AN-NUUR 
Na.176 Shaaban  1419, Novemba 20 - 26, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa
 
  • Ni kesi ya tuhuma ya kashfa
  • Kesi ya kukishambulia kituo kusikilizwa Nov. 24
KESI mojawapo ya mihadhara iliyofunguliwa na serikali mwishoni mwa mwaka wa jana (1997) dhidi ya Waislamu sita imefutwa na mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Jijini hapo Novemba 13, mwaka huu. 

Washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa wakikabiliwa na tuhuma ya kutoa maneno yenye lengo la kukashifu Biblia Takatifu, Wakristo, Jeshi la Polisi na viongozi wakuu na kutishia usalama wa nchi. 

Watuhumiwa hao ni pamoja na Uliza Rashid (37), Swalehe Rashid (30), Ramadhani Mkwangu (30), Ally Majapa (42), Ally Athumani (40), Hamisi Swalehe (50) na Ramadhani Hamisi (30). 

Kufutwa kwa kesi hiyo kumezingatia ombi la Wakili wa washitakiwa, Bw. Twaha Taslima aliloliwasilisha mahakamani hapo hivi karibuni. 

Wakili Taslima aliiomba mahakama hiyo iwaondolee wateja wake shauri hilo kwa vile lilikuwa limekwishachukua zaidi ya mwaka mmoja mahakamani hapo bila kusikilizwa. 

Aidha, kutosikilizwa kwa kesi hiyo kwa muda wote kumetokana na mashahidi wa upande wa serikali waliotarajiwa kushindwa kufika mahakamani tangu upelelezi wa kesi hiyo ukamilike hapo Septemba 4, mwaka huu. Hata hivyo haikuelezwa ni kwa nini walishindwa kufika. 

Wakili Taslima aliiambia mahakama hiyo kuwa wateja wake wanayo haki ya kufutiwa kesi hiyo kulingana na kifungu cha 225 (5) cha sheria ya kanuni za mwenendo wa Jinai ya mwaka 1984 kinachoruhusu washitakiwa kufutiwa kesi husika iwapo itafikisha siku sitini (60) mahakamani bila kusikilizwa na pia mwendesha mashitaka wa serikali (PP) au mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa (RCO) kushindwa kutoa sababu za msingi za kuendelea kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani bila kusikilizwa. 

Awali katika kesi hiyo, mwendesha mashitaka wa serikali, Inspekta msaidizi wa polisi, mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Bi. Cypriane William, alidai kuwa mnamo Septemba 23, mwaka jana (1997) huko Mwanyamala A, wilayani Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, washitakiwa kupitia mhadhara wao walitoa maneno yenye lengo la kukashifu imani ya watu wengine. 

Wakati huo huo, kesi nyingine namba 1383/97 ya tuhuma ya kukishambulia kituo kidogo cha polisi cha Msisiri, kilichopo maeneo ya Mwananyamala A, Jijini inatazamiwa tena kuanza kusikilizwa hapo Novemba 24, mwaka huu, katika mahakama ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam. 



Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo 
 

WAZAZI Waislamu wametakiwa kuwasadia na kuwaendeleza watoto wenye vipaji mbalimbali ili kuvikuza. 

Profesa Bukhet Kilonzo ametoa nasaha hizo hivi karibuni akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya 15 ya shule ya sekondari ya Kiislamu ya Jabal Hira iliyoko mjini Morogoro. 

Profesa Kilonzo alisisitiza kwamba ni muhimu wazazi kuwa na mikakati madhubuti ya kuwalea na kuwapa elimu vijana wao kwani hilo ndilo jambo la muhimu zaidi katika Uislamu wao na maisha yao kwa ujumla. 

Profesa Bukhet Kilonzo ambaye ni mtaalam bingwa wa taaluma ya vijidudu vienezavyo maradhi kwa binadamu na wanyama (Sokoine University) ameuomba uongozi wa shule ya Jabal Hira kutoa motisha na kuwa na namna nzuri ya kukaa na waalimu ili kuepukana na tatizo la waalimu kuhama hama. 

Kwa upande wa wahitimu, Profesa Kilonzo aliwaasa wasitosheke na kiwango cha elimu walichokipata kwani hata yeye pamoja na uprofesa wake bado anatafuta elimu. 

Wengine waliokuwa wamehudhuria sherehe hizo ni Dk. Dihenga ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na Imam wa Msikiti Mkuu wa Morogoro Sheikh Kairo. 


Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa:
 
  • Wazazi wakumbushwa wajibu wao
WAZAZI kote nchini wamekumbushwa wajibu wao katika kuwalea watoto hasa walio katika vitivo vya elimu za kati na juu. 

