Katika kuonyesha ubaya wa kumtesa mnyama na kumuua bure, Mtume (saw) aliwaelezea masahaba wake kuwa kuna mwanamke mmoja huenda akawa miongoni mwa watu wa motoni, kwa sababu ya kumfungia paka, asimpe chakula wala asimruhusu akajitafutie chakula mwenyewe, mpaka akafa kwa njaa. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu mbwa ni haramu na najisi. Lakini Mtume (saw) aliwahadithia masahaba wake kuwa mtu mmoja alisamehewa madhambi yake kwa ajili ya kumruhumia mbwa aliyekuwa ana kiu, akampa maji. Ikiwa nafsi za paka na mbwa zinataka ziheshimiwe vipi basi Muislamu wa kweli atathubutu kutoa roho za binadamu wenzake bila ya sababu yoyote? Mwenyezi Mungu anasema: "…atakayemuua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwokoa mtu (akamsaidia aishi) ni kama amewaacha hai watu wote". (Al Maidah 5:32). Kwa vyovyote vile Muislamu haruhusiwi aidhuru nafsi ya kiumbe mwingine. Ni sawa kabisa kuwalaani wale waliotenda kitendo hicho kiovu, kilichosababisha watu 257 kuuawa na zaidi ya 5000 kujeruhiwa. Na pia ni sahihi kuwatafuta waliofanya ukatili huo na kuwahukumu kwa mujibu wa sheria. Lakini bado kuna swali moja ambalo lazima lijibiwe. Kwanini siku zote walengwa wa mabomu wawe ni Marekani? Wamekosa nini, mbona wanachukiwa sana? Haiingii akilini kuwa hao wanaowalenga kuwalipua kwa mabomu wasiwe na sababu ya msingi ya kufanya hivyo! Hao wanaolipua mabomu hujitolea kufa ili watimize hilo lengo lao la kulipua. Basi ni kweli mtu awe tayari kuiangamiza nafsi yake bila ya kuwa na shahaba yoyote? Ni vyema Marekani ikafanya uchunguzi wa kina kuona kwa nini hao walipuaji mabomu wanawaandama wao tu? Mbona hawawalipui Wafaransa, Wajerumani, Wataliano, Warusi, Wajapani na wengineo? Kila likilipuliwa bomu mlengwa ni Marekani, lakini tunaokufa wengi, hata tusiokuwa Wamarekani. Marekani itakapofanya uchunguzi wa kina na kujua sababu ya kuandamwa wao tu, hapana shaka itatunusuru na sisi tusiohusika kuuawa bure. Lakini kama Marekani itaendelea kufanya uchunguzi wa kuwatafuta walipuaji
tu bila ya kuchunguza kwa nini wanaliopua mabomu hayo wajue watatumaliza
kwa kutuua.
|
TAHARIRI HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa
na kesi
Wazazi walia na Mkuu wa shule
Mkwawa
Serikali iache kudhulumu
Waislamu - Bakwata
KESI YA MIRATHI: Hukumu ya
Jaji Agostino yatupwa
Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini
Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga,
mtihani kwenu – Sheikh Akilimali
37 wasilimu Mwanza
Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali
ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni
Marekani?
Profesa amekosea kusema kwamba...
Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani
ni ugaidi
UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma
ya Marekani
Jengeni familia bora
Tuwasaidie Waislamu kielimu
na kiuchumi - Bi Zuhura
Tumieni uhuru wenu vyema
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 4
Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni
Ziara ya Kadinali Pengo Moro
Aonyesha ujuzi wa kutengeneza
Trekta
Waislamu wasizifanye sharia
za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge
Sengerema waomba msaada
Chakula na Lishe
|