|
|
|
Na Abuu Said, Iringa WAZAZI wa Kiislamu wametakiwa kuwalea watoto wao kwa misingi ya Kiislamu na kuwapa elimu ya Tawhiid inayojenga fikra za kumuamini na kumuogopa Allah (sw) na kuwafundisha kutamka ‘Lailaaha Illah llah, Muhammada Rasulullah’ wangali wadogo. Wito huo umetolewa na umoja wa wasomi wa chama cha watalaamu cha Waislamu Tanzania (TAMPRO), Ustadh Salim Khator akitoa mada "Familia ya Kiislamu ndio msingi wa jamii" kwenye semina iliyofuatia ufunguzi wa tawi la TAMPRO la mkoa wa Iringa hivi karibuni. Ili kuhakikisha ndoa na familia za Waislamu zinakuwa za furaha na amani ni wajibu wa mume na mke kuwa makini katika kuchagua mwenza kwa kuzingatia mipaka iliyowekwa na Allah (sw) katika Qur’an, mafundisho ya Mtume (saw) na ushauri wa wazazi au walezi. Alisisitiza kwamba maisha ya mapenzi, huruma na ushirikiano kati ya mume na mke yatapatikana endapo mke na mume watakuwa wacha Mungu na wenye tabia njema anayoiridhia Allah (sw) na kama watakuwa na elimu ya kuwawezesha kujua vilivyo mazingira ya Uislamu wao na jinsi ya kuwapatia watoto wao malezi ya Kiislamu. Amesema kwasababu ndoa ndio msingi mkuu wa familia na kwa sababu maendeleo na ustawi wa jamii na kuzorota au kuparaganyika kwa jamii kunatokana na umadhubuti au udhaifu wa familia, Allah (sw) ametoa mwongozo maalumu wa kuchagua mke au mume mwema. Akitoa mada juu ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa TAMPRO wa Taifa, Ustadh Pazi Mwinyimvua amewataka Waislamu kujiwekea mikakati itakayowawezesha kuanzisha vyombo vyao vya habari ili kuondokana na hali ya sasa ya vyombo vyote muhimu vya habari kuwa na mlengo wa nchi za Kimagharibi na hivyo kufanya kazi kwa maslahi ya nchi za Magharibi na kupiga vita Uislamu. Alisema lengo kuu la vyombo vya habari vya nchi za Maghabiri ni kupandikiza umataduni wa nchi za Magharibi na ustaarabu wa Magharibi ambao haulingani na maadili ya Kiislamu wala maadili ya Kiafrika. Utamaduni wa nchi za Magharibi amesema, unaathiri fikra, tabia za vijana na kusababisha mmonyonyoko wa maadili ambao pamoja na mambo mengi, unaathiri maendeleo ya vijana mashuleni. Mtoa mada wa tatu aliyetoa mada kwenye semina hiyo ya siku moja alikuwa Ustadh Hashim Saiboko, aliyezungumzia wajibu wa wasomi katika kulingania Uislamu na kumcha Mwenyezi Mungu. Mambo yaliyozingatiwa kwenye mada yake yalikuwa kwamba Mwenyezi Mungu ametuumba sisi wanaadamu na majini ili tumuabudu, kwamba Allah (sw) ni Muumba wa viumbe vyote, mbingu na ardhi na vyote vilivyomo, kwamba ndiye mtoa elimu na mengine yote kwa waja wake na kwamba kuna kufa, kufufuliwa siku ya hesabu na watu na majini kuingizwa peponi na motoni kulingana na amali zao. Ametoa wito kwa Waislamu kuchangia walichonacho kwenye ujenzi wa shule, kuanzisha shughuli za kiuchumi na za maendeleo mbalimbali, kuboresha maisha yao na ya vizazi vyao na kuwa waadilifu sehemu za kazi, ziwe za kuajiriwa au miradi yao wenyewe. Mipango ya tawi la TAMPRO la mkoa wa Iringa ni pamoja na kufundisha vipindi vya dini vyuoni na mashuleni, uanzishaji na uimarishaji wa madrasa kwa kina mama, kina baba na watoto wa maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Iringa na vijijini. Waliochaguliwa kuongoza tawi la TAMPRO Iringa ni Ustadh Musa Mdidi Mwenyekiti,
Ustadh Jumaa Amiri Makamu Mwenyekiti, Suleiman Mwalukuta Mweka hazina,
Ustadh Saleh Kasera Katibu Mkuu na Ustadh Shams Elimi Naibu Katibu Mkuu.
