|
|
| MGOGORO
WA CHWAKA NA MARUMBI
Serikali ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi Na Mwandishi Wetu, Pemba GAZETI moja binafsi la kila siku toleo la Jumamosi Agosti 22, 1998 liliripoti kwamba KMKM imewajeruhi wanakijiji sita wa Chwaka. Habari hizo zimedai kwamba askari hao wa kikosi maalum cha kuzuia magendo (KMKM) walichukua hatua hiyo kufuatia malumbano makali kati yao yaliyotokana na uvuvi wa samaki katika eneo la Michamvi. Likiendelea kuelezea mkasa huo, gazeti hili limeeleza kwamba askari hao wakiwa katika boti waliwachukua wavuvi wa kijiji cha Uroa na kuwafuata wavuvi wa Chwaka eneo la Michamvi na kuwapiga. Kwa mujibu wa gazeti hilo tukio hilo lililotokea mwishoni mwa wiki lilisababisha askari hao kurusha risasi hewani ili kutuliza ghasia. Walioshuhudia walidai kwamba wavuvi sita waliojeruhiwa waliingizwa katika boti za KMKM na kupelekwa kambi ya kikosi chao, na baadaye kuadhibiwa na askari hao kabla ya kupelekwa kituo cha polisi cha Mwera. Watu hao pia walidai kuwa waliandikishwa maelezo yao katika kituo cha polisi na kisha kujidhamini wenyewe na kutakiwa kuripoti kituoni hapo siku iliyofuata. Wananchi hao waliojeruhiwa walieleza wasiwasi walionao kutokana na tukio hilo, ambalo walidai kwamba lilikuwa limejaa jazba za kisiasa kati ya wakazi hao na vijiji viwili jirani. Hili ni tukio la tatu kwa wananchi wa maeneo hayo kupigana ambapo katika moja ya matokeo hayo, mtu mmoja tayari amekwishapoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya. Wakazi hao wa Chwaka walimweleza mwandishi wa habari hizo ambaye aliamua kufuatilia suala hilo kijijini huko kwamba asili ya ugomvi wao ambao una muda wa karibu miaka mitano sasa ni uvuvi wa juya ambao wanadai kwamba wao walianza kuutumia miaka mingi iliyopita. Walidai kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 wakazi wa kijiji cha Marumbi waliwaambia wakazi hao wa Chwaka kwamba mara tu CCM itakapoingia madarakani, uvuvi huo wataukomesha. Wakazi wa sehemu hizo mbili wanadaiwa kugawanyika katika makundi mawili ya CUF na CCM. Katika ugomvi uliotokea mwishoni mwa mwaka jana watu 23 kutoka kijiji cha Chwaka walikamatwa na kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya wilaya iliyoko Mwera. Kitu cha kushangaza ni kwamba watu wote waliokamatwa walikuwa ni kutoka upande wa Chwaka tu wakati ugomvi huo ulihusisha watu wa vijiji viwili. Walidai kwamba mtu mmoja ambaye alikwenda kuwasikiliza wenzake naye aalitiwa ndani na kudaiwa kuwatukana polisi. Pamoja na polisi, vyombo karibu vyote vya wavuvi hao vilichukuliwa na polisi na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uvuvi ambalo ndio pato pekee kwa wakazi wa sehemu hizo. Katika tukio jingine, wakazi wa Marumbi waliwanyang’anya madau watoto wadogo toka Chwaka katika hali ya kulipiza kisasi kufuatia tukio la mwanzo. Watoto hao inadaiwa walilazimika kuogelea hadi kwao ambapo wazee wao tayari walikuwa wakiwatafuta kwa muda mrefu. Katika hali hiyo ya kulipizana kisasi, wananchi wa Chwaka nao waliamua kuwakamata na kuwapiga wakazi wa Marumbi ambao wanadaiwa walikwenda kutafuta chambo huko Chwaka. Katika tukio la mwaka 1996 ambalo mtu mmoja alipoteza maisha, Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour alikwenda kijiji cha Marumbi na kuzungumza na wakazi wa kijiji hicho na baadaye kupiga marufuku uvuvi wa aina yoyote katika maeneo hayo. Pamoja na hatua hiyo, Dk. Salmin vile vile alimfukuza aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati kutokana na kutolishughulikia ipasavyo suala hilo. Hata hivyo katika hali ya kushangaza Dk. Salmin alishindwa kwenda kuzungumza na wanakijiji wa Chwaka pamoja na ukaribu uliopo baina ya vijiji hivyo. Baada ya mwandishi wa habari hizi kuwadadisi wakazi hao nini hasa kiini cha ugomvi wao huo, wanakijiji hao walikiri kwamba ugomvi huo umechangiwa zaidi na ushabiki wa kisiasa baina ya wakazi wa vijiji hivyo