|
|
|
Ndugu Mhariri HIVI karibuni Novemba 7, 1998 alifariki kiongozi wa Kitaifa wa Jumuiya kubwa ya Kiislamu BARAZA KUU, Sheikh Abas S. Kilima. Yeye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo. Kwa mujibu wa Baraza Kuu, taarifa (Press Relies) zilipelekwa katika vyombo vyote vya habari Redio, TV na magazeti. Vyombo hivyo, ila baadhi tu havikuona umuhimu wa kutangaza msiba na mazishi ya kiongozi wa Kiislamu kama vinavyofanya kwa viongozi wa Makanisa, CCM na dola. Hatua hiyo ya vyombo vya habari imewawezesha Waislamu kufanya tathmini ya kukua kwa mtandao wao wa habari. Baadhi ya vyombo vya habari ila vichache, tunavyovipongeza kwa dhulma kususia kifo na mazishi ya Katibu Mkuu wa Baraza Kuu, Waislamu mtu kwa mtu, madrasa kwa madrasa, Msikiti kwa Msikti n.k. walipeana taarifa kama nyuki. Mazishi ya kiongozi huyo wa Kiislamu yalikuwa si ya kawaida. Maelfu kwa maelfu ya Waislamu waliziba barabara kubwa ya Morogoro na kwa muda usiopungua masaa mawili magari yalilazimika kusimama. Serikali kwa upande wake ilitoa rambirambi kwa kumwaga makundi ya polisi wa wazi na wa siri ambao hata hivyo walitawanyika bila kusema au kufanya lolote. Ninachopenda kuwasisitiza Waislamu ni kuwa huu mtandao wetu wa habari ndio wa kutegemea sana. Tunaposikia mtu anapiga kelele usiku "Yalla ndugu zangu Waislamu" lazima tutoke haraka. Unapopata au kusoma habari yoyote mdokeze ndugu yako Muislamu. Kuuza au kununua ni jambo dogo sana mbele ya Allah ukilinganisha na kukimbilia tukio muhimu linalohusu Uislamu. Habari yoyote iliyoandikwa/kutolewa na "fasik" tusiiamini mpaka tupate ufafanuzi kutoka katika taasisi ya Kiislamu inayokubalika. Mohammed Haule,
Masheikh waache kujishughulisha na mambo ya laghwi Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi katika gazeti lako lenye manufaa kwa ummah wa Kiislamu ili nitoe machache yenye kusikitisha. Ninasikitika kuandika haya, lakini imenibidi niandike kwa kuzingatia Hadith ya Mtume (s.a.w.) pale aliposema: "Mwenye kuona miongoni jambo lolote lenye kuchukiza basi akemee kwa ulimi wake..." (mpaka mwisho wa Hadith). Ni aibu kubwa kwa Uislamu na Waislamu kwa ujumla pale viongozi wetu ambao ni Masheikh wanapojishughulisha zaidi na mambo yasiyo na manufaa yoyote hapa duniani wala akhera. Mfano mmoja ni Sheikh (namuhifadhi kwa jina) maarufu, pia anajulikana sana kama ni mwanaharakati wa Kiislamu pale anapojiweka mbele na kuwa ni kiongozi mkuu wa usuluhishi wa mgogoro wa klabu moja ya mpira wa miguu, pia ni mdhamini wa klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi. Alhaji anapopoteza muda wake kwa kuwasuluhisha wanaoshughulishwa na njaa za matumbo yao. Je, hija yake ilikuwa ni mabruur? Tukumbuke 2000 haipo mbali nasi panapo uhai, lakini Masheikh zetu wamekaa kujishughulisha na yale yasiyohusiana hata theluthi na Uislamu. Ikiwa viongozi ndio wapo hivi hawajishughulishi na maendeleo ya Uislamu, hiyo 2000 ndiyo tutegemee nini? Naona Sheikh huyo ameghafilika na wengine kadhalika ambao wanajishughulisha na mambo ya laghwi, nimewajibika kuwazindua kama Muislamu mwenye kupenda maendeleo ya Waislamu na Uislamu. B.R. Ally,