Ofisi zake za muda zitakuwa ghorofa ya kwanza ya jengo la madrasa ya jumuiya
ya Dhiinurein, eneo la Wilolesi mjini Iringa utahitaji kulipa shilingi
3,000 kwa kiingilio na shilingi 500 ada ya kila mwezi.
Tuwasaidie Waislamu kielimu na kiuchumi - Bi Zuhura HAJAT Zuhura Jamal ni Muislamu aliyesilimu katika maajabu. Anatoa wito wa kuwasaidia Waislamu waliorejea kwa kuwapa elimu ya dini pamoja na nguvu za kiuchumi. Mwandishi wetu SAID RAMADHANI KISSIMBA alipata fursa ya kuongea na mwanaharakati huyu wa kike katika moja ya ziara zake mkoani Rukwa. BI. Zuhura inawezekana likawa jina geni kwa baadhi ya Waislamu nchini, lakini katika vitongoji na vijiji vya mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Rukwa jina hili ni maarufu na linafahamika na Waislamu wengi vijijini. Bi. Zuhura Jamal, mama aliyezaliwa karibu miaka 45 iliyopita huko Songea mkoani Ruvuma alikuwa ni Mkristu wa madhehebu ya Roman Catholic mpaka mwaka 1985 lakini alipata ujumbe kutoka kwa Allah (sw) wa kumtaka kufuata dini ya Allah (sw). Kusilimu kwake mama huyu kulileta dosari kubwa katika ndoa yake na mumewe. Mumewe alikataa kuingia katika dini ya Kiislamu na hivyo kusababisha kuvunjika kwa ndoa yao. Baada ya kutokea kwa mambo hayo, Bi. Zuhura aliamrishwa kutoka na kufikisha ujumbe wa Allah (sw) na hapo ndio ukawa mwanzo wake wa safari ndefu ya kuwatembelea Waislamu hasa vijijini ambao wengi wao hawafahamu vizuri kuishi katika mfumo wa Kiislamu. Bi. Zuhura tayari amekwisha tembelea vijiji vingi vya mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya na pia amekwisha tembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo (Zaire), pamoja na mkoa wa Rukwa, ambao umekuwa na idadi kubwa ya Waislamu wapya wakiwa hawana msaada wowote wa maendeleo ya dini yao na hata nguvu za kiuchumi za kuinua hali zao za maisha. Katika mikakati ya ziara zake vijijini, moja ya mbinu anazotumia za kuleta ufanisi ni kuongea na viongozi wa dini katika maeneo aliyotembelea ili kutafuta njia za kuondoa matatizo yanayowakabili Waislamu na kuimarisha umoja wa Kiislamu. Moja ya ziara zilizomhuzunisha Bi. Zuhura ni pale alipotembelea vijiji vya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambako alikuta Waislamu wengi vijijini wamekwisha poteza itikadi ya dini yao na kujiingiza katika mambo ya ulevi, wakati akina mama vijijini nao hawafahamu jinsi ya kujisitiri katika mavazi ya Kiislamu. Bi. Zuhura alisema, "Kila mara ninapokutana na Waislamu wenzangu wanawake hasa vijijini na kuwaelezea historia yangu ya Kiislamu, walishangaa sana, lakini niliwaomba wajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha yao na kuwaonya wasitegemee misaada au wafadhili", alisema mfadhili ni Allah (sw) na kwamba kufanya kazi ya halali ni ibada kubwa. Mwanaharakati huyu alisema, "Waislamu tuna deni kubwa mbele ya Allah (sw), kama hatutawaelimisha na kuwazindua Waislamu hawa vijijini ili wafahamu miiko na taratibu na maadili ya dini. Tatizo siyo kujenga Misikiti tu bali ni pamoja na kuwafundisha jinsi ya kujitwaharisha, kuswali, jinsi ya kuendesha familia ya Kiislamu na uanzishwaji wa miradi midogo midogo ya kiuchumi na mambo mengine ya dini". Jambo jingine lililomshtua Bi. Zuhura ni pale alipotembelea nchi ya Kongo (Zaire), eneo la Moba ambako alikuta idadi ya wanawake wa Kiislamu ni kubwa zaidi kuliko ya wanaume hali ambayo inasababisha wanawake wengi wakose waume, jambo hili hata hapa Tanzania linaanza kujitokeza. Alisema, "Allah (sw) alikwishafahamu tatizo la ndoa tangu mwanzo na kutufahamisha katika kitabu chake kitukufu (Qur’an) kwamba wanaume wanaruhusiwa kuoa wanawake hadi wanne ( ili kuleta uwiano halisi wa kijamii) ili mradi pawe na uadilifu katika mfumo mzima wa maisha yao ya kifamilia. Mama huyo ametoa wito kwa wanaume wa Kiislamu nchini na duniani kufuata suna hiyo Mitume (as) katika ndoa ili kuwahifadhi wanawake wasioolewa ambao nao wana matamanio ya kimwili kama binadamu wengine na wasingependa kuvuka mipaka ya Allah (sw) kwa kufanya uzinifu. Bi. Zuhura alisema ndoa za kidini, zitaondoa pia idadi ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa ambao ni mwanzo wa matatizo ya mirathi, maadili na huduma bora za kijamii. Mwanaharakati huyu wa dini ametoa wito kwa Waislamu walio na uwezo kumkopesha Allah (sw) kwa kuwasaidia Waislamu wenzetu wasio na uwezo na Mwenyezi Mungu (sw) atawalipa ujira mwema. Alishauri Waislamu kufungua shule za sekondari za Kiislamu vijijini pamoja na shule za awali licha ya watu binafsi, mashirika na vyama visivyo vya kiserikali kuanzisha miradi ya kibiashara, ufugaji na kilimo ili kuinua uwezo wa kiuchumi wa Waislamu vijijini. Mama huyo alisema hadithi nyingi za Mtume Muhammad (saw) zinaelezea umuhimu wa kufanya kazi halali na kwa ufanisi ili kupata ujira halali kwa maendeleo ya jamii nzima. Bi. Zuhura anatoa shukrani kwa Allah (sw) kwa kumjalia yeye kutembelea
maeneo hayo ya vijijini na anaaomba viongozi wote wa dini pamoja na waumini
kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa faida ya hapa duniani na kisha akhera.
Tumieni uhuru
wenu vyema
Wito huo umetolewa na Sheikh Kombo Ally Fundi wakati akihutubia Waislamu wa mjini Iringa hivi karibuni. Sheikh huyo alitoa mifano mbalimbali kutoka katika Qur’an na Sunnah, yenye kuonyesha misimamo ya wanawake waliopita ambao walifanya juhudi za kusimamisha haki. Aidha, aliwataka akinamama wa Kiislamu kutumia vizuri uhuru wa kutoa maoni katika kurekebisha mambo yasiyo sahihi ndani ya jamii yetu. Alitoa mfano wa mkataba wa Hudaybiyah ambapo mama wa waumini, Ummu Salamah (r.a) alimpa ushauri mzuri Mtume (saw) na Mtume akaufuata ushauri huo. "Huu ni ushahidi madhubuti kuwa Uislamu haumkatazi mwanamke kutoa maoni yake", alisema Sheikh huyo. Nasaha za Sheikh Kombo zimekuja katika kipindi ambacho jamii inalazimishwa ikubali kuwa Uislamu unamkandamiza mwanamke katika masuala mbalimbali kama vile mgawanyo wa mali na uhuru wa kutoa maoni na kufanya maamuzi. Sheikh Kombo alisisitiza kuwa maoni na jitihada za akinamama kupigania haki zizingatie mipaka iliyowekwa na sheria ya Kiislamu. Baadhi ya wapita njia waliokuwa wakisikiliza hotuba hiyo kupitia vipaza sauti vya Masjid Taqwa, walionyeshwa kuvutiwa mno na ujumbe huo, na walishangazwa na ukimya wa Waislamu mjini Iringa katika suala la kuueneza Uislamu kwa njia ya mikutano ya wazi. "Sisi tusio Waislamu, tunaweza kujifunza mengi kutoka kwa Waislamu,
lakini tatizo kubwa la Waislamu wa hapa, ni kutopenda kufanya mahubiri
hadharani", alisema kijana mmoja mkazi wa Frelimo aliyejitambulisha kwa
jina la William Kibassa.
|
TAHARIRI HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa
na kesi
Wazazi walia na Mkuu wa shule
Mkwawa
Serikali iache kudhulumu
Waislamu - Bakwata
KESI YA MIRATHI: Hukumu ya
Jaji Agostino yatupwa
Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini
Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga,
mtihani kwenu – Sheikh Akilimali
37 wasilimu Mwanza
Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali
ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni
Marekani?
Profesa amekosea kusema kwamba...
Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani
ni ugaidi
UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma
ya Marekani
Jengeni familia bora
Tuwasaidie Waislamu kielimu
na kiuchumi - Bi Zuhura
Tumieni uhuru wenu vyema
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 4
Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni
Ziara ya Kadinali Pengo Moro
Aonyesha ujuzi wa kutengeneza
Trekta
Waislamu wasizifanye sharia
za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge
Sengerema waomba msaada
Chakula na Lishe
|