viwili. Wakazi wa Chwaka wamehusishwa na CUF na wale wa Marumbi CCM. Mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ali Khamis Salim alidai kwamba wakati wa vyama vya ASP na ZNP karibu wakazi wote wa Chwaka walikuwa ni wafuasi wa ASP. Kutokana na sababu ambazo Bwana huyo alikataa kuzieleza anadai kwamba baada ya kuja kwa vyama vingi, vijana wengi wa eneo hilo waliamu kujiunga na chama cha CUF. Aliendelea kudai kwamba katika hali isiyoeleweka kwamba imetokana na msingi gani uvuvi wa juya uzuiliwe, uvuvi ambao ulishazoeleka muda mrefu katika vijiji hivyo. Bwana Ali Khamis Salim aliendelea kudai wao wanadhani kwamba hatua hiyo ni kuwakomoa wananchi wa Chwaka tu kwani wenzao wa Marumbi waliendelea na uvuvi bila ya kuchukuliwa hatua yoyote pamoja na kwamba maeneo hayo yana vituo vya KMKM na polisi. Alidai kwamba kutokana na kuwa wananchi wa maeneo haya wanategemea uvuvi tu kupata riziki yao, wakazi hao waliamua kuvunja agizo la Rais na kuendelea na shughuli hiyo ya uvuvi hali ambayo anadai ilisababisha yeye pamoja na wenzake kadhaa kulazwa ndani kwa muda wa siku kumi na nne (14) na kisha kufunguliwa kesi ya jinai namba CC 232/97. Mwananchi mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina la Hassan Mjimbo (76) alimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba ni kwa vipi mtu mzima kama yeye akashiriki katika ugomvi wa watoto. Bwana huyo alidai kwamba pamoja na kutohusika na ugomvi huo, alikamatwa na kutupwa ndani kisha naye kufunguliwa mashitaka pamoja na wenzake wasiopungua ishirini na tatu. Watu hao kwa pamoja walidai kwamba wakati wa tukio la mwaka jana askari hao walikuja kuwakamata wakati wa sala ya Ijumaa na nusra sala hiyo ilikuwa isisaliwe kutokana na hofu waliyokuwa nayo wakazi hao baada ya kuona kundi kubwa la askari wa KMKM, polisi, JKU, mgambo na FFU. Wakazi hao walidai kwamba msako huo uliendelea kwa muda wa siku kadhaa nyumba hadi nyumba na kumkamata kila kijana wa kiume, hatua ambayo ilisababisha vijana wengi kukikimbia kijiji hicho na kuhamia mjini hali ambayo iliwazidishia ugumu wa maisha familia zao. Wakazi hao walilalamika kwamba serikali haionyeshi juhudi zozote za kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu bali badala yake inaonyesha kuupalilia kwa kuwalinda watu wa Marumbi. Waliendelea kudai kwamba ugomvi huo umekuwa ni vigumu kumalizika kwa vile viongozi wa jimbo hilo ndio wamekuwa wakiupalilia kwa maslahi yao ya kisiasa. Hata hivyo walidai kwamba hatua hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa kwa chama cha CUF kupata wafuasi zaidi kutoka maeneo hayo kutokana na hali ya mateso wanayoyapata. Wakazi hao walilalamika kwamba wakazi wa Marumbi wameshindwa
kutambua kwamba wao ni raia wa Zanzibar kabla ya kuwa CCM, hivyo nao wana
wajibu wa kufuata sheria na katiba ya nchi kama raia wengine.
|
TAHARIRI HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa
na kesi
Wazazi walia na Mkuu wa shule
Mkwawa
Serikali iache kudhulumu
Waislamu - Bakwata
KESI YA MIRATHI: Hukumu ya
Jaji Agostino yatupwa
Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini
Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga,
mtihani kwenu – Sheikh Akilimali
37 wasilimu Mwanza
Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali
ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni
Marekani?
Profesa amekosea kusema kwamba...
Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani
ni ugaidi
UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma
ya Marekani
Jengeni familia bora
Tuwasaidie Waislamu kielimu
na kiuchumi - Bi Zuhura
Tumieni uhuru wenu vyema
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 4
Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni
Ziara ya Kadinali Pengo Moro
Aonyesha ujuzi wa kutengeneza
Trekta
Waislamu wasizifanye sharia
za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge
Sengerema waomba msaada
Chakula na Lishe
|