Ndugu Mhariri, Nakiri kusoma makala ya Ndugu Jackson Urassa katika AN-NUUR Na.174 la Novemba 6-12, 1998. Kwanza napenda kumpongeza ndugu Jackson kwa makala yake iliyoonyesha kuwa yeye ni mtu mwenye akili zilizotulia, asiyehamaki na mwenye nia ya kujifunza. Nashauri wasomaji wengine waige mfano huu mzuri wa Ndugu Jackson. Pili namshukuru kwa ushauri wake kuwa nisijisifu. Lakini maneno yangu aliyoyanukuu, mimi nimeyaiga toka kwa huyo aliyemwita "Mwanatheojia mkongwe" yaani Paulo. Na maneno hayo (1 KOR 2:10-15) niliyanukuu kabla ya kuandika yangu. Hivyo kama ni kufanya uadilifu, basi angeanza kumshutumumu Paulo kisha mimi. Lakini Paulo alimsifu, mimi akanishutumu kwa kitendo kile kile kimoja. Hata hivyo hayo sio ya msingi. Cha msingi sana ni maswali aliyouliza. Hivyo naona nianze kujibu maswali yake moja kwa moja. Naanza na swali lake analosema huyo Roho Mtakatifu nimempata wapi. Kwa bahati mbaya sana wahubiri Wakristo wanasisitiza sana kuwa, huwezi kuwa na Roho Mtakatifu hadi uamini imani ya Kikristo. Hiyo sio kweli kabisa. Roho Mtakatifu kwa mujibu wa tafsiri aliyoitaja Ndugu Jackson, ni nguvu au uwezo mtakatifu. Nguvu na uwezo mtakatifu unahusiana na Mwenyezi Mungu peke yake. Na huzitumia nguvu hizo apendapo, au humpa nguvu au uwezo huo mtu ye yote amtakaye awe na dini au mpagani. Uwezo mtakatifu hauhusiani na mambo ya dini tu. Bali hata uvumbuzi usio wa kawaida hufanywa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu yaani uwezo mtakatifu (Roho Mtakatifu), japo wavumbuzi wenyewe ni watenda dhambi. Tukirudi katika mambo ya kidini, uwezo mtakatifu umefanya kazi hata kabla ya kuzaliwa Yesu (a.s.). Kwa mfano"Mbingu na Ardhi n.k. vimeumbwa na tamko lenye uwezo mkuu la Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu alitamka tu viwe na vikawa. Huo ni uwezo (Roho) mtakatifu. Aidha kuzaliwa kwa Isaka, Samson, Yohana mbatizaji, Yesu Kristo, kuvushwa Waisrael baharini n.k. vyote vimefanyika kwa uwezo (Roho) mtakatifu. Hivyo Mwenyezi Mungu (S.W.) humpa Roho Mtakatifu mtu yeyote amtakaye ili afanye kazi maalum kwa faida ya watu na viumbe vingine. Nadhani nitashangaza sana, kama sio kutoaminika kabisa nikisema kuwa, sijawahi kukanyaga katika mlango wa chuo cha theolojia chochote na wala sijawahi kuwa hata mhudumu wa kanisa. Aidha, utaalamu (profession) wangu ni tofauti kabisa na theolojia. Lakini vyote vinavyofanyika katika vyuo vya theolojia ninavijua, vitabu vyote muhimu vinavyotumika huko, ninavijua na ninavyo. Kuhusu tafsiri ya jumla ya Roho Mtakatifu iko katika AN-NUUR Na. 160 Uk. 14 la Julai 31 August 6, 1998 na sio toleo Na. 60 kama inavyoonekana katika makala yangu katika AN-NUUR Na. 169 (sio 199). Hayo ni makosa ya kawaida. Yanaweza kutokana na mwandishi, mchapaji au mashine. Hivyo japo makala hiyo haijakamilika, lakini kipande kilichokwisha chapishwa kimetoa tafsiri zote muhimu za Roho Mtakatifu. Kwa hiyo Ndugu Jackson soma makala hiyo, inshallah utaelewa. Ama kuhusu ufafanuzi zaidi juu ya Uislamu kulingana na makala yangu "utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu" (AN-NUUR Na. 171 Uk14), nakushauri kuwa, ili uweze kuielewa kirahisi sana, inabidi kwanza ufahamu kwa ufupi historia ya Uislamu katika siku za mwanzo za Umma huu wa mwisho. Ni vyema ujue vipi Muhammad alipewa Utume, kulitokea nini baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kuusimamisha kikamilifu Uislamu n.k. Hivyo mwone Mwislamu yeyote mwadilifu anayefahamu hayo, kisha yalinganishe na Unabii wa Isaya nilioufasiri. Mwisho nawatakia wasomaji wote wenye nia ya kujielimisha juu ya Uislamu, mafunzo mema na Allah (s.w.) yuko pamoja nao. Wabillah Tawfiiq, Sheikh Bernard P. Nyangasa,
Ndugu Mhariri NATOA masikitiko yangu kwa Baraza la Usalama la Marekani na sio Umoja wa Mataifa kile inachokifanya dhidi ya Iraq. Mimi naungana na wenzangu kupinga uvunjaji haki za binadamu nchini Iraq. Kilichopo kwa Mmarekani nchini Iraq ni Saddam na sio silaha za nyuklia (sumu) Saddam amewekewa vikwazo vya uchumi hata kabla ya matokeo ya ukaguzi kutoka kwa tume ya Richard Bulter. Nyuklia zipo Iraq, lakini India na Pakistani viliondolewa vikwazo hivyo, na ili hali silaha zake hazikuteketezwa.Mmarekani atapambana kwa silaha gani nchini Iraq? Vita vya Marekani kwa Saddam vinasababishwa na kushindwa katika vita vya Ghuba, ikiwa inasaidiwa na mataifa 28. Mimi ninahoji, Je! itakapogundulika ni hatua gani zaidi zitachukuliwa kwa Saddam kama ni kweli? Kama wakaguzi watakosa, Marekani ipo tayari kurudisha hasara zote zilizosababishwa na vikwazo vya uchumi? Kwanini iwe Iraq, Libya, Sudan na zisiwe Pakistani, India, Kuwait, Misri, Indonesia? Kwanini Marekani isipeleke manuari za kivita Congo, ambapo wananchi wanateseka katika nchi yao bila hata kosa walilolifanya, nani wa kubeba lawama? Ubabe huu wa Marekani, kutawala baraza la Umoja wa Mataifa, kuingilia mambo ya ndani ya nchi, kama Malaysia hivi sasa Je! tutaupa jina gani? Marekani ni firauni wa leo, mwisho wake ni kuangamia tu, kama alivyoangamia firauni wa Misri. Mwisho namuomba Rais Saddam aache kupigana kama Mwarabu, arejee kwenye Uislamu wa kweli, ashirikiane na wanaharakati wa Kiislamu. Akitekeleza haya Marekani na washirika wake watafyata mkia mara moja. Mpenda Amani, Mohamedi Mchomvu,
|
YALIYOMO
Maoni Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha Sakata la
mabucha ya Nguruwe kuibuka upya
Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni MACHO YA
SHUTUMA
Serikali
yatakiwa iwachukulie hatua wauaji
Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni Silaha yetu
ni kura ya pamoja
Anuani
ya fikra
Tunahitaji
"UN' ya Waislamu!
Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao Wanafunzi
Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa
Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja Someni muiokoe jamii kimaadili Kesi
nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini Chakula
na lishe
|