Meneja wa shule ya sekondari ya Thaqafa ya mjini Mwanza Bw. Maruzuku Magongo alitoa ukumbusho huo wakati wa mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo hivi karibuni mbele ya Bodi ya shule, wazazi na wanafunzi wenyewe kwenye ukumbi wa shule hiyo. 

Bw. Maruzuku aliyasema hayo mara baada ya mkuu wa shule hiyo Mwalimu Hamza Kayemba kumaliza hotuba yake iliyokuwa na malalamiko pamoja na masikitiko kwa mienendo mibaya inayoonyesha kushuka kwa maadili miongoni mwa jamii za sasa. 

Mwalimu Kayamba alisema kuwa Thaqafa sekondari Mwanza iliamua kufuata sheria za shule nchini na taratibu za malezi ya Kiislamu barabara na matokeo yake ni idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa na kuamua kuacha shule, wengine kufukuzwa na baadhi yao kuhama, wazazi wengi hawako karibu na walimu ili kushirikiana kuwarudi watoto mara wafanyapo mambo ya hovyo. 

Alisema kuwa wanafunzi ambao walikuwa wanasheherekea kumaliza kidato cha nne mwaka huu shuleni hapo, walianza wakiwa 200 lakini watakaofanya mitihani ni 103 tu, waliobakia wote kwa sababu mbalimbali hawako shuleni Thaqafa. 

Alitoa ushauri kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kwa ujumla kuwa karibu na uongozi wa shule na walimu kwa ujumla ili kushirikiana kuwarekebisha watoto ili wawe ni kizazi bora cha baadaye. 

"Kwa kuwa kidato cha nne si vyema siku kama hii kuita ni mafahali, kwani kazi iliyo mbele yao bado ni kubwa na inahitaji subira na nidhamu ya hali ya juu, miaka minne waliyokaa hapa Thaqafa Mwanza haitoshi kusheherekea ila iwape picha tu ya mwanzo mgumu wa vitivo vya elimu ya juu", Bw. Maruzuku alisema. 

Akikazia kampeni za sasa za taifa za uzinifu "salama" aliwashauri waachane kabisa na uasherati kwa ujumla wake. 

"Hakuna cha kondomu, maradhi ya zinaa mwisho wake ni kifo tu, lugha ya kuwa na mpenzi mmoja, tumia kondomu ni ya hatari mno, mtaangamia bure", alisema. 

Akimalizia hotuba yake, Bw. Maruzuku Magongo aliwaomba wazazi na walezi kwa pamoja kuwadhibiti watoto kutokuwa na muda mwingi wa kupoteza (free time) aliwashauri watoto kutopoteza muda kwenye magenge, kusoma magazeti ya kipuuzi na vichekesho ambavyo haviwasaidii chochote, vitabu vya matusi, vipindi vya upuuzi vya TV na video, pia waache kulala na uvivu ni vitu vya kupigwa vita sana. 

Katika hafla hiyo mzee Hezron Ndonho kwa niaba ya wazai alitoa shukrani za pekee kwa mkuu wa kitengo cha dini ya Kiislamu shuleni hapo kwa nasaha zake bora kabisa. 

Alisema kuwa anaamini kabisa kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.) hakusema maneno hayo ila aliambiwa na Allah (s.w.) kuwa sema, yaani atwambie sisi. 

Mkuu huyo wa kitengo cha dini (Mudir) Ustadh Mussa Juma Kondo katika nasaha zake aliwafafanulia Hadith ya Mtume isemayo: "Fanya mambo matato, kabla ya kufikwa na matano mengine". 

Aliyataja mambo haya kuwa ni: Utumie ujana wako katika mambo ya kheri kabla ya uzee, utumie afya yako katika mambo ya kheri kabla ya kifo, utumie wasaa wako (nafasi) kabla ya shughuli nyingi, itumie mali yako (utajiri) kabla ya umasikini, utumie uhai wako (maisha) kabla ya kifo. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
Maoni 
Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha 

Sakata la mabucha  ya Nguruwe kuibuka upya 
Na Mwandishi Wetu  

Kondom sio kinga ya Ukimwi 

Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni 

MACHO YA SHUTUMA 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Serikali yatakiwa iwachukulie hatua wauaji 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni 

Silaha yetu ni kura ya pamoja 
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC  U.S.A 

Anuani ya fikra 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Kuukaribisha mwezi mtukufu 

Tunahitaji "UN' ya Waislamu! 
Na Said  Rajab 

Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana 

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2 
Na Ustaadh Kupa Pazi Said 

Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa 

Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo 

Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao 

Wanafunzi Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa 
Na Iddi M. Katiba, Mwanza 

Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah 

Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja 

Someni  muiokoe jamii kimaadili 

Acheni Shirki 

Kesi nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa 
Na Muhibu Said 

Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza 

Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa 

Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini 

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Umuhimu wa chakula katika shule za awali]  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita